CHAMA CHA MAPINDUZI

 

 

 

 

 

 

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TATU (1995-2005) NA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2000

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kimetolewa na Makao Makuu ya CCM

S.L.P. 50, DODOMA.

 

Aprili, 2005

 

 

 

UTANGULIZI

 

1.     Serikali ya Awamu ya Tatu  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitekeleza Ilani mbili za Uchaguzi za CCM; yaani Ilani ya 1995 na ile ya 2000.  Sura ya kwanza ya taarifa hii inaelezea kwa ufupi mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka kumi cha 1995-2005 cha uongozi wa Awamu ya Tatu.  Maelezo hayo yana umuhimu mkubwa wakati huu tukijiandaa kwa Awamu ya Nne ya uongozi wa nchi yetu.  Kutokana na ukubwa wa mafanikio hayo ambayo yameweka msingi wa maendeleo ya haraka zaidi kwa nchi yetu,  Awamu ya Nne itawajibika kuyaendeleza. 

 

2.     Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu inamaliza muda wake wa kikatiba wa kuwa madarakani, ni vyema kuchukua fursa hii ya kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, pia kugusia japo kwa muhutasari mafanikio ya Awamu hiyo.

 

3.     Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2000 ilikuwa ni programu ya utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000 Hadi 2010.  Lakini pia ilisadifu kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa.

 

4.     Sura zote zilizobaki za taarifa hii zinaelezea kwa ufafanuzi utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2000 yakiwa ni  sehemu ya maandalizi ya Ilani ya 2005 ambayo imechapishwa katika kijitabu tofauti.  Utekelezaji wa Ilani ya 2000 kwa upande wa Zanzibar unaelezewa katika Sura ya Sita.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

SURA YA KWANZA

 

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TATU:1995-2005

 

 

5.     Uchaguzi Mkuu wa 2005 utafanyika katika mazingira ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaingia katika awamu mpya ya uongozi (Awamu ya Nne) baada ya Awamu ya Tatu iliyoanza 1995 chini ya Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa kumaliza muda wake kwa mafanikio makubwa.  Katika kipindi chake cha kwanza  cha uongozi cha  1995 – 2000, Awamu ya Tatu ilifanya kazi nzuri ya kukamilisha kwa mafanikio makubwa utekelezaji wa sehemu ya pili na ya mwisho ya Mwelekeo wa CCM Katika Miaka ya Tisini.  Utekelezaji  huo ulifanyika kupitia Ilani ya CCM ya Uchaguzi  Mkuu wa Oktoba, 1995.  Aidha katika kipindi chake cha pili na cha mwisho  cha 2000 - 2005, Awamu ya Tatu imeweza kutekeleza kwa mafanikio makubwa   ya kujivunia, sehemu ya kwanza ya Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000 Hadi 2010 kupitia   Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2000.

 

6.     Mafanikio ya Awamu ya Tatu kutokana na utekelezaji wa dhati wa Sera na Ilani  za CCM yanadhihirika katika mkakati wa urekebishaji wa uchumi wa nchi  kutoka  uchumi  uliodumaa  hadi kufikia uchumi uliochangamka na unaokua.  Mafanikio hayo ya msingi yameweza  kuzaa mafanikio katika Sekta zote za Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa na kuiweka Tanzania katika njia ya uhakika ya maendeleo na kupambana na umaskini.

 

7.     Kwa jumla, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita mafanikio makubwa yamepatikana yanayoendana na matarajio ya Dira ya Taifa ya 2025 hasa katika nyanja kuu zifuatazo:-

 

(a)            Utulivu wa kisiasa.

(b)            Utawala bora.

(c)             Utulizaji wa misingi ya uchumi mkuu (stabilization of macro-economic fundamentals)

(d)            Ukuaji mkubwa wa sekta ya Madini

 

8.     Mafanikio hayo ni kama yafuatavyo:-

 

 

 

(a)    Mafanikio Katika Uchumi

               

(i)     Pato la Taifa limeongezeka kutoka Dola (za Kimarekani) 5.6 bilioni mwaka 1995 hadi Dola 9.8 bilioni mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 75.

 

(ii)    Pato la kila mtu limeongezeka kutoka Dola 160 mwaka 1995 hadi Dola 260 mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 62.5.

 

(iii)    Ukuaji wa Pato la Taifa  umeongezeka kutoka asilimia 3.6 mwaka 1995 hadi  asilimia 6.7mwaka 2004.

 

(iv)    Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 27.1 mwaka 1995 hadi asilimia 4.2 mwaka 2004.

 

(v)    Asilimia ya Watanzania wanaoishi kwa kipato cha chini ya Dola moja ilishuka kutoka 50 mwaka 1995 hadi 20 mwaka 2004.

 

(vi)    Utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji  wa  Mashirika ya Umma umeweza  kuiondolea Serikali mzigo mzito wa kuendesha uchumi moja kwa moja.  Ubinafsishaji umeanza kujenga mazingira   ya ongezeko la tija  na ufanisi katika uzalishaji wa bidhaa   za viwandani.  Baada ya  kubinafsishwa  makampuni na mashirika hayo sasa yanaipatia Serikali  mapato makubwa badala ya kuendeshwa kwa ruzuku ya Serikali.

 

(vii)   Mauzo ya nje ya bidhaa yameongezeka kutoka thamani ya Dola 682.9 milioni mwaka 1995 hadi Dola 1,165.9 milioni mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 70.7

 

(viii) Akiba ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagizia bidhaa kutoka nje imeongezeka kutoka uwezo wa kukidhi mahitaji ya mwezi 1.6 mwaka  1995 hadi mahitaji ya miezi 9 mwaka 2004.

 

 

 

(ix)    Ruzuku ya Serikali Kuu kwa Serikali za Mitaa ambazo ni chombo cha  wananchi wenyewe cha kusimamia maendeleo yao kule kule waliko, imeongezeka kutoka Shilingi 12.3  bilioni  mwaka 1995/96 hadi shilingi 392.2 bilioni mwaka 2004/05.  Hili ni ongezeko la asilimia 3,088.6(yaani zaidi ya mara 30).

 

(x)    Kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mikakati ya kuweka mazingira mazuri  ya  kuvutia vitega uchumi na kupambana na rushwa, hivi  sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika Afrika  katika kuvutia uwekezaji. Mwaka 2004 Tanzania ilipata tuzo ya kuwa nchi ya kwanza Afrika kwa uwekaji wa mazingira mazuri ya uwekezaji. Uwekezaji wa moja kwa moja wa mitaji kutoka nje umeongezeka kutoka Dola 50.2 milioni mwaka 1995 hadi Dola 247.8 milioni mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 394.

 

(xi)    Kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mikakati ya kupambana na rushwa na kuziba mianya ya ukwepaji  wa  kulipa kodi pamoja na zoezi la ubinafsishaji wa mashirika ya umma, hatua ambayo imeboresha uzalishaji, makusanyo ya mapato ya Serikali yameongezeka kutoka wastani wa shs. 25 bilioni kwa mwezi, mwaka 1995 hadi wastani wa sh. 160 bilioni kwa mwezi, mwaka 2005.  Hili ni ongezeko la asilimia 540.

 

(xii)   Tanzania ilitimiza masharti ya Mpango wa Kuzifutia Madeni Nchi Zenye  Madeni Makubwa (HIPC) na hivyo kuingizwa katika Mpango huo mwaka 1999.  Kutokana na hali hiyo, kuanzia mwaka 2002/2003 hadi 2004/2005, Tanzania ilitekeleza Mkakati wa Kupunguza Umaskini (MKU) ambapo fedha ambazo zingetumika kulipia madeni ya nje yaliyofutwa, sasa zilielekezwa katika sekta teule za huduma za jamii na kiuchumi na miundombinu  zinazowagusa moja kwa moja wananchi wa kawaida kwa manufaa ya pamoja.  Sekta hizo ni elimu, afya, maji, barabara za vijijini, kilimo na utawala bora, hususan Mahakama.

 

(xiii) Kutokana na juhudi za makusudi za kuimarisha utalii kwa lengo la kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira, idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka watalii 295,000 mwaka 1995 hadi 582,000 mwaka 2004.  Hili ni ongezeko la asilimia 97.3  Aidha, mapato yatokanayo na utalii nayo yameongezeka kutoka Dola 259 milioni mwaka 1995 hadi Dola 746 milioni mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 188.0.  Nafasi za ajira kwenye Sekta ya Utalii zimeongezeka kutoka 96,000 hadi 160,750 sawa na ongezeko la asilimia 67.4

 

(xiv) Kutokana na utekelezaji wa sera za makusudi za kuvutia wawekezaji  wakubwa na teknolojia ya kisasa katika uchimbaji wa madini, hasa dhahabu, imefunguliwa migodi mikubwa Nzega, Geita, Kahama, Mara n.k.  Kutokana na maendeleo hayo, uuzaji wa madini umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka thamani ya Sh. 452.0 milioni mwaka 1995 hadi Sh. 22,786.0 milioni mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 4,941.

               

(xv)   Kutokana na utulivu wa mazingira ya kisiasa na kiuchumi, biashara imechangamka nchini.  Mchango wa Sekta ya Biashara kwa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.4 mwaka 1995 hadi asilimia 16.8 mwaka 2004.  Mchango wa Sekta ya Fedha umeongezeka kutoka asilimia 5.9 hadi asilimia 12.1 katika kipindi hicho.  Mchango wa Sekta ya Viwanda nao uliongezeka kutoka asilimia 4.5 hadi 8.7.  Aidha, mchango wa Sekta ya Madini kwa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 0.1 mwaka 1995 hadi asilimia 3.0 mwaka 2004.

 

(b)    Mafanikio katika Huduma za Kiuchumi Na Miundombinu

               

Barabara na Madaraja

 

 

(i)     Toka mwaka 2001, Serikali imekuwa ikitenga Sh.1.8  bilioni kila mwezi kwa ajili ya ujenzi wa barabara nchini.  Fedha hizo kwa pamoja na zile za Mfuko  wa Barabara na za wahisani zimewezesha uimarishaji na utanuzi wa kiasi kikubwa wa mtandao wa barabara kuu na za vijijini nchi nzima.  Urefu wa barabara za lami nchini umefikia kilomita 4,837 mwaka 2004.  Kwa upande wa barabara  za  changarawe/udongo, urefu umefikia kilomita 80,063 mwaka 2004.  Aidha, wakati ujenzi wa barabara   kwa kiwango cha lami ukiwa unaendelea kwa kasi, barabara za changarawe/udongo za Taifa, Mikoa,  Wilaya  na  za Vijijini ziko katika hali nzuri ya kupitika kuliko zilivyokuwa 1995 kutokana na kufanyiwa matengenezo  ya mara kwa mara.

 


(ii)    Ujenzi wa Daraja la Mto Rufiji linalojulikana sasa kama Daraja la Mkapa ulikamilika mwaka 2004 na hivyo kuifungulia milango ya maendeleo  ya kiuchumi Mikoa ya Kusini.

 

Mawasiliano

 

                (iii)    Tanzania katika kipindi hiki imeshuhudia ongezeko kubwa la mtandao wa mawasiliano, hasa ya simu za mkononi.  Idadi ya watu wanaomiliki simu (za aina zote) imefikia  watu 2,115,591 mwaka 2004.

 

Uchukuzi na Usafirishaji

 

(iv)    Reli ya Dodoma - Singida  ilifunguliwa katika kipindi  hiki.  Aidha, kwa  jumla, huduma za usafirishaji na uchukuzi wa abiria na mizigo kwa njia za barabara, reli, maji na anga zimekuwa bora zaidi kwa kiwango  kikubwa mijini na mikoani kuliko zilizvyokuwa mwaka 1995

 

Umeme

 

(v)    Katika sekta ya umeme, Mradi wa Gesi ya Songosongo umekamilika na kuunganishwa na mfumo wa uzalishaji wa umeme wa Gridi ya Taifa  mwaka 2004. Aidha, mradi wa umeme wa Kihansi ulikamilika.  Miradi hiyo imeliongezea Taifa uhakika wa upatikanaji wa umeme.

 

(vi)    Hadi  kufikia mwishoni mwa mwaka 2004, Serikali ilikwishafikisha umeme katika miji iliyo Makao Makuu ya Wilaya  8 kati ya 18  zilizoahidiwa na CCM katika Ilani yake ya Uchaguzi ya 2000.  Ufikishaji  umeme katika miji mingine 6 ulikuwa umefikia hatua kubwa kwa ajili ya ufunguzi mwaka 2005.  Miradi ya ufikishaji umeme katika miji 5  iliyobaki iko katika hatua za maandalizi ya awali.

 

Sekta ya Fedha

 

                (vii)   Sekta ya Fedha, hasa huduma za mabenki, imeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na kufunguliwa mabenki kadha makubwa ya biashara na ya rasilimali.  Mabenki hayo yameweka msingi wa kuwawezesha wawekezaji kwa kuwapatia mikopo  na hivyo kuchangamsha harakati za kiuchumi na kupambana na umaskini.

 

(c)    Mafanikio Katika Huduma za Jamii

 

                Kuongezeka kwa ubora wa huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii ni miongoni mwa manufaa ya kukua kwa uchumi wa taifa ambayo wananchi wa kawaida vijijini na mijini wameanza kuyafaidi kwa pamoja. 

 

Elimu

 

(i)     Katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2000, uliandaliwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) mwaka 2002 kama sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini (MKU) na ni matunda ya Tanzania kuingia katika HIPC.  Aidha, Mpango wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulibuniwa kwa ajili ya kusaidia nguvu za wananchi kwa kutumia mbinu shirikishi kama ilivyoelekezwa  na Sera  za CCM na Ilani zake, katika juhudi zao za kujiondolea  kero.  Kiasi cha asilimia 60 ya miradi ya TASAF katika Wilaya 40 za kwanza za majaribio imekuwa katika sekta  ya Elimu.  Chini ya mipango hiyo miwili, yafutayo yamefanyika na yanaendelea:-

 


·        Kufutwa kwa ada ya shule za msingi za Serikali mwaka 2003.

               

·        Shule nyingi zimekarabatiwa nchi nzima.

                            

 

 

·        Idadi ya vyumba vya madarasa ya elimu  ya  msingi imeongezeka kutoka vyumba 57,708  Mwaka 1995 hadi  vyumba 96,215  Mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 66.7

 

·        Idadi ya shule za msingi za Serikali imeongezeka kutoka 10,891mwaka 1995 hadi 13,533 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 24.3.

                       

·        Idadi ya watoto walioandikishwa Darasa la Kwanza kila mwaka imeongezeka kutoka 712,593 mwaka 1995 hadi 1,368,315 mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 47.9

                       

·        Idadi ya wanafunzi katika ngazi ya elimu ya msingi imeongezeka kutoka wanafunzi 3,877,643 mwaka 1995 hadi wanafunzi 7,083,063 mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 82.7.

                       

·        Uandikishaji katika ngazi ya elimu ya msingi kwa kutumia kigezo cha GER (wanafunzi wote kama  asilimia  ya idadi ya watoto  wa rika husika la umri wa miaka 7 - 13) umeongezeka kutoka asilimia 77.5 mwaka 1995 hadi asilimia 106.3 mwaka 2004.

                       

·        Uandikishaji katika ngazi ya elimu ya msingi  kwa kutumia kigezo cha NER (wanafunzi wa miaka 7 - 13 kama asilimia  ya watoto wote wa rika husika la miaka 7 - 13) umeongezeka kutoka asilimia 55.3 mwaka 1995 hadi asilimia 90.5 mwaka 2004.

                       

·        Kiwango cha kufaulu katika Mtihani wa Darasa la Saba kimefikia asilimia 48.6 mwaka 2004 kutoka asilimia 14.6 mwaka 1995.

 

·        Idadi ya watahiniwa wanaofaulu mitihadi ya ufundi stadi imeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 1995 hadi asilimia 70 mwaka 2004.

 

·        Idadi ya watahiniwa wa Mitihani ya Ufundi Stadi imeongezeka kutoka 11,000  mwaka 1995 hadi 22,000 mwaka 2004 ambalo ni ongezeko la watahiniwa 11,000 sawa na asilimia 100.

 

·        Idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari imeongezeka kwa asilimia 117.

 

·        Viwango vya kufaulu katika shule za sekondari vimeongezeka kutoka asilimia 24.6 hadi asilimia 38.8 kwa sekondari za kawaida na asilimia 70.7 hadi 80.7 kwenye sekondari za juu.

 

·        Idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma imeongezeka kutoka 7,785 mwaka 1995 hadi 32,681 mwaka 2004/05 sawa na ongezeko la asilimia 319.8.  Kwa upande wa wanafunzi wa kike, waliongezeka kutoka 1,135 hadi 10,039 sawa na ongezeko la asilimia 784.5.

 

        (ii)    Baada ya mafanikio mazuri ya kusisimua ya MMEM, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) kuanzia mwaka 2004.  Ada ya shule za sekondari  za kutwa za Serikali imepunguzwa kwa asilimia 50 wakati hatua nyingine za kukarabati na kujenga majengo ya sekondari nchi nzima zinaendelea.

 

Afya

               

(iii)    Chanjo za watoto chini ya umri wa miaka mitano zimefikia asilimia 90 mwaka 2004. Kwa kiwango hicho, Tanzania imevuka kiwango cha kimataifa cha asilimia 80.

 

(iv)    Pamoja na janga la UKIMWI, Sensa ya Taifa ya 2002 imeonyesha kwamba matarajio ya kuishi ya Mtanzania yameongezeka kutoka umri wa miaka 50 mwaka 1988 hadi miaka 51 mwaka 2002.

               

(v)             Mifuko  ya Afya ya Jamii imeanzishwa ili  kuwawezesha              wananchi wa kawaida  vijijini na mijini kukabiliana na gharama za tiba.  Aidha, Bima ya Afya  imeanzishwa kwa ajili ya wafanyakazi wa Sekta ya Umma.

 

(vi)    Ukarabati mkubwa wa hospitali kuanzia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mpaka  hospitali za Mikoa na Wilaya ama umekamilika au uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.  Mashine za “X-Ray” na “Ultra-sound” na jenereta zimefungwa katika hospitali za Wilaya, Mikoa na Rufaa.

 

(vii)   Katika harakati za kuongeza ubora wa utoaji wa huduma za afya, kumekuwa na ongezeko la mtandao wa vituo vya kutolea huduma nchi nzima kama ifuatavyo:-

 

·        Hospitali kutoka 194 mwaka 1995 hadi 221 mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 14.

 

·        Vituo vya afya kutoka 343 mwaka 1995 hadi 433 mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 26.2. 

 

·        Zahanati kutoka 3,832  mwaka 1995 hadi 4,622 mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 20.6.

 


        (viii) Kufutwa kwa kodi kwenye vyandarua  na bidhaa zinazosaidia vita dhidi ya malaria.

 

(ix)           Programu kabambe ya kukabiliana na janga la UKIMWI imeanzishwa na inatekelezwa.

 

(x)             Kwa jumla uhaba wa dawa uliokuwepo miaka ya tisini sasa haupo tena.

 

 

 

 

 

 

Maji Mijini na Vijijini

 

(x)    Idadi ya wakazi mijini wanaopata huduma ya maji safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 60 mwaka 1995 hadi asilimia 74.0 mwaka 2004.

 

(xi)    Idadi  ya wananchi  vijijini wanaopata maji safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 1995 hadi asilimia 53.5 mwaka 2003

 

(xii)   Sambamba na miradi midogo midogo ya maji inayoendelea nchi nzima, miradi mikubwa ya maji ya Dodoma na Chalinze imekamilika.  Aidha, miradi  kabambe ya Dar es Salaam na kuvuta maji toka Ziwa Victoria kwenda Shinyanga Mjini na Kahama imeanza na inaendelea.

 

Ardhi na Makazi

 

(xiii) Uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi na wa wananchi mmoja mmoja umeongezeka katika ujenzi wa majumba, na hivyo kubadili sura ya Jiji la Dar es Salaam na miji mingine kwa kiasi kikubwa.

 

(xiv) Mwamko unaoongezeka wa kujenga nyumba nzuri miongoni mwa wananchi  vijijini unabadilisha kwa kasi sura ya vijiji vingi  nchi nzima.

 

(xv)   Mradi wa kupima viwanja 20,000 katika jiji la Dar es Salaam umepunguza  bughudha katika kupata viwanja na kuziba mwanya mkubwa wa rushwa iliyokuwa ikiwasumbua wananchi.

 

(d)    Mafanikio Katika Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi

               

Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ni sera iliyokusudiwa kuwajengea mazingira Watanzania yanayowawezesha kufaidi  mmoja  mmoja manufaa ya kukua kwa uchumi wa Taifa katika kuongeza vipato vyao kutokana na juhudi zao za kupambana na umaskini.  Katika kipindi hiki, Serikali ya CCM imeweza kuchukua hatua kadha za kuyafikisha kwa wananchi mmoja mmoja manufaa  ya kukua kwa uchumi wa Taifa kama ifuatavyo:-

 

(i)     Kufuta kodi ya maendeleo mwaka 2004 na nyingi nyingine ambazo zilikuwa kero  kwa wananchi na ambazo pia zilidumaza ari ya kupambana na umaskini.  Hatua hii imewakombolea wananchi kipato chao kilichokuwa  kikiwatoka ambacho sasa wanakitumia wenyewe katika harakati zao za kupambana na umaskini.  Pia imeziba mwanya wa rushwa uliokuwa ukiwasumbua sana wananchi, kupitia kodi hii.

 

(ii)    Serikali imeanza kutoa fidia kwa mbolea na baadhi ya dawa za mifugo  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji wa  Wananchi Kiuchmi unaowasaidia kupambana na  umaskini kwa namna ambayo itawaongezea kipato.

 

(iii)    Pamoja na kuongezeka na kushamiri kwa harakati za kujiajiri, ajira katika sekta rasmi pia zimeongezeka.  Idadi ya waajiriwa katika sekta  rasmi ya umma na isiyokuwa ya umma imeongezeka kutoka 817,626 mwaka 1990 hadi 1,179,155 mwaka 2000.  Hili ni ongezeko la nafasi 361,529 za ajira sawa na asilimia 44.  Hii ni kinyume na imani ya baadhi ya watu kwamba eti ajira imepungua.

 

(iv)    Mshahara wa kima cha chini wa kisheria umeongezeka kutoka Shs. 5,000/=  mwaka 1995 hadi Shs. 48,000/= mwaka 2004 likiwa ongezeko la asilimia 174.4 Ukilinganisha na kushuka kwa mfumuko wa bei katika kipindi hicho kutoka asilimia 27.1 hadi asilimia 4.1, ni dhahiri kwamba kipato cha mfanyakazi kimeongezeka.

 

(v)    Mwaka 2004, Serikali ya CCM ya Awamu ya Tatu ilitunga Sera ya utekelezaji  ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na kutunga sheria ya  utekelezaji wa sera hiyo. Hatua hizo ni utekelezaji wa ibara za 6 na 7 za Ilani ya CCM ya 2000 zilizotoa na kufafanua dhana na Sera ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi.  Katika utekelezaji wa Sera hiyo, imeandaliwa mikakati miwili ifuatayo ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

 


·        Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA).  Mkakati huu wa miaka mitano umeandaliwa mwaka 2005 kuchukua nafasi ya Mkakati wa Kupunguza Umaskini (MKU) ambao  umemaliza muda wake wa miaka mitatu kwa mafanikio makubwa.  MKUKUTA unakusudiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kujenga mazingira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ili wachangie kwa kiwango kikubwa zaidi ukuzaji wa uchumi wa Taifa na wao wenyewe kuumiliki na kuuendesha uchumi huo na kujiongezea kipato na hivyo kuondokana na umaskini.

 

·        Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA):  Mkakati huu ambao ni sehemu ya MKUKUTA unakusudiwa kuweka utaratibu rahisi na mwepesi wa kuzitambua rasilimali (hasa ardhi na nyumba) na biashara wanazomiliki wananchi bila ya kuzisajili na hatimae rasilimali hizo zirasimishwe kwa kusajiliwa.  Zikisharasimishwa, rasilimali hizo zitaweza kutumika kama dhamana za mikopo kutoka mabenki na taasisi nyingine za fedha.  Hatua hiyo itawaongezea wananchi uwezo wa kupambana na umaskini kwa kutumia rasilimali zao ambazo hivi sasa ni mfu na wakati huo zitakuwa hai, na kuwapatia mitaji.

 

 

        (e)    Mafanikio ya Kisiasa

 

Utengamano wa Kisiasa

 

(i)     Mazingira yaliyowezesha mafanikio haya makubwa ya kiuchumi na kijamii ni kuwapo kwa amani na utulivu wa kisiasa nchini.  Serikali ya CCM ya Awamu ya Tatu imeweza kuendelea kujenga na kudumisha  hali ya amani na utulivu kwa kipindi chote cha uongozi wake tangu ilipoingia madarakani. 

 

Kupanuka na Kuimarika kwa Demokrasia na Utawala Bora

 

(ii)             Katika kipindi hiki, demokrasia imeendelea kupanuka na kuimarika katika nyanja za uhuru wa kuabudu, kutoa maoni, kuanzisha asasi zisizo za Kiserikali na uhuru katika nyanja mbalimbali zinazowagusa  wananchi vikiwemo vyombo vya habari, vyama vya siasa na kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na  Utawala Bora.

 

(iii)           Idadi ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu imeongezeka kutoka 13 mwaka 1995 hadi 18 mwaka 2005.

 

(iv)           Kwa upande wa vyombo vya habari, katika miaka 10 iliyopita, idadi ya magazeti ya kila siku imeongezeka kutoka 22 hadi 42; magazeti ya kila wiki kutoka 67 hadi 171, na vituo vya redio kutoka 2 hadi 63.

 

                   Mapambano Dhidi ya Rushwa


 

(v)    Kuimarika kwa taasisi za demokrasia na utawala bora pamoja na mazingira ya ukweli na uwazi yamejenga mwamko na hamasa ya kupambana na rushwa miongoni mwa wananchi.  Hayo pamoja na hatua za makusudi za Serikali za  kuziba mianya ya rushwa na kuwachukulia  hatua za kisheria na kiutawala wanaobainika kujihusisha na rushwa kufuatia mapendekezo ya Tume ya Warioba, kiwango cha rushwa kimeanza kuonyesha dalili za kupungua.  Katika  tathmini za Kimataifa kama zile za Taasisi ya Uwazi (Transparency International)  kiwango cha rushwa kimeshuka kwa kiasi cha asilimia 84 katika kipindi cha 1998-2004. Tanzania sasa  si miongoni tena mwa nchi zinazoongoza kwa rushwa Afrika na hata duniani. Aidha, kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia, katika kipindi cha 1996-2004, Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika iliyopiga hatua kubwa kuimarisha utawala bora kwa vigezo vyote vitatu vya Sauti na Kuwajibika kwa Wananchi; Utendaji wa Serikali; na Kudhibiti Rushwa.

 

Usalama wa Raia na Mali Zao

 

                (vi)    Kwa kuongozwa na Sera ya  CCM ya kuwa na jeshi dogo la usalama na raia lakini lenye uwezo mkubwa wa kitaaluma na kinyenzo, Serikali  imekuwa ikichukua hatua za makusudi kuviimarisha vyombo vinavyoshughulikia  usalama wa raia na mali zao ili  kuviongezea ufanisi. Kutokana na hatua hizo, kuna dalili za kupungua kwa uhalifu  nchini kwani idadi ya matukio yote ya uhalifu yaliyoripotiwa Polisi imepungua  kutoka 460,578  mwaka 1995 hadi 261,098 mwaka 2004.  Huu ni upungufu wa asilimia 76.4.  Makosa yenye sura ya ujambazi miongoni mwayo yalipungua kutoka 9,061  mwaka 1995  hadi 8,693 mwaka 2004, ukiwa  ni upungufu  wa asilimia 4.2.  

 

(vii)   Katika kutekeleza sera ya CCM ya kuwashirikisha wananchi katika ulinzi na usalama wao na wa mali zao, Serikali imo katika hatua za awali za kuweka utaratibu wa Polisi Jamii ambao utavishirikisha vikundi vya aina mbali mbali vya ulinzi wa jadi na vya kujiajiri kwa uhakika na ufanisi zaidi.

 

(viii) Kuhusiana na wahalifu wanaohukumiwa vifungo magerezani, mtazamo umebadilika kuelekea katika kuthamini haki zao za kibinadamu na dhana ya  urekebishaji   wa tabia zao.  Kutokana na mwelekeo huo, juhudi za makusudi za kupunguza msongamano magerezani na kuwafundisha wafungwa amali za kujitegemea zimefanywa kwa njia zifuatazo:-

 


·        Kupanua magereza yaliyopo na kuongeza mapya.

 

·        Kuongeza ubora wa lishe,  matibabu, malazi, usafi na mavazi kwa wafungwa magerezani.

 

·        Misamaha ya mara kwa mara ya Rais.

 

·        Parole na vifungo vya nje.

 

·        Kuanzishwa kwa utaratibu wa huduma kwa jamii ambapo wahalifu  wataohukumiwa  vifungo vya muda mfupi kwa baadhi  ya  makosa  hawatopelekwa magerezani na badala yake watatumikia vifungo vyao kwa kufanya kazi kwenye miradi ya jamii wakiwa majumbani mwao.

 

·        Kufufua  miradi ya uzalishaji mali magerezani  kama  vile kilimo, ufugaji, ufundi stadi, ujenzi n.k.

 

10.    Mafanikio  yote  haya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yamepatikana  kutokana  na uadilifu na umakini wa utekelezaji wa Sera  na Ilani za CCM chini ya usimamizi wa uhakika wa CCM yenyewe.   Ili kuyaendeleza  mafanikio hayo, ni muhimu Serikali ya Awamu ya Nne iwe tena ya CCM. 

 

11.    Serikali ya Awamu ya Nne itawajibika kujenga juu ya msingi wa mafanikio haya.  Itapaswa kuyaendeleza mafanikio haya kwa nguvu na kasi mpya na wakati huo huo kupanua upeo wa masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuyaendeleza ili kukidhi matarajio ya Watanzania na kudumisha matumaini yao.  Katika kipindi cha miaka 10 ijayo tutapaswa kuelekeza juhudi zetu katika kukuza uchumi kwa kuchangamsha harakati za kiuchumi ambazo zitawezesha yafuatayo:-

 

(a)            Kuzalisha ajira.

(b)            Kuongeza tija.

(c)             Kujenga utajiri wa nchi.

(d)            Kuboresha kiwango cha maisha cha Watanzania.

 


TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM YA MWAKA 2000

 

 

     SURA YA PILI

 

UCHUMI

 

Hali Iliyofikiwa

 

12.    Uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa bora na  thabiti tangu Serikali ya Awamu ya Tatu iingie madarakani mwaka 1995 kufuatia utekelezaji wa kina uliofikiwa katika marekebisho mbalimbali ya uchumi na ujenzi wa mazingira ya kiuchumi yenye kuvutia wawekezaji.  Katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2000, usimamizi wa utekelezaji wa sera za mapato, matumizi na fedha uliendelea kwa makini zaidi.  Viashiria vya mafanikio hayo yaliyoleta kutengamaa kwa uchumi mkuu ni pamoja na kuongezeka kwa mitaji katika sekta za umma na sekta binafsi, na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni.

 

13.    Hali ya ukame iliyojitokeza  katika baadhi ya mikoa nchini mwaka 2003, haikuathiri sana utulivu wa uchumi na hii ni ishara ya mafanikio makubwa ya mageuzi yetu ya uchumi.  Wastani wa ukuaji wa Pato la Taifa kutoka mwaka 2000 hadi mwaka 2004 ulikuwa asilimia 5.7 kwa mwaka.  Ukuaji halisi wa Pato la Taifa mwaka 2004 ulikuwa asilimia 6.7, ukiongezeka kutoka asilimia 4.9 mwaka 2000.

 

14.    Ukuaji wa uchumi katika kipindi hicho ulichangiwa hasa na hatua za kisera na kimkakati zilizochukuliwa na Serikali katika jitihada zake za kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii.  Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na zifuatazo:-

 

(a)    Kuendeleza kwa msukumo mkubwa na kwa ufanisi  zaidi hatua za kujenga uchumi unaoendeshwa na soko kwa ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.

 

(b)    Kutekeleza kwa ufanisi mikakati ya kutengemaza uchumi (macro-economic stability);

 

(c)    Kutekeleza kwa ufanisi mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa  mapato na kudhibiti matumizi ya Serikali.  Ukusanyaji wa mapato uliongezeka kwa wastani wa Sh. 77.5 bilioni mwaka 2000 hadi wastani wa Sh. 160.0 bilioni mwaka 2005.

 

(d)    Kutekeleza kwa ufanisi sera za kudhibiti ujazi wa fedha, kupunguza mfumuko wa bei, urekebishaji wa Mashirika ya Umma na ulipaji wa madeni ya nje na ndani. Juhudi hizo zimeiongezea nchi  imani kwa wahisani.  Mfumuko wa bei ulishuka kutoka asilimia  6.0 mwaka 2000 hadi asilimia 4.1 mwaka 2004.  Aidha, urekebishaji wa mashirika ya umma unaelekea mwishoni. 

 

(e)            Mikakati ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wa ndani na nje, na kuweka mazingira mazuri ya utawala bora kwa lengo la kukuza rasilimali na kuongeza ajira.  Hadi Desemba 2004, jumla ya miradi 2,527 ilikuwa imeidhinishwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC).  Miradi hiyo inakadiriwa kutoa nafasi 498,539 za ajira.  Ukuzaji rasilimali uliongezeka kutoka Sh. 1,281,046 milioni mwaka 2000 hadi Sh.2,593,501 milioni mwaka 2004.

 

(f)     Kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya  Maendeleo inayotoa mwelekeo wa muda mrefu wa maendeleo ya Tanzania, na pia kwa kuzingatia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).

 

 

 

SURA YA TATU

 

SEKTA ZA UZALISHAJI MALI

 

Kilimo

 

15.    Tanzania ni nchi inayotegemea kilimo kama nguzo yake kuu ya uchumi katika kuleta maendeleo na kuondoa umaskini.  Kilimo huajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania na karibu asilimia 80 ya Watanzania wanaoishi vijijini wanategemea kilimo kwa chakula chao na mapato ya fedha za kununulia mahitaji yao mengine.  Kilimo kilichangia wastani wa asilimia 47 ya Pato la Taifa na wastani wa asilimia 29.1 ya mapato ya fedha za kigeni kati ya 2000-2003.  Tanzania huzalisha zaidi ya asilimia 95 ya chakula kinachotumika nchini na hununua cha kujazia pengo lo lote linapotokea kutoka nje.  Mwaka 2003/2004 Taifa lilijitosheleza kwa chakula kwa asilimia 90 kutokana na hali ya ukame ulioyakabili baadhi ya maeneo ya nchi. Viwanda vingi husindika mazao yanayotokana na kilimo na, kwa hiyo, hutumia mazao ya kilimo kama malighafi.  Kwa hiyo, kilimo kimeendelea kutoa mchango katika uchumi wa Taifa na kina uwezo wa kutoa mchango zaidi iwapo matatizo yanayokwamisha kukua kwa uzalishaji katika kilimo yatapatiwa ufumbuzi wa kudumu, kwa kuzingatia modenaizesheni.

 

16.    Katika kipindi cha 2000-2005 hatua mbali mbali zilichukuliwa na Serikali katika jitihada za kupunguza matatizo yanayokwamisha kilimo, zikiwemo zifuatazo:-

 

(a)                                    Kuandaa na kukamilisha miradi 75 ya umwagiliaji mashambani yenye eneo la hekta 27,470 na mabwawa 6 yenye hekta 860.

 

(b)                                    Kurejeshwa kwa utaratibu wa kutoa ruzuku kwa pembejeo za kilimo kwa kuanzia na mbolea kwa baadhi ya mikoa.

 

(c)                                     Kuweka utaratibu bora zaidi wa kuwawezesha waagizaji na wasambazaji wa  pembejeo na zana za kilimo kupata mikopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo kupitia benki kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji na urejeshaji wa mikopo.

 

(d)                                    Kuratibu kwa ufanisi zaidi upatikanaji wa mbegu bora, kusimamia ubora wa mbegu hizo na kuzalisha mbegu za msingi katika mashamba ya mbegu yanayosimamiwa na Serikali.

 

(e)                                    Kutoa ruzuku kwa Halmashauri za Wilaya ili kuendeleza kilimo.

 

(f)                                      Kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki ya Ardhi.

 

(g)                                    Ubinafsishaji wa baadhi ya mashamba makubwa.

 

(h)                                    Kuanzisha mradi wa kuboresha miundombinu ya masoko ikiwa ni pamoja na kujenga magulio, kuboresha barabara za vijijini na kujenga maghala ya kuhifadhia chakula.

 

17.    Matokeo ya hatua hizo na nyinginezo zenye mwelekeo wa modenaizesheni ni pamoja na yafuatayo:-

       

(a)            Tija katika baadhi ya mazao imeongezeka.  Kwa mfano katika maeneo yanayolima mpunga kwa njia ya umwagiliaji, tija imeongezeka kutoka wastani wa tani 1.8 kwa hekta mwaka 2000/2001 hadi tani 5.0 kwa hekta mwaka 2003/2004.

 

(b)            Uzalishaji wa mazao makuu ya biashara hususan sukari, chai, tumbaku na mkonge uliongezeka katika kipindi cha 2000/2001 – 2003/2004 kama ifuatavyo:-

 

(i)     Sukari: Kutoka tani 135,534 hadi tani 228,000 likiwa ni ongezeko la asilimia 68.2.

 

(ii)    Tumbaku: Kutoka tani 28,000 hadi tani 46,725 likiwa ni ongezeko la asilimia 66.9.

 

(iii)    Chai: Kutoka tani 26,386 hadi tani 30,700 likiwa ni ongezeko la asilimia 16.3

 

(iv)    Mkonge: Kutoka tani 20,500 hadi tani 23,858 likiwa ni ongezeko la asilimia 16.4.

 

(c)             Uzalishaji wa mazao ya chakula uliongezeka kutoka tani 7.3 milioni mwaka 1999/2000 hadi tani 15.6 milioni mwaka 2003/2004 sawa na ongezeko la asilimia 113.7.

 

(d)            Kiwango cha Tanzania kujitosheleza kwa chakula kimefikia wastani wa asilimia 95 katika kipindi hiki kutoka asilimia 92 mwaka 2000/2001.

 

(e)            Ukuaji wa sekta ya kilimo umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2000 hadi asilimia 5.1 mwaka 2004.

 

Mifugo

 

18.    Sekta ya mifugo ni muhimu sana katika kusaidiana na kilimo kukuza uchumi wa Taifa, kulilisha Taifa, kutoa ajira kwa wananchi na juhudi za kupambana na umaskini.  Katika kipindi kilichopita cha 2000-2005 sekta ya mifugo, Serikali ya CCM iliendelea kuchukua hatua mbali mbali kwa lengo la kuyapunguza matatizo yanayoikwaza na kuiingiza katika mtiririko wa modenaizesheni.  Zifuatazo ni miongoni mwa hatua hizo:-

       

(a)            Kutekeleza mikakati ya kuendeleza Sekta ya Mifugo kupitia ugani, tiba, kinga, usambazaji wa maji na uboreshaji wa malisho.

 

(b)            Kuimarisha kituo cha madume cha Usa River cha kuzalishia mbegu bora za ng’ombe, ambapo uwezo wa kituo hicho umeongezeka kutoka kuzalisha dozi 190,000 za mbegu mwaka 2000 hadi dozi 230,000 mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 21.1.

 

(c)             Kuendeleza mashamba ya ng’ombe ya Sao Hill, Mabuki, Nangaramo, Ngerengere, Kitulo na Kibaha kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mitamba na kuisambaza kwa wafugaji wadogo chini ya utaratibu wa “kopa ng’ombe/mbuzi lipa ng’ombe/mbuzi”.

 

(d)            Ubinafsishaji wa baadhi ya ranchi za Serikali umeanza kwa kuzikata katika ranchi ndogo ndogo na kuwauzia wawekezaji wadogo wa Kitanzania katika kutekeleza Mkakati wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi  kwa kufuga kibiashara.  Ranchi zinazohusika ni pamoja na Mkata, Mzeri, Dakawa, Kalambo, Usangu, Kikulula, West Kilimanjaro, Kitengule, Misenyi na Uvinza.

 

(e)            Kutenga maeneo ya hekta 20,000 (kila moja) kwa ajili ya kutumika kama ranchi za mfano katika baadhi ya mashamba ya mifugo.

 

(f)              Utengaji wa maeneo kwa wafugaji kwa lengo la kupunguza migogoro baina ya wafugaji na wakulima.  Utaratibu huo ulianza kutekelezwa kwa ufanisi katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Iringa, Dodoma, Pwani na Mwanza.

 

(g)            Kuhimiza uanzishaji wa vikundi vya ushirika wa wafugaji. Zaidi ya vikundi 200 vimeanzishwa kuanzia 2000 hadi 2004.

 

(h)            Kutoa elimu na mafunzo kwa wafugaji kuhusu matumizi bora ya ardhi, hasa uwiano wa mifugo na malisho, kutunza nyanda za malisho, umuhimu wa kupunguza mifugo kwa kuiuza, na umuhimu wa kutibu mifugo kwa wakati na namna ya kudhibiti na kukabili magonjwa ya mlipuko.

 

(i)               Ujenzi/ukarabati wa malambo 280 kuanzia 2000 hadi 2004 kwa lengo la kuwapunguzia wafugaji haja ya kuhama hama.

 

(j)               Miundombinu ya masoko ya mifugo iliendelea kuhuishwa kwa kukarabati vituo vidogo vidogo vya kupumzikia na kuhifadhia mifugo, minada ya awali na ya sekondari na minada ya mipakani.  Aidha, machinjio ya kisasa ikiambatana na Chuo cha Ukataji wa Nyama imejengwa Dodoma.

 

19.    Kutokana na hatua hizo na nyingine za kawaida za ugani, uzalishaji katika Sekta ya Mifugo uliongezeka kama ifuatavyo:-

       

 (a)   Nyama ya  Ng’ombe:  Kutoka tani 175,000 mwaka 2000 hadi tani 184,000 mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 5.1.

 

(b)    Nyama ya Kuku:  Kutoka tani 45,000 mwaka 2000 hadi tani 63,000 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 40.0.

 

(c)    Mayai:  Kutoka mayai 450 milioni mwaka 2000 hadi mayai 910 milioni mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 102.2.

 

(d)    Nyama ya Mbuzi, Kondoo na Nguruwe:  Kutoka tani 5,800 mwaka 2000 hadi tani 6,000 mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 3.4.

 

(e)    Ngozi ya Ng’ombe:  Kutoka vipande 1.3 milioni mwaka 2000 hadi vipande 1.6 milioni mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 23.1.

 

Uvuvi

20.    Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi 2004 hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa Ilani katika sekta ya uvuvi ni pamoja na:-

 

(a)    Elimu ya ufugaji samaki ilitolewa kwa wafugaji samaki  katika mikoa ya Ruvuma, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Kigoma, Singida na Kagera, na kwa wakulima wa mwani 9,000 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Tanga.

 

(b)    Kuandaa Mpango Kamambe wa Kuendeleza Uvuvi nchini ambapo miradi 15 yenye kipaumbele iliainishwa.  Katika kutekeleza mpango huo ujenzi wa masoko ya samaki ya Dar es Salaam na Mwanza ulikamilika.

 

(c)    Kuimarisha doria kwa kuhudumia maboti 11 ya doria yaliyoko Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Mtera na Nyumba ya Mungu.  Aidha, maboti 4 ya doria yalinunuliwa kwa ajili ya kuimarisha doria katika bahari na maeneo ya maeneo ya maziwa, na vikundi 511 vya ulinzi wa raslimali za uvuvi viliendelezwa katika Ziwa Victoria.

 

(d)    Kurekebisha Sheria ya Uvuvi Namba 6 ya mwaka 1970 na kuwa Sheria Namba 22 ya mwaka 2003 ili kutekeleza Sera ya Uvuvi ya mwaka 1997 na kuzingatia mabadiliko ya shughuli za uvuvi ambazo zimepanuka sana.

 

(e)    Kuhakikisha usalama wa mazao ya uvuvi kwa walaji kwa kuimarisha shughuli za kudhibiti ubora wa mazao ya uvuvi.  Sampuli 2,616 za udongo, samaki na maji zilifanyiwa uchunguzi wa kimaabara nchini na nje ya nchi na kuonekana kuwa katika viwango vinavyokubalika kimataifa.  Uhakiki wa mazao ya uvuvi ulisaidia kuhakikisha usalama wa walaji na pia soko.

 

(f)     Sekta binafsi ilihamasishwa kuanzisha viwanda vya kusindika samaki ambapo viwanda 20 vimejengwa na vingine vinaendelea kujengwa.

 

(g)    Vikundi vya wavuvi wadogo wadogo vimeendelea kuundwa na kupatiwa mikopo.

 

(h)    Mabwawa ya kufugia samaki yameongezeka kutoka 10,000 mwaka 2000 hadi 14,000 mwaka 2004, ikiwa ni ongezeko la asilimia 40.

 

21.    Matokeo ya hatua hizo ni kwamba wavuvi wadogo wadogo wameongeza tija ya uzalishaji na idadi ya meli za uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) imeongezeka kutoka meli 5 mwaka 2000 hadi meli 78 mwaka 2004.  Kutokana na ongezeko hilo la meli, biashara ya mazao ya uvuvi iliongezeka toka Dola 64,635,114 mwaka 2000 hadi Dola 129,605,815 mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 100.6.

 

Maliasili za Wanyamapori na Misitu

 

22.    Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi 2004 hatua zilizochukuliwa  na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ilani ni pamoja na:-

 

 

(a)    Kuwezesha TAWIRI kupata idadi ya wanyamapori kwa madhumuni ya kuandaa viwango vya matumizi kwa kufanya sensa katika mapori ya akiba, hifadhi za taifa na maeneo mengine yenye wanyamapori.  Matokeo ya sensa yalionyesha kuwa idadi ya tembo iliongezeka kufikia 120,000 mwaka 2004 ikilinganishwa na 88,000 mwaka 2000.  Hili ni ongezeko la asilimia 36.4.

 

 

 

 

(b)    Kutathmini viwango vya matumizi (quota) ya wanyamapori ambapo katika kipindi hiki jumla ya wanyamapori 7,623,237 waliidhinishwa kwa ajili ya biashara ya nyara.

 

(c)    Kutenga maeneo ya ardhi oevu yenye umuhimu wa kimataifa (Ramsar Sites) ambapo jumla ya kilometa za mraba 47,563.35 zilitengwa kwa ajili hiyo.

 

(d)    Kuandaa mipango ya Uendeshaji wa mapori ya akiba ambapo rasimu za mipango ya usimamizi wa mapori 18 ya akiba ya Mkomazi, Umba, Rungwa, Kizigo, Muhesi, Selous, Ikorongo, Grumeti, Muyowosi, Kigosi, Maswa, Burigi, Biharamulo, Ibanda, Rumanyika, Usangu, Mpanga-Kipengele na Ugalla ziliandaliwa.  Aidha, Mipango ya Usimamizi kwa mapori ya akiba ya Mkomazi, Selous, Rungwa, Kizigo na Muhesi ilipitiwa.

 

(e)    Kuweka mazingira ya kuwezesha jamii kuhifadhi wanyamapori kwenye ardhi za vijiji ambapo Kanuni na Mwongozo kwa ajili ya kushirikisha wananchi katika uhifadhi wa wanyamapori, hususan uanzishaji wa Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs) ziliandaliwa.

 

(f)     Kuanzisha na kusimamia WMAs ambapo vijiji 74 katika Wilaya 10 vilitenga maeneo ya ardhi yenye jumla ya kilometa za mraba 15,272.27 kwa ajili ya kuanzisha WMA.  Wilaya zilizohusika ni Liwale, Tunduru, Namtumbo, Morogoro (V), Rufiji, Monduli, Sikonge, Urambo, Babati na Kiteto.

 

(g)    Kununua ndege moja na magari 50 kwa ajili ya kuimarisha doria dhidi ya ujangili.

 

 

 

 

(h)    Hifadhi ya Taifa ya Kitulo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 273 ilitengwa na Pori la Akiba la Saadani lenye kilomita 1,141 lilipandishwa hadhi na kuwa Hifadhi ya Taifa.

 

(i)     Jumla ya miti 292,428,845 ilipandwa katika mikoa yote Tanzania Bara katika kampeni ya kupanda miti na kuhifadhi mazingira.

 

(j)     Kuhamasisha wananchi kupanda na kutunza miti na kuhifadhi uoto wa asili ambapo wananchi wa Mkoa wa Shinyanga walihifadhi maeneo ya “ngitiri” yenye zaidi ya hekta 300,000.  Aidha, wananchi wa vijiji 95 katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Morogoro na Dodoma walihamasishwa kutenga na kuhifadhi maeneo ya hifadhi ya misitu ya asili.  Wananchi wa vijiji katika mikoa ya Tabora, Lindi, Pwani, Morogoro na Iringa walitenga hekta 33,000 kuwa misitu ya hifadhi ya vijiji.

 

Utalii

 

23.    Katika kipindi cha 2000 hadi 2004 biashara ya utalii iliendelea kukua.  Pamoja na kuathiriwa na vita vya Irak, ugaidi n.k. idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka kutoka watalii 501,660 mwaka 2000 hadi watalii 578,812 mwaka 2003. 

 

24.    Katika kuimarisha biashara ya utalii,  miongoni mwa mambo yaliyofanyika ni pamoja na:-

 

(a)    Kuanzishwa kwa chombo kinachmilikiwa na sekta binafsi kiitwacho Tourist Comfedation of Tanzania ambapo chombo hiki kwa kushirikiana na Serikali kimeandaa Tourism Directory.

 

(b)    Kubaini maeneo mapya ya utalii wa utamaduni ambapo vivutio vya utalii wa utamaduni katika maeneo mapya vilibainishwa katika mikoa ya Singida, Lindi, Mtwara, Mbeya, Iringa, Dar es Salaam, Kagera na Mara.

 

(c)    Kuendeleza masoko ambapo mkakati wa pamoja wa kuendeleza masoko ya utalii katika Jumuiya ya Ulaya, Canada na Japan uliandaliwa.  Jumla ya majarida 120,000, majalada 33,000 na mabango 85,000 yalichapishwa na kusambazwa katika ofisi zetu za Ubalozi nchi za nje na maonyesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.  Aidha, nakala 44,600 za filamu za video zilisambazwa kwa wadau mbali mbali. 

 

(d)    Kuandaa Sera ya Mambo ya Kale katika jitihada za kupanua wigo wa vivutio vya kiutalii.

 

(e)    Kutekeleza mpango wa uhifadhi na uendelezaji wa maeneo ya kihistoria ambapo majengo ya kihistoria ya miji ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara pamoja na jengo la Livingstone yalikarabatiwa.

 

(f)     Sekta ya Utalii imezalisha nafasi 322,258 za ajira katika kipindi  cha 2000 hadi 2004.

 

Viwanda

 

25.    Katika kipindi kilichopita, Serikali katika utekelezaji wa Ilani iliendelea kutekeleza sera ya ubinafsishaji.  Pia iliandaa Sera Endelevu ya Viwanda, Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo na Sera ya Utekelezaji ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi.   Sera zote hizo zilisaidia sana  katika kuimarisha viwanda.  Aidha, yalianzishwa maeneo maalum ya uzalishaji kwa ajili ya kuuza nje (EPZ).  Viwanda vingi vimepata wawekezaji wapya wenye uwezo wa kuingiza teknolojia mpya na uzoefu wa kuendesha viwanda kisasa.

 

26.    Matokeo ya hatua hizo za ubinafsishaji wa viwanda ni pamoja na:-

 

(a)    Kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa viwandani na hivyo kukidhi mahitaji ya wananchi.  Kwa mfano, uzalishaji wa nguo uliongezeka kutoka mita za mraba 73.6 milioni mwaka 2000 hadi mita za mraba 109.8 milioni mwaka 2004; usagishaji wa ngano kutoka tani 162,634 mwaka 2000 hadi tani 333,789 mwaka 2004; uzalishaji wa chuma kutoka tani 11,182 mwaka 2000 hadi tani 46,559 mwaka 2004.  Ongezeko kubwa la uzalishaji lilipatikana pia katika bia, sigara, bati, saruji, biskuti na tambi; utengenezaji wa kamba za katani, uuzaji nje wa samaki wa kusindikwa; n.k.

 

(b)    Kuongezeka kwa ukuaji wa Sekta ya Viwanda kutoka asilimia 4.8 mwaka 2000 hadi asilimia 9.0 mwaka 2003.  

 

(c)    Kuongezeka kwa thamani ya miradi iliyoidhinishwa kutoka Tshs. 123.8 bilioni mwaka 2000 hadi Tshs. 239.6 bilioni mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 93.5.

 

(d)    Kuongezeka kwa ajira viwandani kutoka 153,938 mwaka 2000 hadi 207,571 mwaka 2003 sawa na ongezeko la asilimia 34.8.

 

Madini

 

27.    Serikali katika kutekeleza Ilani ya CCM ya 2000 katika Sekta ya Madini iliongozwa na Sera ya Madini ya mwaka 1997; Sheria ya Madini ya mwaka 1998 na Kanuni za mwaka 1999.  Sera hiyo ililenga kuvutia wawekezaji binafsi.  Azma ya kuwavutia wawekezaji imefanikiwa  kwa kiwango kikubwa.  Utafiti wa madini uliongezeka na migodi mikubwa ilifunguliwa.  Ushiriki wa sekta binafsi katika utafutaji na uchimbaji wa madini umewezesha  kuwepo  kwa migodi yenye hadhi ya kimataifa kama vile Geita Gold Mine, Kahama Mining, Buhemba Gold Mine (Musoma), Afrika Mashariki Gold Mine (Tarime) na Tulawaka Gold Mine (Biharamulo).  Kwa upande wa wachimbaji wadogo wadogo, wamekuwa wakipatiwa mafunzo katika nyanja mbali mbali kama vile uchimbaji salama wa madini, utunzaji wa mazingira, utafutaji wa madini, biashara ya madini, masuala ya afya n.k.  Aidha, wachimbaji wadogo wadogo walifundishwa namna ya kupata mikopo kutoka SIDO na taasisi nyingine zinazotoa mikopo.  Kutokana na hatua hizo, sekta ya madini imeweza kupata mafanikio yafuatayo katika kipindi cha 2000-2005:-

 

(a)    Tanzania kwa sasa inazalisha takriban tani 50 za dhahabu kwa mwaka na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uzalishaji wa dhahabu Barani Afrika.

 

(b)    Sekta ya Madini imekuwa kati ya sekta zenye kasi kubwa ya ukuaji.  Ukuaji uliongezeka kutoka asilimia 13.9 mwaka 2000 hadi asilimia 14.1 mwaka 2004 ikiwa ilifikia kilele cha asilimia 17.0 mwaka 2003.

 

 (c)   Mchango wa sekta ya madini katika mauzo ya nje uliongezeka kutoka asilimia 26.9 mwaka 2000 hadi asilimia 51.4 mwaka 2004 na hivyo kuongoza katika mauzo ya nje ikilinganishwa na mauzo ya bidhaa nyingine.

 

(d)    Mchango wa sekta ya madini kwa mapato ya fedha za kigeni umekua kutoka Dola za Kimarekani 178.2 milioni mwaka 2000 hadi dola za Kimarekani 543.0 milioni mwaka 2004.  Hili ni ongezeko la asilimia 204.8.

 

(e)    Watafutaji na wachimbaji madini wakubwa na wadogo hulipa ada za leseni na mrabaha kwa madini wanayouza.  Tangu mwaka 2000, maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa na Wizara yaliongezeka kutoka Shilingi 7.441 bilioni mwaka 2000/01 hadi Shilingi bilioni 22.786 mwaka 2003/04, likiwa ni ongezeko la asilimia 206.2.

 

(f)              Migodi mikubwa imekuwa ikisaidia katika utekelezaji wa miradi ya jamii kama vile afya, elimu, maji na barabara.  Huduma hizo huvinufaisha vijiji vinavyozunguka migodi hiyo.  Baada ya uchimbaji madini kufikia kikomo, majengo ya migodi hiyo yatatumika katika huduma za jamii kama vile kuanzisha shule au huduma nyingine kulingana na vipaumbele vya wanajamii katika eneo husika.

 

(g)            Ajira rasmi katika migodi mikubwa imeongezeka kutoka 1,781 mwaka 1997 hadi 7,082 mwaka 2003 likiwa ni ongezeko la asilimia 297.6.  Aidha, mwaka 2003 inakadiriwa kuwa zilizalishwa nafasi 42,000 za ajira nje ya migodi kutokana na kuwapo kwa migodi hiyo.  Kwa upande wa kujiajiri, inakadiriwa walikuwapo wachimbaji wadogo zaidi ya 500,000 waliokuwa wamejiajiri wenyewe.

               

Biashara

 

28.    Biashara ni muhimu sana katika jitihada za kuongeza pato la wananchi na kuendeleza uchumi. Dunia ya sasa ya utandawazi imeegemea sana kwenye biashara ya kimataifa.  Kwa kutambua hilo, Serikali imeweka msukumo wa pekee katika kukuza mauzo ya bidhaa zetu nje na kuongeza wingi na ubora wa bidhaa katika soko la ndani.  Kutokana na msukumo huo hatua zifuatazo zilichukuliwa katika kipindi kilichopita:-

 

(a)            Kuondoa kero ya ulipaji wa kodi ya makisio (provisional tax) kabla ya hata kuanza biashara yenyewe.  Serikali iliweka wazi masharti ya kuanzisha biashara, viwango vya ada kwa aina mbalimbali za biashara na hivyo kupunguza vishawishi vya rushwa. 

 

(b)            Kushiriki katika majadiliano kuhusu mfumo wa biashara kimataifa. Mwezi Julai, 20001,  Tanzania iliandaa Mkutano wa Mawaziri wa Biashara kutoka nchi maskini sana (LDCs) uliofanyika Zanzibar.  Tamko Rasmi la Zanzibar (Zanzibar Declaration) liliweka msimamo wa pamoja katika mikutano ya Shirika la Biahsara la Dunia (WTO) ya Doha, Qatar mwezi Novemba, 2001 na Cancun, Mexico, mwezi Septemba 2003.  Ushirikiano huo ulizuia upitishaji wa agenda ambazo zingeendeleza na kuimarisha maslahi ya nchi kubwa dhidi ya nchi changa.  Mchango wa Tanzania katika kujenga nguvu hii ulikuwa mkubwa.

 

(c)             Ili kukuza maendeleo ya kiuchumi, na hasa viwanda na biashara, Serikali iliendelea kushirikiana na nchi majirani, hasa za  Afrika Mashariki kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

 

(d)    Kutunga Sheria ya kudhibiti uingizaji holela wa bidhaa kutoka nje ili kuilinda nchi yetu isigeuzwe kuwa dampo la bidhaa hafifu kutoka nje.

 

(e)    Kuanzisha maeneo huru ya biashara.

       

(f)     Kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo katika taaluma za ujasiriamali, namna ya kupata mikopo kutoka Mifuko mbali mbali na Mabenki, na kurahisisha taratibu za kupata mikopo chini ya Mkakati wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi.

       

(g)    Kupunguza mlolongo wa leseni kabla ya kuanzisha biashara.

 

(h)    Kutungwa sera na mikakati ifuatayo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kuwezesha ukuaji wa biashara kubwa na ndogo:-

       

(i)     Sera ya  Utekelezaji ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi.

                (ii)    MKUKUTA

                (iii)    MKURABITA

 

29.    Kutokana na hatua hizo na nyinginezo, mafanikio makubwa yamepatikana yakiwemo yafuatayo:-

 

(a)            Ukuaji wa Sekta ya Biashara uliongezeka kutoka asilimia 6.5 mwaka 2000 hadi asilimia 7.4 mwaka 2004.

(b)            Mauzo ya nje yaliongezeka kutoka Dola 663.3 milioni mwaka 2000 hadi 1,142.0 milioni mwaka 2003, likiwa ni ongezeo la asilimia 72.2.

 

(c)             Biashara imechangamka zaidi nchini

 

Maendeleo ya Ushirika

 

30.    Ilani ya CCM katika kipindi cha 2000-2005 iliweka malengo yaliyokusudia kuimarisha na kuendeleza ushirika kama njia ya kumwezesha Mtanzania wa kawaida hupambana na umaskini.  Katika utekelezaji, hatua kadhaa zilichukuliwa na mafanikio kupatikana kama ifuatavyo:-

 

(a)            Serikali ilibadilisha Sera ya Ushirika ya mwaka 1997 na kuifanyia marekebisho Sheria ya Ushirika ya mwaka 1991 ili kuzifanya shughuli za ushirika ziendane na mabadiliko katika uendeshaji uchumi wa soko.  Sera ya Maendeleo ya Ushirika ilitungwa mwaka 2002 na Sheria Mpya ya Vyama vya Ushirika ilitungwa upya mwaka 2003.

 

(b)            Wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimba madini wadogo wadogo wameanza kuingia katika utaratibu wa kuanzisha vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOs).

 

(c)             Vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa vimeongezeka kutoka 803 Mwaka 2000 hadi 1,719 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 114.1

 

(d)            Baadhi ya Mikoa na Wilaya imeanzisha benki za ushirika k.v. Kagera Farmers Cooperative Bank, Kilimanjaro Cooperative Bank na benki za wananchi za Dar es Salaam Community Bank na Mufindi Community Bank.

 

(e)            Hisa na akiba za wanachama zimeongezeka kutoka Shilingi 14.04 bilioni mwaka 2000 hadi Shilingi 42.98 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 20.6

 

(f)              Wanachama wa vyama vya Ushirika wa akiba na mikopo wameongezeka kutoka 133,134 mwaka 2000 hadi wanachama 251,631 mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 89.0.

 

(g)            Mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka shilingi 11.52 bilioni mwaka 2000 hadi shilingi 54.14 bilioni mwaka 2004 sawa na asilimia 370.0.

 

(h)            Umeanzishwa utaratibu wa kutoa dhamana ya mikopo kwa vyama vya ushirika (na wafanyabiashara binafsi ili kununulia mazao (Export Credit Guarantee Scheme).  Dhamana hiyo imevisaidia sana vyama vya ushirika kununua mazao ya wakulima katika ushindani na makampuni binafsi. Wanachama wameanza tena kuwa na imani na vyama vyao vya ushirika.  Bila ya utaratibu huo baadhi ya vyama vya ushirika vingekufa.

 

(i)               Vyama vya ushirika vimeruhusiwa kuuza moja kwa moja mazao ya wanachama wake nje ya nchi.

 

(j)               Vyama vya ushirika vimepewa uwezo wa kushitaki moja kwa moja wale wanaosababisha wizi na ubadhirifu katika ushirika.

 

(k)             Chuo cha Ushirika Moshi kimepandishwa hadhi na kuwa Chuo Kikuu Kishiriki (cha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine).

 

Maendeleo Ya Masoko

 

31.    Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza soko la ndani na la nje kwa kupitia mikataba na makubaliano mbalimbali.  Jitihada kubwa zimefanywa katika kuwaelimisha wakulima kuzalisha mazao kibiashara na hasa kuzingatia mahitaji ya soko, hususan ubora, madaraja na ufungashaji.  Katika kipindi cha 2000/2001 – 2004/2005, Tanzania imejipatia mafanikio kutokana na kuongezeka kwa uuzaji wa mazao yaliyomo katika makubaliano hayo.  Tanzania ni mwanachama katika mikataba na makubaliano kama vile:-

 

(a)    Soko la Amerika kwa mujibu wa “African Growth and Opportunity Act” – AGOA.

 

(b)    Jumuiya ya Ulaya (EU) chini ya utaratibu wa “Every thing But Arms. (EBA)”

 

(c)    Upendeleo maalumu unaotolewa na baadhi ya nchi marafiki.

 

(d)    Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

(e)    Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

 

32.    Ununuzi na mauzo yanayofanywa na makampuni yanayosafirisha mazao ya biashara asilia (traditional export crops) kama kahawa, chai, tumbaku, mkonge na pamba umekuwa ukiongezeka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita isipokuwa zao la pamba.  Katika kipindi cha 1995 hadi 2000, uzalishaji wa zao la pamba ulishuka kwa asilimia 14.  Hata hivyo, katika kipindi cha 2000 hadi 2004, zao hilo pamoja na lile la tumbaku yameonekana kuongezeka zaidi kuliko mazao mengine.

       

33.    Matatizo yanayoendelea kuathiri uzalishaji usiwe mkubwa zaidi ni pamoja na kutegemea zaidi mvua, mabadiliko ya hali ya hewa (hasa ukame), uduni wa miundombinu ya masoko ambayo imekuwa ikiongeza gharama za usafirishaji, upungufu wa taarifa za mahitaji ya masoko hasa ya nje, upungufu wa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nje.

 

34.    Katika jitihada za kupunguza matatizo na kuongeza ufanisi, hatua zifuatazo miongoni mwa nyingine zilichukuliwa katika kipindi kilichopita:-

 

(a)    Kuendelea na maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane).

 

(b)    Kuwashirikisha wazalishaji katika Maonyesho ya Kimataifa kama yale ya mboga mboga na matunda kule Rostock, Ujerumani (2003/2004) na Maonyesho ya Mazao ya Chakula kule Moscow (2004/2005).  Maonyesho ya Rostock yameanza kuwanufaisha wakulima wadogo wadogo kwa kuingia mikataba (contract farming) ya kuyauzia makampuni makubwa ambayo yanashughulikia biashara ya kimataifa.

 

(c)    Kuanzishwa kwa mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Masoko Vijijini.  Mradi huu unatekelezwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa lengo la kuwa na soko la uhakika la mazao yanayozalishwa na wakulima.  Mradi huu unatekelezwa katika Wilaya za Kongwa na Mvomero.

 

(d)    Kuanzishwa kwa Programu ya Kuendeleza Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo (Agricultural Marketing Systems Development Programme).  Moja ya malengo ya programu hii ni kuimarisha miundombinu ya masoko vijijini hasa barabara na maghala ili kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji hivyo bidhaa zetu kuweza kushindana na bidhaa kutoka sehemu yo yote duniani.

 

(e)    Kuandaa Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo Yenye mwelekeo wa kuwaunganisha wazalishaji wakubwa na wadogo kwa upande mmoja na wanunuzi/wasindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo kwa upande mwingine kwa lengo la kupata soko la uhakika na bei nzuri.

       

 

 

 

 

SURA YA NNE

 

SEKTA ZA MIUNDOMBINU NA

HUDUMA ZA KIUCHUMI 

 

Ardhi

 

35.    Ardhi   ni sekta yenye umuhimu mkubwa katika ujenzi wa uchumi wetu na upunguzaji wa umaskini nchini.  Katika kipindi  cha 2000-2005, Serikali imeendelea kuboresha maisha ya wananchi kwa kupambana na kero mbali mbali za ardhi na makazi.  Hatua zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ifuatavyo:-

 

(a)    Sera ya Taifa ya Ardhi, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Ardhi ya Vijiji na Sheria ya Mahakama za Ardhi zimeendelea kutumika ipasavyo.  Aidha wananchi wameendelea kuelimishwa kuhusu Sheria za Ardhi ili waitambue ardhi wanayomiliki kuwa ni raslimali ya kuwaondolea umaskini na waweze kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi hiyo. 

 

(b)    Sheria ya Ardhi ya Vijiji imeziwezesha Halmashauri za Vijiji kupata vyeti vya Ardhi ya Vijiji na kusajili Hatimiliki za Kimila za Ardhi kwa wakazi wake;

 

(c)    Umilikaji wa ardhi kimila vijijini umeboresha usalama wa miliki na umetoa fursa ya kutumia hati miliki hizo kama dhamana katika Vyombo vya Fedha, Mahakama na Taasisi za Elimu ya Juu;

 

(d)    Katika Mikoa minane ya Tanzania Bara mipaka ya Vijiji 2048 imepimwa kwa kutumia vifaa vya kisasa.  Mikoa hiyo ni:  Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Morogoro, Ruvuma, Shinyanga na Singida;

 

(e)    Msukumo mkubwa ulielekezwa katika upimaji wa viwanja mijini na vijijini na pia wa mashamba makubwa kwa ajili ya uwekezaji.  Mikoa yenye idadi kubwa ya mashamba yaliyopimwa ni:  Mbeya (12,660); Dar es Salaam (1,261); Pwani (1,097); Arusha (608); Tanga (325); Morogoro (238); Kilimanjaro (207); Kagera (151) na Iringa (99).  Kumbukumbu zimetunzwa kwa kufungua majalada 52,000 ya viwanja na mashamba na kuyaingiza kwenye Kompyuta;

 

(f)     Kwa kutumia Mabaraza ya Usuluhishi wa Ardhi na Mabaraza ya Nyumba, jumla ya mashauri ya ardhi 5,703; kesi za nyumba 6,765; rufaa za ardhi 581 na rufaa za nyumba 523 zilisikilizwa na kutolewa uamuzi;

 

(g)    Umeanzishwa mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara (MKURABITA) ambao utaihusu sana sekta ya ardhi kwani wananchi wengi wanamiliki rasilimali ya ardhi kwa njia zisizo rasmi.

 

Nishati

 

36.    Nishati (hasa umeme) ni nyenzo ya msingi katika uchumi kwani viwanda na shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea umeme.  Katika kipindi cha 2000 - 2005, hatua zilizochukuliwa kuikuza sekta hii na mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:-

 

(a)            Katika kipindi cha 2000 – 2005, umeme umepelekwa katika miji mikuu ya Wilaya nane zifuatazo: Geita, Igunga, Mbarali, Meatu, Mkuranga, Ruangwa, Tandahimba na Sikonge.  Hadi kufikia mwisho wa mwaka 2005, miji mikuu ya Wilaya za Ngara, Biharamulo, Rufiji, Serengeti, Ukerewe na Urambo itakuwa imepatiwa umeme.  Hatua zimeanza kuchukuliwa ili kufikisha umeme katika miji ya Wilaya za Bukombe, Kilindi,  Simanjiro, Kibondo na Kasulu.

 

(b)            Kati ya mwaka 2002 na 2004, umeme ulisambazwa kwa vijiji 197;

 

(c)             Urekebishaji wa uendeshaji wa TANESCO.

 

(d)            Gesi ya Songo Songo ilianza kuzalisha umeme Oktoba 2004 kwa kuendesha mitambo 4 ya Ubungo yenye uwezo wa kuzalisha MW 112 za umeme.  Pia viwanda vya bia (TBL), saruji (Wazo Hill) na Kioo Limited vimeanza kutumia gesi hii kama nishati katika uzalishaji;

 

(e)            Zimeandaliwa taratibu za kuanza kuunganisha umeme katika miji na vijiji vilivyomo mipakani na nchi za Zambia, Uganda na Kenya

 

(f)              Umesainiwa mkataba wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay kwa ajili ya miji ya Mtwara na Lindi;

 

Barabara

 

37.    Mtandao wa barabara ambao umeendelea kujengwa upande wa Tanzania Bara una urefu wa kilomita 84,950.  Kati ya hizo, Serikali Kuu husimamia kilomita 10,300; Serikali za Mitaa kilomita 49,950 na Vijiji kilomita 24,700.  Ukiondoa kilomita 795 za barabara kuu na kilomita 673 za barabara za Vijijini ambazo ziliendelezwa katika kipindi cha 1995-2000, mafanikio ya kipindi cha 2000-2005 ni haya yafuatayo:-

 

(a)            Jumla ya kilomita 28,051 za barabara kuu na  30,653 za barabara za Mikoa zimetengenezwa;

 

(b)            Madaraja 2,790 ya barabara kuu na  2,144  ya barabara za Mikoa yametengenezwa;

 

(c)             Kuzifanyia matengenezo makubwa  km. 989 na ya kawaida km. 2716 ya barabara za Mikoa ya Ruvuma na Iringa Kusini.

 

(d)            Ujenzi wa daraja la Mto Rufiji  (Daraja la Mkapa) ulikamilika na  lilifunguliwa Agosti, 2003.

 

(e)            Hadi kufikia mwaka 2004/2005 wa Fedha, Serikali inaendelea na kuzifanyia matengenezo kilomita 13,474 za barabara na madaraja 1,692 katika barabara kuu na za Mikoa;

 

(f)              Kutokana na kuimarisha ukusanyaji wa kodi nchini, Serikali imebuni na kuanza kutekeleza Mradi Maalum wa Ujenzi wa Barabara Kuu kwa kiwango cha lami kwa kutumia fedha zetu wenyewe.  Jumla ya kilomita 469 zinajengwa katika kiwango cha lami kwa utaratibu huu;

       

(g)            Kukaribishwa kwa Sekta binafsi  kushiriki katika ujenzi wa miradi ya barabara, madaraja na majengo ya Serikali;

 

(h)            Kukamilishwa na  kuidhinishwa rasmi kwa Sera ya Taifa ya Ujenzi ambayo ni Mwongozo wa utekelezaji wa shughuli zote za Sekta ya Ujenzi.

 

(i)               Kuvifanyia ukarabati vivuko 8 vya:-

 

Pangani (Tanga), Ruhuhu (Ruvuma), Ilagala (Kigoma), Kigongo - Busisi na Kome (Mwanza), Magogoni (Dar es Salaam), Rufiji (Pwani) na Kyanyabasa (Kagera).

 

(j)               Vilinunuliwa vivuko vipya vya: Kilombero, Bugolora-Ukara na Kilambo (Tanzania - Msumbiji).

 

(k)             Baadhi ya Barabara kuu  za jiji la Mwanza zilitengenezwa kwa kiwango cha lami.

 

Usafiri na Uchukuzi

 

38.    Katika kipindi cha 2000-2005, hali ya usafiri na usafirishaji kwa jumla iliendelea kuwa nzuri kutokana na miundombinu ya barabara na reli kuwa bora zaidi na vyombo vya usafiri na usafirishaji wa ardhini, baharini na angani kuongezeka.  Hatua zilizochukuliwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana yalikuwa kama ifuatavyo:-

       

(a)            Sekta binafsi iliendelea kuleta mapinduzi katika usafirishaji mijini na vijijini kwa kuongeza idadi na ubora wa mabasi na njia (routes) yaliyohudumia.  Hivyo hivyo kwa malori ya uchukuzi wa mizigo.

 

(b)            Yalifanyika maandalizi ya kuanzisha mradi wa mabasi ya usafiri wa haraka (CBRT) jijini Dar es Salaam.

 

(c)             Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilitandika kilometa 62.5 mpya za reli na kumwaga kokoto kilometa 112 katika maeneo mbalimbali.  Injini 92, mabehewa 469 ya mizigo na 48 ya abiria yalikarabatiwa.  Aidha, ujenzi wa njia ya mawasiliano kati ya Morogoro na Tabora ulikamilika.

 

(d)            TAZARA nayo ilikarabati mabehewa 2,736 ya mizigo na 142 ya abiria pamoja na njia ya reli kwa kuchomelea kutoka Dar es Salaam hadi Igurusi (kilometa 657).

 

        (e)    Ili kuimarisha ubora wa huduma za uchukuzi kwa wananchi waishio kando kando ya maziwa makuu, Serikali ilijenga magati ya Kinesi, Bugando, Nansio na Shirati.  Yote yako katika Ziwa Victoria.  Aidha, ukarabati wa gati la Kasanga umekamilika na ujenzi wa gati la Karema katika Ziwa Tanganyika; Kiamkwikwi,  Maisome na Kome katika Ziwa Victoria unaendelea.  Maandalizi ya ujenzi wa gati la Manda na  Mbamba Bay yalifanyika.

        

(f)     Kwa upande wa ukanda wa Mtwara ambao unaanzia bandari ya Mtwara hadi Mbamba Bay na kuunganisha mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma) na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, mpango wa utekelezaji ulikamilishwa.  Wawekezaji walihamasishwa kuwekeza katika maeneo mbalimbali kama vile barabara, reli, usafiri kwa njia ya maji na   anga, kilimo, utalii na viwanda.

 

(a)            Katika kuboresha usafiri wa anga, juhudi zilizofanywa ni pamoja naKununua Meza na Radio za kuongozea ndege Zanzibar, Arusha, Mwanza na kufungwa katika viwanja hivyo; kufunga mitambo ya mionzi ya jua,  kuboresha nguvu za umeme katika viwanja vya Kigoma, Mtwara, Songea na Zanzibar; kununua mitambo ya kuongozea ndege katika viwanja vya ndege vya Mtwara na Mbeya; kuzindua huduma za Rada kwa saa 24 Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam; na kununua vifaa vya kuzimia moto.  Aidha, ujenzi wa Uwanja mpya wa Ndege wa Songwe, Mbeya uliendelea na  matengenezo mbalimbali ya viwanja vilivyopo yalifanyika ili kuwezesha ndege kutua na kuruka kwa usalama.

 

(h)    Ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kutoka uwezo wa kuhudumia makontena 10 kwa saa mwaka 2000 hadi 25 mwaka 2005.  Kwa kigezo hicho, Bandari hiyo hivi sasa ndiyo yenye ufanisi mkubwa kuliko zote katika eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika.

 

Mawasiliano

 

39.    Sekta ya mawasiliano imeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii nchini mwetu katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, hasa kutokana na kupanuka kwa haraka sana kwa mtandao wa simu za mikononi na matumizi ya mtandao wa internet.  Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hatua zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:-

 

(a)    Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) iliweka mtambo wenye uwezo wa kupokea malipo kabla ya huduma (pre-paid system) katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma na Zanzibar.  Aidha, ilipanua huduma za simu za mezani kwa kuifikisha katika maeneo muhimu ya uchumi kama vile migodi ya dhahabu ya Kahama na Buhemba, Kiwanda cha Saruji cha Tanga, Kiwanda cha Sukari cha Kagera na kwenye Mashamba ya Chai ya Kibena na Mufindi.  Pia mitambo ya zamani ya analogue ilibadilishwa kwa kuweka mitambo ya kisasa aina ya digital katika baadhi ya miji.  Mtandao wa simu nchini umefikia wamiliki 5 wa simu kwa kila watu 100 (yaani teledensity ya 5/100).

 

         (b)   Katika eneo la simu za mkononi, kampuni mpya ya Celtel ilianza kutoa huduma ikiongezea juu ya zile zilizokuwa zikitolewa na Vodacom, Zantel na Mobitel.

 

         (c)   Idadi ya wenye simu za mezani na za mkononi iliongezeka kutoka 300,237 mwaka 2000 hadi 2,115,591 mwaka 2004.  Hili ni ongezeko la asilimia 604.6.

 

         (d)   Serikali imeweza kuweka mtandao wa tovuti katika vituo vya mikoa 26 (regional points) isipokuwa mitatu ambayo ni Lindi, Rukwa na Ruvuma.  Tanzania sasa ina internet Service Providers 25 na internet cafes 4,000.

 

         (e)   Utoaji huduma kibiashara umesaidia Shirika la Posta kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zake kwa wateja.Idadi ya makampuni yenye leseni za kutoa huduma za posta imeongezeka kutoka makampuni 13 mwaka 2000 hadi makampuni 29 mwaka 2004.

 

         (f)    Tanzania iliongeza kasi ya kuingia katika mfumo wa Jamii Habari (Information society). Huu ni mfumo wa maisha ambamo jamii ina haki na uwezo wa kuwasiliana, kujifunza na kupashana habari bila vikwazo.  Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali ilitoa Sera ya Habari mwaka 2003 ili kuleta mabadiliko katika matumizi ya teknolojia za habari na mawasiliano (TEKNOHAMA).  Vituo vinane vya mawasiliano (telecenters) vimejengwa.  Vituo hivyo ni pamoja na Tanzania Global Distance Learning Centre  (Dar es Salaam); Sengerema Telecenter, Kasulu Internet Café; Ngara UNHCR Telecenter, Wino Telecenter; Multipurpose Telecenter Kinampanda, Mpwapwa na Mtwara.  Vituo hivi vinatumiwa na jamii katika kueneza matumizi ya TEKNOHAMA.

 

Fedha

 

40.    Sekta ya Fedha ni huduma ya kiuchumi ambayo ni mwezeshaji mkuu siyo tu wa shughuli za kiuchumi, bali pia hata miundombinu.  Kupanuka na kuendelea kwa Sekta ya Fedha kumechangia kwa kiasi kikubwa katika kuchangamsha biashara na kukua kwa uchumi.

 

41.    Kufikia mwaka 2004, Sekta ya Fedha iliweza kuchangia asilimia 12.1 katika Pato la Taifa.  Huduma za mabenki ziliimarika ambapo baadhi yake yalianza tena kutoa mikopo kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na mikopo kwa vyama vya ushirika kwa ajili ya kununulia mazao ya wakulima.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

SURA YA TANO

 

 

SEKTA YA HUDUMA ZA JAMII

 

Elimu

 

42.    Elimu ni nyenzo ya msingi katika jitihada za kujenga uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea na kuwawezesha kiuchumi wananchi.  Uchumi wa kisasa unahitaji watenda kazi wenye maarifa yanayohusu kanuni na maarifa ya kumudu vitendea kazi vya aina mbalimbali. Aidha, elimu ni sehemu ya mkakati muhimu wa Kitaifa wa kukabiliana na changamoto za utandawazi na modenaizesheni ya uchumi na sekta zote nyingine. Kwa kuzingatia hoja hizi, elimu imekuwa ikipewa umuhimu mkubwa na CCM na Serikali zake.

 

43.    Katika kipindi cha 2000-2005, Serikali imepanua, kuimarisha na kuboresha elimu kwa kiwango cha juu.  Bajeti ya elimu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka kwa lengo la kutekeleza majukumu katika sekta ya elimu.  Mgao wa Elimu katika Bajeti ya Serikali umeongezeka kutoka asilimia 21.8 mwaka 1999/2000 hadi kufikia asilimia 35.6 mwaka 2003/2004 kwa ajili ya kupanua, kuimarisha na kuboresha elimu.

 

Elimu ya Awali

 

44.    Elimu ya Awali ni muhimu katika kuwajenga watoto katika msingi imara wa elimu.  Mafanikio yaliyopatikana katika Elimu ya Awali ni kama ifuatavyo:-

 

(a)    Idadi ya shule za awali zilizoandikishwa, za Serikali na zisizo za Serikali, imefikia 12,984 mwaka 2004.

 

(b)    Madarasa ya Elimu ya Awali katika shule za msingi za Serikali yameongezeka kutoka 5,234 mwaka 2000 hadi kufikia 9,701 mwaka 2004.  Ongezeko hili la madarasa 4,457 ni sawa na asilimia 85.3.

 

(d)            Watoto wa umri wa miaka 5-6 walioandikishwa kwa Elimu ya Awali nchini wameongezeka kutoka 310,933 mwaka 2000 hadi 960,470  ikiwa ni ongezeko la watoto 649,537 sawa na asilimia 208.9.

 

Elimu ya Msingi

 

45.    Serikali ya CCM ya Awamu ya Tatu imeweka mkazo mkubwa kwenye elimu ya msingi ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanaostahili elimu hiyo wanaipata na wanaipata kwa kiwango kilicho bora.  Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imebuni Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) 2002-2006.  MMEM umeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia mashuleni.  Mpango huu umehakikisha kwamba yanakuwepo majengo mazuri na ya kutosha  ya shule, walimu, vitabu vya kiada na ziada, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na mkao sawa darasani.

 

46.    MMEM ukisaidiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kwa ushirikishaji  mkubwa wa wananchi umeleta mabadiliko makubwa katika sekta ndogo ya elimu ya msingi kama ifuatavyo:-

 

(a)    Kuanzia mwaka 2002 hadi 2004 yamejengwa madarasa 45,000; nyumba za walimu 8,527; kununuliwa madawati 285,898 na matundu ya vyoo 98,827.  Aidha kazi ya ujenzi wa majengo mapya ilikwenda sambamba na ukarabati wa majengo ya zamani nchi nzima.

 

(b)    Idadi ya shule za msingi za Serikali imeongezeka kutoka 11,608 mwaka 2000 hadi 13,533 mwaka 2004 ambalo ni ongezeko la shule 1,925 sawa na asilimia 16.6.

 

(c)    Lengo maalum la uandikishaji (GER) la asilimia 85 ifikapo mwaka 2002 lilivukwa kwa kufikia watoto wote walioandikishwa kuwa asilimia 98.6 ya idadi ya rika husika mwaka 2002 na kuongezeka hadi asilimia 106.3 mwaka 2004. GER       kwa jumla iliongezeka kutoka asilimia 77.6 mwaka 2000 hadi asilimia hiyo 106.3 mwaka 2004, lengo la Ilani likiwa limekiukwa.

 

(d)    Idadi ya wanafunzi katika shule za msingi imeongezeka kutoka 4,382,410 mwaka 2000 hadi 7,083,063 mwaka 2004.  Ongezeko hili la wanafunzi 2,700,653 ni sawa na asilimia 61.6.

 

(e)    Kima cha watoto wa rika lengwa la elimu ya msingi (miaka 7-13) walioko shuleni imeongezeka kutoka asilimia 58.8 mwaka 2000 hadi 90.1 mwaka 2004.

 

(f)     Upatikanaji wa vitabu vya kiada umeongezeka kutoka uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi 8 katika madarasa ya I-IV hadi wanafunzi 1.3.  Kwa madarasa ya V-VII.

 

(g)            Kiwango cha kufaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kimeongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2000 hadi asilimia 48.6 mwaka 2004.  Idadi ya wanafunzi walioendelea na masomo ya sekondari iliongezeka kutoka 74,432 mwaka 2000 hadi 147,490 mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 90.2.

 

(h)    Serikali imetoa mafunzo kwa Kamati za Shule za Msingi nchi nzima ili wajumbe wa Kamati hizo wajue wajibu na madaraka yao katika kupitisha na kusimamia mipango yote na matumizi ya fedha za shule.

 

(i)     Serikali imefuta ada na michango mbalimbali ya shule za msingi kwa lengo la kuifanya elimu ya msingi kuwa bure na lazima ili isiwe kikwazo kwa watoto wa familia maskini kujiunga na kubakia shuleni hadi wahitimu elimu hiyo.

 

                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                     

Elimu ya Sekondari

 

47.    Ili kupanua, kuimarisha na kuboresha elimu ya sekondari, Serikali imebuni Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) 2004-2009.

 

48.    Katika kipindi cha 2000-2005, hatua zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:-

 

(a)    Kutokana na juhudi kubwa za wananchi, idadi ya shule za sekondari imeongezeka kutoka 927 mwaka 2000 hadi 1,333 mwaka 2004.  Ongezeko hili la shule za sekondari 406 ni sawa na asilimia 43.8.

 

(b)    Idadi ya wanafunzi wa Kidato cha 1-6 imeongezeka kutoka 261,896 mwaka 2000 hadi 435,642 mwaka 2004 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 173,746 sawa na asilimia 66.3.

 

(c)    Idadi ya wanafunzi wasichana katika shule za sekondari imeongezeka kutoka 120,248 mwaka 2000 hadi 204,528 mwaka 2004.  Hili ni ongezeko la wanafunzi wasichana 84,280 sawa na asilimia 70.1.

 

(d)    Mwachano kati ya idadi ya wasichana na wavulana umezidi kupungua.  Wanafunzi wasichana walikuwa asilimia 45.9 ya wanafunzi wote mwaka 2000 na asilimia 46.9 mwaka 2004.

 

(e)    Serikali ilitenga ruzuku maalum katika Bajeti yake sh. 1.1         bilioni mwaka 2002; sh. 2.5  bilioni mwaka 2003 na sh.        4.3 bilioni mwaka 2004 kwa ajili ya kugharamia elimu ya sekondari ya watoto wa familia maskini.

 

(f)     Serikali imepunguza ada ya elimu ya sekondari katika shule za Serikali kutoka shilingi 40,000 hadi shilingi 20,000.

 

(g)    GER ya Kidato cha 1-4 imeongezeka kutoka asilimia 8.5 mwaka 2000 hadi asilimia 13.0 mwaka 2004.

 

(h)            GER ya Kidato cha 1-6 imeongezeka kutoka asilimia 6.4 mwaka 2000 hadi 7.4 mwaka 2004.

 

(i)     Ufaulishaji katika Mtihani wa Kidato cha 4 katika Daraja la I-III shule za serikali uliongezeka kutoka asilimia 35.6 mwaka 2000 hadi asilimia 45.6 mwaka 2004.

 

(j)     Ufaulu Kidato cha 6 Daraja la I-III uliongezeka kutoka asilimia 81.4 mwaka 2000 hadi asilimia 86.4 mwaka 2004.

 

Elimu ya Ualimu:

 

49.    Katika kuhakikisha kuwa mipango ya MMEM na MMES inatekelezwa ipasavyo, Serikali imeongeza nafasi za mafunzo ya ualimu na kutoa ajira mpya kwa walimu. Mafanikio yaliyopatikana kipindi kilichopita katika elimu ya ualimu ni kama ifuatavyo:

       

(a)    Idadi ya wanafunzi wa mafunzo ya ualimu tarajali wa Daraja A katika Vyuo vya Ualimu imeongezeka kutoka 3,303 mwaka 2000 hadi 24,873 mwaka 2004.  Ongezeko hili la wanafunzi 21,570 ni sawa na asilimia 653.0

 

(b)    Idadi ya wanafunzi wa mafunzo ya ualimu tarajali wa Stashahada katika Vyuo vya Ualimu imeongezeka kutoka 2,511 mwaka 2000 hadi 4,693 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 2,182 sawa na asilimia 86.9.

 

(c)    Jumla ya walimu wapya 37,261 wa Daraja A na Stashahada wameajiriwa kati ya mwaka 2000 na 2004.  Miongoni mwa walimu hao, 15,000 ni wale waliohitimu mafunzo ya ualimu miaka iliyopita wakati ajira ilipokuwa imesitishwa.  Uajiri wa walimu hao uliondoa kero kubwa iliyokuwa ikisemwa sana katika jamii.

 

(d)    Kuanzia mwaka 2003, wanafunzi wa mafunzo ya ualimu tarajali wamekuwa wakiajiriwa moja kwa moja baada ya kuhitimu mafunzo yao.

 

(e)    Kati ya mwaka 2000 na 2004, vibali vya ajira mbadala viliombwa na kutolewa ili kujaza mapengo ya jumla ya walimu 1,134 walioacha au kuachishwa kazi kutokana na sababu mbalimbali.

 

Elimu ya Juu

 

50.    Ili Taifa liweze kuwa na maendeleo endelevu na kuondokana na umaskini, elimu ya juu ni lazima ipewe kipaumbele.  Katika kipindi cha 2000-2005, elimu ya juu imepata mafanikio yafuatayo:-

 

(a)            Idadi ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki imeongezeka kutoka 14 mwaka 2000 hadi 20  mwaka 2004 ambalo ni ongezeko la vyuo 6 sawa na asilimia 42.9.

 

(b)            Idadi ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki Binafsi vimeongezeka kutoka 9 mwaka 2000 hadi 13 mwaka 2004 ambalo ni ongezeko la vyuo 4 sawa na asilimia 44.4.

 

(a)            Idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma imeongezeka kutoka wanafunzi 21,983 mwaka 2000 hadi wanafunzi 40,184 mwaka 2004 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 18,201 sawa na asilimia 82.8.

 

(b)            Idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu binafsi imeongezeka kutoka 1,373 mwaka 2000 hadi 2,764 mwaka 2004 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 1,391 sawa na asilimia 101.3.

 

(c)             Idadi ya wanafunzi wa kike katika vyuo vikuu imeongezeka kutoka 5,213 mwaka 2000 hadi 11,782 mwaka 2004 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 6,569 sawa na asilimia 126.01.

 

(d)            Kwa lengo la kupanua uwezo wa kutoa huduma za afya, Serikali imetoa udhamini kwa wanafunzi madaktari 256 wa mwaka wa kwanza (2004/2005) na 128 wa mwaka wa pili wanaosoma kwenye vyuo vikuu binafsi, na vyuo vikuu vya umma wenye udhamini binafsi.

 

(e)            Serikali imeanzisha Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa lengo la kusimamia Mfuko wa Elimu ili kuinua ubora wa elimu, kuongeza udahili wa wanafunzi na upatikanaji wa elimu hiyo kwa usawa.

 

(f)              Mfuko wa Elimu ulioanzishwa mwaka 2001, hadi kufikia Desemba 2004 ulikuwa umetoa shilingi bilioni 16.1 kwa taasisi za umma na binafsi.

 

(g)            Hadi kufikia Desemba 2004, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) lilikuwa limefanikiwa kuvipatia ithibati vyuo 22 na usajili vyuo 126 kwa lengo la kutoa elimu ya ufundi.

 

(h)            Mwaka 2004, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilikikabidhi Chuo cha TANESCO Morogoro kwa Taasisi ya Kiislamu (Islamic Foundation) kwa matumizi kama Chuo Kikuu.

 

(i)               Hadi kufikia Desemba 2004, Baraza la Ithibati la Elimu ya Juu (HEAC) lilikuwa limetoa ithibati kwa vyuo vikuu vya umma na binafsi 8, limesajili vyuo vikuu 11 na limetoa barua ya kuviendesha vyuo vikuu 4.

 

(j)               Kutungwa kwa Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu.

 

 

 

 

 

Elimu ya Ufundi

 

51.    Elimu ya Ufundi ina nafasi ya msingi katika kupanua maendeleo na matumizi ya sayansi na teknolojia ambayo ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea.  Elimu ya Ufundi imepata mafanikio yafuatayo katika kipindi cha 2000 - 2005:-

 

(a)            Idadi ya wanafunzi katika vyuo vya ufundi imeongezeka kutoka 2,049 mwaka 2000 hadi 2,103 mwaka 2004 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 54 sawa na asilimia 2.6.

 

(b)            Idadi ya wanafunzi wa kike katika vyuo vya ufundi imeongezeka kutoka143 mwaka 2000 hadi 245 mwaka 2004 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 102 sawa na asilimia 71.3.

 

(c)             Vyuo vya ufundi stadi vilivyosajiliwa na VETA vimeongezeka kutoka 574 mwaka 2000 hadi 794 mwaka 2004 ikiwa ni ongezeko la vyuo 220 sawa na asilimia 38.

 

(d)            Idadi ya wanafunzi katika vyuo vya ufundi stadi imeongezeka kutoka 4,525 mwaka 2000 hadi 15,554 mwaka 2004 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 11,029 sawa na asilimia 243.

 

(e)            Idadi ya wanafunzi katika vyuo vilivyosajiliwa na VETA imeongezeka kutoka 38,400 mwaka 2000 hadi 50,075 mwaka 2004 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 11,675 sawa na asilimia 30.

 

(f)              Uwiano kati ya wasichana na wavulana katika vyuo vya ufundi stadi VETA ulikuwa asilimia 21 mwaka 2000 na kuongezeka hadi asilimia 38 mwaka 2004.

 

(g)            Idadi ya stadi zinazofundishwa katika vyuo vya ufundi stadi zimeongezeka kutoka 38 mwaka 2000 hadi 90mwaka 2004 ikiwa ni ongezeko la stadi 52 sawa na asilimia 137.

 

 

(h)            Idadi ya walimu wanafunzi wa ufundi stadi imeongezeka kutoka 28 mwaka 2000 hadi 114 mwaka 2004 ikiwa ni ongezeko la walimu wanafunzi 86 sawa na asilimia 307.

 

 

Elimu ya Watu Wazima

 

52.    Ili kuzipa msukumo jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi na kujenga uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea, inabidi kutoa kipaumbele kwenye Elimu ya Watu Wazima, hususan elimu yenye manufaa ambayo inaendeleza maarifa ya kisasa yenye kuwasaidia wahusika kuongeza ufanisi na tija katika kazi zao wanazozifanya.  Mafanikio yaliyopatikana katika elimu ya watu wazima katika kipindi cha 2000 - 2005 ni haya yafuatayo:-

 

(a)            Kupunguza ongezeko la watoto na vijana wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa kutumia utaratibu mpya wa elimu ya msingi bure na ya lazima.

 

(b)            Serikali imeanzisha Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA).

 

(c)             Serikali imeboresha utoaji wa elimu ya watu wazima kwa kutumia mbinu shirikishi ya reflekti ambapo walengwa wanajifunza kusoma, kuandika na kuhesabu kwa namna inayowasaidia kujiongezea ujuzi katika shughuli zao za kiuchumi katika maeneo yao.

 

Afya

 

53.    Sekta ya Afya ambayo ina umuhimu mkubwa sana katika kupambana na umaskini na kuleta ustawi wa jamii imeshuhudia maendeleo makubwa katika miaka 10 ya uongozi wa Awamu ya Tatu.  Katika mageuzi yaliyoanzia 1993, mabadiliko yasiyo kifani yametokea katika Sekta ya Afya kufuatia kutekelezwa kwa shabaha ya kuinua kiwango cha ubora wa huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi, pamoja na kuboreshwa kwa ufanisi wa menejimenti na utendaji wenyewe.

 

54.    Katika kipindi cha 2000 hadi 2005, hatua zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:-

 

(a)            Kuanzisha na kutekeleza sera ya uchangiaji huduma za afya iliyolenga kuongeza uwezo wa Serikali kugharimia huduma za afya.  Kero mbalimbali zimeondolewa au kupungua sana kufuatia kutekelezwa kwa sera hiyo zikiwemo:-

 

(i)     Upatikanaji wa dawa na vifaa vya tiba katika hospitali umeongezeka.

 

(ii)    Kufanyika kwa ukarabati wa majengo ya kutolea huduma za afya palepale fedha zilipokusanywa kumeboresha huduma.

 

(iii)    Msamaha wa kuchangia gharama za huduma za afya kwa watoto, akina mama wajawazito, wasiojiweza pamoja na wagonjwa sugu ulitolewa na unaendelea kuwafaidia wahusika.

 

(b)    Kuanzishwa na kuendelea kuimarika kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.  Sera hiyo imewawezesha watumishi wa sekta ya umma kukabiliana na gharama za tiba kwa manufaa yao na wategemezi wao na imeendelea kupatikana kwa ubora stahiki.  Hadi kufikia Aprili, 2004 idadi ya wanachama imeongezeka kwa asilimia 44 kufikia 242,508, kulinganisha na 167,989 mwaka 2003.

 

(c)    Kuendelea kutolewa kwa huduma za chanjo kwa watoto kwa viwango vya kuridhisha na kufikia asilimia 90 kwa mwaka 2003/2004.  Kiwango hicho ni zaidi ya kile kinachokubalika kimataifa.  Kuhusu ugonjwa wa Polio, mafanikio makubwa yamepatikana ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO) limeiweka nchi yetu katika kundi la nchi zinazotazamiwa kutangazwa kuwa hazina ugonjwa huo.

 

(d)    Hospitali zimeongezeka kutoka 203 mwaka 2000 hadi 220 mwaka 2005.  Vituo vya afya vimeongezeka kutoka 367 mwaka 2000 hadi 395 mwaka 2005.  Limekuwepo pia ongezeko kubwa katika ujenzi wa zahanati kutoka 3,984 mwaka 2000 hadi 4408 mwaka 2005, likiwa ni ongezeko la asilimia Zahanati 424 sawa na asilimia 10.6.

 

(e)    Ukarabati mkubwa wa hospitali na majengo mengine ya tiba kuanzia Hospitali ya Taifa Muhimbili mpaka hospitali za wilaya umekamilika au uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.  Jumla ya majengo 475, vituo vya afya 60, hospitali 84 na vyuo vya afya 43 yalifanyiwa ukarabati huo.  Mashine za “X-ray” na “Ultrasound” na jenereta zimefungwa katika hospitali za wilaya, mikoa na rufaa.  Jumla ya Hospitali  98 za Serikali zikiwemo 70 za Wilaya, 20 za Mikoa,  4 maalum na 4 za rufaa zimehusika.

 

(f)     Tanzania ipo mstari wa mbele duniani katika vita dhidi ya malaria.  Katika bajeti ya 2004/2005 Serikali ilifuta kodi kwenye vyandarua na bidhaa zinazosaidia vita dhidi ya malaria pamoja na kuanzisha mpango wa hati punguzo.  Hali hiyo imesaidia sana kupunguza maambukizo ya malaria hasa kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga.  Uhamasishaji wa jamii kutumia vyandarua vyenye viuatilifu umeendelea.  Aidha, utekelezaji wa majukumu ya kutoa mafunzo kwa wataalamu mbali mbali wa afya katika kukabiliana na malaria; kutoa tiba sahihi na tiba ya tahadhari kwa wajawazito, utafiti; udhibiti wa milipuko ya malaria katika maeneo husika na katika ngazi ya jamii, vinaendelea kwa nguvu.

 

(g)    Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika miaka mitano iliyopita ziliendelea kutolewa zikiwa na mwelekeo wa kuongeza wingi na ubora wake.  Miongoni mwa mafanikio mbalimbali yaliyopatikana, ni kuendelea kutolewa bila malipo kwa huduma kwa wanawake wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.  Utaratibu huu umekuwa na mvuto mkubwa  nchini kote.

 

55.    Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI  imeendelea kutoa kipaumbele katika maeneo mbalimbali husika ikiwa na lengo la kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI na kutoa huduma kwa waathirika na kupata mafanikio ambayo baadhi yake ni yafuatayo:-

 

(a)    Katika kuhakikisha upatikanaji wa damu salama, Serikali ilinunua na kusambaza vipimo vya damu dhidi ya maambukizo ya UKIMWI (HIV Test Kits) 1,100,000 katika hospitali zitoazo damu kwa wagonjwa nchini.  Hatua hiyo ilinusuru watu zaidi ya 120,000 kupata damu yenye virusi na kuambukizwa na UKIMWI.

 

(b)    Vituo 400 kote nchini vinatoa huduma za Ushauri Nasaha vikiwemo na visivyo vya kiserikali. 

 

(c)    Dawa za kurefusha maisha kwa waathirika wa UKIMWI (ARV) zilinunuliwa kati ya mwezi Oktoba 2004 na mwaka 2005, na zilitolewa kwa waathirika 44,000.

 

Maji

 

56.           Hatua nyingi zilizochukuliwa katika kipindi cha 2000 – 2005 zililenga katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maji ya 2002 iliyotolewa baada ya kuifanyia mapitio ile ya 1991.  Sera imeweka msisitizo katika ushirikishwaji wa wanachi katika kupanga, kujenga, kuendesha na kumiliki miradi ya maji mijini na vijijini.  Mafanikio yake yamedhihirika katika maeneo yafuatayo:-

 

 

 

(a)    Serikali imeweka na kuboresha mtandao wa kuchunguza na kukusanya takwimu za maji yaliyopo juu na chini ya ardhi katika kuhakikisha rasilmali maji inapatikana kwa ubora na wingi unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya kijamii na kiuchumi.  Kati ya mwaka 2000 hadi 2004, Serikali iliendelea kuboresha mtandao huo kwa kuimarisha vituo 176 kwa ajili ya kukusanya takwimu kuhusu maji juu ya ardhi na vituo 3 kwa maji chini ya ardhi.

 

(b)    Kati ya mwezi Novemba 2000 hadi Disemba 2004 Serikali ilifanya utafiti katika maeneo mbalimbali nchini ili kutambua maeneo yanayofaa kuchimba visima vya maji kwa matumizi mbalimbali.  Zoezi hilo limeongeza maeneo ya kuchimba visima virefu na vifupi vya maji kutoka maeneo 497 mwaka 2000 hadi kufikia maeneo 1033 mwaka 2004.  Jumla ya maeneo 3082 yalipatikana kwa ajili ya kuchimba visima virefu na vifupi.

 

(c)    Kwa kutambua kwamba asilimia 43.4 ya rasilimali za maji katika nchi yetu zipo katika mabonde tunayoshirikiana na nchi nyingine, Serikali kati ya mwaka 2000 hadi 2004 ilifanya majadiliano na nchi husika ili kuweka utaratibu shirikishi na endelevu wa kusimamia matumizi na kutunza rasilmali maji chini ya Vyombo na Taasisi mbali mbali kama ifuatavyo:-

 

(i)     Kamati za Usimamizi na Uongozi za Mto Songwe.

 

(ii)    Kamati ya Majadiliano ya Bonde la Mto Nile (Nile Basin Initiative).

 

(iii)    Marekebisho ya Itifaki Juu ya Rasilimali za Maji Shirikishi katika nchi za SADC.

 

(iv)    Mkataba wa Makubaliano wa nchi za Tanzania, Msumbiji na Malawi.

 

(v)    Makubaliano ya Kuanzisha Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi.

 

(vi)    Itifaki ya Maendeleo Endelevu ya Bonde la Ziwa Victoria.

 

(d)    Katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2004 Serikali iliendelea kuimarisha mfumo wa kusimamia rasilimali ya maji katika mabonde 9 (Mto Pangani, Mto Rufiji, Ziwa Victoria, Mto Wami/Ruvu, Ziwa Nyasa, Ziwa Rukwa, Ziwa Tanganyika, Bonde la Kati la Ziwa Eyasi, Bububu na Manyara, na Mto Ruvuma).  Hadi kufikia Juni 2004, zilikwishafunguliwa Ofisi za Maji na Bodi za Maji za Mabonde yote 9 tofauti na awali zilipokuwa ofisi 2 tu.

 

(e)    Kumekuwepo na utaratibu na ufuatiliaji wa ubora na usafi wa maji ili kulinda afya za wananchi.  Mwaka 2000 sampuli za maji 13344 zilipimwa na Maabara Kuu na kuongezeka hadi kufikia sampuli 20707 mwaka 2004.

 

(f)     Kufuatia jitihada za ukarabati wa mifumo ya maji ya miji mikuu ya mikoa, upanuzi wa mifumo iliyopo, utafutaji wa vyanzo vipya na uimarishaji wa uwezo wa uendeshaji wa Mamlaka husika, kiwango cha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa mijini kimeongezeka kutoka asilimia 63.1 mwaka 2000 hadi asilimia 74 mwaka 2004.

 

(g)    Idadi ya wananchi vijijini wanaopata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao imeongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2000  hadi asilimia 53.5 mwaka 2004.

 

(h)    Hadi kufikia Desemba 2004, Kamati za Maji 8725 zilianzishwa ikilinganishwa na 6,086 zilizokuwepo mwaka 2000, likiwa ni ongezeko  la asilimia 43.4.

 

(i)    Mifuko ya maji vijijini iliongezeka kutoka 5,384 mwaka 2000 yenye thamani ya Sh. 765,700,890 hadi kufikia 7,254 yenye thamani ya Sh. 1,275,765,842/= mwaka 2004.

 

(j)     Mamlaka nane za maji mijini katika miji ya Arusha, Tanga, Moshi, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Tabora na Dodoma hivi sasa zinajitegemea katika gharama zote za uendeshaji zikiwemo za umeme, mishahara na madawa ya kusafishia maji.

 

(k)    Uwekezaji kwenye miradi ya maji  mijini na vijijini umeongezeka.  Hadi sasa imetekelezwa miradi yenye thamani ya Sh. 20.4 bilioni katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tabora, Arusha, Moshi na Tanga.  Vivyo hivyo, kwa upande wa uondoaji majitaka, miradi ya thamani ya Sh. 11.4 bilioni katika mikoa ya Morogoro, Tabora, Mwanza, Iringa, Arusha, Moshi na Mwanza imekamilika.

 

(l)     Ujenzi wa mradi  mkubwa wa maji kwa fedha za Serikali yetu kwa ajili ya wananchi wa miji ya Shinyanga na  Kahama kupitia vijiji kadhaa umeanza mwezi Mei 2004.   Awamu ya kwanza imepangwa kukamilika mwishoni mwa 2005.

 

(m)   Ukodishaji wa huduma za maji safi na maji taka jijini Dar es Salaam umekamilika.  Ukodishaji huu umewezesha kupata mkopo wa 164.6 bilioni zitakazotumika kuboresha huduma za maji jijini pamoja na maeneo ya Kibaha na Bagamoyo.  Kazi ya ukarabati wa miundombinu ya maji imeanza.  Kwa hatua hii matatizo ya maji yatapungua kama sio kutoweka kabisa.  Kutokana na mapato yatakayoongezeka katika kuboresha huduma ya maji, mradi hautategemea tena fedha kutoka Serikalini.

 

Ardhi na Maendeleo ya Makazi

 

57.    Makazi yaliyopangwa yanasaidia kuhakikisha kwamba kunakuwa na matumizi bora na endelevu ya rasilimali za ardhi.  Aidha, makazi yaliyopangwa na yenye miundombinu na huduma muhimu yanachangia katika kuongeza tija na kuendeleza uchumi wa watu wanaoishi katika maeneo hayo na hatimaye kupunguza umaskini.

 

58.    Maendeleo ya makazi yamepata mafanikio yafuatayo katika kipindi cha 2000 – 2005:-

 

(a)    Kutokana na uhaba wa viwanja katika miji nchini, mwaka 2002/2003 Serikali ilibuni na kutekeleza Mradi wa Kupima Viwanja 20,000 katika Jiji la Dar es Salaam.

 

(b)    Upimaji wa mipaka ya vijiji 2,048 umefanyika katika mikoa 8 kwa kutumia vifaa vya kisasa vya “Global Positioning System”.  Mikoa hiyo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Morogoro, Ruvuma, Shinyanga na Singida.

 

(c)    Jumla ya vikundi 22 vya ujenzi na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi wa gharama nafuu vimeanzishwa katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Kilimanjaro, Pwani, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Singida, Manyara, Arusha na Mara.  Vikundi hivyo vinaendesha shughuli za ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu kwa kutumia teknolojia rahisi na sahihi.

 

(d)    Halmashauri 25 zimepatiwa mikopo ya jumla ya shilingi                   310,128,665 kwa ajili ya kupima viwanja.

 

(e)    Shirika la Nyumba la Taifa limezifanyia matengenezo nyumba zake 15,875 nchini kote.

 

(f)     Shirika la Nyumba la Taifa limejenga nyumba za makazi na biashara 264 nchini kote zenye thamani ya shilingi bilioni 47.84. Shirika la Nyumba la Taifa limeuza nyumba ndogo ndogo na za kati 4,268.  Nyumba 660 zinaendelea kulipiwa na wateja kwa awamu.

 

(g)    Hadi Juni, 2004 watumishi 502 ambao ni sawa na asilimia 30.6 ya waombaji wote wameidhinishiwa mikopo na Bodi ya Mfuko wa Mikopo yenye jumla ya Shilingi 1.6 bilioni.

 

(h)    Mpango wa kutambua ardhi katika maeneo ya makazi yasiyopangwa Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwapatia wenye nyumba leseni za makazi, uliendelea kutekelezwa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

SURA YA SITA

 

 

UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM YA UCHAGUZI MKUU  WA MWAKA 2000 KWA UPANDE WA ZANZIBAR

 

 

Utangulizi:

 

59.    Historia ya uchaguzi kwa Zanzibar ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa inatoa taswira kwa vyama vya upinzani kutokubali matokeo yake pale vinaposhindwa, na hivyo kuitia nchi katika vurugu, fujo na uvunjifu wa amani.  Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1995 na yale ya mwaka 2000 yanadhihirisha kutokomaa kwa vyama vilivyoanzishwa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi kwani bado siasa za chuki, fujo na vurugu  ndio mtaji wao wa kisiasa na kutafuta huruma ya jumuiya ya Kimataifa.

 

60.    Kama ilivyotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1995 vyama vilivyoshindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2000, viliyakataa tena matokeo na  kuendeleza tabia ya vurugu, fujo na kuifikisha nchi katika hali mbaya ya kuitia doa kwa matukio ya tarehe 26 na 27 Januari, 2001.  Hata hivyo, baada ya matukio hayo, CCM kikiwa Chama tawala na kama ambavyo kilifanya baada ya vurugu na fujo zilizofuatia matokeo ya Uchaguzi wa mwaka 1995, kiliwajibika kutoa uongozi kwa kuiondoa nchi katika hali hiyo na kuirejesha katika amani na mshikamano.  Wajibu huu wa CCM kujitokeza na kutoa uongozi katika mazingira ya fadhaa kimsingi ni utekelezaji wa Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2000 hadi 2010, kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 114 (b)(kama ilivyo sasa).

       

61.    Ni kutokana na mazingatio hayo, haja ya mazungumzo ilijitokeza na Mwenyekiti wa CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin W. Mkapa, aliitisha mazungumzo hayo, ambayo hatimae yaliwawezesha Viongozi Wakuu wa CCM na CUF kutiliana saini makubaliano ya Muafaka hapo tarehe 10 Oktoba 2001, na kuwawezesha Wazanzibari  kuendelea  kuishi kwa umoja, amani na utulivu.

 

62.    Aidha, kutokana na utekelezaji  wa Sera sahihi za CCM, heshima ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla ilirejea na kutoa nafasi nzuri zaidi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na CCM kwa pamoja kuendeleza harakati za kuimarisha uchumi wa Taifa kwa kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na kupunguza kasi ya umaskini.

 

Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 2000 - 2005

 

63.    Mbali na misukosuko ya kisiasa iliyosababishwa na matukio ya tarehe 26 – 27 Januari 2001, hujuma za kigaidi za tarehe 11 Septemba 2001 nchini Marekani, vita vya Irak  pamoja na magendo ya karafuu yaliyoendeshwa na wapinzani,  utekelezaji wa  Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, kwa upande wa Zanzibar, umefanikiwa sana.   Mafanikio hayo yanajidhihirisha katika maeneo makuu yafuatayo:-

 

Kuimarisha Uchumi:

 

64.    Katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar, mafanikio yafuatayo 

         yamepatikana:

 

Kuimarisha utendaji na ukusanyaji wa Mapato ya Serikali

 

(a)   Sheria  za Kodi na Makampuni zimefanyiwa mapitio ya kina na kurekebishwa.  Miongoni mwa Sheria  hizo ni Sheria ya VAT, Hotel Levy, Stamp Duty, Mafuta, Ada ya Bandari na  Ada ya Uwanja wa Ndege.

 

(b)    Udhibiti wa mapato na matumizi ya fedha na mali za Serikali umeimarishwa.  SMZ imefungua hesabu zake katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na mfumo wa “Central Payroll System” na MTEF umeanzishwa na mafunzo kwa watendaji na elimu kwa walipa kodi imeendelea kutolewa.

(c)    Mfumo wa utendaji wa serikali, madaraka ya watendaji na uwajibikaji umefanyiwa tathmini na programu za mageuzi ya fedha na uchumi, utawala bora na mageuzi ya kitaasisi na watendakazi zimeanza kutekelezwa.

         

Kuendeleza ujenzi wa Misingi Mipya ya Uchumi

 

(d)    Sera mpya ya Uwekezaji yenye vivutio vingi zaidi imeanzishwa na Sheria ya Kulinda na Kuhifadhi Vitega Uchumi na kuundwa kwa Mamlaka moja ya Uwekezaji imepitishwa.

 

(e)  Jumla ya miradi mipya 67 yenye mtaji wa thamani wa (U$ 117,326,310) imeidhinishwa na miradi mingine minane yenye thamani ya (U$ 69.42) milioni imewekezwa na kuanza kutoa huduma katika Mamlaka ya Maeneo huru ya Kiuchumi.

 

(f)    Katika Mamlaka ya Bandari Huru, jumla ya miradi tisa imeanzishwa na kutoa fursa ya ajira kwa wafanyakazi   wazalendo 3210.  Aidha, Serikali imeingia mkataba na Kampuni binafsi wa kuliendeleza eneo huru la Fumba litakalojulikana kama “Zanzibar World Zone”.

 

(g)    Ili kuwavutia wawekezaji, eneo lote la Micheweni limepimwa lna kuwekwa mipaka.  Aidha, kazi ya ujenzi wa njia ya umeme hadi Nyamanzi pamoja na ofisi mbili katika eneo la Fumba, imekamilishwa.

 

Uimarishaji wa Taasisi na Mashirika ya Serikali.

 

(h)    Sheria ya Mitaji ya Umma ya mwaka 2002, imepitishwa  ili kuyawezesha mashirika ya Serikali kujiendesha kibiashara.

 

(i)        Miradi ya ujenzi wa majengo ya vitega  uchumi vya Mashirika yafuatayo, imekamilika na kuanza kutoa huduma za  kibiashara:-

 

(i)       Jengo la Kitega – Uchumi la Shirika la Biashara

        la Taifa (ZSTC) Kinazini – Unguja.

 

(ii)      Majengo ya  Afisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii

          (ZSSF) Kilimani – Unguja na Tibirinzi – Pemba.

 

(iii)      Jengo la Bandari huru – Maruhubi.

 

(j)     Shirika la Uvuvi na Shamba la Mipira, yamefanyiwa tathmini na kukodishwa pia Kiwanda cha Maziwa kimefanyiwa tathmini na kuuzwa  kwa mwekezaji wa ndani.

 

Manufaa ya Jumla

 

65.    Kutokana na mafanikio hayo ya utekelezaji wa sera za CCM na mageuzi ya kiuchumi, manufaa yafuatayo yameweza kupatikana:-

 

(a)    Kiwango cha mapato ya Serikali kimeongezeka kutoka T.Shs. 46.7 bilioni  mwaka 2000, hadi T.Shs. 51 bilioni mwaka 2004. 

 

(b)  Kiwango cha ukuaji wa uchumi kimeongezeka kutoka asilimia 4.2 mwaka 2000 hadi asilimia 6.5 mwaka 2004.

 

   (c)   Kiwango cha mfumko wa bei kimeendelea kuwa chini ya wastani wa asilimia 10.

 

Sekta ya Uchumi

 

66.    Kwa upande wa sekta ya Uchumi, mafanikio yafuatayo  

yamepatikana:-

 

Kilimo

       

(a)    Vituo vya Utafiti wa Kilimo cha Kizimbani – Unguja na Matangatuani Pemba, vimeimarishwa.  Aidha, Sheria ya uanzishaji wa Chuo cha Kilimo – Kizimbani, imepitishwa.

 

(b)            Wakulima wadogo wadogo 160 na vikundi 52 vya wanawake, wamepatiwa mafunzo na mbinu za kilimo bora, matumizi ya mbolea za kimaumbile na kilimo mchanganyiko.

 

(c)             Wafanyakazi 122 wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ndani na nje ya nchi.  Tafiti mbali mbali  zimefanywa ili kuendeleza uzalishaji wa mbegu bora za mazao  ya chakula na biashara. Wastani wa miche 300,000 ya mikarafuu imeoteshwa na kusambazwa kwa wakulima kila  mwaka.

 

(d)            Mpango Mkuu wa Kilimo cha Umwagiliaji maji (Zanzibar Irrigation Master Plan), umeandaliwa na kukamilishwa. Jumla ya hekta 8,000 zimeonekana kufaa kwa kilimo hicho.

 

Mifugo

 

(e)     Huduma za kinga na tiba kwa mifugo, zimeendelezwa.  Jumla ya ng’ombe 23,520 walipatiwa chanjo dhidi ya maradhi ya vibuma, mbavu, miguu na midomo na mbwa 2,655 walipatiwa chanjo dhidi ya maradhi ya kichaa cha mbwa.

 

(f)     Ili kuwaendeleza wafugaji, Jumuiya ya Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa na Jumuiya ya Wafugaji wa Kuku zimeanzishwa.  Wafugaji wadogo wadogo 242, wamepatiwa mafunzo na taaluma za ufugaji bora na wananchi 310 wamepatiwa ng’ombe wa maziwa baada ya kupatiwa mafunzo ya utunzaji wa ng’ombe hao chini ya mpango wa “kopa ng’ombe lipa ng’ombe”.

 

(g)    Kiwanda cha Maziwa cha Maruhubi baada ya kubinafsishwa, kimefufuliwa na kuanza kazi ya usindikaji wa maziwa na mtindi.  Hatua hii imetoa fursa nzuri ya soko la maziwa kwa wafugaji. 

 

Uvuvi 

 

(h)    Wavuvi wadogo wadogo katika vijiji 19 Unguja na Pemba, wamepatiwa mafunzo na mikopo ya vifaa na zana za uvuvi.   Wananchi wa vijiji viliyopo chini ya Mradi wa Menai wamepatiwa mafunzo  na msaada wenye thamani ya T.Shs. 12.4 Milioni ili kuendeleza miradi yao ya kijamii na kiuchumi.

 

(i)     Utafiti wa zao la mwani aina ya “Cottonii”, umefanyika na wakulima kupatiwa mafunzo na mbinu bora za uzalishaji.

 

(j)     Ujenzi wa soko jipya la samaki la Malindi, umekamilika. 

Aidha, kuimarika kwa Sekta ya Utalii, kumepanua sana soko     la mazao ya baharini hasa samaki, pweza, kamba n.k.

 

Mazingira

 

(k)    Wananchi wamehamasishwa na kuelimishwa juu ya athari za uchafuzi wa mazingira.  Jumuiya na vikundi 14 vya kijamii  vimeanzishwa ili kusimamia hifadhi na utunzaji wa mazingira   katika maeneo yao. Siku ya Mazingira Duniani (tarehe 1 – 5 Juni) imeadhimishwa kila mwaka.

 

(l)    Ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda umefanywa na miongozo ya kufuatwa na wenye viwanda ili kuhifadhi    mazingira imetolewa. 

 

(m)  Utunzaji wa misitu ya asili na maeneo maalum ya baharini umeimarishwa.  Jumla ya miti 56,200 imepandwa katika maeneo mbali mbali mijini na vijijini na Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Jozani imeanzishwa.

 

 

 

 

 

Utalii

 

(n)    Mpango Mkuu wa Kuendeleza Shughuli za Utalii (Tourism Master Plan) umeandaliwa. Kikosi cha Ulinzi wa Watalii (Tourism Patrol) kimeanzishwa. Chuo cha Hoteli cha Maruhubi kimeimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kisasa na wataalamu.

 

(o)    Hatua ya kuitangaza Zanzibar katika maonyesho mbali mbali ya Kimataifa ili kupanua wigo wa masoko mapya imetekelezwa.

 

(p)    Ili kuwavutia watalii wa daraja la kwanza, ujenzi wa hoteli kubwa za kisasa umeendelezwa.  Miradi ya ujenzi wa Renco Hotel Ltd, Zamani International na Ocean Beach Resort, imeanzishwa huko Nungwi na Kiwengwa.

 

Viwanda

 

(q)    Rasimu ya Sera na Mpango wa Viwanda Vidogo Vidogo na vya Kati, imekamilishwa.  Viwanda vipya vitatu (Zanzibar Kool, Kiwanda cha Kokoto na Kiwanda cha Chokaa) vimeanzishwa chini ya sekta binafsi na kutoa fursa ya ajira kwa wananchi.

 

(r)     Vikundi 45 vya wanawake, vimepatiwa mafunzo na ujuzi wa kusindika vyakula vya matunda.  Aidha, mfuko maalum wa kuwaendeleza wazalishaji wadogo wadogo umeanzishwa na maeneo ya Saateni na Maruhubi yametengwa kwa shughuli za uzalishaji na maonyesho ya kibiashara.

 

(s)    Kiwanda cha ushoni cha Vikosi vya SMZ kimeanzishwa.

 

Biashara

 

(t)     Sera mpya ya Biashara imeandaliwa na Jumuiya ya Wafanya biashara, Wenye Viwanda na Wakulima imeundwa upya.  Aidha, mazungumzo na nchi mbali mbali duniani yameendelezwa ili kukuza ushirikiano na kupanua soko la biashara.

 

(u)    Sheria ya Mizani na Vipimo imefanyiwa mapitio na

kurekebishwa.   Vikwazo katika uendeshaji wa biashara vimeondoshwa na wafanyabiashara wa ndani wamehamasishwa kuuza bidhaa zaidi nje ya nchi.  Bidhaa zisizo za asili  zimezalishwa na kusafirishwa nje ya nchi.

 

Ardhi

 

(v)    Ardhi imeendelea kuwa ni mali ya Serikali.  Sheria ya umilikaji ardhi ambayo inaruhusu ardhi kutumika kama dhamana na kuwawezesha wananchi kupata mikopo kutoka katika vyombo vya fedha, imepitishwa.

 

(w)   Jumla ya viwanja 4,234 vimepimwa na kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makaazi, vitega uchumi, kilimo na biashara.  Mbinu za udhibiti na ukusanyaji wa mapato na kodi za viwanja  zimeimarishwa. 

 

Ushirika

 

(x)    Kwa kushirikiana na Shirika la ILO, programu maalum ya Uimarishaji wa Sekta ya Ushirika imeanzishwa na Sheria ya Vyama vya Ushirika imefanyiwa mapitio na kurekebishwa.

 

(y)    Kazi ya ukaguzi wa vyama vya ushirika na utoaji wa mafunzo, imeendelezwa. Jumla ya vyama vya ushirika 43 vimeanzishwa na kusajiliwa rasmi.

       

Miundombinu ya Kiuchumi

 

67.    Katika sekta ya Miundombinu ya Kiuchumi, mafanikio yafuatayo yamepatikana:-

 

Barabara

 

(a)   Jumla ya km 120.55 za barabara, zimejengwa kwa kiwango  cha lami na kukamilika, kama ifuatavyo:-

 

Ø         Unguja

 

·        Makunduchi    Mtende   km 5.5    (Barabara kuu)

·        Kitogani        Paje     km 11.2     (Barabara ya Vijijini)

·        Kaebona      Kaepwani   km 4.5   (Barabara ya Vijijini)

·        Bambi         Njia nne   km 6        (Barabara ya Vijijini)

·        Amani         Welezo   km 0.75     (Barabara ya Mjini)

·        Mazizizini –    Chukwani   km 7      (Barabara ya Mjini)

·        Kidimni   _   Kitope/Kitundu, Ndagaa na Machui

  Ring roads  29.6        (Barabara ya Vijijini)

 

Ø         Pemba

 

·        Chake           Vitongoji     km 7        (Barabara Kuu)

·        Chake           Wesha        km 7        (Barabara kuu)

·        Kilindini       Micheweni  km 6        (Barabara ya Kijijini)

·        Mkoani         Chake        km 36      (Barabara kuu)

 

(b)   Jumla ya km 32.2 za barabara zimeanza kujengwa na kazi bado    inaendelea.  Barabara hizo ni:-

 

Ø         Unguja

 

·        Jang’ombe    -  Mpendae    km 1.2    (Barabara ya Mjini)

·        Amani            Mtoni        km 4      (Barabara ya Mjini)

·        Mahonda       Donge/Mkokotoni   km 14    (Barabara ya Vijijini)     

 

 

 

 

 

 

Ø     Pemba

 

·        Mtuhaliwa   -  Chokocho     km 13    (Barabara ya Vijijini)

 

(c)   Sheria ya kusimamia matumizi ya barabara na vyombo vya moto, imerekebishwa.  Huduma ya usafiri hasa Mjini na Ukaguzi wa magari umeimarishwa.

 

Huduma za Posta na Simu

 

(d)    Shirika la Posta Tanzania, limeendelea na juhudi zake za kuimarisha huduma za usafirishaji wa barua, vifurushi, fedha na mawasiliano ya internet kati ya Zanzibar na nchi nyingine duniani.

  

(e)            Kampuni ya Simu Tanzania (TCCL) kwa kushirikiana na makampuni mengine binafsi ya simu za mikononi (ZANTEL, MOBITEL, VODACOM na CELTEL) imeendelea kuimarisha huduma za simu kwa wananchi mjini na vijijini.  Aidha, idadi ya watumiaji wa simu imeongezeka kutoka asilimia 8 mwaka 2000 hadi asilimia 15 mwaka 2004, na kufanya Zanzibar kufikia nafasi ya kwanza Barani Afrika kwa watumiaji wa simu.

 

Bandari

 

(f)     Kazi ya upembuzi yakinifu na utayarishaji wa zabuni ya matengenezo ya bandari ya Malindi,  ujenzi wa chelezo cha Malindi  na ujenzi wa barabara itokayo chelezoni hapo hadi bandarini zimekamilika.

 

(g)    Gati ya Wete imefanyiwa matengenezo na kuanza kutoa huduma kwa majahazi na meli za aina ya landing craft”.  Minara yote ya kuongozea meli imefanyiwa matengenezo na kuwekewa taa zenye kutumia nguvu za jua “solar – power”.    Maboya mapya 18, boti ya kuongozea meli na tishali vimenunuliwa.

 

Usafiri wa Majini

 

(h)     Shirika la Meli limeweza kujiimarisha kwa kuzifanyia

matengenezo makubwa meli zake zote (m.v Mapinduzi, m.v. Maendeleo na m.v. Ukombozi) na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kuingia ubia na wawekezaji binafsi.

 

(i)     Makampuni binafsi ya Azam Marine, Sea Star Service, Afrika Shipping, Sea Express, Mkunazini Shipping Enterprise na Panda II Enterprise yameendelea kuwekeza na kuongeza idadi ya boti za abiria na meli za mizigo.

 

Usafiri wa Anga

 

(j)     Utayarishaji wa Mpango Mkuu wa Uendelezaji wa kiwanja cha ndege cha Unguja, umekamilika.  Aidha, kazi ya utanuzi wa njia ya kurukia ndege imeanza kutekelezwa.

                                                                         

(k)    Wafanyakazi wa viwanja vya ndege wamepatiwa mafunzo na vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa abiria na mizigo. Majengo ya abiria na kumbi za wageni mashuhuri (VIP) yamefanyiwa matengenezo.  Aidha, njia ya kurukia ndege katika Uwanja wa Karume – Pemba, imejengwa upya.

 

Umeme

 

(l)     Kazi ya usambazaji umeme katika Vijiji (88) imekamilika, kati yake (57) vya Unguja na (31) vya Pemba.  Kituo cha usambazaji umeme cha Mpendae – Unguja na vinu vyote (3) vya umeme Kisiwani – Pemba, vimefanyiwa matengenezo makubwa.  Hatua hii imewezesha asilimia 80 ya vijiji vya Zanzibar, kuwa na huduma ya umeme.  Aidha, asilimia 53 ya makaazi (House hold) na asilimia 55 ya wananchi wote wa vijijini kufikishiwa huduma ya umeme.

 

(m)  Jumla ya  “transforma” 30 zilizokuwa na uwezo mdogo au kuharibika, zimebadilishwa na njia mpya ya umeme mkubwa (HT) yenye urefu wa Km 10,452 na Km 7,133 za umeme mdogo (LV) zimejengwa Unguja na Pemba.

 

(n)   Vituo vipya 39 vya kusambazia umeme vimejengwa Unguja na Pemba na mita 13,500 za umeme wa TUKUZA zimesambazwa katika maeneo mbali mbali ya Mji wa Zanzibar.

 

(o)    Mbinu za udhibiti na ukusanyaji wa mapato zimeimarishwa na mauzo ya umeme yameongezeka kwa kiwango cha asilimia 80.  Aidha, utafiti wenye lengo la kufahamu bei muafaka ya kuuzia umeme ili kuwavutia wawekezaji na kupunguza umaskini umefanywa.

       

Huduma za Jamii

 

68.    Katika sekta ya Huduma za Jamii, mafanikio yafuatayo 

yamepatikana:-

 

Elimu

 

(a)    Kiwango cha uandikishaji wa watoto waliofikia umri wa kuanza elimu ya msingi (darasa la kwanza) kimeongezeka kutoka asilimia 94.6 mwaka 2000 hadi asilimia 100 mwaka 2004.  Mafanikio haya yameiwezesha Zanzibar, kuvuka kiwango cha malengo ya milenia ya kimataifa kabla ya mwaka 2015.

 

(b)    Madarasa 133 yalifanyiwa matengenezo na mengine mapya 783 yamejengwa.  Madawati 15,833 na meza 2,657 zimenunuliwa na kusambazwa katika skuli mbali mbali.

 

(c)    Idadi ya skuli za Serikali na binafsi zimeongezeka kutoka 331 mwaka 2000 hadi 465 mwaka 2004.  Jumla ya skuli 66 za maandalizi zimefunguliwa, mbili za Serikali na 64 za binafsi.  Skuli za msingi 28 zimefunguliwa, 21 za Serikali na 7 za binafsi.  Aidha, Skuli 20 za msingi na kati zimefunguliwa, 16 za Serikali na 4 za binafsi.  Kwa upande wa sekondari, skuli 23 zimefunguliwa, zikiwemo 20 za Serikali na 3 za binafsi.    Aidha, ujenzi wa skuli ya Sekondari ya Mchepuo wa Biashara – Tomondo, umekamilika na kuanza kutoa huduma.

 

(d)    Idadi ya vijana waliofaulu kujiunga na Kidato cha   Tatu  imeongezeka kutoka asilimia 31.6 mwaka 2000 hadi asilimia  43.1 mwaka 2004.  Kidato cha nne asilimia 77.3 mwaka 2000 hadi asilimia 92.3 mwaka 2003.  Kidato cha tano,    kutoka wanafunzi 305 mwaka 2000 hadi 2,076 mwaka 2004.

 

(e)  Kituo cha Taifa cha Walimu kimeanzishwa na vituo tisa vya Kanda vimejengwa katika kila Wilaya.  Chuo cha Ualimu cha Nkurumah kimefanyiwa matengenezo makubwa na Chuo cha Ualimu Wete – Pemba, kimeanzishwa.  Idadi ya Vijana wanaojiunga na mafunzo ya ualimu, imeongezeka kutoka 962 mwaka 2000 hadi 2653 mwaka 2004.  Aidha, mafunzo ya Diploma ya Elimu ya Msingi yameanzishwa.

 

(f)     Skuli za Ufundi za Mikunguni na Kengeja zimeimarishwa na kupatiwa vifaa.  Chuo cha Ufundi cha Karume, kimepatiwa  maabara na vifaa vya kisasa na kuwa kituo cha Mafunzo kwa jamii na mawasiliano ya moja kwa moja (Video Conferencing).

 

(g)    Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) kimeanzishwa, na kufanya idadi ya vyuo vikuu vya Zanzibar kufikia vitatu. Chuo  kimeanza kufundisha masomo ya Ualimu wa Sanaa,  Lugha, na Sayansi ili kuwaandaa walimu wa skuli za sekondari.

 

Elimu ya Watu Wazima

 

(h)    Kiwango cha idadi ya watu wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu kimeongezeka kutoka asilimia 60 mwaka 2000 hadi asilimia 73.4 mwaka 2004.  Idadi ya madarasa ya kisomo cha elimu ya watu wazima imeongezeka kutoka 329 mwaka 2000 hadi 446 na ile ya wanakisomo imeongezeka kutoka 5114 hadi 8,007 katika kipindi hicho.

 

(i)     Idadi ya vituo vya elimu ya amali, imeongezeka kutoka 39, mwaka 2000 hadi 72  mwaka 2004.  Aidha, idadi ya vituo vya  kujiendeleza (Qualifying test) vimeongezeka kutoka 21 na wanafunzi 2,298 mwaka 2000 hadi 42 na wanafunzi 4,938 mwaka 2004.

 

Utamaduni na Michezo

 

(j)     Rasimu za Sera za Utamaduni na Michezo zimekamilika.  Sheria za Uundaji wa Baraza la Sanaa, Baraza la Kiswahili la Zanzibar na Mfuko wa Kutunza Kumbukumbu za Historia ya Zanzibar, zimepitishwa. Aidha, Bodi  ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonyesho imeundwa upya na Umoja wa Waandishi wa Vitabu na Washairi, umeanzishwa. Huduma za makumbusho zimeimarishwa na Makumbusho Kuu ya kisasa imeanzishwa katika jengo la Beit-el-Ajab.

 

(k)    Michezo ya aina mbali mbali imeimarishwa hususan mpira wa miguu ambapo timu ya vijana walio na umri chini ya miaka 19 ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati  mwaka 2003.  Chama cha Mpira wa miguu (ZFA) kimefanikiwa kupata uanachama kamili wa Shirikisho la Mchezo wa Mpira wa Miguu kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na Shirikisho la Afrika (CAF) na juhudi za kuwa mwanachama kamili wa FIFA zinaendelea.

 

Afya

 

(l)     Elimu ya Afya imeendelea kutolewa na Wananchi 

wameelimishwa jinsi ya kujikinga na aina mbali mbali ya maradhi ya kuambukiza.  Kamati za malaria na maradhi ya kuambukiza zimeanzishwa katika ngazi za Wilaya na Shehia. Idadi ya vyandarua 31,400 vyenye dawa vimesambazwa kwa wananchi na matumizi ya vyandarua yameongezeka kutoka asilimia 3 mwaka 2000 hadi asilimia 20 mwaka 2004.

 

(m)  Huduma za matibabu kwa wananchi zimeimarishwa na Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Hospitali ya Wagonjwa wa Akili ya Kidongo Chekundu kwa Unguja na Hospitali za Mkoani, Chake na Wete kwa Pemba zimefanyiwa matengenezo makubwa na kupatiwa vitendea kazi, madawa na vifaa vya kisasa.  Jumla ya vituo vipya vya afya (12) vimejengwa, vinane kwa Unguja na vinne Pemba, chini ya Mpango wa Kuwashirikisha Wananchi wenyewe katika maeneo yao.

 

(n)    Huduma za Mama na Mtoto zimeendelezwa na asilimia 90 ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano wamepatiwa huduma za chanjo.  Aidha, watoto 139 wenye matatizo ya moyo walipelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi.

 

(o)    Viwango vya malipo na maslahi ya wafanyakazi wa Sekta ya Afya vimerekebishwa na mpango wa mafunzo umeendelezwa.  Jumla ya wafanyakazi 92 wamepatiwa mafunzo katika Chuo cha Afya – Mbweni, 288 walipelekwa Tanzania Bara  na 30 walipelekwa nje ya nchi.

 

Vita dhidi ya Ukimwi

 

(p)  Tume ya UKIMWI Zanzibar imeanzishwa na rasimu ya Mpango wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria imekamilika.  Aidha, rasimu ya Mpango wa Kuimarisha  huduma za Maabara kwa lengo la kupunguza maambukizo ya UKIMWI kutoka kwa Mama na Mtoto imekamilika.

 

(q)   Kitengo cha kudhibiti UKIMWI (ZACP), Kamisheni ya UKIMWI (ZAC) pamoja na Asasi mbali mbali zisizokuwa za Serikali (AZISE)  zimeendeleza juhudi ya kuelimisha wananchi jinsi ya kujikinga na UKIMWI.  Jumla ya vituo 12 vya ushauri nasaha na huduma za upimaji wa VVU vimefunguliwa.  Huduma za ufuatiliaji wa wagonjwa wa UKIMWI na kuwapatia tiba zimeanzishwa.

 

Maji

 

(r)     Hatua za kuwawezesha wananchi  kupata huduma ya maji safi na salama  mijini na vijijini, imeendelea kutekelezwa. Jumla ya miradi (75) ya maji vikiwemo visima vipya 18 na matangi mapya 14 ya kuhifadhia maji yenye ujazo tofauti yamejengwa, kati yake 6 kwa Unguja na 8 kwa Pemba.

 

(s)    Jumla ya vijiji 95 na wakaazi 495,508 wamepatiwa huduma  ya maji safi na salama, kati yake vijiji 28 na wakazi 124,407 wa Pemba na vijiji 67 yakiwemo baadhi ya maeneo ya Mji wa Zanzibar na wakaazi 371,104 wa Unguja.  Mafanikio haya yamewezesha asilimia 70 ya wananchi wote wa Zanzibar mijini na vijijini kupatiwa huduma ya maji safi na salama.

 

(t)     Sera ya Maji ya Taifa, tayari imekamilika.  Aidha, kazi ya usanifu wa mradi wa maji kwa Mji wa Zanzibar, chini ya msaada wa Japan, imekamilika.

 

Makaazi

 

(u)    Kazi ya ujenzi wa nyumba bora za kisasa imeendelezwa kwa kasi kubwa.  Jumla ya nyumba 30 za mkopo nafuu katika    eneo la   Mombasa Unguja, fleti 24 katika nyumba za maendeleo Michenzani tayari zimekamilika na ujenzi wa fleti 24 nyingine umo katika hatua za mwisho.  Aidha, ujenzi wa nyumba Nam. 10 Michenzani, ambayo itakuwa na jumla ya fleti 142 pamoja na maduka unaendelea.

 

(v)   Jumla ya nyumba 22 zilizomo katika eneo la Mamlaka ya Mji Mkongwe, zimefanyiwa matengenezo makubwa na majengo mengine 827 yamefanyiwa matengenezo ya kawaida.

 

(w)   Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar imeendelezwa na kuingizwa katika orodha wa UNESCO wa urithi wa Kimataifa. Mji wote wa Zanzibar sasa umekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Miji ya Urithi wa Kimataifa “Organisation of World Heritage Cities” (OWHC).

 

Vyombo vya Habari

 

(x)    Studio za TVZ zimeimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kisasa na kituo cha Mkanjuni – Pemba, kimepatiwa mtambo  mpya wa kurushia matangazo.  Aidha, mpango wa kuunganisha matangazo ya TVZ na BBC  umeanzishwa.

 

(y)    Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) imeimarishwa, Studio ya Pemba imepatiwa vifaa vya kisasa na utaratibu wa kurusha matangazo yake ya moja kwa moja, umeanzishwa.

 

(z)    Tume ya Utangazaji imeanzishwa.  Radio “Spice FM” ya Sauti ya Tanzania Zanzibar, Televisheni mbili za binafsi (Zanzibar Cable Television na Furaha Cable Television)  zimeanzishwa. 

 

(aa)  Chuo cha Waandishi wa Habari (chini ya Idara ya Habari  Maelezo) kimeimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kisasa na Asasi nne zisizokuwa za Serikali za waandishi wa habari (Zanzibar Press Club, Pemba Press Club, Zanzibar Media Women Forum na Journalist Association of Zanzibar) zimeanzishwa.

(bb) Mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya habari yameendelea kutolewa na jumla ya wafanyakazi 84 wamepatiwa fursa za masomo.

 

Maeneo Mengine Ya Kipaumbele

 

69. Katika maeneo mengine muhimu, mafanikio yafuatayo yamepatikana:-

 

Utawala Bora 

 

(a)    Ili kuimarisha utawala wa sheria, uwazi, uadilifu na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali, Wizara ya Nchi (AR) Katiba na Utawala Bora imeanzishwa na mabadidliko ya Nane na Tisa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 yamepitishwa.  Aidha, bendera ya Zanzibar imeanzishwa.

 

(b)   Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imeanzishwa na Sheria ya Mwenendo wa Jinai imerekebishwa ili kutoa fursa kwa waendesha mashtaka wa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kufanya  usimamizi na uendeshaji wa kesi mahakamani  badala ya Polisi. Aidha sheria mbali mbali zimeimarishwa na kurekebishwa.

 

Demokrasia

 

(c)    Elimu ya uraia imeendelea kutolewa na dhana ya haki za binadamu, demokrasia, utawala bora na wajibu wa watumishi wa umma katika mfumo wa vyama vingi imepewa msisitizo.

 

(d)    Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar imefanyiwa marekebisho. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imerekebishwa na Daftari la Kudumu la Wapiga kura limeanzishwa.

 

 

 

 

Madaraka ya Wananchi

 

(e)  Rasimu ya awali ya Sera mpya  ya Serikali za Mitaa, imetayarishwa na kuwasilishwa kwa wadau mbali mbali.

 

(f)     Kamati za maendeleo za Mikoa na Wilaya zimeanzishwa. Katika ngazi ya Shehia kamati za maendeleo zimeundwa na kuwashirikisha kikamilifu wananchi katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo.  Jumla ya miradi 73 yenye thamani ya T.Shs. 2,246,761,187/= imetekelezwa chini ya mpango wa TASAF, kati yake  33 ikiwa Pemba na 40 Unguja.  Wananchi  wamechangia asilimia 20 ya gharama zote za miradi hiyo. 

 

Vita Dhidi ya Rushwa

 

(g)    Ili kujenga mazingira mazuri ya kuendeleza vita dhidi ya rushwa. uamuzi wa kuunganisha masuala ya rushwa na maadili ya viongozi na kuunda taasisi moja ya kuzuia rushwa na kusimamia maadili ya viongozi, umefikiwa.  Rasimu ya awali ya Muswada wa Sheria ya Kuzuia Rushwa na Kusimamia Maadili ya Viongozi, tayari imekamilika na Mpango wa Zanzibar wa Kuimarisha Utawala Bora, umeandaliwa.

 

Ulinzi na Usalama

 

(h)  Vikosi vyote vya SMZ vimeimarishwa kwa kupatiwa mafunzo, vifaa na vitendea kazi. Sheria ya kuanzishwa kwa Kikosi cha Valantia imepitishwa ili kukipa nguvu za kisheria katika utekelezaji wa kazi na majukumu  yake.

 

(i)   Vikosi vya SMZ kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Polisi, vimeshiriki kikamilifu katika kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao na kushiriki  katika shughuli mbali mbali za maendeleo ukiwemo ujenzi wa nyumba za  Michenzani.

(j)  Vikosi vya SMZ, hususan KMKM vimeshiriki  katika  mapambano dhidi ya magendo ya karafuu na hujuma nyingine za uchumi na  kujenga mahusiano mema na wananchi wanaoishi karibu na maeneo yao.   Chuo cha Ufundi cha JKU kinatoa mchango mkubwa katika kuwapatia vijana elimu ya amali na stadi mbali mbali za ufundi.

 

Kuyaendeleza Makundi Mbali Mbali

 

70.    Katika kuyaendeleza makundi mbali mbali ya kijamii, mafanikio yafuatayo yamepatikana:-

 

Watoto

 

(a)    Sera ya Uhai, Hifadhi na Maendeleo ya watoto, imetayarishwa na utafiti wenye lengo la kufahamu ukubwa wa tatizo la ajira kwa watoto “rapid assessment” umefanywa.  Mafunzo yametolewa  kwa wadau mbali mbali juu ya Mkataba Nam. 182 na 138 wa ILO kuhusiana na suala la ajira kwa watoto.

 

Wanawake

 

(b)    Hatua ya kurekebisha sheria zinazowabagua na   

kuwadhalilisha wanawake katika usawa na maslahi yao imetekelezwa. Sheria ya makosa ya kujamiiana na sheria ya kuwalinda wari, wajane na vizuka, zimerekebishwa na Sera ya Hifadhi na Maendeleo ya Wanawake, imetayarishwa.

 

(c)    Mradi maalum wa kuinua kipato cha wanawake ili kupunguza ajira mbaya kwa watoto umeanzishwa. Jumla ya vijana wanawake 3,434 wameunganishwa na mashirika yanayotoa mikopo likiwemo PRIDE, WEDTF na CHANGAMOTO na kupatiwa mikopo yenye thamani ya T.shs. 405 milioni.

 

(d)    Hatua ya kuwashirikisha  wanawake katika ngazi mbali mbali za maamuzi ya kisiasa, utawala, uongozi na menejimenti, imeendelea kutekelezwa.  Marekebisho ya Nane ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,  yameongeza idadi ya viti vya wanawake katika BLW (viti maalum) kutoka asilimia 15 hadi 30.  Aidha, wanawake wamepatiwa nafasi za elimu na kuwa na mazingira mazuri ya kupata elimu kuanzia skuli za msingi hadi vyuo vikuu.

 

Vijana

 

(e)    Sera ya Maendeleo ya Vijana imetayarishwa na rasimu ya awali ya Sera ya Elimu  ya Amali na Mafunzo, imekamilika.  Mradi wa Elimu Mbadala na Mafunzo ya Elimu ya Amali umeanzishwa na  Kituo cha Elimu ya Amali cha Mwanakwerekwe kimefanyiwa matengenezo na kuimarishwa.

 

(f)  Jumla ya vijana 1,534 wamepatiwa ajira kupitia sekta binafsi na wengine 360 wamepatiwa mafunzo na ujuzi katika fani mbali mbali za ufundi.  Mahkama ya kazi imeanzishwa.

 

Walemavu

 

(g)    Ili kulinda na kusimamia haki, usawa na maendeleo ya watu wenye ulemavu, Baraza la Taifa la Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu, limeanzishwa chini ya uongozi wa Afisi ya Waziri Kiongozi.  Aidha, Sera ya Walemavu imepitishwa na rasimu ya awali ya Sheria ya Walemavu imekamilika.

 

(h)    Hatua za kuelimisha jamii juu ya masuala mbali mbali ya kuwaendeleza watu wenye ulemavu, zimetekelezwa.  Jumla ya watu 219 wenye ulemavu wamepatiwa mafunzo ya uendeshaji wa biashara ndogo ndogo Unguja na Pemba pamoja na kupatiwa mkopo wa kujiendeleza.  Watu 193 wenye ulemavu wa kutosikia (viziwi) wamepatiwa mafunzo ya lugha ya ishara.  Aidha, kazi ya utengenezaji wa visaidizi vya walemavu hasa viatu na fimbo  katika Hospitali ya Mnazi Mmoja inaendelezwa.

 

Shughuli za Wananchi za Kujitegemea

 

71.    Ili kuendeleza na kuimarisha shughuli za wananchi za kujitegemea, hatua ya kuutambua  na kuupatia usajili rasmi Umoja wa Wafanyabiashara ndogo ndogo (Jua Kali), Umoja wa Wenye Magari ya daladala na Umoja wa Watembezaji Watalii imetekelezwa.  Eneo maalum la Saateni, limetengwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na kazi ya kulijenga na kulitengeneza  inaendelea vizuri. Mfuko maalum wa kuwaendeleza wazalishaji wadogo wadogo, umeanzishwa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

          SURA YA SABA

 

 

MAENEO MENGINE MUHIMU

 

Utawala Bora na Haki za Binadamu

 

72.    Umuhimu wa kipekee umekuwa ukitolewa na Chama Cha Mapinduzi kuhusu suala la ujenzi na uimarishaji wa utawala bora na demokrasia katika nchi.  Kwa  takriban miaka 13 sasa (1993 - 2005) Serikali, chini ya uongozi na usimamizi thabiti wa CCM imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika utumishi wa umma  ngazi za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

 

73.    Kwa kupitia Programu ya Kuboresha Utumishi Serikalini (1993-1999); Programu ya Kuboresha Utendaji Kazi na Utoaji Huduma Bora (2000-2011) katika utumishi wa Umma na Programu ya Maboresho ya Serikali za Mitaa (1998-2008) lengo kuu limeendelea kuufanya utumishi wa umma nchini kuwa chombo chenye kutukuka; chenye kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi endelevu; wenye kuleta matumaini; na unaoweza kutokomeza umaskini katika karne hii. Mabadiliko  makubwa pia yamefanyika katika mfumo, muundo na menejimenti ya Serikali za Mitaa kwa makusudi ya kuimarisha madaraka ya wananchi.  Matokeo yake ni kujenga misingi ya utawala bora na demokrasia, na kudhoofisha kabisa hulka za "Miungu-watu" katika ngazi za Kata, Vijiji, Vitongoji na Mitaa.  Utashi huu wa kisiasa umeweza  kuwa na matokeo katika uimarishaji wa Serikali za Mitaa kwa kuzipa madaraka zaidi ya uamuzi (Political decentralisation); na kuzipa mamlaka zaidi ya uamuzi juu ya matumizi ya fedha (finacial decentralisation); kuzipa mamlaka zaidi juu ya masuala ya uendeshaji (administrative decentralisation).  Hali hii imepelekea kwenye kujenga misingi ya uwajibikaji, yenye kuzingatia demokrasia, uwazi, mipango shirikishi, sheria, kanuni, na taratibu ndani na nje ya vikao.

 

74.    Kwa upande wa haki za binadamu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliundwa mwaka 2001 na inafanya kazi zake kwa uhuru na uwazi.  Kuundwa kwa Tume hiyo kumeiwezesha Tanzania kuwa na mfumo mzuri na wa uhakika wa kufuatilia masuala ya haki za binadamu.

 

Sheria

 

75.    Sheria ni huduma muhimu ya kiuchumi kwani ni mwezeshaji wa msingi katika kujenga mazingira mazuri ya kuvutia vitega uchumi na kukuza biashara.  Mfano wa sheria unapotetereka kiasi cha kuonekana kuwa haki haitendeki kwa wakati au haitendeki kabisa, wawekezaji hawavutiki kuleta mitaji yao.

 

76.    Katika kipindi cha 2000-2005, Sekta ya Sheria ilipewa uzito mkubwa kuliko ilivyokuwa miaka mingi iliyopita.  Yafuatayo ni miongoni mwa mambo makubwa yaliyoweza kufanyika katika kipindi hicho:-

 

(a)            Kuanzishwa kwa Mahakama ya Biashara.

 

(b)            Kufunguliwa Ofisi mbili za Kanda za Mahakama Kuu, Dar es Salaam na Bukoba.