USHINDI WA
Kasi inaongezeka ya mbio za wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa katika
nafasi ya urais, ubunge/uwakilishi na udiwani, kwa Uchaguzi Mkuu wa 2005 hapa
nchini. Sambamba na kasi ya kuelekea ukingoni hapo tarehe 30/10/2005, ni
kupanda kwa mapigo ya moyo ya wagombea wengi hususan wale wa nafasi ya urais.
Hali ni shwari kabisa kwa Komredi, Ndugu yetu na Shujaa wa kitanzania, Jakaya
Mrisho Kikwete. Mapigo ya Moyo ya ndugu yetu Kikwete yako barabara. Kwake, uhakika
wa ushindi, uliombatana na ari mpya ya kubeba bendera ya taifa la Tanzania ili
kuonesha uaminifu, uadilifu, utiifu, utayari na umahiri wa kuwatumikia
watanzania vinaongeza kasi-msingi. Lengo ni kuhimili nia ya kweli ya kujenga
Tanzania yenye neema tele na itakayohimili Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.
Ushiriki wa Amani na Utulivu uliooneshwa na CCM katika awamu mbalimbali
zinazojenga mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu 2005 ulipata tafsiri pogo toka kwa
vyama vingi vya upinzani. Wao waliamini huo ulikuwa ni mpito kuelekea NARC kama
ambavyo wapinzani hao walivyotamani iwe. Waliiombea CCM dua mbaya. Walisahau
kuwa Dua za kuku hazimpati Mwewe. Kosa kubwa ni kwa Vyama hivyo vya upinzani
kujifanya kusahau kwamba Amani na Utulivu ni Sera ya CCM, ambayo iliasisiwa ndani
ya harakati za kudai Uhuru, ambao ndiyo kiini cha utaifa tunaojivunia. Amani na
Utulivu ndiyo mzizi wa chemchem inayozaa umakini, historia ya ushindi,
mshikamano, umoja wa kitaifa, muungano, sera zinazotekelezeka, mvuto wa CCM kwa
wananchi, na hivyo wananchi kuipa CCM kura za Ushindi wa Kishindo.
Mchecheto, hekaheka, hofu na taharuki ya kushindwa ya vyama vya upinzania,
imekuwa ikizua mkakati wa kampeni ulioacha wananchi makini wakijiuliza maswali
yasiyo na majibu. Mfano, tumeshuhudia kampeni zilizopambwa na ufahari wa Fuso
lukuki zikihama kutoka eneo hili hadi lile mithili ya wanyama jamii ya Nyumbu
wa Masaimara. Hii ni hofu ya kushindwa kwani hata pale vyombo vya serikali
vyenye dhamana ya kulinda raia na mali zao, vilipopiga marufuku matumizi ya
Fuso kusafirisha abiria, ndugu zetu hawa walikaidi mtindo mmoja. Wananchi
wanapata mashaka ya kuwapa kura ndugu hawa ambao kwao ni kawaida kukaidi sheria
na taratibu za nchi za kulinda Amani na Utulivu wa nchi yetu.
Hofu ya kushindwa kwa Vyama vya Upinzani inavuta kasi. Sasa kampeni
zinapambwa na vituko vya karne na vya kutisha. Tumeshuhudia matumizi ya mawe,
mapanga, kuzusha uongo, uchokozi kwa vyombo vya Dola ati tu wapate huruma kwa
mataifa ya nje. Mkakati huu kamwe siyo ustaarabu wa taifa letu, na unakiuka
misingi ya ulinzi wa Amani na Utulivu wa taifa. Ni kituko kushawishi wananchi
wakupigie kura kwa kuzusha vurugu ambazo zinaangamiza maisha ya wananchi hao
unaodai unataka kuwatumikia. Ndugu zetu hawa kamwe siyo wenzetu na wanayo
malengo mengine tofauti yale ya usajili wao kama vyama vya siasa vya Tanzania.
Mchecheto wa kushindwa uliovunja rekodi ya karne ni ule wa kampeni za
kutumia helikopta. Hili nalo limezua maswali mengi yasiyo na majibu. Hiki ni
miongoni mwa vyama vilivyolalamikia sana CCM na serikali zake, kwamba zina
matumizi mabaya ya rasilmali za nchi. Ni hawahawa waliohoji kuhusu ununuzi wa ndege
ya serikali “ya Rais”. Ni hawahawa wamekuwa wakilalamikia ufinyu wa ruzuku
wanayopewa na serikali. Wananchi tuna haki ya kuhoji ni wapi wamepata mifedha
mingi ya kununua/kukodi helikopta. Iwapo ni misaada, tunahitaji kujua mataifa
au mashirika yanayohusika na undani wa mikataba na makubaliano yao. Na iwapo ni
mifedha kutokana na mkopo, ni haki yetu wananchi wapiga kura, kabla ya kupiga
kura tuelezwe vyanzo vya mapato na utaratibu watakaotumia kulipa deni kubwa
kiasi hicho. Ni hatari kukichagua chama ambacho kitaanza kutuingiza katika
madeni makubwa hata kabla chama hicho hakijaingia madarakani.
Helikopta hupita hewani na hivyo kumfanya mgombea kuwa mbali na uhalisia wa
mazingira ya wananchi. Iwapo hivi sasa mgombea ameanza kuonesha cheche za
kujiweka mbali na wananchi, ni hatari sana kumpa kura zetu, kwani mara akiingia
madarakani ndiyo hataonekana kabisa. Madai kwamba helikopta inarahisisha
kufanya mikutano mingi kwa wakati mmoja, ni kebehi kubwa kwa wananchi. Wananchi
siyo vifaranga ambavyo mgombea anaona kuvitotoa kwa wingi kutampa faida kubwa
ya ki-fedha.
Lakini, wananchi tunapata mashaka makubwa pale tunaposhuhudia baadhi ya
wagombea, hususan wa nafasi ya urais, wakiogopa kujitambulisha na asili ya
vyama vyao. Wagombea hawa kamwe hawavai Sare za Vyama vyao. Hekima zinasema,
“tija huanzia nyumbani”. Iwapo wagombea hawa hawapendi kujifungamanisha na
asili yao na hata kujivunia hadharani, watatushawishi namna gani tuwaamini kuwa
hawatautosa u-Tanzania wetu ambao ndiyo asili na fahari ya taifa letu?.
Sera za vyama vya siasa mbali na utambulisho, ni kielelezo cha uzalendo wa
kweli na fungamano la uaminifu wa utaifa. Ni kutudanganya kwa ndugu zetu hawa
kudai kwamba wanao uwezo wa kubeba bendera ya taifa kubwa, wakati hawana
utayari wa kuvaa bendera ya vyama vyao hadharani. Wananchi wapigakura tuna haki
ya kuwa na mashaka kuhusu hili. Kama nia ni kuonesha mavazi ya kimapinduzi, au
kuiga mavazi ya Mwl. Nyerere wakati anadai Uhuru, hekima isiyotia shaka
ingekuwa ni kujenga dhamira hiyo juu ya msingi wa kitanzania unaowakilishwa na
alama halali za vyama vya siasa husika. Ni vigumu kwa wananchi kutofautisha
kati ya NGOs na Vyama vya siasa. Wananchi watahofu kutoa kura zao zenye thamani
kwa wagombea ambao hawana udhamini unaotambulika na unaoaminika. Mtu huyo,
akichaguliwa, na itokee avuruge, kisha atoroke, wananchi watamdai nani?. Na hii
dhana ya “Wakati wa Mwl. Kudai Uhuru”, ni hatari, kwani inabeza Uhuru na Utaifa
wetu ulioasisiwa na Mwl. Nyerere, Baba yetu tunayemheshimu na kumthamini .
Ndiyo sababu wananchi wengi wa Tanzania na walio na mapenzi mema na nchi
yao, bado wanaelekeza kura zao zote kwa CCM. Wagombea wote wa CCM, wake kwa
waume daima huona fahari na kujitambulisha wazi pasipo mashaka kwa kuvaa Sare
za CCM. Hii ni moja ya kiashiria cha msingi kinachotupa uhalali wa kukiri kuwa
Ushindi wa Ndugu yetu Jakaya Kikwete uko wazi na hauna mashaka. Ng’ara Kikwete,
Ng’ara CCM.
Dhana ya kufaa kuongoza nchi inayoendelea kama Tanzania haipimwi kwa uwezo
wa Chama cha siasa kusimamisha mgombea urais kila inapofika wakati wa uchaguzi.
Nchi siyo sawasawa na gari la mabua. Uongozi unahitaji kuwepo kwa mifumo ya
kifikra, kisiasa, kiuchumi, kimwelekeo nk ambayo imetanda kama mizizi nchi
nzima kwa uwiano unaohimili falsafa ya uongozi, utawala na kutumikia watu. Ni
Chama Cha Mapinduzi peke yake ndicho kwa sasa kinatosheleza sifa hii. Ndiyo
maana tunasema pasipo kusita kwamba ni CCM pekee inayofaa kukabidhiwa tena uongozi
wa Tanzania 2005.
Vyama vya upinzani vina mtandao hafifu wa uhai na uongozi mithili ya madoa
doa na viraka katika nchi. Kinadharia na kiutendaji mawasiliano kati ya viraka
hivyo ni magumu na pingamizi/kikwazo kwa uhai na uimara wa taifa linalovuta
kasi ya maendeleo ili kukabiliana na changamoto za utandawazi. Umoja, Amani,
mshikamano na utulivu wa taifa vitakuwa hatarini.
Aidha uongozi wa nchi siyo ubingwa wa kukosoa, kuona mapungufu peke yake na
kushindwa kuona mafanikio. Upofu huu wa vyama vya upinzani wa kuto kuona mafanikio
ya CCM, umewafanya washindwe kujitambua kuwa hata wao wamezaliwa, wamekua ndani
ya historia ya CCM. Iwapo CCM haijafanya jambo zuri hata moja, basi na viongozi
wa vyama hivyo vya upinzani ni zao-mapungufu hayo wanayoyahubiri. Wananchi tuna
haki ya kukataa kuwapa kura zetu, kwani tuna mashaka na umakini wa vyama hivyo.
Ubingwa wa kukosoa wachezaji siyo ubingwa wa kucheza. Tumeshuhudia mabingwa
wa kukosoa katika soka kama wakiwekwa uwanjani kucheza, hawana stamina,
wanaboronga kiasi cha kutia kichefuchefu. Wananchi wanachohitaji kusikia kutoka
kwa vyama vyote vya siasa ni sera zinazotekelezeka na zinazoonesha namna
wananchi watakavyoshirikishwa na kuwezeshwa katika kulijenga taifa lao na
kuleta maendeleo yao binafsi na nchi nzima. Ni CCM peke yake ndiyo ina Ilani
inayotosheleza kuwatambua, kuwajali, kuwathamini na kuwatumikia Watanzania.
Chonde Watanzania, Chagua CCM, Chagua Kikwete.
Kikwete atakuwa na mahali pa kuanzia. Tofauti na vyama vya upinzani ambavyo
vitakuwa vinaanza upya na hivyo kuwa na hatari ya kuvuruga kabisa misingi ya
uchumi na utaifa wetu. Kikwete atakuwa anaendeleza mafaniko yote ambayo
yamefanywa na CCM katika historia ya uongozi wake hapa nchini. Ni rahisi sana
kwa wananchi kujua tunaeleka wapi tukiwa na uongozi wa CCM. Wananchi tumekuwa
sehemu ya mabadiliko makubwa na madogo na tumeonesha ushirikiano na
ushirikishwaji wa hali ya juu. Tukimchagua Kikwete, hakutakuwa na muda wa
kupoteza wa kujiandaa na kuelewa mazingira, na hata kufanyia mazoezi sera. Mara
tu Kikwete akishika usukani, maendeleo ya Taifa yatasonga mbele kwa ari mpya,
nguvu mpya na kasi mpya. Hakika tutaokoa muda. Vyama vya upinzani, vitapoteza
muda, kwani badala ya kuvuta kasi kwenda mbele, vinaweza kuvuta kasi ya kwenda nyuma,
na hata ya kutukoroga, na kutuchanganya. Mfano rahisi ni namna viongozi
wanavyovaa mavazi yasiyo na maana wazi kwa wananchi.
Kikwete anao uzoefu wa kulitumikia taifa hili katika nyanja na kada
mbalimbali. Uzoefu uliotukuka katika ushirikiano wa kimataifa umempa uzoefu
mkubwa sana wa kuongoza nchi vema na kuiepusha na athari hasi za utandawazi.
Kikwete amekuwa mstari wa mbele katika kujenga suluhu kwa njia ya mazungumzo
katika nchi za Maziwa makubwa. Zaidi, Kikwete anakijua vema chama chake CCM.
Amekua na kuitumikia CCM katika umri wake wote. Kamwe hataiangusha CCM. Aidha,
Kikwete amekua na kulelewa katika uongozi wa Mwl. Nyerere. Hivyo, atakuwa
mrithi mzuri wa fikra za Baba wa Taifa. Chini ya uongozi wa Kikwete, Uhuru,
Utaifa, Amani na Utulivu utasonga mbele kwa kasi mpya.
CCM ina historia ya kushinda. CCM itashinda tena kwa kishindo 2005. Ushindi
huu unasubiriwa kwa hamu na vijana wote wa Tanzania. Zaidi, vijana wanafunzi na
wale wa Vyuo vya Elimu ya Juu. Kiu ya matumaini ya Vijana hawa wa shule na vyuo
inatokana na ukweli kwamba, Ndugu yetu Jakaya Kikwete na familia yake ni zao
halisi la shule za hapa nchini na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Ndugu Kikwete
ni tunda halisi lenye mizizi katika harakati za Uhuru wa Tanzania na Utaifa
wetu, ambavyo vilivuta kasi sambamba na majira alipozaliwa shujaa huyu. Hakika,
vijana na wanazuoni wote wanayo kila sababu ya kukiri waziwazi kwamba watampa
mwenzao na ndugu yao Kikwete kura zote za ndiyo. Ng’ara Kikwete, Ng’ara CCM.
Pamoja na ari waliyokuwanayo watanzania, hususan vijana ya kumpa kura zote Kikwete,
ni vema utayari huo uwe ni mtaji-msingi wa kumuunga mkono Ndugu Kikwete
kutekeleza kwa ufanisi yale yote aliyowaahidi watanzania, na ambayo yamo katika
Ilani ya Uchaguzi ya CCM-2005. Vijana mpeni Kikwete ushirikiano, muwe tayari
kufanya kazi kwa bidii, muwe na moyo wa kulipenda taifa lenu, moyo wa
kujitegemea na kukataa umasikini. Aidha, vijana muwe na ubunifu, utii wa sheria
na hofu ya Mungu ili kwa pamoja muweze kujenga Tanzania yenye Neema tele kwa
Ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Ni Tanzania ambamo vijana mnaishi leo na
kesho.
Tuendelee kuwapa vyama vya upinzani muda zaidi wa kukua na kuotesha mizizi
ya uhai nchi nzima. Kinyume na hapo bado Watanzania tutaendelea kuwa na mashaka
ya kuvikabidhi vyama hivi uongozi wa nchi yetu, Mama, Tanzania.
Watanzania tuendelee kuwa na msimamo na utulivu huku tukitunza vyote;
Shahada za kupigia kura na dhamira ya kumpa ndugu yetu Jakaya Kikwete, CCM kwa
ujumla, kura zetu zote za ndiyo. Chini ya uongozi wa Kikwete, Maisha Bora kwa
kila Mtanzania yatapatikana.
Nguvu ya Hoja.
Abiyani Chuo Kikuu.