Umahiri wa CCM na Sera ya Ajira

 

Katika mchakato wa uchanguzi wa mwaka 2005, kuna ukweli usiopingika kwamba katika  vyama vyote, Chama cha mapinduzi (CCM) kimeonesha umahiri mkubwa katika kunadi ilani inayotoa majibu sahihi ya kuwawezesha watanzania kusimamia uchumi kwa kuwa na ajira za uhakika .

 

Kwa kupima matamshi ya mgombea urais wa chama hicho, ni wazi kabisa kuwa mazingira ya ajira zaidi ya milioni moja zitakuwa wazi na zitafikiwa na kila mtanzania ambaye anao utayari wa kufanya kazi.

 

Katika hilo hakuna shaka yoyote kwani maandalizi na mazingira ya ajira hizo kwa watanzania wa jinsi zote, na wa rika mbalimbali yameshawekwa tayari, kinachotakiwa ni watanzania kukiweka chama hicho madarakani ili kiweze kutimiza ahadi zake, na hasa kutekeleza yale yaliyoko katika ilani ya uchaguzi ya  chama hicho.Yote yatawezekana pale watanzania wote watakapoamua kutoa kura zao za ndiyo kwa wagombea wa kiti cha  uraisi wa Jamhuri ya muungano, urais wa Zanzibar, wabunge , wawakilishi na madiwani.

 

Kwa wale ambao hawakumbuki ama hawajawahi kusikia, Serikali ya Tanu na ASP tangu uhuru  na baadaye CCM, zilikuwa na sera ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anatakiwa kuwa na maisha bora.Huu ni ukweli usiopingika. Kama mtakumbuka fika kwamba , baada ya upembuzi yakinifu uliofanywa na waasisi wa vyama vya TANU na ASP,hasa baada ya nchi yetu kupata uhuru,  Katika mwaka 1967 Serikali ilichukua hatua ya makusudi yenye lengo la  kuondoa tofauti katika  umilikaji wa njia kuu za uchumi  na kudhamiria kuondoa matabaka ya watu ili kuhakikisha kuwa njia kuu za uchumi zina bakia mikononi mwa wazalendo  na msimamizi mkuu ikiwa ni serikali.

 

Hatua hii ya kijasiri na ya kihistoria ya kutoa ajira kwa wazalendo inakumbukwa na wengi hasa pale serikali ilipoamua kutaifisha mabenki, mashamba, viwanda, na taasisi mbalimbali zitoazo huduma na pia kuunda mashirika na makampuni mbali mbali ili kuwamilikisha wananchi uchumi wao na kutoa ajira ya uhakika kupitia sera yake Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

 

Bado watanzania walio wengi wanazo kumbukumbu vichwani mwao kuhusu mwitikio wa hatua hiyo.Kila kitu kiliwezekana,ukilinganisha na uchanga wa nchi hii na mapungufu yaliyokuwa yameachwa na watawala wa kikoloni. Lakini kuwezekana huko kulichangiwa zaidi na uimara wa uongozi makini  wa waliokuwa madarakani kwa kuungwa mkono na watanzania wazalendo wa nchi hii. Ngonjera mashairi na sanaa nyinginezo zilizochangia kueleza malengo makuu na madhumuni ya Azimio la Arusha kwa kupitia vyombo vya upashanaji wa habari kama vile redio na magazeti katika miaka hiyo ya 1967 na kuendelea na hata wale waliokuwa mashuleni mtakumbuka nyimbo zilizoimbwa katika mchakamchaka, sherehe mbalimbali za kitaifa na hata katika mikusanyiko mingineyo.

 

 

Lengo la serikali katika kipindi hicho ilikuwa ni kuufanya uchumi wa Tanzania umilikiwe na watanzania kupitia dola na kuhakikisha kuwa ajira ya kwa wazalendo waliokuwa na sifa na elimu ya kuweza kushika madaraka na vyeo vilivyokuwa vimeachwa wazi na wakoloni , na serikali iliwawezesha kufanya hivyo, wakati huo huo  kundi lingine la wazalenzo wakiendelea kuchapa kazi ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara .

 

Lakini katika miaka ya mwishoni na mwa mwaka themanini na mwanzoni mwa  tisini kutokana na mabadiliko ya uchumi duniani sera ya ujamaa na kujitegemea haijabadilika ila badala ya uzalishaji mali, usafirisha wa bidhaa nk. kuendeshwa na dola, kwa sasa uzalishaji mali, na huduma mbalimbali za umma zinamilikiwa na wananchi kupitia ushirika, makampuni( kwa mtindo wa kumiliki hisa) ,na vikundi mbalimbali vya wananchi vya uzalishaji mali na utoaji huduma.Lengo ni kuwa uchumi umilikiwe na wananchi na serikali kukusanya kodi kuelekeza nguvu zake Katika huduma za kijamii.

 

Katika mikakati mbalimbali ya CCM ni kuona kwamba wananchi wa Tanzania wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yao. Sera ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi imebuniwa kama njia ya uhakika ya kuwapa Watanzania uwezo na fursa ya kulifikia lengo hilo la kumiliki na kuendesha uchumi wa nchi. Aidha, Sera hii ina lengo la kuona kwamba Watanzania kwa mamilioni wanashiriki kwa ukamilifu katika harakati za kukuza uchumi wetu na kuondoa umaskini Kupitia Mkakati wa Kuinua Uchumi na Kuondoa Umasikini (MKUKUTA). Wakati huo huo, utekelezaji wa dhati wa sera hii ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi itatuepusha na balaa la kuwa na jamii ambayo ina matajiri wachache walionacho na wananchi walio wengi wasio nacho.

 

Ili utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ifanikiwe, CCM inaamini na inawashirikisha wananchi katika mambo makuu yanayolenga kuleta  mafanikio ya Tanzania kwa ajili ya watanzania wote wa mijini na vijijini.Kwa njia ya ushirikishwaji huu Chama Cha Mapinduzi katika mwelekeo huu kinatoa wito kwa Watanzania kudhamiria yafuatayo:

 

 Kwanza kukubali kuwa kujitegemea kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ndio msingi wa maendeleo na kutokomeza umaskini. Kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi ana wajibu wa kujiwezesha kwa kuishi kwa jasho lake, yaani kwa kufanya kazi. Mtaji wa maskini ni nguvu (na akili) zake mwenyewe. Uwezeshaji kutoka katika vyanzo vingine vya misaada ni njia ya kumuunga mkono yule aliyekwishaonesha azma ya kuanza kujikomboa mwenyewe..

 

Watanzania walio wengi wanayonafasi ya  kuendeleza vipaji vyao au kuwa na mali au nyenzo za kuzitumia katika kujiendeleza kimaisha. Katika miaka mitano ya Ilani hii CCM itazielekeza Serikali kuweka mipango ya kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kujiendeleza kimaisha..

 

CCM inapata faraja kuu kwa kuona kwamba tayari wananchi wamekwishaanza kuchukua hatua za maksudi katika kujikwamua na suala hili la kila mwenye uwezo wa kubuni kazi na kufanya kazi anafanya hivyo bila hofu yoyote .serikali ya CCM inahakikisha kuwa amani inapatikana kwa mwenye kudhanilia kufanya kazi afanye kazi. Mifano ni mingi lakini kwa uchache kila mtu anashuhudia namna vijana wanavyotumia vipaji vyao katika kujiajiri kwa njia ya vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali katika kilimo, mawasiliano ya simu, biashara ndogo ndogo na hata katika nyanja ya burudani mbalimbali.

 

Inaeleweka pia kuwa watu wetu wengi wanao uwezo wa kujitegemea na kujiendeleza kiuchumi japo kuwa wana elimu ndogo au maarifa na ujuzi mdogo.Serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi inaendelea kutoa Elimu ya kawaida na mafunzo ya ufundi stadi na maarifa ya kazi ni uwezeshaji wa msingi sana kwa binadamu. Serikali zitaimarisha mipango ya elimu ya watu wazima yenye manufaa pamoja na mafunzo ya fani mbalimbali za stadi za kazi mijini na vijijini. Mafunzo haya yatahusu kilimo, biashara, ufugaji, utunzaji wa vitabu, n.k. Serikali zitaongoza shughuli hizi za kutoa elimu na maarifa ya kazi kwa wananchi zikishirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali.

 

CCM inaamini kuwa Ushirika ndio njia kuu ya uwezeshaji kwa wananchi walio wengi. Ushirika ni njia ya kukusanya nguvu. Ushirika uko wa aina nyingi. Lakini ushirika wa kuweka na kukopa una umuhimu wa kimkakati katika harakati za kukuza uchumi na kutokomeza umaskini kwa sababu unawawezesha wanachama wa ushirika huo kuwa na chombo chao cha kuwapatia mikopo (mitaji) kwa uhakika na kwa masharti nafuu. Aina nyingine za ushirika ni pamoja na ushirika wa wakulima wa mazao na mifugo, ushirika wa biashara, ushirika wa huduma kama migahawa, ushirika wa wavuvi, ushirika wa wachimba madini, ushirika wa ujenzi, n.k. Kwa vile ushirika ndiyo njia kuu ya uwezeshaji wa wananchi, CCM itazisisitizia Serikali juu ya umuhimu wa kuandaa maafisa wa ushirika waadilifu, wataalamu na wenye uzalendo.

 

Ili kuwakomboa watanzania, Serikali ya CCM inaendelea na  utaratibu wa kuzipa uhai wa kisheria ardhi na nyumba ambazo hadi sasa hazikutambuliwa kisheria. Kwa utaratibu huu wenye ardhi na nyumba hizi wanaweza kupata mikopo kwa kuweka ardhi na nyumba hizo dhamana.Utaratibu huu unaitwa MKURABITA, yaani Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania. Lengo lake ni kuwafanya wananchi waliokuwa hawakopesheki sasa wakopesheke na hivyo kuingia katika mchakato wa uchumi hai.

 

Wananchi wengi wana uwezo, maarifa na dhamira ya kujitegemea kiuchumi. Mipango mizuri ya mikopo ya masharti nafuu inaweza kuwafanya wengi wao wakajiajiri na hivyo kuboresha maisha yao na kutoa mchango katika uchumi wa taifa. Shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji madini, biashara, n.k. zinaweza kushamiri iwapo utakuwapo utaratibu madhubuti wa mikopo yenye masharti nafuu. Upatikanaji wa mitaji kwa njia ya mikopo ni kikwazo kikubwa kwa watu wengi. Serikali za CCM ziwajibike katika kuweka mfumo muafaka wa mikopo kwa wananchi.

 

Kuna fani za shughuli za kiuchumi ambazo Watanzania hatuna uzoefu nazo. Fani mojawapo ni ya ujasiriamali. CCM itazishauri Serikali kuwa na mipango ya kuwapa fursa wajasiriamali Watanzania wanaoinukia kupata uzoefu wa wajasiriamali wa nchi nyingine za Kusini. Aidha, katika madarasa ya ujasiriamali na biashara, mifano halisi ya mafanikio katika nchi nyingine itatolewa kama mifano Kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa na kuwatanabahisha kuwa mifugo ni mali; waitumie ili kuboresha hali ya maisha yao.

 

CCM inaendelea kuwa karibu na wananchi wote katika kusikiliza na  kupokea kilio cha ajira cha wananchi, hasa vijana. CCM imelipa na itaendelea kutoa kipaumbele  suala la ajira kwa kuzingatia  umuhimu mkubwa wa wananchi na hasa vijana kuwa na uhakika wa kupata ajira na kufanya kazi  katika kipindi cha miaka mingi ambayo CCM itakuwa madarakani kwa maana ya mwaka2005-2010.

 

Lengo la CCM ni kuhakikisha  kwamba ajira mpya zaidi ya milioni moja zinapatikana katika miaka mitano ijayo. Ajira ziko za aina mbili: Ajira katika maana ya kazi ya kulipwa mshahara katika sekta ya umma (Serikali na vyombo vyake) na katika sekta binafsi (iliyo rasmi na isiyo rasmi). Ajira katika maana ya kujiajiri binafsi  katika kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, kuchimba madini, udereva, ufundi, ualimu, uhasibu, kuendesha mgahawa, ushonaji, uandishi, uanasheria, uhandisi, ukandarasi n.k.

 

Nafasi za mpya ajira katika sekta ya umma zitakuwa nyingi kwenye sekta ya ualimu kutokana na upanuzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu unaoendelea. Sekta ya afya pia itatoa ajira mpya nyingi kwa upande wa waganga na wauguzi kwa vile sekta hii lazima ipanuke kukidhi mahitaji ya wananchi. Sekta ya ujenzi vile vile ina nafasi ya kutoa ajira mpya nyingi.

 

Serikali za CCM  itaendela kuhimiza na kuvutia wawekezaji katika viwanda, migodi, kilimo, n.k. ili nafasi za ajira ziendelee kuongezeka. Mkakati mpya wa Serikali wa kuanzisha maeneo maalum ya uchumi (SEZs) umekusudiwa kuibua nafasi nyingi mpya za ajira. Eneo la kujiajiri ndilo lenye nafasi tele za ajira katika nchi yetu. Katika kipindi cha Ilani hii, CCM itazihimiza Serikali zielekeze nguvu zake kwenye kuwawezesha wananchi, hasa vijana na wanawake, kwenye shughuli za kujiajiri vijijini na mijini. CCM inatoa wito kwa wananchi wajitokeze kuitikia wito wa kujiajiri na pia wakubali kutobagua kazi maana wahenga wamesema mchagua jembe si mkulima.

 

 

CCM itaendeleza jitihada zakena Serikali kuona kwamba mipango ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inaandaliwa kwenye kila Wilaya. Kila Wilaya ina rasilimali za kutosha, mradi tu watu wanaamua kuibua maendeleo yao. Mchango wa fedha (kwa ajili ya mikopo) kutoka Serikali Kuu na wa taasisi zisizo za Kiserikali inakusudiwa upelekwe Wilayani huko huko.Serikali zitatakiwa kuzielekeza Ofisi za Halmashauri za Manispaa, Miji na Wilaya na Ofisi za CCM za Wilaya (Idara ya Uchumi na Fedha) zijijengee uwezo wa kuwashauri wananchi wanaoomba mikopo kuhusu maandalizi ya michanganuo ya miradi inayokubalika.

 

CCM inaamini kuwa pamoja na suala la kukaribisha wawekezaji nchini ili kukuza uchumi na kuongeza ajira, itautumia uwezo mkubwa wa fedha uliopo katika mashirika ya hifadhi za jamii (pensheni) yaani NSSF, PPF, LAPF na Mfuko wa Pensheni ya Serikali. Tayari NSSF na PPF wameweza kuwekeza katika miradi ya nyumba (k.m. NSSF wamejenga mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mabibo) na kusaidia kutatua matatizo makubwa ya kijamii.

 

CCM kwa kushirikiana na wawekezaji inahakikisha kwamba Serikali inafanya mashauriano ya msingi na uongozi wa mifuko hii ili kupata njia muafaka za kuifanya mifuko hii ishiriki katika uwekezaji na hivyo kuliongezea nguvu taifa ya kukuza uchumi wake kwa kasi zaidi. Utaratibu wa kuitumia mifuko ya hifadhi ya jamii kuchangia katika ukuzaji wa uchumi wa nchi unatumika sana katika nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza. Kwa maelezo haya mafupi, tumewapa mwanga juu ya  dhamira ya CCM kuweka mazingiza bora ya ajira -Tanzania.

 

Abiyani Nguvu Ya Hoja

Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam