MAHOJIANO YA RADIO UHURU NA KATIBU WA ITIKADI NA UENEZI WA CCM MHE. OMAR R. MAPURI TAREHE 10 NOVEMBA, 2005

 

Swali:      Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ulifanyika tarehe 30 Oktoba, 2005 na CCM imejipatia ushindi mnono kwa Urais, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani.  Unajisikiaje kama Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa?

 

Jibu:        Najisikia mwenye furaha kubwa sana kwani Wazanzibari wamezizima ngebe za CUF.  Aidha, katika CCM, ushindi huo tuliutarajia na Mwenyezi Mungu ametuthibitishia matarajio yetu hayo.  Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais Amani Abeid Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) kwa ushindi wa asilimia 53.2 alioupata ambao kwa mazingira ya siasa za Zanzibar, ni mkubwa wa kishindo.  Nawapongeza pia Wawakilishi na Madiwani walioshinda kwa tiketi ya CCM.

 

Swali:      Ndugu Mapuri umesema kwamba CCM mlikuwa mnautarajia ushindi huo.  Ni kitu gani kilikupeni matumaini hayo.

 

Jibu:        Ni mambo mengi yaliyotupa matumaini ya ushindi, lakini nitataja mawili tu ambayo ndiyo ya msingi.  Kwanza, ni utekelezaji uliofanikiwa sana wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2000 uliofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Karume.  Maendeleo makubwa yamepatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Unguja na Pemba kutokana na utekelezaji huo wa Ilani katika nyanja za uchumi, miundombinu, huduma za jamii na kadhalika.  Pamoja na kwamba Wazanzibari wengi hupiga kura kwa misimamo ya ukereketwa wa vyama kama nitakavyofafanua baadaye, tuliamini kwamba wapo pia wasiokuwa wachache ambao wangepiga kura kwa kuzingatia maendeleo yaliyopatikana katika kipindi hicho.  Jambo la pili kubwa lililotupa uhakika wa kushinda ni zingatio la historia ya siasa za ushindani Zanzibar.  Katika chaguzi karibu zote za kutafuta uhuru katika miaka ya 1950 na 1960, chama cha Afro-Shirazi kilikuwa kikipata kura nyingi zaidi kuliko za chama cha Hizbu na mshirika wake ZPPP kwa pamoja, hata pale kilipozidiwa idadi ya viti.  Mfano, ni uchaguzi wa mwisho kabla ya Mapinduzi uliofanyika mwaka 1963.  Ingawa Afro-Shirazi Party ilipata viti 13 tu vikilinganishwa na 18 vya Hizbu na ZPPP, lakini ilipata asilimia 54.2 ya kura halali (au 53.1% ya kura zote zilizopigwa).  Hapa njama za kuinyima ushindi Afro-Shirazi Party kwa kutumia mbinu ya ukataji wa majimbo inadhihirika.  Maeneo yaliyokuwa ngome za Afro-Shirazi yalipatiwa majimbo machache kiidadi lakini makubwa kwa idadi ya watu lakini yale yaliyokuwa ngome za Hizbu na ZPPP yalipatiwa majimbo mengi lakini madogo madogo.  Halafu ikawekwa sheria kwamba anayepata majimbo mengi ndiye mshindi.  Haya ni miongoni mwa mazingira yaliyoifanya Afro-Shirazi inyimwe haki ya kuunda Serikali pamoja na kuwa ndiyo iliyokuwa na watu wengi zaidi.  Hii ndiyo maana ule uhuru wa Zanzibar wa 1963 uliokabidhiwa kwa vyama vya wachache waliokuwa vibaraka wa Sultani tunauita kule Zanzibar kuwa wa bandia.  Na hiyo ndiyo miongoni mwa sababu kuu zilizohalalisha Mapinduzi matukufu ya 1964.  Sasa nikirudi kwenye hoja yangu ya kwa nini tulikuwa na uhakika wa kushinda; ni kwamba baada ya chama cha CUF kuundwa mwaka 1992 kufuatia kuruhusiwa tena kwa mfumo wa vyama vingi baada ya miaka 28 ya mfumo wa chama kimoja, wale waliokuwa wafuasi wa vyama vya zamani vya Hizbu na ZPPP waliona (kwa kuambiwa na waanzilishi wa CUF) kwamba vyama vyao vilivyokuwa vimepigwa marufuku vimerudi kwa jina la CUF.  Afro-Shirazi nao wakaganda kwa CCM.  Pamoja na kwamba ipo mifano michache ya Hizbu na ZPPP wa zamani kuingia CCM na Afro-Shirazi wa zamani kujiunga na CUF, mwelekeo wa jumla unabaki kwa kiasi kikubwa kuwa ule ule wa Hizbu/ZPPP kuwa CUF na Afro-Shirazi kuwa CCM.  Na wazee wa pande zote mbili hufanya bidii kubwa kuwarithisha watoto wao mitazamo hiyo.  Sasa kwa vile Afro-Shirazi walikuwa wengi zaidi, tuliamini kwamba CCM ni wengi zaidi pia.  Na matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu ya CCM kupitia Rais Karume kupata ushindi wa asilimia 53.2 yamethibitisha usahihi wa utabiri wetu.

 

Swali:      Ndugu Katibu wa Itikadi na Uenezi, wakati nyinyi CCM mnafurahia ushindi wenu, Seif Sharrif Hamad alijitangazia ushindi wa asilimia 61 usiku wa tarehe 30 Oktoba, 2005 na kusababisha maandamano ya kusherehekea ushindi huo yaliyofanywa na baadhi ya wafuasi wa CUF mjini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba, 2005.  Aidha, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza rasmi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar vilionekana vipeperushi mjini Dar es Salaam vikionyesha kwamba Seif Sharrif Hamad alipata ushindi wa asilimia 50.63 na Ndugu Karume alipata asilimia 49.37 tu.  Unawaambia nini wananchi kuhusu madai haya?

 

Jibu:        Madai hayo yote ni upuuzi na ubabaishaji mtupu.  Kwanza kabisa, kwa mujibu wa sheria za nchi, chombo pekee chenye mamlaka ya kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani Zanzibar ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.  Kwa hivyo kitendo cha Maalim Seif kutangaza matokeo yake na kujitangaza mshindi kilikuwa cha kukiuka sheria na hivyo kilikuwa haramu.  Kwa hivyo na matokeo yenyewe aliyoyatangaza yalikuwa haramu.  Pia ni dhahiri kabisa matokeo hayo hayakuwa sahihi.  Tukianza na yale matokeo ya awali aliyoyatangaza Maalim Seif tarehe 30 Oktoba, 2005.  Matokeo hayo yalitangazwa wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea. La kujiuliza hapa ni Maalim Seif aliyapata wapi matokeo hayo kama si kuyabuni tu?  Na alifanya hivyo kwa makusudi kujenga mazingira ya kukataa matokeo sahihi na halali baada ya  kutangazwa rasmi na Tume ya Uchaguzi kama yangeonyesha kuwa ameshindwa, kwa madai ya kubuni kuwa ameibiwa kura au amenyang’anywa ushindi.  Aidha, yalikuwa pia maandalizi ya vurugu kwani alijua kuwa akishawajenga watu wake na hisia za ushindi wasingekubali matokeo ambayo yangeonyesha kuwa wameshindwa, na hivyo, kujiingiza katika vurugu.  Na hivyo ndivyo ilivyotokea.  Huu umekuwa mtindo wa kawaida wa Maalim Seif ambao aliutumia mwaka 1995 na hata 2000.

 

Kwa yale  matokeo waliyoyatoa kwa vipeperushi baada ya matokeo rasmi kutangazwa na Tume, CUF walidhihirisha kutapatapa kwao pale waliposahau kuwa safari ni wagombea sita ndio walioshiriki uchaguzi wa Rais, na siyo mawili tu.  Kwa mujibu wa matokeo hayo, Maalim Seif eti alipata ushindi wa asilimia 50.63 na Rais Karume eti asilimia 49.37.  Ukijumlisha tarakimu hizi unatapata asilimia 100.  Inafaa CUF waulizwe, je wale wagombea wengine wanne wa vyama vya Jahari Asilia, DP, NRA na SAU hawakupata hata kura moja?  Inadhihirisha wazi wazi kuwa takwimu zote hizo ni za kubuni.  Zaidi ya  hivyo, kitendo chenyewe cha kutangaza matokeo  mawili yaliyo tofauti kinadhihirisha kutapatapa kwa Maalim Seif na CUF yake na kinawashushia hadhi na kuwa kuwafanya wasiaminike.

 

Swali:      Ndugu Mapuri uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka huu umeshuhudiwa na waangalizi wengi mno wa kimataifa na wa ndani isivyokuwa kawaida.  Ulipoahirishwa uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano, hata waangalizi wa kimataifa  waliokuwa awali wamepangiwa maeneo ya Bara walikwenda Zanzibar.  Aidha, tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi mbili zilizopita  za miaka ya 1995 na 2000, safari hii vikundi vingi vya waangalizi vimeutangaza uchaguzi wa mwaka huu kuwa ulikuwa huru na wa haki.  Hata hivyo, vipo vikundi vichache ambavyo bado vinasita kutamka kama uchaguzi ulikuwa huru na wa haki mpaka mamlaka husika zifanye uchunguzi juu ya dosari  vinavyodai kuziona vikundi hivyo ili kuondoa shaka.  Nini tathmini na maoni yako kuhusu hali hii?

 

Jibu:        Kimsingi mtazamo wangu ni kwamba kwa uchaguzi wetu kuwa huru na wa haki, si lazima upate baraka za waangalizi wa kimataifa au wa ndani.  Mimi niliziona chaguzi za 1995 na 2000 kuwa huru na za haki pamoja na kwamba waangalizi wengi walikuwa na mawazo tofauti.  Hata hivyo, lazima nikiri kwamba nimefarijika sana kuwa wengi wa waangalizi waliotazama uchaguzi wetu mwaka huu wameuona kuwa huru na wa haki.  Jambo moja limenibainikia.  Nalo ni kwamba makundi makubwa ya waangalizi yaliyokuwa na mitandao mipana iliyoenea nchi nzima ndiyo yaliyotoa tathmini ya kuaminika ya upeo wa nchi nzima.   Makundi hayo aghlabu ndiyo yaliyouona uchaguzi wa mwaka huu kwa ujumla wake kuwa ulikuwa mzuri, huru na wa haki, pamoja na kuwapo kwa dosari ndogo ndogo za hapa na pale.  Mifano ya makundi kama hayo ya waangalizi ni yale ya SADC, Jumuiya ya Madola, TEMCO, EISA, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Nchi Huru za Afrika na kundi la waangalizi lililowakilisha makanisa mbalimbali ya Afrika.  Kwa upande mwingine, ni vikundi vidogo vidogo vya waangalizi vilivyokuwa na mitandao finyu ndivyo vinavyoonekana kuwa na shaka juu ya hadhi ya uchaguzi huo kuwa ulikuwa huru na wa haki.  Hii inaelekea ni kwa sababu tathmini za vikundi kama hivyo zilijengwa juu ya msingi wa viliyoyaona katika eneo dogo tu, hususani la Mji Mkongwe na kuzifanya tathmini hizo zionekane kana kwamba ni za nchi nzima.  Lakini Mji Mkongwe ni jimbo moja tu kati ya majimbo 50 yaliyofanya uchaguzi.  Aidha, hata katika hilo jimbo la Mji Mkongwe, ni vituo vitatu tu ndivyo viliyvoripotiwa sana kukumbwa na hizo dosari zinazotajwa katika ripoti za waangalizi na kupigiwa chapuo na vyombo vya habari hasa vile vya nje.  Vituo hivyo ni Kiwanda cha Madawa, Forodhani na Bwawani ambavyo ni kati ya jumla ya vituo 1,617 vilivyokuwapo nchi nzima.  Kwa hivyo si sahihi, si haki na ni upotoshaji mkubwa kuzikuza dosari ndogo ndogo zilizoonekana katika eneo dogo sana kama hilo na kuzifanya zionekane kuwa ni za nchi nzima.  Lakini naamini pia kwamba miongoni mwa hao waangalizi wanaosita kutamka kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, wapo waliokuja na mitazamo ya jumla kwamba uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki Barani Afrika kama haukiondoi madarakani chama tawala hasa kama ndicho kilichopigania uhuru na kuung’oa ukoloni.

 

Swali:      Ndugu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM miongoni mwa dosari zilizotajwa sana katika ripoti za waangalizi na kutangazwa sana na vyombo vya habari hasa vya nje, ni kwamba ulinzi ulikuwa mkali mno kiasi cha kuwatisha wapiga kura.  Wewe mwenyewe ulikuwako Zanzibar siku ya uchaguzi.  Hili unalielezea vipi?

 

Jibu:        Mimi Ndugu Mtangazaji naliona dai hili la watu kutishika na ulinzi uliokuwapo kuwa ni upuuzi mtupu.  Kama wapiga kura wangetishika kweli wasingejitokeza kwa wingi wa kiwango cha zaidi ya asilimia 90 ambacho ni adimu kufikiwa hasa katika hizo nchi za Magharibi zinazojifanya kuwa walimu wa demokrasia.  Ukweli ni kwamba ulinzi mkali uliokuwepo ambao ulikwishaahidiwa kabla na Serikali, ulikuwa faraja kwa wapiga kura waliokuwa wametishwa sana na viongozi na wafuasi wa CUF wakati wa kampeni.  Ni ulinzi huo ambao uliwahakikishia usalama wao ndio uliowapa imani wapiga kura kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kwa uhuru.  Ulinzi ulioonekana kuwa mkali sana katika eneo la Mji Mkongwe mnamo nyakati za jioni, ulikuwa umeimarishwa baada ya kuongezeka kwa matukio ya kupigwa watu (hususan waliodhaniwa kuwa ni wana CCM) na kuondolewa kwenye mistari ya kwenda kupiga kura.  Kama matukio hayo yangeachiwa kuendelea, ilikuwapo hatari ya uchaguzi kuvurugika kweli katika jimbo hilo.

 

Swali:      Dosari nyingine iliyotajwa na Seif Sharrif Hamad ni kuwa wapiga kura zaidi ya 80,000 walizuiliwa kupiga kura kutokana na kutoonekana majina yao kwenye dafari la wapiga kura.  Hii nayo unaielezea vipi?

 

Jibu:        Hili nalo dhahiri ni dai la kubuni.  Kwa bahati nzuri hata Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kupitia Tamko lake la tarehe 5 Novemba, 2005 lilimsahihisha Maalim Seif kwa kiasi fulani.  Katika Tamko hilo, CUF inadai kuwa ni watu 47,000 ndio eti waliozuiliwa kupiga kura.  Lakini ukweli kwa mujibu wa takwimu rasmi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni kwamba kati ya watu 507,225 waliothibitishwa kuwa wapiga kura halali baada ya uhakiki wa daftari la kudumu la wapiga kura, 460,581 sawa na asilimia 90.8 walipiga kura zao.  Ni watu 46,644 tu (au 47,000 kama walivyotajwa na CUF katika Tamko lao) ndio ambao hawakupiga kura.  Lakini hata hao, haiwezekani kuwa wote hawakupiga kura kwa sababu ya kuzuiliwa kutokana na kutoonekana majina yao katika daftari au kuwa wote ni wafuasi wa CUF.  Wapo waliokwishafariki dunia, wapo waliokuwa safarini nje ya nchi na wapo wengi wengine waliokuwa na dharura mbali mbali zilizowafanya washindwe kwenda vituoni kupiga kura. Hakuna uchaguzi popote duniani ambao wote waliojiandikisha wanapiga kura.  Uhakika ni kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilikuwa imetoa taarifa mapema kabla ya siku ya uchaguzi kwamba watu 2,007 waliondolewa katika daftari wakati wa uhakiki wa mwisho kutokana na kubainika kuwa walijiandikisha zaidi ya mara moja.  Naamini ni miongoni mwa hawa ndio waliokwenda vituoni na kugundua kuwa majina yao hayakuwamo kwenye daftari.  Siyo watu 80,000 aliodai Maalim Seif.  Watu 80,000 ni wengi mno kwa mazingira ya Zanzibar kiasi kwamba kama wote wangekwenda vituoni na majina yasionekane, kungekuwa na fadhaa kubwa vituoni ambayo ingeathiri zoezi lote la upigaji kura.

 

Swali:      Kuna madai pia kwamba watu wengi wakiwemo maaskari walipiga kura zaidi ya mara moja.  Unasemaje kuhusu hili?

 

Jibu:         Hata dai hilo nina matatizo nalo kwani maelezo yote kuhusiana nalo hayajathibitishwa angalau hata kwa mfano mmoja halisi wa mtu aliyekamatwa au angalau wa jitihada za kusaidia vyombo vya dola vimkamate na kumfikisha mbele ya sheria.  Dai hili si cho chote zaidi ya uvumi na simulizi za kufikirika.

 

Swali:      Ndugu Mapuri tupe maoni yako kuhusu madai mengine ya CUF na baadhi ya waangalizi kwamba fomu za matokeo hazikupelekwa katika baadhi ya vituo na kwamba matokeo hayakubandikwa vituoni.

 

Jibu:        Swali hili linapaswa kujibiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.  Lakini niliwahi kumsikia Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mzee Masauni Yussuf akihojiwa na BBC ambapo alizikanusha tuhuma zote hizo.  Lakini mimi nawastaajabu hawa CUF.  Upande mmoja wanasema hawakupewa fomu za matokeo lakini wakati huo huo wanajitangaza washindi. Huu tuuiteje kama si unafiki?

 

Swali:      Zimeelezewa pia fujo nyingi kutokea katika maeneo ya Darajani, Mtendeni na maeneo kadha ya Kaskazini Pemba ambako wameuawa watu wawili – mmoja raia na mwingine askari.  Kwa maoni yako huoni kama fujo hizo ziliingilia zoezi la uchaguzi?

 

 

Jibu:        Ni kweli zilitokea vurugu za hapa na pale katika maeneo hayo zilizosababishwa na wafuasi wa CUF ama wakishangilia ushindi hewa au wakipinga matokeo yaliyotangazwa na Tume.  Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuzidhibiti fujo hizo kabla ya kuleta madhara makubwa zaidi.  Lakini kwa kujibu swali lako, fujo na vurugu zote hizo zilitokea baada ya zoezi lote la uchaguzi kukamilika.  Kwa hivyo hazikuathiri kwa aina yo yote mwenendo wa zoezi la uchaguzi.

 

Swali:      Ndugu Katibu wa Itikadi na Uenezi huoni kama wingi wa dosari zilizotajwa unaweza kuwa umeathiri uchaguzi mzima na hivyo hata matokeo yake?

 

Jibu:        Katika suala hili, wingi si hoja.  Hoja ni usahihi na uzito wa dosari zenyewe.  Lakini kama nilivyojibu kuhusu dosari moja moja, mimi naziona nyingi ya dosari zinazotajwa kuwa si za kweli na chache zenye ukweli fulani hazina msingi wala uzito wo wote wa kuathiri matokeo ya uchaguzi.  Katika hatua hii ningependa kuelezea masikitiko yangu kwa kundi la waangalizi la NDI la Marekani kusita kutamka kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa huru na wa haki.  Nasikitika kwa sababu wote tunajua yaliyotokea katika uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka 2000, hasa katika Jimbo la Florida.  Uchaguzi huo ulikumbwa na madosari makubwa na ya msingi ambapo hata mashine za kuhesabia kura zilishindwa na ikabidi itumike mikono.  Tulisikia mabunda ya kura zilizokuwa zimefichwa vyooni.  Mimi naamini kwamba dosari zilizoukumba uchaguzi huo katika Jimbo la Florida zilikuwa kubwa zaidi kuliko za Mji Mkongwe.  Isitoshe, matokeo ya Florida yalikuwa na taathira kubwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi mzima wa Marekani kwani hatimaye ndiyo yaliyoamua mshindi.  Lakini yale ya Mji Mkongwe hayakuwa na taathira ya kiasi hicho kwani hata kama kura zote halali 9,485 zilizopigwa katika jimbo hilo angepewa Maalim Seif, bado matokeo yangebaki yale yale ya Rais Karume kuwa mshindi.  Kama NDI waliuona uchaguzi wa Marekani kuwa huru na wa haki pamoja na mazonge yote ya Florida, iweje wauone wetu si huru na wa haki kama hawana agenda ya siri?  Nimesoma makala kwenye gazeti la Uhuru la leo tarehe 10 Novemba, 2005 inayoonyesha kwamba hata uchaguzi wa 2004 wa Marekani ulikumbwa na dosari nyingi, lakini hatusikii lugha ya kuutilia shaka.

 

Swali:      Ndugu Mapuri nini mtazamo wako kuhusu uamuzi wa CUF kuyakataa matokeo ya Urais lakini kuyakubali yale ya Uwakilishi na Udiwani?

 

Jibu:        Ni dalili ya kuchanganyikiwa.  Niliwahi kuwasikia hata baadhi ya wafuasi wa CUF wakisema kuwa hawawaelewi viongozi wao kwa uamuzi huo.  Hata mimi siwaelewi. Chaguzi za Urais, Uwakilishi na Udiwani zilifanywa wakati mmoja, katika mazingira yale yale na wapiga kura walioshiriki ni wale wale.  Kama kweli wanaamini kuwa uchaguzi mzima ulivurugika, vipi iwe kwa Urais tu?  Hususani tutazame jimbo la Mji Mkongwe ambalo ndilo linasemwa sana kukumbwa na dosari.  Kama dosari hizo hazikuathiri matokeo ya Uwakilishi, iweje ziathiri ya Urais?  Mimi ningewaelewa kama wangeyakataa kwanza matokeo ya Uwakilishi na Udiwani kabla ya kuyakataa ya Urais.  Kwa sababu hawakufanya hivyo, ni dhahiri kwamba wameyakataa matokeo ya Urais kwa shinikizo tu la Maalim Seif ambaye kwake hulka ya kukataa kushindwa imekwishaota mizizi.  Napenda kuwashauri CUF waanze kukomaa kisiasa.  Wapone uchungu wa kushindwa na wautazame upya uamuzi wao wa kuyakataa matokeo ya uchaguzi wa Urais kwa manufaa ya Taifa.  Napenda kuwakumbusha kwamba katika Muafaka, walipewa karibu kila kitu walichokitaka.  Mifano ni daftari la kudumu la wapiga kura, kushirikishwa katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi, na kushirikishwa kupitia Tume ya Muafaka katika marekebisho ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi na sheria nyingine mbali mbali.  Watanzania wamechoshwa na hulka ya kukataa kushindwa.

 

 

Swali:      Mwisho, uchaguzi wa Zanzibar umekwisha na washindi wamepatikana ambao ni CCM.  Nini matarajio yako na ya CCM kuhusu uchaguzi mkuu ujao wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani wa Bara?

 

Jibu:        Matarajio yetu ni ushindi tu, tena mkubwa sana wa kishindo.  Ushindi wetu wa Zanzibar umezidi kutufyagilia njia yetu ya ushindi katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 14 Disemba, 2005.  Naamini Watanzania hawatopenda kuharibu kura zao kwa kuwapigia wapinzani ambao ni hakika watashindwa vibaya sana.  Kwa nini ujiunge na kambi ya washindwa wakati ya washindi ipo?