MAJUMUISHO YA SEMINA YA WAJUMBE WA NEC, WENYEVITI NA MAKATIBU WA MIKOA ILIYOFANYIKA CHIMWAGA DODOMA TAREHE 24/08/2004

 

1.0         UTANGULIZI

 

1.1           Kwa kuzingatia kwamba, tumekabiliwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hapo mwezi Novemba 2004 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.  Chama Cha Mapinduzi kimeandaa Semina maalum iliyowajumuisha Viongozi wa Chama wa ngazi ya Taifa , Mikoa na Wilaya.

 

1.2           Semina hii ya siku moja ilifanyika katika Ukumbi wa Chimwaga, Mjini Dodoma.

 

2.0         MADHUMUNI YA SEMINA

 

2.1           Kimsingi lengo hasa la Semina hii ni kujenga uelewa mmoja juu ya kukabiliana na changamoto ya Chaguzi hizo na hasa kwa kuzingatia kuwapo kwa daftari la kudumu la wapiga kura ambalo hatujalizoea.

 

3.0         HOTUBA YA UFUNGUZI

 

3.1           Semina ilifunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa.

 

3.2           Akifungua Semina hii Mhe. Mkapa, alisisitiza juu ya umuhimu wa Viongozi wa CCM katika katika ngazi zote kuanza maandalizi na vuguvugu la Uchaguzi ili kuhakikisha kuwa CCM inaendelea kuungwa mkono na kushinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

 

 

 

4.0         RATIBA YA SEMINA

 

4.1           Kwa mujibu wa ratiba Semina ilijadili jumla ya mada kuu tatu, kama ifuatavyo:-

 

(i)                           Uchaguzi ndani ya Dola

 

(ii)                         Daftari la kudumu la wapiga kura

 

(iii)                       Taarifa ya Tume ya Dunia kuhusu Athari za Utandawazi

 

5.0         MAJUMUISHO

 

5.1           Semina inahimiza umuhimu wa Uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji uendeshwe kwa kuzingatia Sheria za nchi na Kanuni zinazotawala Chaguzi hizo, na dola inatakiwa kusimamia kikamilifu sheria hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Siasa za Matusi, Ukabila, Udini na Vitisho hazivumiliwi hata kidogo.

 

5.2           Kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni vizuri tukasimamia kukamilisha kwa ahadi za Chama chetu zilizotolewa katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuondoa kero mbali mbali zikiwemo zile zinazowakabili Viongozi wa ngazi za chini.

 

5.3           Kamati Kuu imeombwa kutafkari tena hali ya maslahi ya Viongozi na Watendaji ndani ya Chama chetu, na kuangalia linaloweza kufanyika kwa kuzingatia hali halisi ya fedha ndani ya Chama.  Lakini muhimu zaidi kila linalowezekana lifanyike ili kila Wilaya, na Mkoa kabla ya Uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais, iwe imepata gari na vitendea kazi vingine.

 

 

 

 

5.4           Viongozi, wakereketwa na Wanachama wanatakiwa kuanzia sasa kuanza kampeni za Chaguzi zinazofuata ili kuhakikisha kwamba Chama chetu kinapata Ushindi wa Kishindo.

 

5.5           Katika kampeni zijazo za ndani ya Chama chetu Viongozi wetu wanakumbushwa kuepuka kabisa kupakana matope na kwa vyo vyote vile tusijenge Mtu au Ubinafsi bali Chama na Maslahi ya Umma yawekwe mbele.

 

5.6           Viongozi na Watendaji ngazi zote za Chama lazima kuanzia sasa kujibu mapigo ya Upinzani papo kwa papo.  Huu ni wajibu wetu sote bila ya kusubiri ngazi za juu kujibu mapigo.  Kila Kiongozi, kila Mtendaji na kada wa CCM aone ni wajibu wake yeye kukisemea Chama chetu na wala isidhaniwe kuwa wapo wengine wanaowajibika isipokuwa yeye.

 

5.7           Katika kukijenga Chama chetu na uhalali wake lazima tutumie kwa nguvu kubwa zaidi vyombo vya habari, kamwe tusibweteke katika hili.

 

5.8           Semina pia imezingatia Umuhimu wa kuwepo kwa daftari la Wapiga kura na kuwataka Viongozi wote ndani ya Chama kuwahimiza Wanachama, wakereketwa na Wananchi wote kujiandikisha ili waweze kupiga kura.

 

5.9           Semina imeridhika sana na kiwango cha maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.  Aidha imewahimiza Viongozi wa Chama na Mamlaka zote zinazohusika kuhakikisha kuwa madaftari ya wakazi yanafikishwa na kutumiwa ipasavyo katika kila Kitongoji kwa mujibu wa sheria.

 

5.10      Wanasemina wameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na hatua za mwanzo za kuanzisha Daftari la kudumu la Wapiga kura.

5.11      Aidha kwa kuzingatia umuhimu wa vyombo vya habari katika kipindi cha Uchaguzi, Wanasemina wameshauri vyombo vya habari vya Chama viimarishwe na kupatiwa nyenzo za kutosha katika kuhimili vishindo vya ushindani katika medani ya siasa.

 

5.12      Wanasemina pia wamehimiza mshikamano kati ya Viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali katika ngazi zote uimarishwe zaidi ili kuleta mafanikio makubwa katika kuleta maendeleo ya nchi.

 

“UTANDAWAZI”

 

5.13      Semina pia imempongeza Mwenyekiti wa CCM Rais Benjamin William Mkapa kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Utandawazi.  Aidha Semina imempongeza yeye na Rais Tarja Halonen wa Finland kwa kutoa taarifa nzuri na ya kihistoria.

 

5.14      Wanasemina wamebaini kuwa kila enzi haikuachwa kukumbwa na dhoruba za utandawazi ambazo zimekuwa na faida na hasara zake.  Taifa letu lichukue nafasi hii na fursa adhimu ya kuimarisha sera zetu za uchumi na uwekezaji ili tufaidike na utandawazi katika enzi hii.

 

5.15      Wawekezaji siyo lazima watoke nje lazima Watanzania wahamasishwe pia wawezeshwe ili nao wawekeze katika nchi yao.

 

5.16      Kila jitihada ifanywe ili tuuze mazao mengi nje baada ya kuyasindika ili kutoa fursa za ajira kwa watu wetu na kuongeza ubora wa bidhaa zetu (Value added).

 

5.17      Semina imeridhishwa sana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Benjamin William Mkapa, katika jitihada zake za kuelimisha umma wa Watanzania, bara lote la Afrika na dunia kwa ujumla juu ya athari na faida za utandawazi.

5.18      Ili kukabiliana na changamoto za utandawazi, wanasemina wanaishauri Serikali na wananchi kwa ujumla kuzingatia masuala muhimu yafuatayo:-

 

(a)    Kujenga tabia ya utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii na kwa nidhamu.

 

(b)            Kuimarisha na kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuzingatia kuwa katika nchi yetu kilimo ndiyo sekta kiongozi na msingi wa uchumi wetu.

 

(c)             Kuimarisha na kutilia mkazo elimu, elimu ya ufundi na teknolojia.

 

(d)            Kujenga na kuimarisha miundo mbinu na njia za mawasiliano.

 

(e)            Kuendeleza sekta ya kilimo na mifugo kwa lengo la kutumia kikamilifu fursa ya soko la AGOA na Mashariki ya Kati.

 

5.19      Serikali inashauriwa kuhimiza uanzishwaji wa kilimo na biashara “Commercial farming” ili nchi yetu iweze kujitosheleza kwa chakula na iweze kuuza nje.