HATUA ILIYOPIGA TANZANIA KATIKA

 MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

 

[Omar R. Mapuri]

 

UTANGULIZI:

 

Rushwa ni miongoni mwa matatizo ya awali kabisa katika historia ya binadamu.  Katika hisotira yote hiyo hadi leo, rushwa katika majina na aina zake nyingi sana ipo kila pahala; katika kila jamii ya binadamu na katika kila nchi, maskini na tajiri.  Jamii za binadamu na nchi zinatofautiana tu katika viwango vya rushwa, lakini hakuna inayoweza kujigamba kwa dhati kuwa haina rushwa kabisa kabisa hata angalau katika upande wa utoaji kama si wa upokeaji.

 

Tanzania ikiwa ni sehemu ya jamii kubwa ya kimataifa, inalo tatizo kubwa la rushwa, na kama ilivyo kwa jamii zingine ulimwenguni, imo katika mapambano ya kudumu dhidi ya sarakani hiyo.  Miongoni mwa hatua za msingi zilizochukuliwa katika hatua mbali mbali za mapambano hayo baada ya Uhuru mwaka 1961 ni kuanzishwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (1966), kutungwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa (1971), kuanzishwa kwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa (1975) ambacho hivi sasa ni Taasisi ya Kuzuia Rushwa, kutungwa kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi (1983) na marekebisho yake yaliyoleta Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Ulioandaliwa (1984).  Pamoja na hatua hizo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiwa Chama tawala kilichoshika hatamu katika mfumo wa chama kimoja, mwaka 1989 kiliunda Kamati iliyochunguza tatizo la Rushwa na ukiukwaji wa maadili ya uongozi.  Kamati hiyo iligundua kwamba tatizo hilo lilikuwa limefikia viwango vya kutisha.

 

Katika Uchaguzi Mkuu wa 1995 ambao ulikuwa wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi, suala la rushwa lilikuwa miongoni mwa vipengele vya msingi vya kampeni za vyama vilivyokuwa vikigombea, kikiwemo CCM.  Baada ya ushindi wa CCM, Rais Benjamin Mkapa aliunda Tume ya Uchunguzi Dhidi ya Rushwa (maarufu Tume ya Warioba).  Tume hiyo ilibaini aina mbali mbali za mianya ya rushwa na kupendekeza hatua za kuiziba na kupambana na tatizo zima la rushwa kwa jumla.  Mapendekezo hayo yalifanyiwa kazi na Serikali kwa njia ya hatua mbali mbali zilizochukuliwa ambazo zitabainishwa baadae katika makala hii.

 

Wakati huu tukielekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005, mjadala umeshamiri miongoni mwa Watanzania kama kiwango cha rushwa nchini kimepungua, kimebaki pale pale au kimeongezeka.  Kutokana na kutotumika kwa vigezo vinavyopimika kwa uhakika, mjadala huo umegubikwa zaidi na hisia na dhana tu.  Wanaodai kuwa rushwa imeongezeka, hawaonyeshi vigezo vinavyopimika kuthibitisha madai yao.  Hivyo hivyo kwa wanaodai kuwa rushwa imepungua au iko pale pale.

 

Kwa bahati nzuri, Taasisi ya Uwazi Duniani (Transparency International) ambayo inafuatilia mwelekeo wa rushwa duniani na jitihada za kupmbana nayo, imebuni kipimo cha rushwa ilichokiita Corruption Perception Index (CPI). Kiswahili labda ni Fahirisi ya Rushwa.  Kipimo hicho kina upeo wa alama kuanzia 0 hadi 10 ambapo 0 inaonyesha kukithiri kwa rushwa (yaani hakuna hata chembe ya uadilifu) na 10 maana yake hakuna kabisa rushwa (yaani uadilifu uliokamilika).  Hata hivyo, kwa lengo la kumrahisishia tafsiri Mtanzania wa kawaida, kipimo hicho tutakiita Fahirisi ya Uadilifu kwa maana ya kwamba inapokuwa ndogo inaashiria upungufu wa uadilifu (au ukubwa wa rushwa) na inapokuwa kubwa ni kinyume chake.

 

Transparency International (TI) hukikokotoa kipimo hicho kutokana na taarifa za utafiti inazozikusanya katika nchi.  Katika tafiti (surveys) hizo za kisayansi, TI hutaka tathmini na maoni ya watu wanaoathirika sana na tatizo la rushwa (kama vile wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi inayotathminiwa) kuhusu tatizo la rushwa na ukubwa wake katika nchi, kwa kutumia njia ya sampuli nasibu.  Ufafanuzi wa Fahirisi ya Uadilifu inavyopatikana uko nje ya upeo wa madhumuni ya makala hii, lakini itoshe tu kukiri kwamba kipimo hicho kinaheshimika sana duniani.

 

Toka mwaka 1995, TI imekuwa ikifanya tafiti na kuchapisha taarifa za kila mwaka zinazoonyesha viwango vya rushwa vya nchi mbali mbali duniani kwa kutumia kipimo cha Fahirisi ya Uadilifu.  Tanzania ilianza kuingizwa katika tafiti hizo mwaka 1998 na imeendelea kuwamo mfululizo hadi sasa.  Katika kipindi hicho, Fahirisi ya Uadilifu ya Tanzania imeongezeka kutoka 1.9 mwaka 1998 hadi 2.9 mwaka 2005.  Ni dhahiri kwa hivyo kwamba kwa kipimo hicho, kiwango cha uadilifu nchini Tanzania kimeongezeka kwa kima cha asilimia 52.6 katika kipindi hicho.  Kwa maneno mengine, kiwango cha rushwa kimepungua kwa kima hicho hicho cha asilimia 52.6.

 

Katika makala hii, zaidi ya kubainisha hatua mbali mbali zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa kupambana na rushwa, tutaonyesha kwa ufafanuzi jinsi Tanzania inavyopiga hatua katika mapambano hayo kwa ulinganisho na nchi jirani za Afrika Mashariki na nyinginezo za Afrika zinazotafitiwa na TI.

 

Suala la Rushwa Katika Ilani za CCM

 

CCM iliingia katika Chaguzi Kuu za 1995 na 2000 na ahadi ya kupambana na rushwa, miongoni mwa ahadi zake kuu za uchaguzi.

 

Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 1995, ahadi ya kupiga vita rushwa iliwekwa katika ibara ya 29 na ilisomeka ifuatavyo:-

 

“29.    Rushwa ni tatizo kubwa katika jamii yetu hivi sasa na ni tishio kwa usalama, utulivu na heshima kwa taifa letu.  Katika miaka mitano ijayo, Serikali za CCM zitapiga vita kwa nguvu zaidi rushwa nchini kwa njia zifuatazo:-

(a)              Kuhakikisha kwamba Serikali za CCM zinazingatia kwa dhati sheria za utawala Bora na Maadili ya Viongozi, pamoja na kutakasa safu za uongozi ndani ya Serikali zote mbili na vyombo vyao vyote.

(b)              Kuendeleza kwa nguvu zote vita vilivyokwishaanzishwa dhidi ya rushwa ndani ya vyombo vyote vya utoaji haki ili haki isiuzwe wala kununuliwa.

(c)               Kuwalinda wananchi wanaowafichua wapokeaji na watoa rushwa.

(d)              Kuona kwamba Serikali inakuwa wazi zaidi katika kuwekeana mikataba, tenda na kandarasi mbali mbali ili kulinda maslahi ya umma wa wakulima na wafanyakazi wa nchi yetu.

(e)              Kuona kwamba Serikali inadhibiti kwa makini zaidi masuala ya uhamiaji, huduma za Bandari na Ushuru wa Forodha ili kupambana kwa ukamilifu na watoaji na wapokeaji rushwa na wakwepaji kulipa ushuru na kodi nyingine katika maeneo hayo.

(f)                Kuona kwamba Serikali zote mbili zinahakikisha kuwa mifumo ya utendaji kazi inapunguza fursa (mianya) ya kutoa na kupokea rushwa”.

 

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, CCM ilikuwa tena na kauli ya ahadi ya vita dhidi ya rushwa na hujuma za kiuchumi.  Ahadi hiyo imo katika ibara za 92 na 93 za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka wa 2000, na inasomeka kwa sehemu kama ifuatavyo:-

 

“92.    Mapambano dhidi ya rushwa ni ahadi na sera ya TANU, ASP na sasa CCM.  Serikali ya Awamu ya Tatu imechukua hatua madhubuti kupambana na rushwa ndani ya CCM, katika vyombo vya umma na jamii kwa jumla ……….”

 

“93.    Baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupambana na rushwa katika kipindi cha uongozi kilichopita, CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo itafanya yafuatayo:-

(i)                Serikali zitaendelea kuchukua hatua za kisheria, kiutawala na kinidhamu kwa wale wote waliobainika walihusika na vitendo vya rushwa.   Katika kipindi hiki, Serikali zitahakikisha haya yote yanaendelezwa ili kufikia lengo linalohitajika, yaani kutokomeza rushwa.

(ii)              Serikali zitaimarisha uwezo na nguvu za wananchi kuwawezesha kuzidisha vita dhidi ya rushwa.  Wananchi wataelimishwa na kuhamasishwa juu ya haki zao, asili na aina ya rushwa, mbinu za kutambua na kukabiliana na vitendo vya rushwa, mbinu za kutoa taarifa za rushwa kwenye vyombo vya dola na namna ya kujikinga dhidi ya athari zinazotokana na kuwaumbua wala rushwa.

(iii)            Serikali zitaendelea kusisitiza kwamba viongozi na watendaji waheshimu utawala wa sheria na utawala bora, na kuzingatia maadili na uadilifu wakati wote wa kuwahudumia wananchi.  Aidha, Serikali zitaendelea kusafisha safu za uongozi na utendaji Serikalini watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwachukulia hatua zinazostahili.

(iv)            Serikali zitaelekeza mapambano dhidi ya rushwa kwenye vyombo vya haki kwa nguvu na kasi kubwa zaidi.  Vyombo vya fedha, hususan, sekta ya ukusanyaji mapato na mabenki vitaangaliwa kwa umuhimu wa pekee ili mapato yanayopaswa kukusanywa na matumizi yake yadhibitiwe.

(v)              Katika kuimarisha uchumi, Serikali zitaendelea kuweka na kusimamia misingi ya uwazi na uwajibikaji katika mikataba, tenda, ununuzi na udhibiti wa viwango vya utekelezaji wake.  Pia Serikali zitachukua hatua za kuhuisha au hata kuvunja mikataba yo yote itakayoonekana utekelezaji wake umegubikwa na vitendo vya rushwa.

(vi)            Serikali zitaendelea kuboresha na kurahisisha taratibu za uwekezaji ili kuondoa vishawishi vya rushwa.  Aidha, Serikali zitafuatilia mtiririko wa uwekezaji kuhakikisha kwamba wawekezaji nao wanafuata sheria, taratibu na maadili ya uwazi na uwajibikaji.”

 

Kuundwa kwa Tume ya Warioba

 

Mara tu baada ya ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 1995, Rais Benjamin Mkapa aliunda Tume ya Uchunguzi Dhidi ya Rushwa, maarufu kwa jina la Tume ya Warioba kutokana na Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu.  Katika ripoti yake yenye uchambuzi wa kina kuhusu hali ya rushwa nchini wakati huo, Tume hiyo ilibaini mianya mingi ya rushwa.  Tume iligundua pia kwamba rushwa ilifikia viwango vya juu kiasi kwamba ilichangia sana katika kudumaza uchumi wa nchi na ilikuwa kikwazo kikubwa katika ufanisi wa utendaji Serikalini ambapo malengo ya kiuchumi na kijamii yalikuwa hayafikiwi.  Mapato ya Serikali yalikuwa yakiingia mifukoni mwa wajanja badala ya kuelekezwa kwenye kukuza uchumi wa nchi.  Hali hiyo iliathiri vibaya imani ya wananchi kwa Serikali.

 

Tume ilipendekeza hatua mbali mbali za kupambana na rushwa zilizogawika katika maeneo mawili makuu ya kimkakati.  Maeneo hayo ni kwanza kuziba mianya ya rushwa na pili kuwafichua na kuwachukulia hatua za kisheria, kiutawala na kinidhamu wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

 

Hatua Zilizochukuliwa

 

Mara tu baada ya kukabidhiwa Ripoti ya Tume ya Warioba, Rais Mkapa alichukua hatua zifuatazo:-

 

 

Hatua hizi zilifungua milango kwa hatua nyingi mahususi zilizokoleza vita dhidi ya rushwa.

 

Kwa upande wa kuziba mianya ya rushwa, hatua zifuatazo ni baadhi ya zilizochukuliwa katika hatua mbali mbali za mapambano dhidi ya rushwa kuanzia 1996 hadi 2004:-

 

Kwa upande wa kukabiliana na watuhumiwa wa rushwa, hatua zifuatazo zimechukuliwa katika hatua mbali mbali za mapambano:-

 

 

 

 

Matokeo Ya Hatua Hizo

 

Hatua hizo za kuziba mianya ya rushwa na kuwakabili wala rushwa, zimechangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ya kiuchumi na kijamii yafuatayo miongoni mwa mengine:-

 

 

Tathmini  Ya Hali ya Rushwa

 

Hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa kupiga vita rushwa toka 1995 hadi sasa ni ushahidi tosha wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya CCM kupambana na rushwa.  Matokeo ya hatua hizo ni kukua kwa uchumi na unafuu katika upatikanaji wa huduma mbali mbali za elimu, hali ambayo inaashiria dalili za kupungua kwa rushwa.

 

Hata hivyo, kutokana na tathmini za kihisia ambazo aghlabu zinaathiriwa na mitazamo na misimamo ya kisiasa, Watanzania wamegawanyika.  Wapo Watanzania wanaoamini kuwa kiwango cha rushwa kimeongezeka katika kipindi cha 1995-2005.  Wapo wanaooamini kuwa haikuongezeka wala kupungua.  Lakini pia wapo wanaoamini kuwa imepungua.  Lakini wote hao huwa hawatoi vielelezo vya kuthibitisha madai yao.

 

Kutokana na ukweli kwamba dhana ya rushwa imesimama juu ya msingi wa hisia kutokana na ugumu wa kuithibitisha, pengine mjadala juu ya kuongezeka au kupungua kwa kiwango cha rushwa si rahisi kutoa jawabu linaloweza kukubalika kwa wote katika jamii.  Kwa maana hiyo, mjadala utaendelea tu wakati wote.  La muhimu kuzingatia ni kwamba mijadala hiyo ndiyo inayochochea mapambano dhidi ya rushwa kwa maslahi ya jamii.

 

Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, wanasayansi hawajapumzika katika kutafuta vigezo vya kitarakimu vya kupimia kiwango cha rushwa katika jamii.  Ndipo TI walipokuja na kigezo cha Fahirisi ya Uadilifu, kilichofafanuliwa katika Utangulizi.  Kipimo hicho kinawezesha kubaini kwa uhakika zaidi kuongezeka au kupungua kwa kiwango cha rushwa katika nchi na kulinganisha viwango vya rushwa baina ya nchi na nchi.  Kwa bahati nzuri, toka 1998, Tanzania imo katika tathmini ya kimataifa ya viwango vya rushwa inayofanywa kila mwaka na TI.  Matokeo ya tathmini hii yanawapa fursa Watanzania kufuatilia mabadiliko (kuongezeka au kupungua) ya viwango vya rushwa nchini na pia kujua nafasi yao katika upeo wa kimataifa.  Makala hii imekusudiwa pia kuwaarifu Watanzania kuwepo kwa kigezo hiki ili nacho wakitumie katika mjadala wa rushwa kwa uelewa na utulivu zaidi.

 

Tathmini za TI

 

Kama ilivyokwishaelezwa, Fahirisi ya Uadilifu ya Taasisi ya Uwawazi Ulimwenguni (TI) ni kipimo kinachowezesha kufuatilia mabadiliko ya viwango vya rushwa  na kulinganisha baina ya nchi na nchi.  Katika sehemu hii ya makala hii tutaitumia fursa hiyo kuilinganisha Tanzania na nchi jirani na washiriki wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, yaani Uganda na Kenya.

 

Jedwali Na. 1 linaonyesha Fahirisi za Uadilifu za Tanzania, Uganda na Kenya kwa miaka 8 toka 1998 hadi 2005.

 

Jedwali Na. 1: Fahirisi za Uadilifu za Tanzania kwa Ulinganisho na za

                         Uganda na Kenya, 1998-2005                  

MWAKA

FAHIRISI ZA UADILIFU (KATIKA 10)

(Corruption Perception Index)

 

Tanzania

Uganda

Kenya

1998

1.9

2.6

2.5

1999

1.9

2.2

2.0

2000

2.5

2.3

2.1

2001

2.2

1.9

2.0

2002

2.7

2.1

1.9

2003

2.5

2.2

1.8

2004

2.8

2.6

2.1

2005

2.9

2.5

2.1

Ongezeko baina ya 1998 na 2004

 

1.0

 

-0.1

 

-0.4

 

Ongezeko kiasilimia

 

52.6%

 

-4.0%

 

-19.0%

 

Chanzo: www.transparency.org

 

 

Inaonekana kwamba Fahirisi ya Uadilifu ya Tanzania imeongezeka kutoka 1.9 mwaka 1998 hadi 2.9 mwaka 2005, likiwa ni ongezeko la asilimia 52.6.  Kwa maana nyingine, kiwango cha rushwa nchini Tanzania kilipungua kwa asilimia 52.6 katika kipindi hicho.

 

Kwa ulinganisho na Uganda na Kenya, Tanzania ilipitwa na nchi hizo kwa uadilifu katika miaka ya 1998 na 1999.  Lakini kuanzia mwaka wa 2000 imezipita mfululizo.  Aidha, wakati Fahirisi ya Uadilifu ya Tanzania iliongezeka kwa asilimia 52.6 baina ya 1998 na 2005, ile ya Uganda imepungua kwa asilimia 4.0 na ile ya Kenya imepungua kwa asilimia 19.0.  Ni dhahiri kwa hivyo kwamba Tanzania ina kiwango cha chini kabisa cha rushwa katika nchi za Afrika Mashariki na inafanya vizuri zaidi kuliko zote katika mapambano dhidi ya rushwa.

 

Tanzania iemonyesha mwelekeo wa kuongezeka ufanisi hata katika upeo wa Afrika.  Jedwali Na. 2 linaonyesha nafasi ya Tanzania katika orodha ya nchi za Afrika zilizotathminiwa na AI kwa kila mwaka, hadi kufikia mwaka 2004.

 

Jedwali Na. 2:  Nafasi ya Tanzania Miongoni mwa Nchi za Afrika katika Uadilifu                                            

Mwaka

Nafasi ya Tanzania

Idadi ya Nchi Zilizoshiriki

Idadi ya Nchi Ilizogawana Nazo Nafasi

Idadi ya Nchi Ziliyoipita

Idadi ya Nchi Ilizozipita

1998

14

17

1

14

1

1999

12

18

0

15

2

2000

12

21

0

14

6

2001

11

16

0

11

4

2002

11

20

2

10

7

2003

11

27

3

12

11

2004

9

36

3

13

19

Chanzo: www.transparency.org

 

ANGALIZO:  Wakati makala hii inaandikwa uchambuzi wa takwimu hizi kwa mwaka 2005

                    haukuweza kufanyika kutokana na kukosekana kwa takwimu za msingi.

 

 

Inaonekana kwamba pamoja na kuongezeka kwa idadi ya nchi za Afrika zilizotathminiwa na AI kutoka 17 mwaka 1998 hadi 36 mwaka 2004, nafasi ya Tanzania katika Fahirisi ya Uadilifu iliongezeka kwa ubora kutoka 14 hadi 9 katika kipindi hicho.  Aidha, wakati mwaka 1998, Tanzania iliipita nchi moja tu, mwaka 2004 ilizipita nchi 19.  Zaidi, mwaka 2004, kwa mara ya kwanza kabisa Tanzania ilizipita nchi nyingi zaidi kuliko ziliyoipita.  Miongoni mwa nchi ambazo awali zilikuwa na Fahirisi ya Uadilifu kubwa zaidi kuliko Tanzania lakini sasa inazipita au iko sawa nazo ni Kenya, Uganda, Ivory Coast, Zambia, Msumbiji, Zimbabwe, Malawi, Algeria na Ethiopia.  Miongoni mwa nchi ambazo wakati wote Tanzania imezipita ni Nigeria, Cameroun, Angola, Chad, Sudan, Sierra Leone, Congo Brazzaville, Niger, Libya na Eritrea.

 

Kwa upande mwingine, nchi za Afrika ambazo wakati wote zimeipita Tanzania kwa uadilifu ni Botswana, Namibia, Mauritius, Afrika Kusini, Misri, Ghana, Senagal na Morocco.

 

HITIMISHO:

 

Kutokana na tathmini hii kwa kutumia vigezo vya ndani na vya Kimataifa, ni maoni yetu kwamba kiwango cha rushwa kimepungua nchini Tanzania kutoka mwaka 1995 hadi 2005.  Hayo ni matokeo ya hatua mbali mbali zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa zilizolengwa mahsusi katika kupambana na rushwa.  Rais Mkapa anastahili sifa za pekee katika mafanikio haya kwa jinsi anavyoongoza mapambano haya kisayansi na kwa ujasiri mkubwa.  Aidha, kwa vile hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa ni za utekelezaji wa Ilani za Uchaguzi za CCM za 1995 na 2000, CCM inayo haki ya kujisifu kwa matokeo mazuri ya hatua hizo.

 

Tathmini hii haionyeshi na wala sisi hatudai kwamba rushwa imekwisha nchini Tanzania.  Rushwa bado ipo, tena katika viwango vya juu.  Lakini inapigwa vita ipasavyo na inapungua; tena kwa uendelevu.  Hata CCM haikuahidi katika Ilani zake kwamba itaimaliza rushwa katika kipindi hiki.  Kutokana na ukubwa na ugumu wa vita dhidi ya rushwa, CCM ingeahidi hivyo ingeuhadaa umma wa Watanzania.  CCM iliahidi kwamba Serikali zake zitapambana vikali na rushwa.  Serikali zimetekeleza na zinaendelea kutekeleza hilo kwa ufanisi mkubwa.  Mara nyingi Rais Mkapa amekuwa akitukumbusha msemo wa wahenga kwamba: ada ya mja hunena, uungwana ni vitendo.  CCM na Serikali zake imedhihirisha uungwana huo katika utekelezaji wa kauli yake ya kupambana na rushwa.