TAARIFA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI,
MHESHIMIWA OMAR R. MAPURI JUU YA KAULI ZA UCHOCHEZI ZA VIONGOZI WA CUF
ALIYOITOA TAREHE 28/1/2004 MJINI DAR ES SALAAM
Ninalaani vikali kauli za uchochezi na za kujenga
chuki na uhasama zilizoripotiwa na vyombo vya habari kutolewa na viongozi
mbalimbali wa CUF tarehe 26/1/2004 mjini Dar es Salaam na 27/1/2004 mjini
Zanzibar.
Kauli kama zile za kuwataka wafuasi wao wajiandae kupambana
na polisi, kupiga wake wa polisi au kufanya vurugu nchini siyo tu ni
za kujenga chuki, bali pia ni za kuhatarisha amani na utulivu wa nchi, jambo
ambalo ni kinyume kabisa na dhamira za mfumo wa vyama vingi. Aidha kauli za kuwataka wafuasi wao wawe
tayari kuwa vizuka na vilema si za kuwatakia mema wafuasi wao.
Kauli hizo zimeripotiwa kutolewa na viongozi hao
katika mikutano ya hadhara eti ya kuadhimisha matukio ya tarehe 26 na 27
Januari, 2001. Nikiyatazama katika
muktadha wa Muafaka Baina ya CCM na CUF ambao Wizara yangu ina nafasi yake mahsusi
katika utekelezaji wake, nayaona maadhimisho hayo kuwa yanakwenda kinyume
kabisa na dhamira ya Muafaka huo.
Viongozi wa CUF husikika sana wakilaumu Serikali na
CCM kuwa tunavunja Muafaka. Lakini
kumbe lawama hizo ni za kuficha tu uvunjaji wa Muafaka unaofanywa na wao
wenyewe CUF. Katika maelezo yake ya
utangulizi, Muafaka unasema ifuatavyo miongoni mwa mengine:
“Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama
Cha Wananchi (CUF) vinakubaliana kimsingi:
KWAMBA lengo na madhumuni makubwa ya
kufikia Muafaka huu ni kusahau yaliyopita na kutekeleza, kwa makusudi
kabisa, makubaliano yetu ili kujenga demokrasia ya kweli na kwa hivyo kuleta
maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii katika nchi yetu.”
Kitendo cha kuadhimisha matukio ya tarehe 26 na 27
Januari, 2001 ambayo yalikuwa ni miongoni mwa agenda zilizofikiwa maelewano
katika Muafaka, si cha kusahau yaliyopita, bali ni cha kuyakumbusha. Hiyo siyo dhamira ya Muafaka. Mbaya zaidi ni kwamba viongozi wa CUF
wanasisitiza kwamba hawasahau kwa kauli yao ya kilaghai kwamba “wanasamehe
lakini hawasahau”. Huo ni uvunjaji wa
wazi wazi na wa makusudi wa Muafaka ambao unatutaka tusahau.
Kipengele kingine cha Muafaka ambacho kwa maoni
yangu naona kinakiukwa sana na CUF ni ibara ndogo ya 1(i) ambayo inasema:
“Vyama vya siasa kuheshimu Katiba na
Sheria za nchi na kuepuka kutumia lugha zinazochochea chuki baina ya vyama
vya siasa, ukabila, uhasama na kutovumiliana”.
CUF wanaonekana kushindwa kabisa kuepuka
kutumia lugha hizo.
Hayo ya Muafaka niyaachie hapo, lakini
nataka umma wa Watanzania uelewe kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania haitoruhusu kisingizio chochote kutumiwa na wanasiasa wenye kiu ya
damu ya Watanzania kuvuruga amani na kuhatarisha usalama wa Watanzania.
Serikali hii na ile ya Mapinduzi ya
Zanzibar ziko madarakani kihalali kwa ridhaa ya wananchi kwa mujibu wa sheria
za nchi. SMT iko madarakani baada ya
Rais Benjamin Mkapa kuzoa kura
5,863,201 sawa na asilimia 71.7 ya kura halali zilizopigwa, dhidi ya kura 1,329,077
tu za Lupumba sawa na aslimia 16.3. SMZ
iko madarakani baada ya Rais Amani Abeid Karume kupata kura 248,095 sawa na
aslimia 67 ya kura halali zilizopigwa dhidi ya 122,000 tu za Seif Sharif sawa
na aslimia 33. Serikali hizi zina
heshima kubwa ndani na nje ya Tanzania.
Napenda viongozi wa CUF na wanasiasa
wenzangu wengine wote waelewe kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania haina unyonge wa aina yo yote na inaendesha shughuli zake kifua
mbele. Haiwezi kutikiswa na vitisho vya
wanasiasa walioishiwa sera.
Wale wanaotayarishwa kupambana na Jeshi
la Polisi eti kwa sababu ni dogo wasidanganyike. Jeshi letu la Polisi lina uwezo wa kukabiliana na hali
yoyote. Ni dogo lakini lenye utaalamu
wa kutosha na ari ya juu kabisa katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda
usalama wa raia kwa kutumia sheria za nchi.
Napenda kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wanasiasa wasiliingize Jeshi
la Polisi katika malumbano ya kisiasa.
Kazi ya Jeshi hilo si siasa bali ni kupambana na wahalifu. Na katika jukumu hilo, Polisi watamwandama
mhalifu yo yote kwa uhalifu wake bila ya kujali itikadi yake ya kisiasa,
kabila, rangi au kitu kingine chochote.
Kwa hivyo, wanasiasa wanaotangaza mapambano na Polisi wasifikiri kuwa
siasa itakuwa kinga kwao.
Lakini pia viongozi wa CUF watakuwa
wanajidanganya na kudanganya wengine kama wataishia kutazama Jeshi la Polisi
peke yake na kuisahau nguvu ya umma iliyo nyuma ya Serikali walioichagua. Kama wanatoa mifano ya nchi ambako nguvu ya
umma ilikuwa dhidi ya Serikali, wajue kwamba hapa Tanzania nguvu ya umma iko
upande wa Serikali. Na kwa bahati
nzuri, kila kukicha nguvu hiyo inaongezeka kama matokeo ya uchaguzi mdogo wa
madiwani wa hivi karibuni yanavyodhihirisha.
Nawaomba wananchi wawe watulivu. Serikali itaendelea kutumia sheria, hekima
na busara kuziviza shari zinazoandaliwa na wanasiasa wenye hulka za kiharamia. Lakini pia nawahakikishia kwamba kama shari
itazuka, Serikali inao uwezo kamili wa kuikabili na kuizima. Lakini Tanzania ya shari na vurugu siyo
tunayojitahidi kuijenga sisi wa Serikali ya CCM.
Kama Tanzania ya shari na vurugu ndiyo
ndoto ya viongozi wa CUF na wanasiasa wengine, basi wakubali pia kwamba ndiyo
inayowaponza na kuwagharimu kwa kunyimwa kura kwani Watanzania walio wengi siyo
wanayoitaka. Vinginevyo wanasiasa hao
wamekwishajua kwamba hawana nafasi ya kushinda uchaguzi, kwa hivyo kama kawaida
yao, wanaanza mapema kutengeneza visingizio vya kukataa matokeo wakati huo
tukielekea Uchaguzi Mkuu wa 2005.
Kama hoja ya kauli za uchochezi
zinazotolewa na wanasiasa ni kutaka uchaguzi mkuu wa 2005 usivurugwe, basi hiyo
pia ndiyo dhamiri ya dhati ya Serikali.
Napenda kuwahakikishia wanasiasa hao na wananchi kwa jumla kwamba
haitoruhusu mtu au kikundi chochote cha watu kuvuruga uchaguzi mkuu kwa
kisingizio chochote kile. Kwa hivyo
kama hiyo ndiyo hofu ya kweli na kama wao wenyewe hawana agenda ya kuvuruga
uchaguzi, basi nawasihi wanasiasa husika waondokane na hofu hiyo na badala yake
wazungumzie mambo ya kuwaletea matumaini Watanzania badala ya kuhubiri maapizo
ya kuwaangamiza katika vurugu na hivyo kuwakatisha tamaa.
Napenda kuchukua fursa hii kuwaasa
wafuasi wa CUF na wananchi wengine kukataa kuswagiwa kwenye matatizo ya ulema,
uzuka na mengine kwani wakipata matatizo hayo, viongozi wao hawatowasaidia bali
wataielekea Serikali hii hii kwa misaada.
Napenda kumalizia kwa kuwaarifu wananchi
kwamba kauli za uchochezi za viongozi wa CUF zinachunguzwa na Polisi kwa lengo
la kuchukua hatua zipasavyo za kisheria.