Ilani ya CCM Habari Mpya Historia ya TANU na ASP Kutoka Magazetini Hotuba

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Taarifa rasmi - Miaka 40 ya Mapinduzi SMS na SMT - Mapuri - 29.7.2003

Taarifa rasmi - Sera ya Uzawa - Mapuri - 27.7.2003

 

Taarifa rasmi - Miaka 40 ya Mapinduzi SMS na SMT - Mapuri - 29.7.2003

Katika kikao chake cha tarehe 26-27 Julai, 2003, Kamati Kuu ya Halmashari Kuu ya Taifa ya CCM ilijadili miongoni mwa mengine, ujasiri wa Afro-Shirazi Party wa kuikomboa Zanzibar kutoka makucha ya wakoloni wa Kiingereza na utawala wa Masultani walowezi, tarehe 12 Januari, 1964. Iliuthamini mchango mkuba wa mashujaa wa Mapinduzi hayo chini ya uongozi wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, ambao walijitoa mhanga wa maisha yao kwa ajili ya uhuru wa kweli wa Wazanzibari. Aidha Kamati Kuu ina fahari kubwa kwamba ASP na hatimaye CCM imeweza kuyaendeleza na kuyadumisha Mapinduzi hayo kwa karibu miaka 40 sasa na kuyawekea msingi imara wa kuyadumisha milele. Imesisitiza kwamba kauli mbiu ya MAPINDUZI DAIMA ni kielelezo cha dhamira ya kweli ya kuyadumisha Mapinduzi hayo na matunda yake ambayo kila mzalendo wa kweli wa Zanzibar na Tanzania nzima anapaswa kujivunia.

Kamati Kuu imetafakari pia ujasiri wa TANU na ASP chini ya Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na Jemadari Mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuwa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Karibu miaka 40 sasa, Muungano wa Tanzania ndio mfano pekee Barani Afrika wa

mafanikio ya utekelezaji wa dhamira ya Waafrika kuungana kikweli. Kwengineko kote jitihada za kuunganisha nchi zimeshindikana. Lakini kwa upande wa Muungano wa Tanzania, juhudi zote za maadui wa Muungano huo za kutaka kuudhofisha na kuusambaratisha zimegonga ukuta na zitaendelea kugonga ukuta. Kamati Kuu ina fahari kubwa kwamba vyama vya TANU na ASP na hatimaye CCM vimeweza kuudumisha Muungano huo kwa kipindi chote hicho na kuujengea msingi imara wa kudumu milele.

Kwa hivyo basi, kwa kuthamini mafanikio hayo makubwa na kuwapa heshima wanayostahili waasisi wa MAPINDUZI na MUUNGANO, Kamati Kuu imezitaka Serikali zote mbili yaani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ziandae sherehe kubwa za aina yake kuadhimisha miaka 40 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo tarehe 12 Januari, 2004 na miaka 40 ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 26 Aprili, 2004.

Kamati Kuu inawataka wananchi wote wasizikubali jitihada zinazojaribu kufanywa na wezi wa fadhila, za kutaka tarehe hizo muhimu katika historia ya nchi yetu zisahaulike.

Omar R. Mapuri
KATIBU MWENEZI WA CCM TAIFA
30/07/2003

Rudi Juu


Taarifa rasmi - Sera ya Uzawa - Mapuri - 27.7.2003

Katika Kikao chake cha tarehe 26-27 Julai, 2003 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa imemteua Ndugu Aron T. Mwasamale kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa. Kabla ya uteuzi huu, Ndugu Mwasamale alikuwa Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Uenezi Makao Makuu ya Chama. Ndugu Mwasamale amepangiwa kujaza nafasi iliyokuwa wazi ya Mkoa wa Iringa.

Aidha Kamati Kuu imejadili kuhusu sera ya uzawa ambayo hivi karibuni imekuwa katika mjadala kwenye vyombo vya habari.

Kamati Kuu imejiridhisha kwamba sera hiyo si ya CCM na wala haina mnasaba wo wote na Mkakati wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi uliomo katika ibara ya 6 ya “Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2000" ambayo inasema ifuatavyo:-

Ingawa Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya Tisini ulitamka kwamba lengo la Ujamaa na Kujitegemea ni kuhakikisha kwamba wananchi wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu, utekelezaji wake umekuwa mgumu kufanikiwa kutokana na ukweli kwamba Watanzania walio wengi, huko nyuma hawakupewa nafasi ya kushiriki katika uchumi wa kisasa wa kilimo, viwanda na biashara. Watanzania walio wengi waliachwa kwenye sekta ya uchumi wa jadi wa kilimo, ufugaji na uvuvi na kuwa vibarua na soko la sekta ya kisasa, hali iliyopelekea hadi leo kuwa pembezoni mwa sekta ya kisasa ya uchumi wa taifa letu. Kutokana na hali hiyo, Chama Cha Mapinduzi kimebuni mkakati wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ambao utawafanya Watanzania walio wengi nao waweze kumiliki na kuendesha uchumi katika nchi yao. Dhana ya Uwezeshaji maana yake ni kuunda mazingira mwafaka yatakayowapatia Watanzania fursa ya kumiliki na kuendesha uchumi wa nchi yao.”

Kamati Kuu imesisitiza kwamba neno “uzawa” si msamiati wa CCM, haliakisi chochote katika sera zake na haliendani na ibara ndogo ya 5(15) ya Katiba ya CCM ambayo inaelezea moja kati ya malengo ya CCM kuwa ni “Kuona kwamba Serikali na vyombo vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wanawake na wanaume bila kujali rangi, kabila, dini au hali ya mtu.”

Kwa hivyo, Kamati Kuu inawataka viongozi na wanachama wote wa CCM wasilitumie neno hilo la “uzawa” katika kuelezea sera za CCM. Aidha, imewataka viongozi na wanachama wanapokuwa na mawazo ambayo wangependa yafikiriwe kuingizwa katika Sera za CCM, watumie utaratibu wa vikao halali vya Chama kuwasilisha mapendekezo yao na waheshimu maamuzi ya Chama baada ya kuyazingatia mapendekezo hayo. Kamati Kuu pia imearifiwa kwamba Serikali hivi sasa imo katika hatua za mwisho za maandalizi ya utekelezaji wa Mkakati wa Uwezeshaji wa Watanzania Kiuchumi kwa kuzingatia maelekezo yaliyomo katika ibara ya saba (7) ya Ilani ya Uchaguzi.

Taarifa hii imetolewa na:

Mhe. Omar Ramadhan Mapuri,
KATIBU MWENEZI WA CCM TAIFA
27/07/2003

Rudi Juu