ASASI ZISIZO ZA KISERIKALI- ZIWE WADAU NA SIYO KIKWAZO

KATIKA MAENDELEO

 

Nadharia ya asasi zisizo za kiserikali inazidi kupata msukumo  na mtizamo mpya kwa siku za hivi karibuni katika ngazi ya dunia na nchi moja moja. Mtizamo na msukumo juu ya asasi zisizo za kiserikali unakwenda sambamba na ongezeko la kasi la idadi ya asasi zenyewe.

 

Kumekuwepo na sababu mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zimechangia wimbi la ongezeko la asasi hizi na chache kati ya sababu hizo ni hizi zifuatazo:- Kwanza ni mabadiliko ya kinadharia na sera katika siasa na uchumi duniani mwanzoni mwa miaka ya sabini kutoka sera zilizotilia mkazo nguvu ya dola katika uchumi na maendeleo na badala yake sera zinazotoa nafasi kubwa kwa sekta binafsi ziliibuka. Sababu ya pili iliyochangia ongezeko la kasi la asasi zisizo za kiserikali ni wimbi la demokrasia ya vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya 1990.

 

Hapa Tanzania asasi zisizo na kiserikali pamoja na vyama vya kiraia idadi yake inazidi kuongezeka. Kwa mujibu wa ripoti ya tume ya Afrika iliyoundwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Bwana Tony Blair ambayo Rais Benjamini Mkapa alikuwa mmoja wa Makamishna wake Tanzania inakadiriwa kuwa na vyama vya kiraia zaidi ya 9000 mpaka kufikia mwaka 1999, ukilinganisha ni 168 tu mwanzoni mwa miaka ya 1990. Ongezeko la idadi ya asasi hizi ni tafsiri iliyo wazi ya utashi wa kisiasa uliopo kwa asasi hizi kutoka katika serikali zote mbili za Chama cha Mapinduzi (CCM).

 

Kimsingi asasi zisizo za kiserikali umuhimu wake unakubalika kwa watu wengi wa kada mbalimbali. Hata hivyo yapo maswali kadhaa tunayopaswa kujiuliza juu ya asasi hizi. Kwa mfano, asasi hizi zinawajibika kwa nani na kwa wakati gani? Ni masilahi ya nani yanapewa kipaombele na asasi hizi katika utekelezaji wa majukumu yake kati ya wafadhiri na wananchi? Je kuwepo kwa asasi zisizo za kiserikali na vyama vingine vya kiraia ni jawabu kamili la matatizo yetu kama jamii? Maswali haya na mengine yatasaidia katika kuibua hoja zitakazoboresha utendaji kazi kati dola na vyama vya kiraia.

 

Kinadharia ni wajibu wa asasi zisizo za kiserikali na vyama vya kiraia kuikumbusha  serikali juu ya wajibu wake kwa wananchi. Katika  kufanya hivyo asasi hizo zinapaswa kuzingatia kanuni, sheria na tararibu za nchi zilizowekwa kwa mujibu wa katiba na si kinyume chake. Ikumbukwe kwamba katika  utawala wa kisheria hakuna mtu au kikundi cha watu au taasisi iliyo juu ya sheria. Katika maisha ya wanajamii waliostaarabika haki na wajibu huenda kwa pamoja. Kwa  maneno mengine, asasi zisizo za kiserikali zinapaswa kwanza kutafsiri kwa vitendo yale wanayohubiri ndani ya asasi zenyewe kabla ya kuinyooshea kidole dola.

 

Hivi karibuni baadhi ya asasi zisizo za kiserkali zimeonekana waziwazi kutoposha kwa makusudi na kubeza mafanikio ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi katika kuwaletea maendeleo wananchi wake hasa katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Rais Benjamin William Mkapa. Inaeleweka wazi kwamba idadi ya wanafunzi wa shule za msingi imeongezeka kutoka milioni tatu na nusu mwaka 1995 na kufikia zaidi ya milioni saba na nusu mwaka 2005, ukuaji wa uchumi umeongezeka kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 3.6 mwaka 1995, mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 27 mwaka 1995 hadi  asilimia 4.5 mwaka 2005, makusanyo na mapato ya serikali yameongezeka kutoka bilioni 25 kwa mwezi mwaka 1995 hadi kufikia zaidi ya bilioni 150 mwaka huu.

 

Rekodi hizi za mafanikiao ya utekelezaji wa sera makini za Chama Cha Mapinduzi si tu zinapaswa kupongezwa na wananchi ambao bado wana imani kubwa na serikali yao lakini pia na asasi zisizo za kiserikali ambao pia na wadau muhimu katika maendeleo endelevu ya nchi yetu. Hatusemi kwamba serikali za Chama Cha Mapinduzi zimetekeleza yote kwa asilimia mia moja, la hasha. Bali tunachosisistiza ni kwamba rekodi hii ya utekelezaji wa sera za Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo chini ya uongozi shupavu wa Rais Mkapa hauwezi kubezwa na mtu yeyote wala asasi yoyote ile.

 

Katika mtizamo ule ule unaolenga kuboresha maisha ya watanzania, serikali makini ya Chama Cha Mapinduzi imebuni mikakati mbalimbali katika kuhakikisha kwamba yale ambayo hayakutekelezwa na serikali ya awamu ya tatu yanatekelezwa na serikali ya awamu ya nne kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Mpango  wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Tanzania (MKUKUTA), Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) na Mpango wa Kuondoa Umaskini Zanzibar (MKUZA) ni ishara ya wazi ya utashi wa kisiasa uliomo ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika kuinua maisha ya watanzania. Katika hili pia tunasema asasi zisizo za kiserikali na vyama vingine vya kiraia vinapaswa kuliona na kuiunga mkono serikali katika juhudi zake na si kubeza na kupotosha juhudi hizo kama ilivyojitokeza kwa baadhi ya asasi hizo hivi karibuni.

 

Upotoshaji wa makusudi wa mafanikio ya serikali ya Chama Cha mapinduzi unapofanywa na mtu au kikundi cha watu au taasisi yoyote ile unaacha maswali mengi bila majibu. Lakini swali kubwa zaidi linaloibuka ni je upotoshaji huu unafanya kwa faida ya nani? Jibu sahihi la swali hili wanalo wapotoshaji wenyewe. Tunahisi kwamba upotoshaji huu unalenga kuikatisha tamaa serikali lakini pia kuigombanisha serikali na watu wake jambo ambalo tunaamini kwamba halitawezekana kwa sababu watanzania bado wana imani na Chama Cha Mapinduzi na serikali zake shupavu.

 

Tunapenda kuzikumbusha asasi zisizo za kiserikali pamoja na vyama vyote vya kiraia kwamba hazikuanzishwa ili ziwe pinzani kwa serikali au ziwe za mbadala wa dola kwa wananchi. Kwa mantiki hii asasi hizi zinapaswa kuonyesha wajibu wao kwa umma wa watanzania kwa kudumisha mshikamano miongoni mwao na hivyo kuwaunganisha wananchi na kuwaleta karibu zaidi na serikali yao. Hili likifanyika kwa moyo wa dhati kabisa ni wazi kwmaba asasi zisio za kiserikali zitakuwa ni mhimili mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu.

 

Kinadharia asasi zisizo za kiserikali zinapaswa kuendeshwa kwa uwazi na ukweli hii ikiwa ni pamoja na kuweka wazi mapato na matumizi ya pesa wanazopata toka kwa wafadhili wawe wa ndani au wa nje. Lakini pia mikataba ambayo asasi hizi inaingia na washirika wao mbalimbali inapaswa kuwa wazi ili wananchi wajue ukweli na undani wa mikataba hii. Kama tulivyokwisha kusema  hapo awali, Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya vyama vya kiraia na asasi zisizo za kiserikali zipatazo 9000. Tunaamini kwamba kwa idadi kubwa kama hii ya asasi zikiachwa kuendesha mambo yake bila utaratibu itakuwa ni hatari kubwa kwa usalama wa nchi yetu. Ni katika msinig huu tunazidi kusisitiza kwamba asasi hizi ni lazima ziwe ni mfano bora kwa kuheshimu taratibu, kanuni na sheria za nchi ili dhana ya utawala wa kisheria iweze kutamalaki.

 

Hivi karibuni hapa nchini kumekua na mazoea kwa baadhi ya asasi zisizo za kiserikali kujikita katika kutoa sura mbaya tu ya utekelezaji wa sera za Chama Cha Mapinduzi kana kwamba hakuna mazuri yaliyofanywa na serikali. Hili limefanyika kwa nguvu zote ikiwa ni pamoja  na kubuni matangazo mbalimbali yanayoonekana katika vyombo mbalimbali vya habari. Sekta ya elimu kwa mfano imekuwa ni mhanga mkubwa katika kubeza mafanikio yake. Hatuna uhakika na nia ya dhati ya asasi kama hizi lakini jambo moja ni dhahiri kuwa kwa kufanya hivyo wanavutia ufadhiri hasa kutoka nje.

 

Katika jamii ya watu waliostaarabika kuwa tayari kukosolewa ni jambo la kawaida. Lakini kukosoa tu bila kutoa njia mbadala nako hakuna maana sana. Tunahisi  kwamba ni wajibu wa mkosoaji kueleza bayana nini kifanyike ili kuboresha kile ambacho anaona ni tatizo. Kwa kushindwa kueleza njia mbadala, tafsiri yake ni kwamba weww ni sehemu ya huo uozo unaodai kuona. Kwa mfano kama unazungumzia kushuka kwa ubora wa elimu au mfumo mbovu wa utoaji elimu bila kugusia juu ya nini kifanyike kuboresha elimu yetu maana yake ni kwamba mfumo huo mbovu wa elimu wewe ni tunda lake ndiyo maana umeshidwa kujenga hoja ya kuboresha kero hiyo.

 

Lakini sisi tunaamini elimu yetu kwa mfano haijashuka na wala si mbovu kama jinsi ambavyo baadhi ya watu wanataka tuamini. Katika hili mifano iko mingi tu. Hivi sasa kuna wataalamu wengi sana kutoka Tanzania wanaofanya kazi ndani ya nchi na nje ya nchi hasa katika nchi za kusini mwa Afrika. Sisi tunajiuiza na tunapenda kuwauliza wakosoaji kwamba hivi kama elimu yetu ingekuwa duni wataalamu hawa ambao tunaamini ni kielelezo cha ubora wa elimu yetu tungewapata wapi?

 

Tunapenda kuhitimisha kwa kutoa wito kwa asasi zisizo za kiserikali kushirikiana  zaidi na serikali yetu katika harakati za kuwaletea watanzania maisha bora badala ya kuonekana kikwazo kwa maendeleo ya nchi. Na hili linawezekana ili mradi kila upande utimize wajibu wake.

Nguvu ya Hoja,

Abiyani Chuo Kikuu.