MKUTANO MKUU WA CCM 2006
HOTUBA YA MWENYEKITI YA KUNG’ATUKA NA KUAGA CHIMWAGA
25 JUNI, 2006
Waheshimiwa Makamu wa Mwenyekiti,
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tz,
Mheshimiwa Mwenyekiti na Rais Mstaafu,
Mheshimiwa Katibu Mkuu,
Mheshimiwa Katibu Mkuu na Waziri Mkuu Mstaafu,
Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Kuu,
Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu,
Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu,
Waheshimiwa Waasisi na Wazee wa Chama,
Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Salaam Aleikum!
Awali ya yote
napenda kujumuika nanyi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa
kutujalia afya njema na kutukutanisha hapa leo hii. Binafsi sina budi nitoe
shukurani nyingi sana kwa wingi wa fadhila na upendo wake ambao umeniwezesha
kuhitimisha miaka kumi ya kuongoza dola na sasa Chama Cha Mapinduzi, kwa amani
na usalama. Mwenyezi Mungu atuongezee baraka zake, abariki mkutano wetu, na
aendelee kuibariki nchi yetu, Amin.
Kwa Nini Nang’atuka
Ndugu Wajumbe:
Huu ni Mkutano Mkuu wa kwanza tangu nihitimishe kazi
mliyonipa mwaka 1995 ya kuongoza nchi yetu katika mkutano kama huo. Bado nakumbuka sana siku ile hapa Chimwaga
nilipochaguliwa kuwa mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi. Leo narudia shukrani
zangu kwa Chama changu kwa imani kubwa mliyonipa, na ushirikiano mkubwa
mlionipa tangu wakati wa kampeni za 1995 na zile za 2000. Aidha narudia
shukrani zangu kwa wote waliojitokeza kugombea Urais mwaka 1995, hususan wale
watatu tuliofika hapa Chimwaga kwenye fainali ya mbio za kutafuta kuteuliwa na
Chama Cha Mapinduzi. Ahsante sana, tena sana, Mheshimiwa Cleopa David Msuya na
Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Wale mliokuwa hapa mwaka 1995 mtakumbuka
mazingira ya uchaguzi ule. Lakini mtakumbuka pia hotuba aliyoitoa Mheshimiwa
Kikwete siku ile. Ilihitaji ujasiri mkubwa kutoa hotuba kama ile. Ilihitaji
uwezo mkubwa wa kudhibiti hisia za kibinadamu. Ilihitaji busara na upendo
mkubwa kwa Chama. Ilihitaji uwezo mkubwa wa kufikiri na kushawishi waliokuwa
wakimuunga mkono wakubali matokeo ya kura na waniunge mkono. Na nyote ni mashahidi
kuwa alitimiza ahadi zake alizozitoa siku ile hapa Chimwaga. Zote hizo ni sifa
muhimu za kiongozi, ambazo nyote mtakuwa tayari mmeziona kwenye uongozi wake wa
Taifa katika miezi sita iliyopita. Kwa hakika hatukukosea. Narudia. Nani kama
CCM?
Naona fahari kubwa zaidi kumwachia Rais Kikwete uongozi
wa Taifa. Sina wasiwasi hata kidogo. Na leo naona fahari kubwa zaidi na sina
wasiwasi kumwachia uongozi wa Chama Cha Mapinduzi ninapowaomba mridhie
mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Ndugu Wajumbe:
Chama Cha Mapinduzi kina utaratibu mzuri wa kupishana
uongozi wa Serikali na uongozi wa Chama. Utaratibu huu pia unamwezesha Rais
anayeondoka madarakani kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Chama kwa miaka miwili
baada ya kuacha Urais. Utaratibu huu unampa nafasi Rais mpya kuunda Serikali na
kuweka vipaumbele vyake bila wakati huo huo kubeba mzigo wa Uenyekiti wa Chama.
Lakini ni vema
mapema iwezekanavyo, akishaunda Serikali na kuweka vipaumbele vyake,
tumkabidhi pia Uenyekiti wa Chama ili mikono yake isifungwe na kasi yake
isipunguzwe, anapotekeleza kazi za Serikali kwa niaba ya Chama.
Mimi ninaridhika
kabisa kuwa wakati wa kumuachia Rais Jakaya Mrisho Kikwete Uenyekiti wa Chama
sasa umefika. Nimeshauriana naye. Yuko tayari, kama ilivyokuwa maisha yake
yote, kukitumikia Chama. Kwa uzoefu wake na uwezo wake mkubwa sina shaka
ametosha kabisa kuwa Mwenyekiti wetu. Naomba Ndugu Wajumbe leo mkubali kwa
kauli moja ya kishindo mapendekezo kwenu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kumchagua
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete awe Mwenyekiti wetu.
Nawashukuru sana wenzangu kwenye Kamati Kuu na kwenye
Halmashauri ya Taifa kwa kunikubalia ning'atuke Uenyekiti kabla ya muda wangu
kikatiba kwisha. Si wote walinikubalia
kwa urahisi, lakini baada ya kusikia hoja zangu na rai yangu wote kwa kauli
moja walikubali. Nataka nanyi mjue sababu nyingine, zaidi ya hizi nilizozitaja
hivi punde, zilizonifanya nifikie uamuzi huu wa kung’atuka.
Ndugu Wajumbe:
Ninazo sababu tano za nyongeza kwa nini nimefikia uamuzi
huu ambazo ni vema ninyi, wanachama wenzetu, na wananchi kwa ujumla, wakazijua:
5. Na mwisho, lakini
muhimu sana, ni kuwa tangu nimeacha uongozi wa Serikali nimepewa majukumu mengi
sana ya kimataifa yanayonichukulia muda mwingi sana kiasi kwamba nahisi
sitakitendea Chama changu haki nikiendelea kuwa Mwenyekiti hasa kwa kuzingatia
kuwa wa kurithi kazi hiyo ya Chama yupo na anazo sifa za kutosha. Kwa wale
ambao hamjui, miongoni mwa mambo mengine, mimi ni Mwenyekiti Mwenza wa Mfuko wa
Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji Barani Afrika. Mimi ni mjumbe wa Tume iliyoundwa
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kuhuisha kazi za Umoja huo kwenye maeneo ya
maendeleo, haki za binadamu, na mazingira, na tunatakiwa kukamilisha kazi hiyo
kabla ya mwezi Septemba mwaka huu. Kwa kuwa wapo walio hodari wa kuzua hisia
potofu ni vizuri niweke wazi kuwa ushiriki wangu katika Tume hizi hauna
mshahara wala mrahaba!! Ni kazi ya
kujitolea. Mimi ni mjumbe wa Tume ya
Kimataifa kuhusu Uwezeshaji Wanyonge Kisheria, yaani MKURABITA ngazi ya
kimataifa. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kuangalia Hatma ya
Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD). Mimi ni
Mwanachama wa Chama kinachoitwa Club of
Madrid ambacho ni Chama kinachowakusanya baadhi ya viongozi wanaoheshimika,
waliochaguliwa kidemokrasia na kuondoka madarakani kidemokrasia, walio tayari
kutumia uzoefu wao kwa manufaa ya dunia yetu, ambayo kwa kweli ni sifa kwa
Chama chetu. Katika mazingira haya naamini nitakitendea Chama changu haki zaidi
kwa kumkabidhi Rais wetu Uenyekiti, na ninaomba mridhie iwe hivyo leo.
Ndugu Wajumbe:
Leo tumekutana tena hapa Chimwaga kuimarisha sifa nzuri
na historia ya kutukuka ya Chama Cha Mapinduzi; historia, kwa ridhaa yenu, ya
uongozi mithili ya mbio za vijiti, uongozi wa kupishana kwa upendo, si kwa
chuki; uongozi wa kupishana kwa bashasha, si kwa kununa; uongozi wa kupishana
kwa maelewano si kwa mafarakano; uongozi wa kupishana kwa heshima na taadhima,
si kwa mizengwe na nongwa. Wanaongojea na wanaotamani hali iwe tofauti
watangoja sana. Tuazimie basi kuwa waendelee kusubiri hivyo daima.
Juzi juzi hapa nilisoma gazetini makala moja ya mahojiano
na Waziri Mkuu mstaafu, Mzee Cleopa David Msuya ambapo, pamoja na mambo
mengine, aliwahakikishia wananchi kuwa CCM inaendelea kuwa moja baada ya
Uchaguzi Mkuu wa 2005. Napenda nirejee kauli yake ninapohitimisha Uenyekiti
wangu wa Chama. Kwa hakika ningesononeka na kusikitika sana kama ningeacha
Uenyekiti wakati Chama kimegawanyika. Na
namshukuru sana kwa kuelezea, kwa uaminifu na haki, mazingira ya kazi na
mafanikio ya serikali zote za CCM toka Uhuru.
Chama Cha Mapinduzi bado ni imara sana, bado ni kimoja.
Ni kweli, kama ilivyo kwa vyama vya siasa kote duniani, yanaweza kuwepo mawazo
tofauti miongoni mwa viongozi na/au wanachama. Utasikia wapo wenye mrengo wa
kulia, wapo wenye mrengo wa kati, na wapo wenye mrengo wa kushoto. Siku hizi
wapo pia wenye mrengo wa kushoto kwa kati, na wengine kulia kwa kati. Ni jambo
la kawaida.
Hatuwezi, na ni
makosa makubwa, kudhani kuwa tutakuwa na Chama au Serikali ambapo watu wote
wanafikiri sawa, wanasema sawa na wana maoni sawa kuhusu kila jambo. Hao
watakuwa ama hawafikirii, au ni wanafiki wakubwa wanaojipendekeza badala ya
kuchangia kwa uwazi kurutubisha sera, mwelekeo na utendaji kwenye Chama. Lakini
tusiruhusu tofauti za mawazo na mapendekezo ziwe sababu au chanzo cha Chama
kugawanyika. Kuhitilafiana, rukhsa; kugawanyika, marufuku. Na kweli ni wajibu
wetu wa kihistoria kuhakikisha mirengo na mawazo tofauti ndani ya Chama
inarutubisha mijadala na kupanua upeo wa hoja na misingi ya maamuzi, lakini
kamwe haiwi kiini au chanzo cha kugombana au kuchukiana.
La muhimu pia ni kujenga utayari kila upande wa
kujitahidi kuelewa na kuheshimu hoja za upande mwingine. Yatakuwa makosa
makubwa kumchukia mwenzako kwa vile tu anayo maoni tofauti nawe. Ndio maana
nasema wanaoona tofauti ya maoni miongoni mwetu wasidanganyike wakafikiri huo
ni mwanzo wa mpasuko wa CCM. Si kweli;
na wala tusiwape faida hiyo. Wao, pamoja na sisi tukubali hiyo kama ushahidi na
kama sehemu muhimu ya demokrasia ndani ya Chama. Lakini sisi wenye Chama tunao pia wajibu mkubwa wa
kuwahakikishia wanachama na wananchi kuwa hatutaruhusu tofauti za maoni
zitupeleke katika kudhoofisha Chama. Na Baba wa Taifa alituasa: Bila CCM
madhubuti, nchi itayumba. Na wananchi wengi nao wanajua hivyo, na waiangalia
CCM kwa makini sana.
Chama cha Mapinduzi na Mageuzi ya Kisiasa
Ndugu Wajumbe;
Chama chetu kina
viongozi; lakini si Chama cha
Viongozi! Chama chetu ni cha Wanachama wake. Wanachama wake ndiyo
wahimili wakuu wa CCM. Nachukua fursa hii basi kuwashukuru wanachama wote wa CCM kwa vile
walivyoimarisha Chama chetu na kukifikisha kilele cha kupigiwa mfano katika
nchi za SADC. Ndugu wanachama, Asanteni sana.
Ndugu Wajumbe,
Ninapong’atuka
naamini ni wakati mwafaka vile vile tujikumbushe na kutafakari mnasaba wa Chama
chetu ili tuandike vizuri historia yetu na tuimarishe mwelekeo wetu. Chama
chetu kiliundwa kiwe na sifa na sura gani? Kiliundwa kiwe Chama cha Ukombozi
cha Wakulima na Wafanyakazi. Azimio la Mkutano Mkuu wa Pamoja wa TANU na ASP wa
l977 uliounda CCM ulitamka hivi:
“Chama tunachokiunda
tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na
vitendo vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji
nchini, na kupambana na jaribio lolote lile la mtu kumuonea mtu au shirika au
chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au
kuzorotesha maendeleo ya Taifa;
Chama tunachokiunda tunataka
kishike barabara hatamu za uongozi wa shughuli zote za umma kwa maslahi ya
wafanyakazi na wakulima wa Taifa letu,
Chama tunachokiunda tunataka
kiwe kiungo kati ya wanamapinduzi wa Tanzania na wanamapinduzi wenzetu kokote
waliko.”
Nashukuru
kwamba Chama kinaendelea kuwa na hulka hiyo. Wananchi wana Imani na CCM.
Ndugu Wajumbe,
Wapo wanaotuhumu kwamba
tumewasaliti waasisi wa Chama chetu na kuwa tumekiuka maslahi ya wananchi wetu.
Matokeo ya Chaguzi Kuu tatu zilizopita katika mfumo wa vyama vingi yanawaumbua na kuwaadhiri. Katika
chaguzi hizo zote CCM ilipata ushindi mkubwa. Tukumbushane.
Mwaka l995 mgombea
Urais kwa tiketi ya CCM alipata ushindi wa 62% ya kura dhidi ya wapinzani
watatu wa vyama vingine. Wagombea Ubunge kwa tiketi ya CCM walipata ushindi wa
viti 214 dhidi ya 45 vya wapinzani wa vyama vingine. Mwaka 2000 mgombea Urais
kwa tiketi ya CCM alipata ushindi wa 72% ya kura dhidi ya wapinzani wa vyama
vingine watatu. Wagombea Ubunge kwa tiketi ya CCM walipata ushindi wa viti 258
dhidi ya viti 37 walivyopata wagombea ubunge wa vyama vingine. Mwaka jana,
2005, mgombea Urais kwa tiketi ya CCM alipata ushindi was 82% ya kura dhidi ya
wapinzani tisa wa vyama vingine. Wagombea Ubunge nao walipata ushindi wa viti
275 dhidi ya viti 44 walivyopata wagombea ubunge wa vyama vingine!!
Kadhalika katika Chaguzi za Zanzibar, ule wa mwaka 1995,
mgombea Urais kwa tiketi ya CCM alipata ushindi wa 50.24% ya kura, na katika
Baraza la wawakilishi wagombea wa CCM walipata viti 26 dhidi ya 24 za
wapinzani. Mwaka wa 2000, mgombea Urais
kwa tiketi ya CCM alipata ushindi wa 67% ya kura dhidi ya 33% za mpinzani wake,
na katika Baraza wagombea wa CCM walipata viti 34 dhidi ya 16 za
wapinzani. Na mwaka 2005 mgombea wa
Urais alipata 53% dhidi ya 47 za wapinzani wake, na katika Baraza, wagombea wa
CCM walipata viti 30 dhidi ya 19 za wapinzani.
Huu ni ushindi wa chaguzi tatu mfululizo na wa kujivunia.
Wananchi wa Tanzania, Wakulima na
Wafanyakazi wa Tanzania, si lofa, si mbumbumbu, si wajinga, si bubu. Kwa
matokeo haya ya ushindi mkubwa wametamka kwa kishindo imani yao kwa Chama Cha
Mapinduzi na Uwezo mkubwa wa Viongozi wa Serikali zake. Wafanyakazi wa mijini
na wakulima wa vijijini wameweka bayana rekodi ya imani yao kwa sera na
utekelezaji wa Chama Cha Mapinduzi. Tumepoteza dira ya Chama? Hapana!!
Jana tulipokea na
kujadili Taarifa za Chama na Serikali zake. Maudhui ya taarifa hizo yametoa
ushahidi tosha kwamba Chama chetu ni madhubuti na viongozi wa serikali zake
wana upeo mkubwa wa utekelezaji. Wanaotaka uthibitisho zaidi kwamba
hatukulegeza kamba au kupoteza dira ya Chama, nawaomba wapitie tena Ilani ya
Uchaguzi wa mwaka jana ya Chama Chetu. Ilani hiyo inashinda zile za vyama
vingine vyote vilivyoshiriki katika uchaguzi. Ina tathmini kamili ya hali
halisi ya nchi na dunia katika nyanja mbali mbali, na hasa hasa kisiasa na
kiuchumi. Imeainisha kwa kina malengo ya maendeleo ya miaka mitano ijayo na
mikakati ya kuyafikia.. Ni ilani ya pekee ambayo maandalizi yake yalishirikisha
kikamilifu wabia wote wa maendelo ya nchi na makundi makubwa yote ya jamii. Ye
yote anayefanya mapitio ya ilani hiyo atazinduka na kukiri kwamba, kwa kigezo
cha ushupavu, umakini, umahiri na uadilifu katika kuyakabili matatizo ya
maendeleo ya nchi, CCM ndicho chama kinachoweza kutoa timu thabiti na murua ya
kuongoza nchi!! Kilichobaki kwangu ni kurejea na kusisitiza kauli mbiu ya Ilani
hiyo kama ilivyo katika Ibara ya 9, uk 9 wa Ilani hiyo: Twendeni basi tukaendeleze kazi ya kukuza uchumi na kupambana na
umaskini kwa “ari mpya, nguvu mpya na
kasi mpya”!!
Ilani
imezingatia Dira ya Taifa
Ndugu Wajumbe,
Narudia.
Hatukupoteza dira. Tukumbushane. Tulipokaribia kuanza karne ya 21, tuliona
umuhimu wa kutafakari changamoto la maendeleo katika karne mpya. Matokeo ya
tafakuri hiyo ni Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025. Nawaomba wajumbe muipitie tena dira hiyo. Mkifanya hivyo
mtaona kwamba katika hoja ya Utaifa na maendeleo ya watu wake hatujapoteza
mwelekeo wala kulegeza kamba.
Dira ya Maendeleo
imetutahadharisha kuwa karne hii itakuwa
ya ushindani mkali, na itatawaliwa na wale wenye uwezo mkubwa kiteknolojia,
tija kubwa katika uzalishaji, miundombinu imara na ya kisasa ya mawasiliano na
uchukuzi na, zaidi ya yote, nguvu kazi yenye ustadi mkubwa na hulka ya
kujituma. Inabainisha jinsi ya kuamsha, kuunganisha na kuelekeza juhudi na
fikra zetu na raslimali za Taifa letu katika maeneo ya msingi ili kufikia
malengo ya maendeleo yaliyoainishwa na kustahimili ushindani huo mkubwa.
Tulipoiandaa,
tulishirikisha na kupata maoni na ridhaa ya wananchi wengi, kutoka sehemu zote
za jamii:- waheshimiwa Wabunge, vyama vyote vya siasa, viongozi wa madhehebu
mbali mbali ya dini, jumuiya za akina mama na vijana, vyama vya wafanyabiashara
na wenye viwanda, wakulima, wasomi, watu mashuhuri katika historia ya nchi yetu
na wananchi wa kawaida. Dira inaelewesha vyema tulikotoka, tulipo na kule
tuendako. Inaelezea sifa za nchi yetu zinazotarajiwa kuwepo ifikapo mwaka 2025
ikiwa ni pamoja na wananchi kuwa na maisha bora na mazuri; amani utulivu na
umoja; utawala na uongozi bora; jamii iliyoelimika na inayojituma katika
masuala ya maendeleo; na uchumi wenye uwezo wa ushindani na wenye ukuaji wa
kudumu kwa maslahi ya watu wote.
Ilani ya Uchaguzi ya
Chama chetu imezingatia vyema Dira ya Taifa ya Maendeleo na hivyo kudhihirisha
vilivyo kwamba CCM imebeba vizuri mamlaka ya kuwa Chama Tawala!! Chama gani
kama CCM? Hakuna!!!
Kujitegemea: Nyenzo Kuu ya Maendeleo
Ndugu Wajumbe,
Narudia.
Hatukupoteza dira ya Chama chetu. Nguzo Kuu ya falsafa yetu ya maendeleo ni
Kujitegemea. Baba wa Taifa alituasa: Uhuru na Kazi, na baadaye Uhuru ni
Kazi! Ubora wa sera zetu za uchumi na maendeleo ya jamii ulikuwa na mvuto
mkubwa kwa mataifa wahisani miaka ya 60 na 70. Matatizo ya uchumi wa dunia
yaliyofuatia, hususan kupaa kwa bei ya mafuta na kuporomoka kwa bei ya mazao
tunayouza nje ya nchi, kuliongezea utegemezi kwa wahisani. Lakini wakati wote
shabaha yetu imekuwa ile ile –
Kujitegemea na kupunguza hisani ya utegemezi. Miaka hii 10 tumejitahidi
kupunguza hisani hiyo katika bajeti ya Serikali, ikapungua toka 48% mpaka 42%.
Serikali ya Awamu ya Nne imeanza kwa kuamua kupunguza hisani hiyo kwa 3% zaidi
katika bajeti mpya. Ndugu Rais na Serikali yako tunawapongeza sana. Kwani kwa
mujibu wa falsafa ya maendeleo yetu, ukweli unabaki pale pale: Mtaji wa maskini
ni nguvu zake mwenyewe!
Ninaposema
haya sina maana ya kupuuza mchango wa wahisani wa kimataifa kwa maendeleo yetu. Sitaki kuwa mchoyo wa shukurani. Nashukuru sana kwa hisani tuliyopata ya
kufutiwa madeni na kuongezewa misaada katika miaka ya karibuni. Na ninaendelea kujenga hoja katika kamisheni
kadhaa za kimataifa, hoja ya mataifa kama letu kufutiwa madeni kabisa,
kuongezewa misaada, na kuandaliwa mfumo wa biashara wa kimataifa utakaozipa
bidhaa za nchi zao thamani na bei za haki zaidi. Maana ni vizuri pia kuipa hisani hii tafsiri
ya kiwango halisi cha matokeo yake.
Nitoe mfano.
Kwenye mkutano wa viongozi wa nchi tajiri na kubwa nane duaniani kule
Gleneagles, Scotland, mwaka jana, waliahidi kuiongeza misaada kwa $21 bilioni,
sawa na 37%. Lakini utafiti wa Shirika
lisilo la Kiserikali la Oxfam umeonyesha kwamba sehemu kubwa ya fedha ilitumika
kufutia madeni, na kwamba ongezeko halisi la misaada yao lilikuwa asilimia 9 tu
(9%)! Na mtaalamu mmoja wa Benki ya
Dunia ameeleza kuwa, kwa wastani, asilimia 70 (70%) ya misaada inatumika katika
nchi inayotoa misaada, kulipia ushauri na wataalamu!! Mtaji wa maskini kweli ni nguvu zake
mwenyewe.
Ndugu Wajumbe na
Watanzania kwa ujumla. Kwa miaka kadhaa
tumekuwa tunatumia kauli mbiu ya kuwa ili nchi iendelee inahitaji mambo manne:
(a)
Watu
(b)
Ardhi
(c)
Siasa Safi, na
(d)
Uongozi bora
Kutokana na mabadiliko na mfumo wa uchumi duniani ulivyo sasa hatuna
budi kusisitiza kuwa pia tunahitaji “mitaji” (mtaji)
Hayo yatatuwezesha kuwa na wimbi la baadaye la Watanzania tunaoendesha
na kumiliki uchumi wetu kwa mitaji yetu wenyewe. Nilipofunga majadiliano ya Taarifa za Chama
na Serikali niligusia kikao kilichopitisha mpango wa Utekelezaji wa Ilani wa
Kata ya Malindi, Lushoto, katika miaka 5 ijayo.
Lengo lililonivutia
Mshikamano na Vyama Rafiki
Ndugu Wajumbe,
Nimekumbusha kwamba Chama chetu kiliundwa kwa matarajio
kuwa kitakuwa “kiungo kati ya wanamapinduzi wa Tanzania na wanamapinduzi
wenzetu kokote waliko”. Dira hii ya
Chama nayo hatukuipoteza. Wengi wenu
mmeshuhudia jinsi wawakilishi wa vyama mbali mbali rafiki toka ndani na nje ya
bara letu, walivyohudhuria mikutano mikuu yetu yote. Tumeshirikiana na vyama rafiki kwa kufanya
ziara zilizowezesha kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kuimarisha vyama, kushinda
chaguzi na kufunza makada. Na kwa namna
ya pekee tumeimarisha uhusiano wetu na vyama vya Ukombozi wa Jumuiya ya SADC,
warithi wa vyama vilivyopigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika. Hatuna budi tuushupalie ushirikiano huu,
kwani Utandawazi si mtihani wa Kiuchumi tu; unaelekea pia kuwa mtihani wa
kisiasa unaotishia uhuru na umoja wa nchi hizo.
Ndugu Rais Kikwete umeamua kuvalia njuga mradi wa
Uandishi wa kuweka kumbukumbu sahihi historia ya ukombozi wa nchi zetu hizi za
SADC na kuuongezea kasi yake kwa hali na mali.
Mradi wa Utunzaji wa Kumbukumbuza Harakati za Ukombizi (Liberation
Heritage Project) ni mojawapo ya nyenzo muhimu kwa maendeleo yetu. Nakupongeza sana sana. Ni vema kabisa kwamba historia ya ukombozi
wetu iandikwe na sisi wenyewe badala ya kutegemea historia iliyo kasuku wa
waliotutawala.
Muungano wa Tanzania
Ndugu Wajumbe,
Kielelezo kikubwa cha Uhai wa Chama chetu ni Uendelevu wa
Muungano wetu. Muungano wa Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kuunda Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, uliasisiwa na vyama vya TANU na ASP, ambavyo baadaye vikaamua
kuungana na kuunda Chama Cha Mapidnuzi.
Ni dhahiri basi kuwa ustawi wa Muungano ni pima-joto ya uhai wa
CCM. Nawashukuru WanaCCM kwa ari yenu
kubwa ya kudumisha Muungano na kustawisha wananchi wake.
Kama Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka jana
ilivyobainisha: “Ushirikiano baina ya
pande mbili za Muungano umekuwa ukikua na maelewano baina ya serikali mbili na
hasa ya wananchi yanaimarika kila kukicha.
Ushirikiano wa kiuchumi na kijamii umeanza kuimarika na mfano mzuri wa
ushriikiano huo umedhihirika katika utekelezaji wa miradi ya TASAF katika
Jamhuri, Bara na Zanzibar”.
Hapana shaka kwamba katika mchakato wa ushirikiano kuna
kero kadhaa. Napongeza kwa dhati ari na
kasi mpya ambayo kwayo Serikali zetu sasa zimewania kushughulikia kero
hizo. Rai yangu ni kwamba wakati huo huo
tusichoke kuelezea, kutetea na kushangilia mafanikio ya Muungano. Mimi naamini kuwa katika mizani ya maendeleo
ya Muungano, mafanikio yanazidi kero zake.
Tumsaidie Rais na Mwenyekiti Mpya
Ndugu
Wajumbe,
Kwa usahihi mkubwa,
Rais wetu, Ndugu Kikwete, amefananisha mtiririko wa kumpata kiongozi wa mbio za
kijiti. Naamini kwa dhati kwamba huu ni wakati muafaka wa kumkabidhi yeye
kijiti cha uongozi wa Chama chetu. Katika chama chetu, kijiti hiki ni Mwenge.
Naamini pia kwamba niliupokea mwenge huo ukiwaka; sikuuzima; na ninaukabidhi
ukiwaka.
Ndugu Wajumbe:
Ombi langu kwenu leo ni kuwa tumsaidie sana Rais wetu
ambaye sasa atakuwa pia Mwenyekiti wetu wa CCM. Anayo kazi kubwa sana
tunayomtwisha. Tusikae pembeni na kumtazama. Tuwe naye bega kwa bega katika
kuimarisha Chama na kutekeleza sera na Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu. Nguvu
yake ni sisi, tukimwacha pekee tutakuwa tunahujumu juhudi zake na Chama chetu.
Na tusimtwishe mno matarajio yetu binafsi kwa uongozi wake. Nasema hivyo kwa
uzoefu wangu, na kwa vile ni jambo la kawaida kwa binadamu kuwa na mategemeo
fulani wakati yanapotokea mabadiliko ya uongozi. Yapo matarajio ya ngazi ya mtu binafsi. Yapo
pia matarajio ya Chama, na yale ya wananchi wengine na Taifa kwa jumla. Si rahisi kwa kiongozi kukidhi matarajio
binafsi ya kila mwanachama au kila kiongozi mwingine. Ahadi niliyotoa mimi
mliponichagua Mwenyekiti na ambayo natarajia ndiyo atakayoitoa Rais kwenu leo
ni kuwa atatumia uwezo wake wote kutimiza matarajio ya Chama na ya Taifa.
Shukrani
Ndugu Wajumbe:
Naomba nimalizie kwa kurudia kutoa shukrani. Miaka kumi iliyopita
hapa Chimwaga mlinichagua kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Leo, baada ya
haya niliyoyasema, sina la kuongeza ila kutoa shukrani zangu za dhati kwa
heshima kubwa mliyonipa, na kwa ushirikiano mlionipa katika miaka hiyo kumi
iliyopita. Kwa msaada wenu nimefanya nilichoweza kwa bidii zangu zote, na leo
nakabidhi kijiti kwa mkimbiaji mwingine wa CCM. Kama mlivyonisaidia naomba
ninyi na mimi tumsaidie na kushirikiana naye kwa upendo na kwa moyo mmoja.
Nawashukuru waasisi wa Chama chetu kwa kazi kubwa
waliyoifanya ya kuanzisha TANU na ASP, na hatimaye kuviunganisha na kuanzisha
CCM. Leo sisi tunasimama juu ya mabega yao, na tunajenga juu ya msingi imara
walioujenga.
Namshukuru sana Mwenyekiti aliyenitangulia, Mzee wetu Ali
Hassan Mwinyi kwa busara zake na kwa upendo wake kwangu. Namshukuru kwa
kuniachia Uenyekiti wa CCM mwaka 1996 kabla ya muda wake kikatiba kwisha.
Namshukuru kwa kunisaidia katika uongozi wangu. Sasa nami niko tayari kuungana
naye katika kumpenda na kumsaidia Mwenyekiti wetu mpya tukiwa wastaafu.
Nawashukuru sana Makamu Wenyeviti niliofanya kazi nao,
Mheshimiwa Dkt Salmin Amour, Mheshimiwa Dkt John Samwel Malecela na Mheshimiwa
Rais Amani Abeid Karume. Walinisaidia sana na tulifanya kazi za Chama pamoja
kwa maelewano na ushirikiano mkubwa. Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Dkt. Salmin, maarufu kama “Komandoo”,
ukomandoo wako daima umesisimua fikra juu ya saa zetu za ukombozi, ustawi wa
jamii na utawala wa haki na hivyo kuhuisha mustakabali wa Taifa. Nakushukuru sana.
Katika ushindani wa siasa ndani na nje ya Chama, hapakosi
kuwa na mashambulio, na mara kadhaa yamemlenga Dkt. John Malecela. Licha ya mashambulio hayo, mara ya moto, mara
ya baridi, mara ya uzushi, daima amedhihirisha msimamo thabiti na mkali, wa
MUUMINI WA CCM. Nakushukuru sana.
Nawashukuru viongozi wengine waasisi na wastaafu
walionisaidia sana, kwa hekima na busara, akiwemo Mzee wetu Rashidi Mfaume
Kawawa. Pamoja na umri wake Mkubwa na
matatizo ya afya, Mzee Kawawa hakukosa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu,
na hakusita kutoa ushauri kwa uaminifu na uwazi. Nakushukuru sana.
Aidha nawashukuru
Mawaziri Wakuu wastaafu, akiwemo Mzee Cleopa David Msuya, Mheshimiwa Jaji
Joseph Sinde Warioba na Dkt. Salim Ahmed Salim na Waziri Mkuu wa Awamu ya Tatu
Mheshimiwa F. T. Sumaye.
Waziri Mkuu Sumaye
ndio aliyeshika kamandi ya askari wa miavuli wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Amefanya kazi nami kwa uaminifu na kwa
taadhima kubwa kwa Chama. Nakushukuru
sana.
Wote hawa na wengine
wanaendelea kuwa hazina kubwa ya Chama Cha Mapinduzi. Nawashukuru wote niliofanya nao kazi kwenye
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa
kwa msaada wao na ushirikiano mkubwa. Naomba kila mmoja ajue kuwa natambua
mchango wake na ajisikie kuwa nimemshukuru sana.
Nawashukuru Makatibu Wakuu wa CCM, Dkt Lawrence Gama na
Philip Mangula, pamoja na Sekretarieti walizoziongoza katika miaka kumi
iliyopita.
Nawashukuru wana-CCM wote kuanzia Wenyeviti wa Mikoa,
Wenyeviti wa Wilaya, Makatibu wao na watendaji wote wa Chama.
Nawashukuru kwa njia ya pekee wananchi wa Dodoma. Siku
zote nilijisikia nipo nyumbani kila nilipokuja hapa, kwa vile ambavyo wamekuwa
wananipokea mimi na wajumbe wote wa mikutano ya Chama kwa upendo mkubwa.
Ahsanteni sana. Na katika shukrani hizo, zipo pia maalumu kwa wanakijiji wa
Chamwino walionipokea kama mwana-kijiji mwenzao kwa miaka kumi, na kunionyesha
upendo na ukarimu mkubwa sana.
Ndugu Wajumbe:
Ipo methali ya Wahabeshi inayosema, “Usimlaumu Mungu kwa
kuumba chui. Mshukuru kwamba hakumuumba chui mwenye mbawa.”
Nami ninapotazama
nyuma katika miaka kumi iliyopita yapo mambo ambayo ningeshukuru kama Mwenyezi
Mungu angetuepusha nayo. Lakini namshukuru sana kwamba hakututwisha mzigo
uliotushinda kwa umoja wetu. Ninapoagana nanyi namwomba kuwa katika kipindi cha
uongozi wa Serikali na Chama tunaomkabidhi ndugu yetu Jakaya Mrisho Kikwete
yasitokee yatakayomshinda yeye akishirikiana nasi. Naamini kwa rehema zake
hivyo ndivyo itakavyokuwa, na CCM itadumu, na itazidi kutoa uongozi bora kwa
nchi yetu na watu wake daima.
Wachangiaji wote
katika mjadala wa jana wamenimwagia sifa kwa maendeleo ya miaka 10 hii. Wengi wamediriki kusema mafanikio ya Uongozi
wangu. Ndugu Wajumbe, nawasihi mzingatie
ukweli huu. Mafanikio hayo ni mafanikio
ya Uongozi wa pamoja. Mafanikio hayo ni
matokeo ya utekelezaji. Na zaidi ya
yote, mafanikio hayo ni matunda ya KAZI YA CHAMA!!
Kuna msanii mmoja
maarufu ambaye daima alikuwa anatamba na kuona fahari kwa kuwa hakuwa
mwanasiasa. Alipoulizwa kwa nini aliona
fahari hiyo, alijibu ni kwa sababu asingeweze kuhimili mzigo wa kuwa sahihi
wakati wote. Nilipokabidhiwa madaraka
nilisema ningaliongozwa na hoja ya Uwazi na Ukweli. Najua sikuwa sahihi wakati wote. Wapo ambao niliwakosea; nawaomba radhi. Wapo ambao sikutimiza matarajio yao; nao pia
nawaomba radhi. Lakini kwa wote
nathubutu kusema: nimefanya bidii yangu yote kuingoza nchi kwa haki. Sasa namaliza ngwe yangu. Nimeitunza Imani ya Chama. Nashukuru kwa zawadi nyingi toka mikoani
mlizotupa mimi na Mama Mkapa. Katika
maisha yetu yaliyobaki tutazihesabu zawadi hizo kama tuzo kwa maisha ya
Utumishi na Uadilifu.
KIDUMU CHAMA CHA
MAPINDUZI!!
MAPINDUZI DAIMA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.