MFUKO WA TASAF UNATEKELEZA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM

 

{Na Omar R. Mapuri}

 

 

Mfuko wa Tanzania Social Action Fund (TASAF) umekuwa maarufu sana Tanzania nzima kutokana na kazi kubwa na nzuri unaofanya katika Wilaya 40 za majaribio.  Mfuko huo unachangia nguvu za wananchi katika miradi ya huduma za jamii wanayoiamua na kuianzisha wao wenyewe kwa lengo la kuondoa kero zinazowakabili.  Kwa utaratibu huo, Mfuko umewezesha kukamilika kwa miradi mingi ya wananchi iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu hasa ya  mabanda ya shule za msingi na sekondari, zahanati, masoko na maji.  Kwa jumla,  mfuko wa TASAF unaonekana mkombozi katika wilaya za majaribio zinazofaidika nao na umejenga matumaini katika sehemu nyingine za nchi ambako haujafika.  Taarifa za kufurahisha ni kwamba Mfuko huo sasa unaingia katika awamu yake ya pili ambapo utaenea nchi nzima.

 

Kama kawaida yao, wapinzani wetu walijaribu kuubeza Mfuko huo na maendeleo unayoyaleta.  Lakini walipogundua kwamba haubezeki kutokana na wananchi kuwapuuza kila walipojaribu kuubeza, wapinzani hao walianza kujishirikisha nao.  Hata Pemba ambako viongozi wa chama cha upinzani cha CUF kwa muda mrefu waliwazuia wafuasi wao kushiriki shughuli za maendeleo, wapinzani sasa wanashiriki kikamilifu katika miradi ya TASAF na mingineyo ya wananchi.  Lakini pia wanautumia ushiriki wao huo kujaribu kupotosha chanzo na madhumuni ya TASAF.  Wanadai kwamba eti chanzo cha TASAF ni wahisani na kwamba eti Mfuko huo hauhusiani na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

 

Pamoja na kwamba tunajua kuwa wana CCM na wananchi wenye uelewa wa mambo wameubaini na kuupuuza upotoshaji huo, ili kuondoa utata tumeona tuna wajibu wa kuwafahamisha wote namna TASAF ilivyokuja, na hasa  jitihada mahsusi za Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa, Mwenyekiti wa CCM.

 

Chimbuko la TASAF

 

Chimbuko la wazo la kuwa na vyanzo vya fedha za kusaidia nguvu za wananchi ni sera ya msingi na ya siku nyingi ya CCM ya kuwashirikisha wananchi katika kujiletea maendeleo yao.  Programu  ya Chama Cha Mapinduzi ya miaka ya themanini ilielekeza kwamba wananchi wachangie kwa hali na mali katika maendeleo yao hasa katika sekta ya huduma za jamii, ili kusaidiana na Serikali katika kuharakisha maendeleo.  Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 1990 ilitoa msukumo wa utekelezaji wa sera hiyo.  Katika kutekeleza Ilani hiyo, Serikali zilianza kutenga katika bajeti zao, mafungu ya fedha za kusaidia nguvu za wananchi.  Ibara ya 38(b) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 1995 ilielezea mafanikio makubwa ya utekelezaji wa sera hiyo ambapo wananchi walianzisha miradi mingi ya huduma za jamii.

 

Kutokana na mafanikio hayo, sera hiyo ya kuwashirikisha wananchi katika maendeleo yao na kujiondolea kero iliendelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 1995.  Kwa mfano, kuhusiana na sekta ya Elimu, Ilani hiyo iliahidi ifuatavyo katika ibara yake ya 14(ii) “… Aidha,  michango ya hali na mali ya jamii nzima ya Tanzania kwa njia ya kujenga Taifa itaendelea kuhimizwa ili kuimarisha ubora wa elimu”.  Kuhusu maji, Ilani hiyo ya 1995 iliahidi “kuhimiza ukamilishaji wa miradi ya maji ambayo haijaanza kufanya kazi na vile vile kufufua miradi ambayo haitoi huduma ipasavyo” katika ibara yake ya 16(ii).  Mwelekeo ulikuwa huo huo katika sekta ya afya na nyinginezo za huduma za jamii.

 

Mara tu baada ya kushika madaraka ya Urais katika kipindi chake cha kwanza mwaka 1995, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa aliibaini kazi iliyokuwa mbele katika utekelezaji wa sera hii.  Jinsi wananchi walivyokuwa wamehamasika katika kuanzisha miradi yao, mafungu ya bajeti za Serikali ya kusaidia nguvu za wananchi hayakutosha kabisa, kwani miradi mingi ilikuwa imekwama ikisubiri mchango wa Serikali.  Ndipo kwa kutumia haiba yake na umaarufu aliokuwa amekwishajijengea kimataifa, aliwasiliana na Benki ya Dunia kwa nia ya kupata chanzo kingine kipya cha kusaidia nguvu za wananchi,

zaidi ya bajeti ya Serikali na misaada mingine ya nchi za nje na Asasi zisizokuwa za Serikali (AZISE au NGOs).  Benki ya Dunia ikamkubalia na ndipo maandalizi ya TASAF yalipoanza.

 

Kuanza kwa TASAF

 

Kama ilivyoelezwa katika toleo la kwanza la “Mkereketwa”, TASAF ilianza rasmi kutekelezwa mwaka 2000.  Kwa upande mwingine, sera ya kuwashirikisha wananchi katika maendeleo yao iliendelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2000 kwa kuahidi kama ifuatavyo:-

 

(a)            “Kukamilisha miradi yote ya ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, madawati, vyoo vya wanafunzi na kuendelea kuwahamasisha wananchi waendelee kujenga shule mpya za kutwa za sekondari kwa kila tarafa au kata”.  (Ibara ya 54(i)).

 

(b)         “Kuendelea kutoa kipaumbele katika shughuli za ujenzi na ukarabati wa Hospitali, vituo vya afya na zahanati, kwa kushirikisha wananchi, mashirika ya dini, sekta za watu binafsi na jumuiya nyingine za wananchi”. (Ibara ya 57(i)).

 

(c)          “Kushirikisha kikamilifu nguvu za wananchi katika hatua zote za kutoa huduma ya maji ….” (Ibara ya 59(iii)).

 

(d)            “Kuwahamasisha na kuwashajiisha wananchi wa jinsia na marika yote ili washiriki kikamilifu katika harakati za maendeleo”.  (Ibara ya 87(i)).

 

TASAF kama Mkakati wa Kutekeleza Ilani ya CCM

 

Inadhirika kwa hivyo kwamba TASAF haikuja yenyewe tu bila ya malengo.  TASAF ni mkakati ulioandaliwa na Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa, Mwenyekiti wa CCM kwa lengo na madhumuni ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.  Kwa maneno mengine, huwezi kuitenganisha TASAF na Ilani ya Uchaguzi ya CCM au sera za CCM kwa jumla.  Mafanikio ya TASAF ni mafanikio ya CCM.

 

Kwa hivyo, wale wapinzani wanaoona mambo yanakwenda vizuri na wakapenda kujinasibisha na mafanikio hayo, wasione vyaelea; vimeundwa.  Tena vimeundwa na CCM.  Wao walie tu.  Hata hivyo, wajione huru kufaidi matunda ya sera za CCM zinazofanya kazi, lakini bila ya kuwababaisha wananchi.

 

Nani kama CCM?  Hakuna.