TAARIFA
YA KATIBU WA ITIKADI NA UENEZI TAIFA WA CCM KUHUSU VURUGU ZILIZOFANYWA NA WAFUASI
WA CUF HUKO BAGAMOYO
Katika taarifa yangu kwa vyombo vya habari ya
tarehe 7Juni,2005, nilitoa kwa CUF siku saba (7) kulaani vitendo vilivyofanywa
na wafuasi wake huko Bagamoyo tarehe 5 Juni,2005 na kuwaomba radhi waathirika
wa vurugu hizo. Nilisema bayana kwamba
kama hawakufanya hivyo ndani ya kipindi hicho, basi sisi CCM tutaamini kwamba
vurugu hizo zilikuwa na baraka za viongozi wakuu wa CUF na pengine walizipanga
na kuziandaa kwa makusudi. Aidha, niliongeza kwamba kama tutaridhika kuwa huo
ndio ukweli, basi tutafikiri upya kuhusu uhusiano na mashirikiano yetu na CUF.
Leo zimekamilika siku saba (7) na CUF imeshindwa
kuzilaani vurugu hizo na kuwaomba radhi waathirika. Kwa hiyo, natangaza rasmi kwamba vurugu zile za Bagamoyo
zilibarikiwa na viongozi wa juu wa CUF na uwezekano ni mkubwa kwamba
walizipanga na kuziandaa kwa makusudi.
Na hili si la kushangaa kwani mara nyingi viongozi wa juu wa CUF
wamekuwa wakisikika hadharani wakitoa kauli za kuwachochea vijana wao kupitia
kauli mbio yao ya “Wanaume mapanga shaa shaa shaa.” Yaani wanoe mapanga.
Tukio la Bagamoyo ni matokeo ya uchochezi huo.
Napenda pia kutangaza rasmi kwamba tutaendelea
kutafakari juu ya uhusiano na ushirikiano
wetu na CUF. Tutaendelea kufuatilia kauli na vitendo vyao. Mwelekeo wa mabadiliko ya uhusiano na
ushirikiano utategemea vitendo na kauli zao.
Tamko langu la tarehe 7 June lilikuwa na vipengele
vitatu ambavyo niliwataka viongozi wa
CUF wavitolee kauli. Vipengele hivyo
ni:-
Katika
maelezo yao ya tarehe 9 Juni, 2005, viongozi wakuu wa CUF hawakugusia chochote
kuhusu vipengele viwili vya kwanza.
Kushindwa kuzilaani vurugu hizo peke yake kunatosha kuwa ushahidi wa
kuhusika kwa viongozi hao katika kuzibarikia vurugu hizo. Kukanusha kwao kuwa chanzo cha vurugu hizo
ni unafiki na uzandiki mtupu, kama kweli walikuwa wakiamini walivyokuwa
wanasema kwamba eti CCM ndio ilikuwa chanzo, ingekuwa rahisi kwao kuzilaani vurugu hizo. Lakini wameshindwa kuzilaani kwa kuchelea
kuwavunja moyo wahuni waliowatuma kwenda kufanya vurugu hizo. Kwa vyovyote vile huwezi ukakodi gari zaid
ya 70 na kuyajaza wahuni, ukawamwaga kijiji kidogo cha Bagamoyo, wakafanya
vurugu halafu ukajidai huhusiki na vurugu hizo. Hakuna atakayekuamini hata ukijieleza kwa bidii kiasi gani.
Kwa upande wa kuyshindwa kuomba radhi, hii
haitushangazi. Hii ni kwa sababu kuomba
radhi kunahitaji uungwana, na CUF haina uungwana huo. Mbaya zaidi ni pale
viongozi hao wa CUF walipojaribu kujisafisha kwa kutumia uongo. Sijapata kuona watu wenye uhodari wa
kuhusika na uongo na kujieleza kwa kujiamini kama viongozi wa CUF.
Nilitoa mifano mitatu tu ya uongo waliousema mchana
bila ya aibu.
Sina haja ya kuendelea na uongo mwingine mwingi tu
walioutoa viongozi wa CUF, kwamni naamini Watanzania wamekwishaubaini. Masuala mengine yako mahakamani, si vizuri
kuyazungumzia.
Ni jambo la faraja kwamba Watanzania wanazidi
kuielewa nia mbaya ya viongozi wa CUF, kwa amani ya nchi yetu. Ushahidi ni jinsi chama hicho kinavyozidi
kukimbiwa na watu kama ilivyotokea wiki iliyopita huko Pemba.
Namalizia kwa kukitahadharisha chama cha CUF kwamba
kama hakitabadilisha mwenendo wake mbaya wa kutishia amani na usalama, kitaendelea
kukimbiwa na Watanzania. Narejea kauli
yangu ya wiki iliyopita kwamba kisitafute mchawi, kwani mchawi ni chenyewe.