HOTUBA YA NDUGU OMAR R. MAPURI, KATIBU WA ITIKADI NA UENEZI WA CCM ALIYOITOA KWENYE MKUTANO MKUU WA WANASALAMU WA RADIO UHURU

TAREHE 11 JUNI, 2006 MJINI KISARAWE

 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Ndugu Mwinshehe Mlao,

 

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Pwani, Ndugu Amina Makilagi,

 

Katibu wa CCM, Wilaya ya Kisarawe, Ndugu Sofia Kilingo,

 

Ndugu Urembo Mawamba, Mwenyekiti wa Wanasalamu na Mjumbe

              wa Bodi ya Wakurugenzi ya Radio Uhuru,

 

Ndugu Juma Penza, Mkurugenzi Mtendaji wa Radio Uhuru,

 

Ndugu Wanasalamu wa Radio Uhuru,

 

Wageni Waalikwa,

 

Mabibi na Mabwana.

 

 

 

 

Utangulizi wa Pongezi

 

Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kukupongezeni kwa dhati kabisa Wanasalamu wote wa Radio Uhuru kwa kuandaa mkutano wenu huu mkuu ambao unakukutanisheni Wanasalamu kutoka maeneo yote ya nchi inakosikika Radio Uhuru.  Kufanikiwa kwa mkutano huu ni kielelezo wazi cha kushamiri na kuendelea kuimarika kwa umoja na udugu wa familia hii kubwa ya Wanasalamu wa Radio Uhuru.  Mpaka sasa sina taarifa ya kuwepo kwa umoja wa aina hii wa wasikilizaji wa Radio nyingine yo yote nchini, zaidi ya Radio Uhuru.  Wala sina taarifa ya kuwapo kwa umoja wowote wa watazamaji wa televisheni wala wa wasomaji wa magazeti.  Umoja wenu ni wa aina ya pekee nchini, na kwa hilo, munayo haki ya kujivuna na kujiona wenye fahari.  Zaidi ya kuunganishwa na Radio Uhuru, mumejikuta wenyewe mkijenga maeneo mengine ya mshikamano ya kijamii na kiuchumi.  Najua mnaendeana shughuli za misiba kama vile mazishi, kuhani na hata kwa njia ya salamu za rambirambi.  Mnafarijiana kwenye matatizo kama vile magonjwa au mikosi mbali mbali ya kimaisha.  Mnaendeana shughuli za furaha kama vile arusi, maulidi (birthdays), ngoma za kucheza mwana, n.k.  Mnatembeleana mtu kwa mtu na hata familia kwa familia.  Nina taarifa pia kuwa mnasaidiana hata katika shughuli zenu za kiuchumi za kujitafutia riziki.

 

Yote haya na mengine mengi ambayo sikuyataja yameujenga umoja wenu hadi kufikia hatua  ya udugu wa kifamilia, au upendo mmoja aliouzungumzia Bob Marley katika wimbo wake wa “One Love” aliouteua Mwenyekiti Mawamba katika tangazo lake la mkutano huu.  Sasa hivi tunazungumzia siyo mtandao tu, bali familia ya Wanasalama na wasikilizaji wengine wa Radio Uhuru.  La kufurahisha zaidi ni kwamba mmewaingiza na watangazaji na watumishi wengine wa Radio Uhuru katika familia hii kubwa,adhimu na ya aina yake.  Hii sasa ndiyo inakuwa familia ya Radio Uhuru. Huwezi kukuta pengine popote mtandao mkubwa wa kifamilia wa aina hii zaidi ya Radio Uhuru.  Nakupongezeni tena na nina fahari kubwa nanyi.

 

Shukrani

Baada ya maelezo hayo ya pongezi, sasa napenda kuwashukuru waandalizi wa mkutano huu  kwa kunitunuku fursa hii ya kuwa mgeni rasmi.  Ulipofikishwa kwangu mwaliko na Mwenyekiti Mawamba niliupokea kama kitu nilichokuwa nikikisubiri kwa hamu.  Hii ni kwa sababu na mimi hufurahia sana kushiriki mikutano kama hii ambapo hupata fursa ya kuwaona na kuwajua Wanasalamu hasa katika mazingira ambapo kila siku wanajitokeza wapya.  Kwa mfano majina ya akina Zico, Asia Damumbaya, Pondamali Kufakwaja na Rais Mtarajiwa wa 2045 ambayo na mengine yanayotamba katika anga za Radio Uhuru wakati huu yameanza kusikika hivi karibuni tu.  Pengine nami nitapata fursa ya kuwaona na kuwajua baadhi yao na hivyo kufarijika kwani nami najisikia kuwa mwanafamilia wa Radio Uhuru.  Nakushukuruni sana kwa mwaliko huu ambao kama msingenipa, ni hakika nisingejisikia  vyema.  Asanteni sana. Kwa mwaliko huu, mmenipa pia fursa ya kuwaelezea Wanasalamu na wasikilizaji wengine wa Radio Uhuru, mambo mbali mbali ya kisera na kimkakati kuhusu Radio yetu tuipendayo.

 

 

 

 

Historia Fupi ya Umiliki wa Radio Uhuru

 

Radio Uhuru ilianzishwa kwa mara ya kwanza na makada wa CCM mwaka 1999 kwa malengo ya msingi ya kibiashara lakini pia kuipatia CCM fursa ya kuitumia kwa shughuli za kiuenezi kwa kiasi fulani.  CCM iliitumia fursa hiyo wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2000.  Hata hivyo, kwa vile Radio haikuwa ya CCM na wamiliki japokuwa walikuwa makada wa CCM lakini walifungika na maadili ya utangazaji wakati wa uchaguzi, fursa ya kuitumia Radio ilitolewa pia kwa vyama vingine.

 

Baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika, wamiliki wa Radio Uhuru walielekea  zaidi kwenye biashara na mwaka 2002 waliamua kuuza sehemu kubwa ya hisa zao kwa kampuni moja ya nje ya nchi.  Wamiliki wapya waliibadilisha jina na mwelekeo Radio hiyo ambapo sasa iliitwa Uhuru FM na vipindi vikabadilika kabisa na hata watangazaji sawia.

 

Kwa upande wa pili, CCM nayo baada ya mauzo hayo, ilijikuta imeondokewa na chombo muhimu cha uenezi ilichokuwa imeanza kukitegemea.  Mwaka 2004, CCM ilipitisha uamuzi wa kuwa na Radio yake yenyewe badala ya kutegemea tu fadhila.  Baada ya kuzingatia ukweli kwamba Radio Uhuru ya awali ilikwishajulikana  na kuzoeleka na  kuwa tayari ilikwishakuwa na mtandao wa wasikilizaji madhubuti, CCM iliwakabili wamiliki wa Uhuru FM ili waiuzie.  Kwa bahati ilisadifu pia kuwa hata wao walikuwa tayari wanafikiria kuiuza Radio hiyo baada ya kubaini kuwa ilikuwa imekimbiwa na wasikilizaji.  Waliona ingekuwa bora zaidi kuanzisha Radio yao mpya  ambayo itaanza na wasikilizaji wapya badala ya kutegemea kuwabadili mawazo wale wa Radio Uhuru, yaani akina Mzee Mawamba na wenzake.

 

Ilikuwa ni katika mazingira hayo ndipo CCM ilipoamua rasmi kuinunua Radio Uhuru mwaka 2004.  Lakini hata baada ya uamuzi huo, CCM ilikuwa bado na mtazamo wa kutoonekana inaimiliki na kuiendesha moja kwa moja Radio hiyo.  Kwa hivyo iliikabidhi kampuni moja kuinunua na kuiendesha Radio hiyo kwa niaba yake.  Kampuni hiyo nayo ikaunda kampuni tanzu ya Peoples’ Media Communications Limited (PMCL) ya kuiendesha Radio hiyo.

 

Kwa bahati mbaya, utaratibu huo wa umiliki na uendeshaji ulitoa mwanya kwa migogoro ya kiuongozi na kiutendaji iliyoathiri ufanisi  na hata kuhatisha uhai wa Radio Uhuru, ambayo sina haja ya kuifafanua hapa.  CCM ikaunda Kamati ya Kupendekeza Utaratibu Bora wa Kuendesha Radio Uhuru – maarufu kwa jina la Kamati ya Mikidadi kutokana na jina la Mwenyekiti wake,  Ndugu Mikidadi Mahamoud,  Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ilala.

 

Kamati hiyo iliwasilisha mapendekezo yake Chamani na Chama kikapitisha utaratibu mpya wa kumiliki na kuendesha Radio Uhuru kwa kuzingatia mapendekezo hayo mwezi Aprili, 2006.  Vifuatavyo ni baadhi ya vipengele vya msingi vilivyo sehemu ya utaratibu huo:-

 

·        CCM sasa inaimiliki moja kwa moja Radio Uhuru badala ya kumiliki kupitia kampuni iliyo mtu wa tatu (third party).

 

·        Kampuni ya PMCL ambayo imepewa jukumu la kuendesha Radio Uhuru, inamilikiwa moja kwa moja na CCM na si kampuni tanzu tena ya kampuni nyingine.

 

·        Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni hiyo inateuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.  Uteuzi wa Bodi ya kwanza tayari umekwishafanywa ambapo Mwenyekiti wake ni gwiji la Itikadi na Uenezi la Chama, Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru, na Wanasalamu wana uwakilishi wao kupitia Mwenyekiti wao Mzee Urembo Mawamba.

 

·        Mkurugenzi Mtendaji wa Radio Uhuru anateuliwa na Kamati Kuu.  Uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza tayari umekwishafanyika ambapo ameteuliwa kada aliyewiva, Ndugu Juma Penza.

 

 

 

 

 

·        Radio Uhuru tayari ina muundo wake wa utumishi ambao utaanza kutumika wakati wowote kuanzia sasa.

 

·        Inatarajiwa kwamba Bodi itapendekeza kwa Chama, sera ya utangazaji ya Radio Uhuru, ambayo bila shaka itaegemea kwenye uenezi wa sera za Chama pamoja na kutekeleza majukumu ya kuelimisha, kuburudisha na kuwafikishia habari wananchi.

 

Historia Fupi ya Mabadiliko ya Mtazamo wa Chama Kuhusu Umiliki wa Radio Uhuru

 

Kama nilivyokwishaeleza, awali CCM haikupenda ionekane inamiliki Radio.  Dhana zilizokuwapo wakati huo ni kwamba Radio ikimilikiwa  wazi wazi na Chama ingekosa biashara na hata wasikilizaji.  Wapinzani wetu walitufanya tuamini kwamba watu wamechoka na propaganda za CCM.  Tuliusahau hata mtaji wetu wa wanachama zaidi ya milioni tatu.  Matokeo yake ni kutumia mbinu ya kuwahamasisha makada wetu waanzishe Radio ambayo isionekane kuwa ya CCM.

 

Lakini pia hata tulipoamua kununua Radio yetu tukaanza na wazo la kuuficha umiliki wetu.

 

Lakini hofu zote hizo zilikujabainika baadaye kuwa hazikuwa za msingi.  Kwanza pale makada wetu walipoiuza Radio Uhuru ya awali kwa watu walioamua kuitenga na CCM, Radio hiyo wakati huo ikiitwa Uhuru FM ilikimbiwa na wasikilizaji.  Kwa hivyo, ilidhihirika waziwazi kwamba kama Radio kukikimbiwa na wasikilizaji, basi si kwa sababu ya kuwa ni ya CCM au yenye mwelekeo wa CCM.  Kutokana na ukweli huo huo, hata hofu kwamba CCM inakimbiza biahsara haikuthibiti.

 

Lakini zaidi ya hivyo, wasikilizaji walifurahi sana mara tu walipoarifiwa kwamba Radio Uhuru imerudi katika ushawishi wa CCM baada ya kununuliwa na Chama mwezi wa Agosti, 2004.  Wakaanza kutafutana tena na kuuimarisha umoja wao.  Mwanzoni mwa 2005 yalipokuja mashindano ya kushindanisha vituo vya Radio nchini, Wanasalamu na wasikilizaji wengine wa Radio Uhuru walijenga hamasa kubwa ya aina yake ya kutafuta ushindi mpaka wakaiwezesha Redio kupata tuzo kwa kipindi chake cha Alfajiri Njema.  Isitoshe, kwa ushindi huo Radio Uhuru ilizishinda hata Radio zenye mitandao ya usikivu wa nchi nzima wakati yenyewe wakati huo ikisikika Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Zanzibar tu.  Hata Arusha na Mwanza ilikuwa haisikiki kutokana na kuharibika kwa mitambo yake.

 

Jambo hilo ndilo lililokuwa la msingi lililonifunua macho kuhusu nguvu kubwa ya uhamasishaji iliyomo katika mtandao wa Wanasalamu wa Radio Uhuru.  Ndipo nilipoifurahia na kuitumia ipasavyo fursa mliyonipa ya ziara za kukabidhi tuzo Mkuranga, Kisarawe, Bagamoyo na Kibaha mwezi Mei na Juni, 2005.  Kwa jinsi mikutano ilivyofanikiwa na hamasa niliyoiona kwenye  mikutano ile na miongoni mwa Wanasalamu, ilinidhihirikia kuwa mtandao wenu ulikuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko hata niliyokuwa nikiifikiria awali.

 

Ilinidhihirikia zaidi kwamba Wanasalamu wengi wa Radio Uhuru kumbe ni wanachama, mashabiki, wanaharakati na baadhi yao hata makada na viongozi wa CCM.  Kipimo changu ni kwamba mtakumbuka kuwa ziara zangu zile nilizifanya kisiasa ambapo ziliratibiwa na viongozi wa CCM.  Hilo lilionekana kukupeni hamasa zaidi na mahudhurio yenu kuwa mazuri tena yenye uchagamfu na msisimko mkubwa.

 

Ni katika mazingira hayo ndipo liliponijia wazo la haraka haraka la kuitumia nguvu hiyo kubwa ya uhamasishaji niliyoigundua miongoni mwenu, katika kueneza sera za CCM.

 

Ndipo nilipoanza kwenye mikutano hiyo kukuombeni kuipigia debe CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu tuliokuwa tunautarajia mwishoni mwa mwaka huo.

 

Nataka nichukue fursa hii kwa mara nyingine tena, kukushukuruni kwa dhati kabisa kwa jinsi mlivyonitekelezea ombi langu kwa uwezo na ufanisi mkubwa mpaka CCM tukapata ushindi wa kishindo uliotuduwaza wote sisi na wapinzani wetu.

 

Mambo yote yaliyoziviza hofu zilizokuwapo kuhusiana na kuitambulisha Radio kuwa ni mali ya Chama ndiyo yaliyonipa nguvu kuanza kujenga hoja kwa viongozi wenzangu ndani ya Chama kwamba hakuna sababu ya kuendelea kuuficha umiliki wetu wa Radio Uhuru.  Nashukuru kwamba hatimaye tumekubaliana na hilo sasa halina ubishi tena.

 

 

Matokeo ya Kuweka Bayana Umiliki wa Radio Uhuru

 

Matokeo ya uamuzi wa Chama wa kuweka bayana umiliki wake wa Radio Uhuru na kuiwekea utaratibu unaoeleweka ni kwamba tumeweza kufanya mengi ya faida yakiwemo yafuatayo:-

 

·        Tuliitumia Radio Uhuru kwa ukamilifu, kwa nafasi na kwa raha zetu katika kampeni za CCM za Uchaguzi Mkuu uliopita.  Mafanikio kila mmoja anayaona.

 

·        Wanasalamu wa Radio Uhuru walijitokeza wazi wazi  bila ya hofu na kwa hamasa kubwa kuipigia ndogo ndogo na kubwa kubwa CCM wakati wakisalimiana na kubadilishana mawazo kupitia vipindi  karibu vyote vya Radio Uhuru.

 

·        Watangazaji wa Radio Uhuru nao walijitanafasi kuipigia kampeni CCM wazi wazi na bila ya woga kwenye vipindi vyao karibu vyote.

 

·        Wasanii wengi wakahamasika na kujitokeza kutunga nyimbo za kisiasa za kuinadi CCM, wagombea wake na sera zake kwani ilipatikana Radio ya kuzipiga, na hivyo na wao kujitambulisha kwa umma.

 

·        Toka wakati huo, kutokana na hamasa iliyojengeka, idadi ya Wanasalamu imekuwa ikiongezeka kila kukicha.  Kuna wakati nilikuwa nikiorodhesha wanasalamu lakini kazi hiyo sasa imenishinda.  Kila siku yanaibuka majina mapya.  Hata misamiati mipya ikaanza kusikika k.v. habari za unju au kulamku macho au nakwenenda.  Halikadhalika majina mapya ya mitaa na vijiji hasa vya Zanzibar yakaanza kusikika ambayo mengine bado yanawapa taabu baadhi ya watangazaji.  Kwa mfano Chwaka bado kuna baadhi ya watangazaji wanaitamka Chakwa.  Lakini yote hayo ni ushahidi wa kukua kwa familia ya Radio Uhuru.

 

·        Uamuzi wa kuweka bayana umiliki wa Chama wa Radio Uhuru umewezesha kuweka uongozi wa Radio kwa kuzingatia siyo tu taaluma, bali pia ukada na ukereketwa wa Chama.  Ndiyo maana tuna Ndugu Juma Penza hapa ambaye ni kada aliyeandaliwa na Chama Cha Mapinduzi kwa muda mrefu.  Amepikwa akapikika.  Amefundwa akafundika katika itikadi na maadili ya Chama.

 

Matokeo ya Mabadiliko ya Uongozi

 

Kuletwa kwa uongozi mpya wa Radio Uhuru kumeamsha uhai mpya katika Radio.  Mara tu baada ya kuanza kazi akiwa Kaimu Mkurugenzi, Januari, 2006, Ndugu Penza alianzisha mchakato kabambe wa mabadiliko ya kiutendaji na kimwelekeo katika Radio Uhuru.  Hadi sasa tumeshuhudia mafanikio mengi kutokana na  mchakato huo yakiwemo yafuatayo:-

 

·        Migogoro ya kiuongozi na kiutendaji imekwisha katika Radio Uhuru.

 

·        Matatizo mengi ya kiufundi yaliyokuwapo ambayo yakiwasumbua watangazaji na wasikilizaji yamepata ufumbuzi.  Mfano ni lile tatizo sugu la kuwapo kwa line moja tu ya simu.  Sasa zipo lines tano kwa ajili ya matumizi ya Wanasalamu na wasikilizaji wengine wa Radio Uhuru.  Wanasalamu sasa wanajimwaga kwa nafasi zaidi, licha ya kuongezeka sana kwa idadi yao.  Rachel Udoba siku hizi hapati nafasi ya kutamba na lile goma lake, wala Angel Akilimali na lile vanga lake la “kuloga kulumangila, Pandu”.

 

Hii ni kwa sababu siku hizi inamaliza simu moja inaingia nyingine.  Hakuna muda wa kutia goma au vanga ila labda kwa kulazimisha kwa kuwacha kupokea simu inayongoja.  Siku hizi hata wale wasikilizaji waliokuwa na mtindo mbaya wa kuzuwia line kwa makusudi kwa nia ya kuhujumu wamekwama, kwani kama atazuwia line moja, nyingine zinafanya kazi.

 

·        Matatizo mengine yaliyopatiwa ufumbuzi ni pamoja na lile la usikivu wa Radio Uhuru Arusha na Mwanza. Sasa akina Mzee Msengesi kule Arusha wamerudi kutamba katika anga za Radio Uhuru na Jaffari Osama na Omary Ogola wanatoa changamoto kule Mwanza. Aidha, hali ya vifaa mbali mbali vya studio sasa ni nzuri zaidi. Yote hayo yamewezekana kutokana na juhudi za Radio Uhuru yenyewe bila ya kutegemea msaada kutoka Chamani.  Huko nyuma, ufumbuzi wa matatizo hayo ulisubiri fedha kutoka Chamani.  Naomba tumpongeze Ndugu Penza na timu yake ya viongozi na watendaji.

 

·        Kutokana na Ari mpya, Ndugu mpya na Kasi mpya iliyoingia Radio Uhuru, sasa umepatikana muda na hata uwezo wa kushughulikia kwa uhakika zaidi suala la usikivu wa Radio Uhuru katika maeneo mengine ya nchi yetu.  Ni hivi kesho

 

kutwa tu, Radio Uhuru itaanza kusikika kwa mara ya kwanza Dodoma.  Baadaye kidogo tu itafuata Lindi na Mtwara na hatimae kidogo kidogo na kwengineko.

 

·        Hivi sasa vimeanza kusikika vipindi vya kuelimisha vikiwemo vya dini, elimu ya uraia na vya kujenga mwamko na kuhamasisha kuhusu maendeleo, n.k.

 

·        Na kwa upande wa siasa, kutokana na kazi ya msingi iliyofanywa na uongozi mpya, wafanyakazi wote wa Radio Uhuru hivi sasa ni wanachama kamili wa CCM na wamekwishafungua Shina la Chama ambalo Mwenyekiti wake ni Violet Mzindakaya Mpogolo a.k.a Sister V a.k.a Mpiganaji.  Pia wamekwishaanzisha darasa la itikadi.

 

Wito kwa Wanasalamu

 

Kwa heshima kubwa na taadhima napenda katika hatua hii kutoa wito kwa Wanasalamu na wasikilizaji wengine wa Radio Uhuru kuendelea kujitokeza na kushiriki vipindi vyote vya Radio yenu vinavyowapa fursa hiyo kwa njia ya simu, ujumbe wa simu, barua au hata kwenda studio wanapokaribishwa.  Wito wangu huo napenda kuugawa katika maeneo mahususi yafuatayo:-

 

·        Kila mtakapohitajika, mjitokeze kwa hamasa zote kufanya kazi za uenezi wa CCM na sera zake kama mlivyofanya wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ambapo mchango wenu kwa ushindi wa CCM unatambuliwa hata na viongozi wa kitaifa wa Chama na Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais Kikwete mwenyewe.  Kazi kubwa ya sasa ni kuhamasishana katika utekelezaji wa Ilani na kushiriki shughuli za maendeleo na kupambana na umaskini.  Ndiyo maana nilifurahi sana hivi karibuni niliposikia salamu ya Mambo Poa ya mwanasalamu mmoja wa Radio Uhuru ikitoa wito kwa wanasalamu wengine kwamba wapande miti kama anavyofanya Juma Kikobesa.

 

·        Wanasalamu mjitokeze kwa wingi katika mijadala ya vipindi mbali mbali vya Radio UHuru.  Miongoni mwa miongozo ya jumla niliyokwishaitoa kwa uongozi wa Radio Uhuru ni kwamba kila kipindi kinachoanzishwa ni lazima kiwe na sehemu ya kuwashirikisha wasikilizaji.  Yaani kwa kadiri inavyowezekana, vipindi viwe shirikishi ili kuwapata fursa wasikilizaji kutoa michango ya mawazo na hata kuonyesha vipaji vyao.  Kwa mfano, kwa utaratibu shirikishi, Kigwa One amefichua vipaji vya uimbaji miongoni mwa wasikilizaji.  Pia Sister V na First Eddy wameweza kufichua kipaji cha utangazaji cha Amina Midundulu pale walipomwalika studio kushiriki kuendesha kipindi.  Aidha, sina haja ya kumtaja Zomboko wa Enzi Hizo.

 

·        Nawapa changamoto Wanasalamu mshiriki mijadala ya kisiasa na mambo ya kijamii kila mnapopata fursa iwe katika kipindi cha Radio au hata mitaani.  Kwa mfano suala la maamuzi ya Mahakama Kuu ya kupiga marufuku takrima katika uchaguzi na kuamuru kuanzishwa kwa utaratibu wa kuwa na wagombea binafsi.  Mijadala yote katika vyombo vya habari iliyofuatia maamuzi hayo ilionekana kuonyesha kuwa Chama Cha Mapinduzi ndicho kilichokomolewa na  kuwa eti ndicho kitachoathirika.  Sijasikia mtu akikumbusha kwamba hata kabla ya uamuzi wa Mahakama, takrima ya kushawishi kujipatia kura ilikuwa tayari ni marufuku katika Kanuni za Maadili za CCM.  Pia kuhusu suala la wagombea binafsi, mbona sijasikia mtu akitanabahisha kuwa uamuzi huo utaweza siyo tu kuvisambaratisha, bali hata kuvimaliza vyama vya upinzani?  Kwa maoni yangu, uwezekano ni mkubwa zaidi kwa vyama vya upinzani kukimbiwa na wagombea wazuri kutokana na migogoro isiyokwisha ndani ya vyama hivyo, kuliko ilivyo kwa CCM ambavyo uzoefu unaonyesha kuwa ni mahiri katika kuyapatia ufumbuzi matatizo kila yanapojitokeza ndani yake.  Maeneo haya na mengineyo yako wazi kuchangiwa mawazo na Wanasalamu na wasikilizaji wengine wa Radio Uhuru.

 

·        Kama ilivyokwishadhihirika, Radio Uhuru imo katika mchakato wa kuanzisha vipindi vyenye mwelekeo wa kuelimisha na kupanua mawazo.  Natoa wito kwa Wanasalamu kujiandaa na kuwa tayari kushiriki katika vipindi hivyo ambavyo aghalabu vitakuwa  shirikishi.  Nitapenda kuona upeo wa Wanasalamu na watangazaji unakua zaidi ya utani wa kawaida kama ule wa Usimba na Uyanga wa Limonga na Halima Karubandika.

 

·        Lakini napenda pia katika hatua hii, kutoa ombi kwa Wanasalamu na wasikilizaji wengine wa Radio Uhuru kwamba ushiriki wenu katika vipindi vya Radio uzingatie nidhamu.  Haipendezi mtu kung’ang’ania line ya simu kwa muda mrefu tena hata baada ya kuombwa kuacha kufanya hivyo.  Utakuta mtu anataka kuwasalimu watu wote, lakini kutokana na wingi wao, hawezi kuwamaliza.  Mwingine anapiga simu lakini ikipokelewa hasemi.  Haipendezi wasikililizaji wa Dar es Salaam na Pwani kuamsha kwa simu siku ya Jumatano kinyume na makubaliano.  Msimnyime raha Rachel Udoba wala msimsumbue Katibu Jakulanga kufunga safari za kwenda kuwakumbusha watu wajibu wanaoujua. 

 

Kuna nyakati atahitajika Mwenyekiti Mawamba au Katibu Jakulanga au msikilizaji mwingine kupanda kwa dharura ya kutoa tangazo au ufafanuzi fulani.  Wasikilizaji wengine watapaoombwa wasipige simu wakati huo wakubali.  Nidhamu na kuzingatia maadili na kufikiriana na kuhurumiana ni mambo ya msingi katika kuimarisha udugu na upendo katika familia yetu ya Radio Uhuru.  Kwa hivyo wakati wote unaposhiriki katika kipindi, wafikirie wenzako badala ya kujifikiria wewe tu.

 

Pongezi Kwa Watangazaji

 

Hotuba yangu haitokuwa imekamilika wala sitokuwa nimetenda haki kama nitaimaliza bila ya neno la pongezi kwa watangazaji wa Radio Uhuru, watumishi wengine wa Radio na uongozi wao.  Toka uanze kazi uongozi wa sasa wa Radio Uhuru sasa napata usingizi.  Siletewi tena mambo ya kusumbua akili na kurusha roho.  Yanakuja yale tu yanayostahiki.

 

Wafanyakazi wote wa Radio Uhuru wanaipenda kazi yao na wanajituma.  Wanaipenda CCM na ni wanachama waaminifu.

 

Watangazaji wanawapenda wasikilizaji wao.  Ni wavumilivu sana, kwani wakati mwingine hukumbana na maudhi kutoka kwa baadhi ya wasikilizaji lakini wanayakabili kwa utulivu na bila ya donge la roho.  Lakini hebu Wanasalamu na wasikilizaji wa Radio Uhuru tujiulize; kwa nini tuwatie watangazaji wetu kwenye mitihani?

 

Watangazaji wetu wote ni wabunifu sana katika kuendesha vipindi vyao.  Kila kipindi kimepata mtu au watu.  Kinapwaya anapopata udhuru.

 

Kwa yote hayo na mengine mengi yanayohitaji muda kuyaorodhesha nawapongeza kwa dhati na kuwaomba waendeleze ufanisi na ubunifu ili Radio Uhuru iendelee kupanda hadhi.

 

Mwisho

 

Mwisho, napenda kuwatakia heri wote mlioweza kuhudhuria mkutano huu na wenzenu wote ambao hawakupata wasaa huo.  Nakuombeni tuendeleze familia yetu hii adhimu na adimu.

 

 

ASANTENI