DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

[Muhammed Seif Khatib]

 

1.                  UTANGULIZI:

 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

Waheshimiwa Wajumbe;

 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo Taasisi inayotakiwa kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,  kwa mujibu wa ibara ya 5(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.  Kwa muda sasa  Tume imekuwa ikifanya mtayarisho kwa ajili hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwahusisha wadau katika hatua za awali.

 

Tume kwa muda mrefu sasa imekuwa ikifanya maandalizi ya kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.  Maandalizi hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwepo mfumo thabiti utakaowezesha kwa ufanisi wa hali ya juu utekelezaji wa zoezi zima ikiwa ni pamoja na wa kisheria upatikanaji wa fedha na kutafakari ushauri wa wataalamu (consultants).

 

Hapo awali, Tume ilitarajia zoezi la kuanzisha Daftari la kudumu la Wapiga Kura lingeanza mwezi Septemba, 2003.  Lakini kutokana na ukosefu wa fedha, ratiba ilipangwa upya ili zoezi lianze Januari, 2004.  Hata hivyo, uhakika wa zoezi hilo kuanza ulipatikana baada ya kiasi cha Tshs.14.2 bilioni, hii ikiwa ni sehemu tu ya gharama zilizoidhinishwa na bunge kwa ajili ya uanzishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.  Kwa hiyo Tume ilirekebisha ratiba yake ambapo hatimaye utekelezaji uliweza kuanza tarehe 01 Machi, 2004.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti,

 

Waheshimiwa wajumbe,

 

Kama wote mnavyofahamu, uandikishaji wa Wapiga Kura ni hatua muhimu katika uchaguzi kwani pasipo na wapiga kura haiwezekani kuwepo na uchaguzi.  Umuhimu wa hatua hiyo ndio unaotiliwa maanani katika kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

 

Katika kukuza demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini mwetu na kuendeleza uwazi na utawala bora, uchaguzi ni moja kati ya nyenzo muhimu sana.  Uchaguzi unaoendeshwa kwa njia za demokrasia, unahitaji kuwepo kwa utaratibu wa wazi na mzuri wa kuandikisha raia wote wanaostahiki kupiga kura.  Orodha ya wapiga kura inapokuwa inaaminika, matatizo mengi yanaweza kupungua sana.  Kutokana na sababu hizo, uandikishaji wapiga kura ni hatua muhimu sana katika uchaguzi.

 

Naomba ifahamike kuwa wakati wa kuandikisha wapiga kura, uandikishaji huo utakuwa tofauti kabisa na mfumo wa uandikishaji tuliouzoea hapo zamani.  Aidha teknolojia itakayotumika, itakuwa tofauti kwa hivyo ni vema viongozi wa CCM  wote kujielimisha zaidi na kupata ufahamu wa kutosha kuhusu zoezi hilo ili na sisi tushiriki kikamilifu tukiwa wadau wa uchaguzi na kuona jinsi ya kuboresha zaidi utekelezaji wake na kuweza kutoa elimu ya kutosha kwa ajili ya uchaguzi.

 

2.            GHARAMA ZA UANZISHAJI WA DAFTARI:

 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

Uzoefu unaonesha kuwa kila uchaguzi unapofanyika kwa utaratibu unaotumika mpaka sasa, gharama za uandikishaji wapiga kura ni kati ya 25 – 30 asilimia ya gharama zote za uchaguzi.  Kwa mfano, kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 gharama za uandikishaji wapiga kura ilikuwa Shs. 20.027 bilioni kati ya shs. 38.5 bilioni ikiwa ni 26.0 asilimia.  Mwaka 2000 gharama za uandikishaji zilikuwa shs. 10.27 bilioni kati ya Shs. 39.89 bilioni zilizotumika kwa shughuli za uchaguzi ikiwa ni 25.7 asilimia.   Gharama hizo za uandikishaji tu wa wapiga kura huigharimu  fedha nyingi serikali hasa katika chaguzi ndogo zinazofanyika kwenye majimbo yanayokuwa wazi kwa nafasi  za ubunge na udiwani gharama ya uandikishaji hujirejea na kuwa kubwa.

 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi  baada ya Uchaguzi Mkuu wa Kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa uliofanyika mwaka 1995, ilibaini matatizo haya na kupendekeza serikalini kwamba kuanzishwe Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo litakuwa na  kumbukumbu za wapiga kura na kutumika katika  chaguzi zote na hivyo kupunguza gharama.  Serekali yetu ilikubali pendekezo hili na kuliingiza katika Katiba ya nchi.

 

Katika zoezi la kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga kura  kwa sasa linatarajiwa kugharimu shs. 36.6 bilioni.   Sehemu kubwa ya gharama hizo ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hasa Kamera, filimu, fomu za OMR na vifuko vya kadi za Wapiga Kura (Lamination pouches).   Aidha gharama za malipo ya Waandishi Wasaidizi zinahusika katika jumla ya gharama hizo.

 

3.            MISINGI YA SHERIA (LEGAL FRAMEWORK):

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

Ibara ya 5 (3)  ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 na Kifungu cha 12 cha Sheria ya Uchaguzi  Na. 1 ya mwaka 1985 vilifanyiwa marekebisho mwezi Januari, 2000 kwa madhumuni ya kuwezesha kuanzishwa Daftari la Kudumu la Wapiga kura lakini kutokana na muda kuwa mfupi na uhaba wa fedha na nyenzo muhimu, Daftari hili halikuweza kuanzishwa kwa ajili ya kutumika katika chaguzi  za mwaka 2000.

 

Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchagua mfumo na teknolojia inayofaa katika kuanzisha Daftari hili iliviangalia tena Vifungu vya Sheria ya  Uchaguzi Na. 1 ya 1985 na ile ya Uchaguzi wa Madiwani Na. 4 ya mwaka 1979, vinavyohusu utaratibu wa uandikishaji Wapiga Kura na kutoa mapendekezo ya Sheria. Mapendekezo hayo yana lengo la  kuwezesha Tume kutekeleza na kusimamia ipasavyo zoezi la uanzishwaji wa utumiaji wa Daftari la Wapiga Kura, Marekebisho hayo tayari  na yameoanishwa kwenye  wa sheria uliopitishwa  na Bunge tarehe 9 Juni, 2004.  

 

Baadhi ya mapendekezo hayo yanahusu:-

 

(i)                 Kutoa mamlaka kwa tume ya Taifa ya Uchaguzi kuandaa na kutunza Daftari hilo kikamilifu.

 

(ii)               Kuiwezesha Tume kuandikisha wapiga kura wote watakaokuwa wamefikia umri wa miaka 18 ifikapo Oktoba, 2005.

 

(iii)             Kuwa  na Daftari la awali (Provisional Voters’ Register).

 

(iv)              Kuweka utaratibu wa kukagua Daftari la awali na kuweka pingamizi na kukata rufaa mahakamani kwa wasioridhika.

 

(v)                Kuwapatia kadi  yenye picha ya mpiga kura waliojiandikisha badala ya shahada.

 

(vi)              Kutoa madaraka kwa Tume kusimamia na kuratibu utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura.

 

4.            FAIDA ZA KUWA NA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA:

 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

Daftari la Kudumu  la Wapiga Kura litahifadhi majina yote ya watu waliojiandikisha kuwa wapiga kura.   Daftari hilo litaandaliwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kuwezesha kumbukumbu za wapiga kura kuhifadhiwa katika kompyuta  (Central Database).

 

Faida  za kutumia  utaratibu huu ni hizo zifuatazo:-

 

(i)                 Utawezesha kupungua kwa gharama za Uchaguzi kama ilivyoelezwa hapo awali, kwa kuwa hatutarudia rudia uandikishaji kama ilivyo utaratibu wa sasa.

 

(ii)               Utawezesha kuwepo kwa orodha sahihi ya kudumu ya Wapiga Kura kwa majimbo na Kata zote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakayotumika katika chaguzi kadhaa bila mtu kulazimika kujiandikisha tena kila uchaguzi unapofanyika.  Usahihi wa Orodha ya Wapiga kura utatokana pia na kuwa na utaratibu wa kuboresha Daftari, kwa kuwaondosha wasiostahiki kuwamo na kuingiza wanaostahiki kuwemo.  Vile vile utaratibu utawekwa wa kurekebisha taarifa za watu ambao wamebadilisha makazi yao au wanaotaka baadhi ya taarifa zao zibadilishwe.

 

(iii)             Utawezesha kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza ya kudai kwamba baadhi ya watu wanajiandikisha zaidi ya mara moja au kuuza shahada kwa watu ambao hawastahiki kupiga kura.  Kuwepo kwa Daftari la Kudumu kutazuia hali hiyo kutokea kwa sababu:

 

·        Kadi zitakazotolewa zitakuwa na picha ya Mpiga Kura

·        Daftari (database) litakuwa na picha, saini na alama ya dole gumba ya Mpiga Kura.

·        Database itakuwa na programu maalumu ya kutambua na kulinganisha alama za dole gumba ili kutambua wapiga kura wote waliojiandikisha zaidi ya mara moja.  Aidha, Wapiga Kura watakaogundulika kufanya hivyo kujiandikisha zaidi ya mara (moja)  wataondolewa katika database na hivyo kupoteza haki ya kupiga kura na pia wanaweza kushitakiwa mahakamani.

 

(iv)              Utawezesha Tume kupanga mipango na kufanya maandalizi ya Uchaguzi mapema na kwa uhakika zaidi kwani Tume itakuwa tayari na idadi ya Wapiga Kura ambayo ndiyo chanzo muhimu cha kuwezesha kufahamu mahitaji halisi katika utekelezaji wa hatua mbalimbali za uchaguzi ikiwa ni pamoja na mahitaji ya vifaa na fedha za uchaguzi.

 

(v)                Utampatia Mpiga kura kitambulisho ambacho kinachoweza kumsaidia katika shughuli nyingine.

 

(vi)              Utamwondolea mpiga kura usumbufu wa kulazimika kujiandikisha kila uchaguzi unapofanyika.

 

(vii)           Utatumia utaratibu mzuri wa teknolojia ya kisasa kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura na utunzaji wa kumbukumbu zinazohusika.

 

5.            MFUMO WA TEKNOLOJIA ITAKAYOTUMIKA KUANDIKISHA WAPIGA KURA:

 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

(i)           Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakaloanzishwa litakuwa katika mfumo wa kompyuta  computerized” na kumbukumbu zake zitakuwa zikirekebishwa mara kwa mara na kutumika katika chaguzi zingine.

 

(ii)         Teknolojia itakayotumika kuchukua taarifa za Wapiga Kura ni Kujaza fomu maalum za OMR (Opitical Mark Recognition).  Ni teknolojia iliyotumika  wakati wa zoezi la sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agosti, 2002 na itatumiwa  pia na Tume ya Uchaguzi ya Zanzíbar (ZEC).

 

6.      KANDA ZA KUANDIKISHA NA TAREHE ZAKE

 

Tume imeamua kuwa uandikishaji wa Wapiga Kura utafanyika kwa  Kanda kwa siku 21 katika kila kanda badala ya  kufanyika wakati mmoja nchi nzima kwa siku 21.  Uandikishaji huo unatarajiwa kuanza Septemba, 2004 katika Kanda saba.  Utaratibu mzima utakuwa kama ifuatavyo:-

 

Na.

Kanda

Mikoa inayohusika

Wakati

1.

Kanda ya Kusini

1.  Lindi

2.  Mtwara

20/09/2004  - 10/10/2004

2.

Kanda ya Nyanda za Juu Kusini

1.  Iringa

2.  Mbeya

3.  Rukwa

4.  Ruvuma

 

28/10/2004 – 17/11/2004

3.

Kanda ya Kati

1.  Kigoma

2.  Tabora

3.  Singida

4.  Dodoma

 

 

05/12/2004 – 25/12/2004

4.

Kanda ya Ziwa

1.  Mwanza

2.  Kagera

3.  Mara

4.  Shinyanga

 

 

12/01/2005 – 01.02.2005

5.

Kanda ya Kaskazini

1.  Tanga

2.  Kilimanjaro

3.  Manyara

4.  Arusha

 

19/02/2005 – 11/03/2005

6.

Kanda ya Pwani

1.  Pwani

2.  Dar es Salaam

3. Morogoro

 

29/03/2005 – 18/04/2005

7.

Kanda ya Zanzíbar

Mikoa yote ya Zanzíbar

Itafuata ratiba ya uandikishaji ya ZEC

 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2005 likikamilika hakutakuwepo na uandikishaji mwingine kwa ajili hiyo.  Hapa  inasisitizwa kuwa mtu yeyote ambaye hataandikishwa kwa wakati kwa kuzingatia ratiba iliyooneshwa hapo juu, hataruhusiwa kupiga kura.  Sisi viongozi  tuhakikishe tunahimiza wananchi kwenda kujiandikisha ndani ya siku 21 kama zinavyoonekana katika ratiba za Kanda.

 

7.         UTARATIBU WA KUANDIKISHA WAPIGA KURA

     

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

(iii)             Kutakuwepo na vituo vya kuandikisha wapiga kura  (Registration Centres).  Vituo hivi vitapangwa na vitakuwa katika majengo ya umma kama  mashule na vyuo.

 

(iv)              Kila kituo cha kuandikisha wapiga kura, kitakuwa na Mwandishi Msaidizi atakayehusika na uandikishaji wapiga kura.

 

(v)                Wanaojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura watapigwa picha mbili bure  na zitakabidhiwa kwa Waandishi Wasaidizi katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.

 

(vi)              Fomu maalum ya  OMR itatumika katika kuandikisha wapiga kura.  Picha moja itabandikwa katika fomu ya OMR na nyingine itawekwa katika kadi ya Mpiga kura.  Mpiga kura aliyeandikishwa atakabidhiwa kadi yake  yenye picha hapo hapo kituoni.  Kadi itatunzwa ili itumike katika chaguzi zitakazofuata.

 

(vii)            Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu vitakuwa na wawakilishi watakaoshuhudia uandikishaji huo unafanywa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

 

 

 

 

 

8.         DAFTARI LA AWALI LA WAPIGA KURA

 

-           Uandikishwaji ukikamilika, fomu maalumu za OMR  zenye taarifa za waliojiandikisha  zote zitakusanywa na kupelekwa makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kuingizwa kwenye “computer”  kwa kutumia mashine maalumu zinazoaitwa “SCANNERS” na kutengeneza Daftari la Wapiga Kura (Database).  Hatua inayofuata ni orodha ya awali ya wapiga kura (Provisional voters’ Register) itachapishwa na kupelekwa kwenye Majimbo na Kata zote nchini.

 

9.         UKAGUZI WA DAFTARI LA AWALI, PINGAMIZI, RUFAA NA MAREKEBISHO

     

      Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

Orodha ya wapiga kura itawekwa katika ofisi ya Afisa Mwandikishaji Msaidizi kwa muda wa siku saba, katika tarehe zitakazopangwa na Tume.  Lengo la zoezi hili ni kuwapatia fursa Wapiga Kura kukagua majina ya wote waliojiandikisha kuwa wapiga kura katika kata.

 

Wakati huo, mtu yeyote aliyejiandikisha kuwa mpiga kura katika jimbo au kata, anaweza kumwekea pingamizi mtu yeyote aliyejiandikisha kuwa mpiga kura kwa maandishi, kwa kutumia fomu maalum zitakazotolewa na Tume yenyewe.  Maafisa waandikishaji watatoa maamuzi ya pingamizi hizo kwa mujibu wa sheria.  Yeyote asiyeridhika na maamuzi hayo, anayo haki ya kukata rufaa mahakamani.

 

Iwapo yatahitajika marekebisho kutokana na maamuzi yanayotokana na pingamizi, marekebisho hayo yatafikishwa Tume kwa kutumia fomu maalum zilizoandaliwa na Tume kwa ajili ya kazi hiyo.  Baada ya kuzipokea fomu hizo, Tume itazifanyia “scanning” na kurekebisha (Daftari) Database.  Baada ya marekebisho hayo sasa Daftari litakuwa tayari.  Daftari la mwisho likichapishwa, Daftari la awali litakuwa limemaliza kazi yake na halitatumika tena.

 

Orodha ya mwisho ya wapiga kura itachapishwa na kutumwa kwa Wasimamizi wote wa uchaguzi.

 

 

10.       UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kukamilika, utakuwapo utaratibu utakaotumika kuboresha Daftari ambao unaandaliwa na Tume.  Uboreshaji huo utazingatia kanuni za msingi zifuatazo:-

 

(i)                 Kutangaza wakati na mahali pa kujiandikisha

(ii)               Kuongeza majina mapya katika daftari ya watakaokuwa wamefikia umri wa miaka 18 au kupata sifa za kuwa wapiga kura kwa mujibu wa sheria, n.k.

(iii)             Kuondoa wale waliokufa au watakaokosa sifa kwa mujibu wa sheria.

(iv)              Kurekebisha taarifa za Wapiga Kura zilizokosewa au za wanaoomba kufanya hivyo.

(v)                Kurekebisha kasoro zozote zitakazoonekana katika Daftari.

(vi)              Kurekebisha taarifa za wapiga kura watakaohama kutoka Kata/Jimbo kwenda Kata/Jimbo lingine

(vii)            Kutoa nafasi kwa walioandikishwa kukagua taarifa zilizopo katika Daftari au zinazokusudiwa kuboreshwa

(viii)          Kuwaruhusu wawakilishi wa vyama vya siasa kuangalia zoezi la uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura.

 

Uboreshaji huu utafanyika kila mara baada ya uchaguzi mkuu kufanyika.

 

11.       ELIMU YA MPIGA KURA

 

     Utaratibu wa kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga

     Kura ni mpya na wananchi hawajauzoea.  Tume inaandaa programu ya.

     kuwaelimisha wapiga kura na itatekelezwa kwa kushirikisha wadau

mbalimbali ili kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.  Kazi hii isiachiwe Tume  peke yake;  sisi viongozi tuliopo hapa ni wadau, kwa hiyo ni lazima tushiriki kikamilifu.   

 

12.       MWISHO

 

Wote tuliopo hapa leo tuliitwa ili tushiriki katika semina hii muhimu kwetu wengi wetu tukiwa karibu sana na wapiga Kura wanachama wa Chama cha Mapinduzi.  Ni jukumu letu kwenda kuwahamasisha kwa nguvu zetu zote wana CCM na wapenzi wa CCM kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kuwa wapiga kura katika tarehe zilizopangwa na Tume ya Uchaguzi ndani ya Kanda zetu.

 

Bila kujiandikisha yeyote anayestahiki kupiga kura, siku ya kupiga kura itapofika hatoruhusiwa kupiga kura.  Tukiwa wadau katika uchaguzi ni lazima tushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kujiandikisha kuwa wapiga Kura.

 

Ni matumaini ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba sote tutachukua nafasi zetu na kutekeleza wajibu katika kufanikisha zoezi la kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.   Zoezi hili likiimarika litasaidia sana kuendesha chaguzi za kuaminika, kukubalika  na za uhakika na hivyo kuimarisha zaidi demokrasia nchini mwetu!

 

13.       HITIMISHO:

                 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

 

Kuwepo kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutakuwa na faida zifuatazo:

 

(i)                 Daftari linapunguza gharama kubwa za kifedha za uandikishaji wapiga kura kila mara uchaguzi unapofanyika au kurudiwa.

(ii)               Daftari linaimarisha uwazi katika zoezi zima la uchaguzi.

(iii)             Daftari linaimarisha demokrasia nchini mwetu katika uchaguzi unaendeshwa ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

(iv)              Daftari linajenga heshima ndani na nje ya nchi yetu kwa kuendesha uchaguzi ulio huru na wa haki.

(v)                Daftari linawaondolea usumbufu wananchi kwa kutotumia muda mwingi katika kujiandikisha kila unapoitishwa uchaguzi na kuutumia muda huo kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.

(vi)              Daftari linahifadhi kumbukumbu muhimu za wananchi ambazo zinaweza kutumiwa kwa mambo mengine muhimu kama vile kutengeneza vitambulisho vya uraia.

(vii)            Daftari litazuia wapiga kura wanaopandikizwa kutoka sehemu nyingine.

(viii)          Daftari litazuia wapiga kura wanaonunua shahada za kupiga kura.

(ix)              Daftari litazuia watu kupiga kura zaidi ya moja.