CHAGUA CCM, CHAGUA KIKWETE CHAGUA MAENDELEO YA WANAWAKE TANZANIA

 

Wanawake ni watu wenye mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania. Wanawake ni wazazi na walezi msingi wa vizazi vyote. Katika Tanzania, wanawake watakumbukwa kwa ushiriki wao katika harakati za kutafuta uhuru. Aidha, wamekuwa mstari wa mbele katika harakati za kuinua uchumi na mageuzi ya kisiasa. Sauti za wanawake ziko juu sana katika kuleta mabadiliko ya kijamii, hususan kupambana na mila na desturi potofu mathalani ukeketaji; ambazo zimekuwa zikileta athari kubwa kwa ustawi wa wanawake wenyewe na jamii kwa ujumla.wa kutambuliwa na kuthaminiwa na usiopimika kwa maendeleo ya taifa.

 

Ni wanawake wa Tanzania ambao wamekuwa wapiga kura waaminifu, na hivyo kuipa CCM ushindi wa kishindo katika chaguzi zote zilizopita tangu nchi yetu ipate uhuru. Ni katika kuwatambua, kuwaheshimu, kuwathamini wanawake hawa, CCM katika Ilani yake ya Uchaguzi imetoa kipaumbele kwa masuala yatakayowaletea wanawake na jamii maendeleo endelevu. CCM inatambua kwamba, wanawake wakiwezeshwa kisiasa, kiuchumi, kielimu na kijamii, taifa zima litakuwa limeinuliwa, hatimaye, kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania.

 

Hata hivyo, ni muhimu kwa wanawake wote kuzingatia kwamba, waipe CCM kura zote za ndio, ili wanawake waweze kunufaika na Sera nzuri za CCM na zinazojali maslahi ya watu wote pasipo ubaguzi katika msingi wowote kama jinsia, dini, rangi, elimu, na mikoa. Wanawake watambue kuwa hawatapoteza kura zao kwa kuamua kuchagua CCM. Kura zao zitakuwa ni mtaji ambao watakuwa wamewekeza katika kisima cha maendeleo kinachopata uhimili wa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya kuelekea katika Tanzania yenye neema tele.

 

Tunasema hivi, kwani CCM ni Chama ambacho kimefanya mengi sana kwa maendeleo ya wanawake ambayo wanawake na jamii wanajivunia. Mifano iko mingi sana. Kisiasa, CCM imezingatia na kuinua ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi. Idadi ya wanawake Bungeni imeongezeka kutoka wanawake 8 sawasawa na asilimia 10, katika kipindi cha 1961 hadi 1965, na idadi ya wanawake kufikia zaidi ya asilimia 20 Julai 2005. Ongezeko kama hili limekuwa pia katika ushiriki wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi mashina, matawi, kata, tarafa, wilaya, mikoa hadi taifa. Idadi ya wanawake imeongezeka pia katika nyanja mbalimbali za utumishi na ajira serikalini na sekta binafsi. Wanawake wengi sana wamepata mwamko mkubwa wa kujihusisha kwenye ajira binafsi isiyo rasmi. Kielimu wanawake wamepewa kipaumbele. Kumekuwa na ufadhili maalum kwa mfano Carnegie mahususi kuinua kiwango cha sifa za msingi za kujiunga na Chuo Kikuu Dar es Salaam. Ipo mifuko mingine mingi, inayotoa ufadhili kwa wanawake ili kuwawezesha kupata elimu katika vyuo mbalimbali vya elimu ya Juu hapa nchini, na hata nje ya nchi.

 

Wanawake na wananchi wote kwa ujumla wanakubaliana na ukweli usiofichika kwamba, mweleko unaonesha wazi kuwa Ndugu yetu Jakaya Kikwete atashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa 2005. Kwa maneno mengine, wanawake wanachohitaji kufikiria, ni kwa namna gani watashirikiana na Kikwete ili kufanikisha azma ya CCM na ahadi nzuri za ndugu Kikwete za kuwatumikia wanawake wa Tanzania ili wawe na maisha bora. Wanawake andaeni mbinu na mkakati wa kutekeleza kwa vitendo mema yote ambayo CCM imekusudia kuwafanyia, kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya.

 

Wanawake watambue kuwa ndugu Kikwete hajifunzi kuongoza. Anao uzoefu wa muda mrefu alioupata kwa muda mrefu akiwa Waziri katika wizara mbalimbali. Kimuundo na kiutendaji, Waziri ni mwakilishi wa Rais katika wizara husika. Zaidi, ndugu Kikwete anao uzoefu wa ujenzi wa Amani na Utulivu. Ameshiriki kwa ari na uwezo mkubwa katika harakati za kuleta amani kwa njia ya mazungumzo, katika nchi za Maziwa Makuu. Wanawake wanatambua kwamba uvunjifu wowote wa Amani na Utulivu, huathiri wanawake na watoto zaidi. Tunaye Kikwete, Nyota ya Amani, wanawake mpeni kura zote za ndio.

 

Kwa upande wa elimu CCM, itahakikisha kuwa inatoa elimu ya awali na msingi kwa wasichana wote na na watu wa jinsia zote, shule za sekondari kwa kila kata, itaimarisha ubora wa vifaa,majengo na walimu, itaimarisha elimu ya kujiendeleza kwa wanawake na elimu ya watu wazima, itaimarisha elimu ya UKIMWI na magojwa mengine na kuhamasisha wanafunzi wa kike kuchukua masomo ya sayansi ili kuhakikisha kuwa wanawake wanashika madaraka katika nyanja za juu na kushiriki katika maamuzi ya kitaifa.

 

Katika sekta ya afya CCM kupitia ilani yake ya 2005/2010 itahakikisha kuwa kuna huduma bora ya afya ya msingi kwa wanawake na watoto wote, kupunguza vifo vya watoto wachanga na watoto chini ya umri wa miaka mitano,kuinua kiwango cha muda wa kuishi kwa wanawake, kuboresha huduma za kiliniki kwa kina mama na watoto kuwa bora na karibu na wananchi, kutoa huduma bure kwa wanawake wasiojiweza na kuimarisha vita dhidi ya UKIMWI.

 

Pia kwenye sekta ya kilimo katika Ilani yake CCM itahakikisha kuwa kilimo cha kisasa ndio msingi wa uchumi wa kisasa, itatoa elimu kwa wanawake juu ya matumizi bora ya ardhi, kushawishi na kueneza kwa wanawake elimu ya utengenezaji na upatikanaji wa mikokoteni ya kuvutwa na wanyama na vinu vya kisasa vya kukobolea na kusagia nafaka. Aidha CCM itahakikisha upatikanaji wa mbegu bora mbolea na pembejeo kwa wanawake, kutoa elimu kwa wanawake kuhusu uvunaji wa maji ya mvua,kuchimba mabwawa na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji. CCM itazingatia kuundwa na kuendeleza mifuko ya mikopo kwa ajili ya wanawake wakulima wadogo wadogo vijijini, na utoaji wa elimu kwa wanawake ya usindikiji na ufungashaji wa mazao ili kuvutia soko na kupunguza uharibikaji wa mazao.

 

CCM itaratibu kuboresha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao, kutoa elimu kwa wanawake juu ya njia rahisi ya kuhifadhi mazao, kushawishi wanawake, kuanzisha na kukuza kilimo cha maua,matunda,mboga na mazao ya viungo vya chakula. CCM itahakikisha upatikanaji wa elimu kwa wanawake juu ya matumizi bora ya mazao ya kilimo ili kuinua lishe na kujenga afya ya familia na jamii. CCM pia itaendeleza kilimo na kukifanya kiwe cha kisasa ili kuweza kutoa ajira kwa wanawake na vijana na kutoa vivutio, zawadi na tuzo kwa wakulima wanawake watakaoongeza maradufu kiasi cha mazao yanaovunwa kwa eka.

 

Katika nyanja ya ufugaji na uvuvi,CCM itafanya yafuatayo; kuboresha mazingira ya ufugaji na uvuvi ili kuinua kiwango cha ushiriki wa wanawake na vijana, kutoa elimu kwa wanawake itakayosaidia kuinua kiwango cha mazao yatokanao na ufugaji na uvuvi, kutoa elimu kwa wanawake juu ya usindikaji na ufungishaji wa mazao yatokano na uvuvi na ufugaji ili kuvutia soko na kuzuia kuharibika kwa mazao hayo. Aidha CCM itaendeleza ufugaji na uvuvu na kuufanya uwe wa kisasa ili kuweza kutoa ajira kwa wanawake na vijana, pia kuhamasisha wanawake wafugaji na wavuvi kuanzisha na kujiunga na SACCOS na kutumia kuwapatia mikopo.

 

Maji pia ni kati ya mambo yaliyopewa kipaumbele kwenye ilani ya CCM 2005/2010. Chamacha Mapinduzi kitahakikisha kuwa kinawawezesha wanawake wa mijini na vijijini kupata maji safi, salama yakutosha na yaliyokaribu na sehemu wanzoishi. CCM itaendeleza ujenzi wa malambo na mabwawa, pia kuunda na kuendeleza ushiriki wa wanawake katika kamati ya maji na mifuko ya maji ya wananchi. CCM itaratibu utoaji elimu kwa wanawake juu ya njia nyepesi na rahisi ya kukinga na kuhifadhi maji ya  mvua, na elimu kwa wanawake juu ya kuvitambua, kuvithamini na kuvutunza vyanzo vya maji.

 

Katika miradi midogomidogo CCM itatoa elimu na kuinua kiwango cha ushiriki kwa wanawake na vijana katika kuanzisha na kuendeleza miradi midogo midogo. CCM itatoa elimu kwa wanawake juu ya ubora wa bdhaa ili kuvutia masoko ya ndani na ya nje ya nchi, na elimu kwa wanawake juu ya utunzaji wa mahesabu na kujenga ubunifu utakaosaidia kuendeleza miradi, kuanzisha vikundi vidogo vidogo vya ushirika vya wanawake, upatikanaji kwa wanwanke wa mikopo yenye masharti nafuu. CCM itatoa elimu kwa wanawake juu ya afya na kinga juu ya UKIMWI.

 

Aidha kwenye sekta ya Nishati CCM katika ilani yake ya 2005/2010 itawarahisishia wanawake upatikanaji wa nishaiti na uhifadhi wa mazingia. CCM itatoa kwa wanawake elimu juu ya matumizi ya njia rahisi na za kisasa za nishati inayopatikana katika mazingira yao, pia kutoa elimu kwa wanawake juu ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa. CCM itatoa elimu kwa wanawake juu ya upandaji miti inayokuwa kwa haraka. CCM itasimamia kuharakisha upatikanaji na usambazaji wa umeme karibu na wananchi. Muhimu pia, CCM  itachochea na kuendeleza vipaji na ubunifu wa wanawake na vijana kuhusu majiko yanayotumia nishati kidogo,na kuimarisha na kuendeleza usambazaji wa huduma ya umeme kwa bei nafuu.

 

Tukiangalia takwimu ya idadi ya watu, Tanzania ni nchi yenye watu wapatao milioni thelethini na nne, ambapo wanaume ni asilimia 49 na wanawake ni asilimia 51. Kutokana na idadi hiyo wanawake wana idadi kubwa kuliko wanaume. Wanawake wote Tanzania ni wajibu wao kujitokeza kupigia kura CCM ili iweze kushinda kwa kishindo. Tuchague chama CCM ambacho kina “sera zilizotulia”,. Maana yake zinazoeleweka, zinazokubalika, zinazotekelezeka, zinazojengwa juu ya misingi ya historia ya Uhuru, na Utaifa wetu na maslahi ya Tanzania inayokwenda na wakati. Aidha, Sera za CCM zimelenga kuinua viwango vya maisha ya kila Mtanzania pasipo ubaguzi wa aina yoyote. bila kupingwa na zinafaa Tanzania

 

Tunatoa pongezi nyingi kwa Chama Cha Mapinduzi kwa kumkabidhi ndugu Kikwete dhamana ya kupeperusha bendera ya CCM na hatimaye afikie kubeba dhama kubwa zaidi ya kubeba bendera ya taifa. Wanawake wote wa Tanzania wanayo imani kuwa sana kwa CCM na ndugu Kikwete. Wanawake wote wanajiandaa tena kwa uaminifu kumpigia kura zao zote za ndiyo ndugu Jakaya Kikwete hapo ifikapo tarehe 30/10/2005. Wanawake wanaijua vema CCM. Hakutakuwa na kubabaika na kufanya majaribio ya sera kama vyama vingine ambavyo havijawahi kushika uongozi wa nchi. CCM Awamu ya Nne itakuwa inaendeleza juu ya yale mema mengi ambayo yameasisiwa na Awamu zilizopita. Ukweli huu unawapa wanawake matumaini makubwa sana ya kusonga mbele kimaendeleo kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya, katika Tanzania itakayoongozwa na ndugu Kikwete. Ndiyo maana tunasema CHAGUA CCM, CHAGUA KIKWETE KWA MAENDELEO YA WANAWAKE TANZANIA.

 

Nguvu ya Hoja,

Abiyani Chuo Kikuu.