CHAMA CHA
MAPINDUZI
TAMKO LA
CHAMA KUHUSU
UCHAGUZI
WA SERIKALI ZA MITAA TANZANIA BARA, NOVEMBA 2004
Imetolewa na:-
Makao Makuu ya CCM
DODOMA.
Agosti 2004
1.
Uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa ngazi ya
Vitongoji, Vijiji na Mitaa ulifanyika Novemba, 1999. Chama Cha Mapinduzi kilipata ushindi mkubwa sana. Wananchi walionyesha imani yao wazi wazi kwa
kuipa CCM ushindi wa asilimia tisini na tano (95%). Viongozi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa waliochaguliwa mwaka 1999
wakiungwa mkono na Halmashauri zao na Serikali Kuu wameweza kuwashirikisha
wananchi katika jitihada za kusukuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii na
kujenga mazingira muafaka ya utawala wa kidemokrasia.
2.
Ushindi mkubwa wa CCM katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa wa mwaka 1999 uliweka jukwaa la kuandaa ushindi wa kishindo wa CCM katika
Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge, Wawakilishi na wa Rais wa mwaka 2000. Ndiyo maana, kwa mtazamo huo huo, CCM
inayapa uzito na umuhimu mkubwa wa kipekee maandalizi ya sasa ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba, 2004.
3.
Lengo na dhamira ya CCM ni kuona kwamba tunapata
ushindi wa kupigiwa mfano katika mwezi Novemba mwaka huu wa 2004 ili utufagilie
njia ya kupata ushindi wa kishindo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005.
4.
Chama Cha Mapinduzi kinatoa Tamko ili kuwaomba
wapiga kura katika Vitongoji, Vijiji na Mitaa kuwachagua wagombea wa CCM katika
nafasi za uongozi katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.
5.
Chama Cha Mapinduzi kinaamini kwamba chenyewe ndicho
Chama peke yake nchini ambacho kwa sasa kinastahili kuendelea kuaminiwa na
wananchi kwa kupewa dhamana ya kuongoza Serikali za Mitaa za Vitongoji, Vijiji
na Mitaa kwa hoja zifuatazo:-
(a) Ndicho
Chama pekee chenye mtandao na uhai kwenye Vitongoji, Vijiji na Mitaa na hivyo,
kinayaelewa na kuyajua matatizo ya wananchi yalivyo huko. Kutokana na ukweli huo, CCM ndicho Chama
kinachostahili kupewa dhamana ya kuziongoza Serikali hizo za Mitaa.
(b) Ndicho
Chama pekee chenye uzoefu wa kuongoza na kuendesha Serikali za Mitaa na uzoefu
ambao umetoa matunda yanayoonekana.
Hakuna Chama kingine ambacho kina uzoefu kama huo.
(c) Ndicho
Chama pekee chenye Sera sahihi juu ya Serikali za Mitaa. Sera hii ni ya kupeleka madaraka kwa
wananchi Vitongojini, Vijijini na kwenye Mitaa na kujenga utawala wa demokrasia
shirikishi.
(d) Aidha,
Sera ya CCM ya kujitegemea inaenda sambamba na Sera ya kupeleka madaraka na
maamuzi kwa wananchi wenyewe pale walipo.
Hivyo, kuiweka CCM madarakani ni kuwa na uhakika kuwa wananchi
wataendelea kuimarisha kujitawala wenyewe na kujitegemea.
6. Nchi yetu bado
iko nyuma na maskini. Serikali ya Awamu
ya Tatu imefanikiwa kuanzisha mchakato wa kuitoa nchi yetu pale tulipokuwa
mwaka 1995 na kutuingiza katika mkondo wa maendeleo endelevu. Ili tupige hatua zaidi tunahitaji kuendelea
kuwa na Serikali Kuu imara na adilifu yenye uwezo wa kusukuma na kuchochea
ukuaji wa uchumi, na hali kadhalika Serikali za Mitaa adilifu na zenye utawala
wa kidemokrasia, zinazowaongoza wananchi wanaochapa kazi kwa bidii na maarifa
kwa kujitegemea. Haya yatapatikana
wananchi wakiichagua tena CCM kuziongoza Serikali za Mitaa katika Vitongoji,
Vijiji na Mitaa.
7. Mwelekeo
wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000 hadi 2010 kwa kiasi kikubwa ulikuwa ni
mwendelezo wa Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya Tisini. Mwelekeo wa Miaka ya Tisini ulibainisha
mtazamo wa jumla na dhamira za msingi za CCM kuhusiana na Serikali za Mitaa
kama ifuatavyo:-
“… Serikali za Mitaa ni
sehemu ya msingi ya madaraka ya umma kwa vile ni Taasisi zinazowezesha wananchi
kujitawala wenyewe kidemokrasia … kwamba, Serikali za Mitaa ni chombo chao
ambacho kinahitaji dhamira yao ya hali na mali, kwa hiyo wasingojee Serikali
zao kuwaendeleza wao bali wazitumie Serikali hizo kujiendeleza wenyewe”.
8. Kwa
upande wake, Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya 2000 – 2010 unakiri usahihi wa msimamo na dhamira hiyo
ya CCM kutokana na uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa sera hiyo. Baada ya kukiri hayo, Mwelekeo huo
unasisitiza juu ya suala la Uwajibikaji wa Serikali za Mitaa kwa wananchi, na
umuhimu wa Serikali Kuu kuziwezesha Serikali hizo kuwa kichocheo cha maendeleo
na kupambana na umaskini. Mwelekeo
wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000 hadi 2010 unasema ifuatavyo katika
ibara zake za 88 na 89:-
“Uzoefu umedhihirisha
umuhimu wa Serikali za Mitaa kama chombo cha wananchi cha kuwashirikisha katika
utawala wa umma…. Zimefanyika juhudi za makusudi … kuongeza uwajibikaji kwa
wananchi. CCM itahakikisha kuwa
uwajibikaji huo kwa wananchi unaongezeka zaidi.” (Ibara ya 88); na
“CCM inaipongeza Serikali
ya Awamu ya Tatu kwa kuanzisha Mpango wa uboreshaji wa Serikali za Mitaa. Pamoja na kuziwezesha Serikali za Mitaa
kutoa huduma za jamii, Mpango huo usisitize pia kuziwezesha Serikali za Mitaa
kuwa kichocheo cha maendeleo ya wakazi wa maeneo yao na kufuta umaskini. Lazima tujenge Serikali za Mitaa
zinazowajibika”. (Ibara ya 89)
9. Kwa hiyo, kwa ujumla wake, sera ya msingi
ya CCM kuhusiana na Serikali za Mitaa inaweza kuelezewa katika matamko
yafuatayo ya kisera:
(a)
CCM inazitambua
Serikali za Mitaa kuwa chombo cha wananchi cha kuwashirikisha katika utawala wa
umma;
(b)
CCM inazitambua
Serikali za Mitaa kuwa chombo cha kuwahamasisha, kuwasaidia na kuwawezesha
wananchi kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yao;
(c)
CCM inazitambua
Serikali za Mitaa kuwa ni kichocheo cha dhamira na jitihada za kupambana
na umaskini miongoni mwa wananchi;
(d)
CCM inawaongoza
wananchi katika mtazamo wa kuzitumia Serikali za Mitaa kama nyenzo katika
kujiletea wenyewe maendeleo na kupambana na umaskini badala ya kuzisubiri
ziwaletee maendeleo na kuwaondolea umaskini;
(e) CCM inazitambua changamoto zinazozikabili Serikali za Mitaa
katika Karne ya 21 ambazo ni kupambana na umaskini, kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali,
kukuza uchumi na kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia fursa zilizopo katika
kujiendeleza wenyewe; na
(f) CCM itaendelea kuhakikisha kuwa Serikali Kuu inaendelea
kuziwezesha Serikali za Mitaa katika kupambana na changamoto zinazozikabili
katika kutekeleza majukumu ya kuwatumikia wananchi kupitia Mpango wake wa
Uboreshaji wa Serikali za Mitaa na mipango mingine.
10. Sera hiyo ndiyo iliyokuwa mwongozo wakati wa kuandaa Ilani
za Uchaguzi za 1995 na 2000 vilivyohusu Serikali za Mitaa. Katika Ilani ya 1995, ibara ya 28
inaelezea dhamira na mikakati ya kuimarisha Serikali za Mitaa. Zipo pia ibara nyingine za Ilani hiyo
zilizogusia masuala ya Serikali za Mitaa.
Kwa mfano, ibara ya 24, hasa sehemu yake ndogo ya (vi) iliyozipa
Serikali hizo jukumu la kuhakikisha zinakuwa na mikakati ya kupambana na
umaskini. Kwa upande wa Ilani ya
2000, ibara ya 90 ndiyo inayolenga zaidi Serikali za Mitaa hasa sehemu yake
ndogo ya (vi) ambayo inazungumzia:
“kuziwezesha Serikali za
Mitaa kupanga mipango itakayoongeza mapato yatakayosaidia kutoa huduma bora za
jamii na kuwa kichocheo cha maendeleo ya wakazi wa maeneo yao na kufuta
umaskini.”
11. Sera na mikakati hiyo ya utekelezaji ndiyo
itaendelea kuongoza
Serikali
za Mitaa zitakazochaguliwa na wananchi baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
wa Novemba 2004.
SURA YA TATU
MAFANIKIO YA KIUCHUMI, KIJAMII NA KISIASA KATIKA
KIPINDI CHA AWAMU YA TATU YA UONGOZI WA CCM
12. Serikali
ya awamu ya tatu ilipoingia madarakani Oktoba, 1995 iliyatambua matatizo
yaliyokuwa yanaikabili nchi yetu ambayo ni pamoja na uwezo mdogo wa Serikali
katika kutoa huduma. Kwa hiyo kazi
kubwa iliyoikabili Serikali katika kipindi hiki ni kubuni mikakati mbalimbali ya kusukuma na kuchochea
maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mikakati hiyo imeleta mafanikio katika nyanja zifuatazo:
Mafanikio katika
Uchumi
(a) Ukuaji wa Pato
la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.6 mwaka 1995, hadi kufikia kilele cha
asilimia 6.2 mwaka 2002. Kutokana na
ukame ulioikumba nchi yetu, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.6 mwaka 2003.
(b) Mfumuko wa bei
umeshuka kutoka asilimia 27.1 mwaka 1995, hadi asilimia 4.4 mwaka 2003.
(c) Ujazi wa fedha
umedhibitiwa na hivyo kuchangia katika kushuka kwa mfumuko wa bei na kuwafanya
watu wajitume zaidi katika kutafuta pesa kwa njia halali.
(d) Uzalishaji
viwandani na katika mashirika sasa ni wa ufanisi mkubwa kufuatia mafanikio ya
utekelezaji wa sera ya ubinafsishaji.
Baada ya kubinafsishwa, makampuni na mashirika hayo yanaipatia Serikali
mapato makubwa badala ya kuendeshwa kwa ruzuku ya Serikali.
Ubinafsishaji
umeweza kuiondolea Serikali mzigo mzito wa kuendesha uchumi moja kwa moja. Aidha umeanza kujenga mazingira ya ongezeko
la tija katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani.
(e) Mauzo ya nje
ya bidhaa yameongezeka kutoka Dola 682.9 milioni mwaka 1995 hadi Dola 1,142.4
milioni mwaka 2003.
(f) Akiba ya fedha
za kigeni kwa ajili ya kuagizia bidhaa kutoka nje imeongezeka kutoka uwezo wa
kukidhi mahitaji ya mwezi 1.6 mwaka 1995 hadi mahitaji ya miezi 8.9 mwaka 2003.
(g) Ruzuku ya
Serikali Kuu kwa Serikali za Mitaa imeongezeka mara 24 kutoka Shilingi 12.3
bilioni mwaka 1995/96 hadi shilingi 292.0 bilioni mwaka wa 2003/04.
(h) Kutokana na
mafanikio ya utekelezaji wa mikakati ya kuweka mazingira mazuri ya kuvutia
vitega uchumi na kupambana na rushwa, hivi sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazoongoza katika Afrika kuhusu kuvutia uwekezaji.
(i)
Kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa
mikakati ya kupambana na rushwa na kuziba mianya ya ukwepaji wa kulipa kodi
pamoja na zoezi la ubinafsishaji wa mashirika ya umma hatua ambayo imeboresha
uzalishaji, makusanyo ya mapato ya Serikali yameongezeka kwa zaidi ya mara nne. Makusanyo hayo yameongezeka kutoka wastani
wa Shilingi 25 bilioni kwa mwezi mwaka 1995 hadi wastani wa Shilingi 120
bilioni kwa mwezi, mwaka 2004.
(j) Tanzania ilitimiza masharti ya Mpango wa
Kuzifutia Madeni Nchi zenye Madeni Makubwa na hivyo kuingizwa katika Mpango huo
mwaka 2000. Kutokana na hali hiyo
kuanzia mwaka 2000 Tanzania imekuwa ikitekeleza Mkakati wa Kupunguza
Umaskini kwa maana fedha ambazo zingetumika kulipia madeni ya nje (ambayo
yamefutwa) sasa zinaelekezwa katika sekta teule za huduma za jamii na
miundombinu ya kiuchumi zinazomgusa moja kwa moja mwananchi wa kawaida. Sekta hizo ni elimu, afya, maji, barabara za
vijijini, kilimo, na utawala bora.
(k) Katika kipindi
hiki Sekta ya Utalii imekua kwa kasi kubwa na kutoa mchango mkubwa katika
kuliingizia Taifa letu fedha za kigeni.
Hii imetokana na juhudi za makusudi za Serikali za kuipa msukumo wa
pekee sekta hii na hasa katika kuitangaza nje na ndani na kuboresha miundombinu
inayosaidia ukuaji wake ikiwa ni pamoja na kuboresha barabara ziendazo kwenye
hifadhi mbalimbali za kitaifa.
Kumekuwepo pia juhudi za kuibua maeneo mapya ya utalii kama vile Kilwa
na Kitulo. Idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka watalii
295,000 mwaka 1995 hadi 576,000 mwaka 2003.
Aidha mapato yatokanayo na utalii nayo yameongezeka kutoka dola 259
milioni mwaka 1995 hadi dola 731 milioni mwaka 2003.
(l) Uuzaji wa
madini nje umeongezeka kutoka Dola 26.37 milioni mwaka 1998 hadi Dola 548.30
milioni mwaka 2003. Dhahabu imechangia
zaidi ya asilimia 90 ya thamani ya madini yote yaliyouzwa nje. Aidha
upanuzi katika Sekta ya madini umeongeza ajira kwa wananchi katika
maeneo mengi. Katika maeneo mengi wenye
migodi hiyo wamechangia katika kuboresha huduma za jamii na miundo mbinu.
Mafanikio katika Maendeleo ya Jamii
13. Kuboreka
kwa huduma mbali mbali za kijamii na kiuchumi ni miongoni mwa manufaa ya kukua
kwa uchumi wa Taifa ambayo wananchi wa kawaida vijijini na mijini wameanza
kuyafaidi kwa pamoja. Kutokana na
kuimarika kwa uchumi wa Taifa na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya
Serikali, imewezekana kwa Serikali kuongeza kwa kiwango kikubwa rasilimali
ilizozielekeza katika huduma hizi ambazo ni zana za msingi katika kupambana na
umaskini.
14.
Mpango wa TASAF kwa
kushirikiana na wananchi umeleta mafanikio makubwa katika maeneo ya elimu,
afya, barabara za vijijini, maji n.k.
Mpango huo ambao ulianza na wilaya 40 za majaribio, sasa utakuwa wa nchi
nzima.
Huduma za Jamii
Elimu
Sekta ya elimu ya msingi imepiga hatua kubwa kama
ifuatavyo:-
(i)
Kufutwa kwa ada za shule za msingi mwaka
2002/2003 kumewezesha kuongezeka kwa
idadi ya wanafunzi wa shule za msingi kutoka 3,877,643 mwaka 1995 hadi
7,083,063 mwaka 2004. Idadi ya watoto walioandikishwa darasa la kwanza kuanzia
mwaka 2000 kwa kila mwaka ni kama
ifuatavyo:-
·
2000 - 897,569
·
2001 - 1,140,554
·
2002 - 1,632,141
·
2003 - 1,481,354
·
2004 - 1,368,315
Mwaka
2004 watoto 1,368,315 wameandikishwa darasa la kwanza sawa na asilimia 83.4 ya
lengo la 1,640, 969. Kati ya walioandikishwa wavulana 697,594 na wasichana
670,721. Kati yao shule za Serikali
watoto 1,361,446 na shule binafsi watoto 6,869.
(ii)
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi
(MMEM) ulioanza kutekelezwa mwaka wa 2002 umekwishaleta mabadiliko makubwa ya
sura za shule za msingi nchi nzima.
Majengo mengi ya shule yamekarabatiwa na mengine mengi mapya yamejengwa.
(iii)
Katika mwaka 2003, kulifanyika ujenzi wa
madarasa 13,342; ofisi za walimu 226; nyumba za walimu 997; vyoo vya shimo
14,700; na kuajiri walimu wapya 15,921 ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi
na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Serikali katika kuhakikisha kwamba mapengo ya walimu katika
baadhi ya shule za msingi na sekondari yanazibwa imeajiri walimu 37,261 kati ya
mwaka 2000 na 2004. Miongoni mwao,
walimu 15,000 ni wale waliokuwa wamekosa ajira baada ya kumaliza mafunzo ya
ualimu miaka ya nyuma. Kwa hiyo kero ya
walimu 15,000 wenye vyeti bila kuwa na ajira imemalizika.
(iv)
Kutokana na mafanikio mazuri ya kusisimua
ya Mpango wa MMEM Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya
Sekondari (MMES). Tayari Serikali
imepunguza ada ya shule za sekondari za
kutwa za Serikali kwa asilimia 50 wakati hatua nyingine za kukarabati na
kujenga majengo ya Sekondari nchi nzima zinaendelea.
Afya
Sekta ya Afya nayo imekuwa na mafanikio makubwa kama
ifuatavyo:-
(i)
Chanjo
za watoto chini ya umri wa miaka mitano zimefikia asilimia 90 na hivyo
kuvuka kiwango cha kimataifa cha asilimia 80 katika mwaka wa 2003. Chanjo ya
Kifua Kikuu ilifikia asilimia 88, polio asilimia 91, kifaduro, pepopunda na
homa ya ini asilimia 89, na surua asilimia 89.
(ii)
Serikali imeanzisha sera ya bima ya afya
ili kuwawezesha wafanyakazi wa sekta ya umma kukabiliana na gharama za
tiba. Kwa ajili ya wananchi wa kawaida
Serikali imeanzisha Mifuko ya Afya ya Jamii.
(iii)
Ukarabati mkubwa wa hospitali kuanzia Hospitali ya Taifa Muhimbili mpaka
hospitali za Wilaya umekamilika au uko katika hatua mbalimbali za
utekelezaji. Mashine za “X-Ray” na
“Ultrasound” na jenereta zimefungwa katika hospitali za Wilaya, Mikoa na Rufaa.
(iv)
Katika harakati za kuboresha utoaji wa
huduma za afya, kumekuwa na ongezeko kati ya mwaka 2000 hadi 2003 la mtandao mzuri wa vituo vya kutolea huduma
nchi nzima kama ifuatavyo:-
·
Hospitali kutoka 224 hadi 249
·
Vituo vya Afya kutoka 459 hadi 574
Nguvu za
wananchi na halmashauri zimetumika katika kujenga:-
·
Zahanati 233 na
·
Vituo vya afya 16
(v)
Serikali imefuta kodi kwenye vyandarua na
bidhaa zinazosaidia vita dhidi ya malaria.
Hali hiyo imesaidia sana kupunguza maambukizo ya malaria hasa kwa akina
mama wajawazito na watoto wachanga.
(vi)
Programu kabambe ya kukabiliana na janga
la ukimwi imeanzishwa na inatekelezwa.
Maji
Mijini na Vijijini
Ukosefu
wa maji safi na salama ni kero ambayo inaendelea kushughulikiwa na Serikali kwa
kushirikiana na wahisani, asasi zisizo za kiserikali na wananchi wenyewe. Mafanikio ya Sera ya Taifa ya Maji
yamejionyesha katika maeneo yafuatayo:-
(i)
Hadi kufikia Desemba 2003 kamati za Maji 8,368
zimeanzishwa na kati ya hizo 7,226 zilikuwa na mifuko ya maji yenye thamani ya
Sh. 13 bilioni.
(ii)
Idadi ya wakazi mijini wanaopata huduma ya maji safi
na salama imeongezeka kutoka asilimia 68 mwaka 1998 hadi asilimia 73 mwaka
2003.
(iii)
Idadi ya wananchi vijijini wanaopata maji safi na
salama imeongezeka kutoka asilimia 48 mwaka 1995 hadi asilimia 53 mwaka 2003.
(iv)
Makusanyo ya mapato ya mamlaka za Maji Mijini
yaliongezeka kutoka Sh. 400 milioni mwaka 1995 hadi Sh. 13.4 bilioni mwaka
2003. Ongezeko hili linatoa fursa kwa mamlaka hizi kuboresha huduma wanazotoa.
(v)
Pamoja na miradi midogo midogo inayoendelea, Serikali
inashughulikia miradi mikubwa ambayo ni pamoja na mradi wa maji toka Ziwa
Victoria kwenda Wilaya za Shinyanga
Mjini na Kahama, mradi wa maji wa Chalinze katika Mkoa wa Pwani, mradi kabambe
wa Jiji la Dar es Salaam nakadhalika.
Huduma za Kiuchumi
Barabara
(i)
Toka mwaka 2001, Serikali imekuwa
ikitenga Sh.1.8 bilioni kila mwezi kwa ajili ya ujenzi wa barabara nchini. Fedha hizo kwa pamoja na zile za road toll na za wahisani, zimewezesha kuboresha kwa kiwango kikubwa
mtandao wa barabara kuu na za vijijini nchi nzima.
Mawasiliano
(ii)
Tanzania katika kipindi hiki imeshuhudia
ongezeko kubwa la mtandao wa mawasiliano, hasa simu za mikononi.
Umeme
(iii)
Katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu Oktoba
2000, Chama Cha Mapinduzi kilitoa ahadi ya kuendelea kushughulikia suala la usambazaji
wa umeme katika miji mikuu ya Wilaya iliyobaki ambayo idadi yake ilikuwa
18. Hadi Julai, 2004 miji mikuuu ya
Wilaya 8 imepatiwa umeme. Nayo ni:
Geita, Igunga, Mbarali, Meatu, Mkuranga, Ruangwa, Tandahimba na Sikonge. Hadi kufikia mwaka 2005 miji mikuu ya Wilaya
za Biharamulo, Ngara, Rufiji, Serengeti, Ukerewe na Urambo itakuwa imepatiwa
umeme. Aidha hatua za awali zimeanza
kuchukuliwa ili kuanza utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme katika miji
iliyobaki ya Bukombe, Kilindi na Simanjiro.
16. Serikali
itaendelea kuweka mazingira bora, lakini tegemeo kuu la kukua kwa uchumi wetu
ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha uwekaji akiba, kuongeza kasi ya
ongezeko la mitaji, kuongeza kasi ya mauzo nje, na wananchi wenyewe kufanya
kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu.
Mafanikio ya Kisiasa
Utengamano
wa Kisiasa
17. Mazingira yaliyosababisha mafanikio
haya makubwa ya kiuchumi na kijamii ni kuwepo kwa amani na utulivu wa kisiasa
nchini. Serikali ya CCM ya Awamu ya Tatu imeweza kuendelea kujenga na kudumisha
hali ya amani na utulivu kwa kipindi chote cha uongozi wake tangu ilipoingia
madarakani mwaka 1995.
18. Rushwa
imendelea kupungua baada ya mianya mingi ya rushwa kuzibwa. Katika tathmini za Kimataifa, Tanzania sasa
imeondoshwa katika kundi la nchi zinazoongoza kwa rushwa duniani na
Afrika.
Kupanuka na kuimarika kwa Demokrasia na Utawala Bora
19. Katika kipindi hiki demokrasia imepanuka na
kuimarika katika nyanja za uhuru wa kuabudu, kutoa maoni, kuanzisha asasi
zisizo za kiserikai na uhuru katika nyanja mbalimbali zinazowagusa wananchi
vikiwemo vyombo vya habari, vyama vya siasa na kuanzishwa kwa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora nakadhalika.
Kupanuka na kuimarika huku kwa demokrasia kumechangia kwa kiwango
kikubwa kuimarisha amani na utulivu.
20. Kwa ujumla manufaa ya ukuaji wa uchumi,
pamoja na ukuaji wa huduma za jamii ni mafanikio dhahiri katika kukua kwa amani
na utulivu na kupanuka kwa demokrasia, na utawala bora. Hayo yote yameweza
kuwafikia wananchi kwa njia mbalimbali ambazo zinazidi kuongezeka na mpya
kubuniwa. Kwa kiasi kikubwa mafanikio
hayo yamewezekana kupitia Sera ya CCM ya Ushirikishaji wa Wananchi Katika
Maendeleo yao.
21. Katika
utekelezaji wa sera hiyo ya ushirikishaji wa wananchi, hasa katika eneo la
kupambana na umaskini, Serikali Kuu inaitambua nafasi ya Serikali za Mitaa
katika kusimamia na kuratibu
utekelezaji huo. Ndiyo maana Serikali
Kuu imechukua hatua za makusudi
kuziwezesha Serikali hizo kutekeleza kwa ufanisi jukumu hilo kwa manufaa ya
wananchi.
SURA YA NNE
KUPAMBANA NA UMASKINI NA
UWEZESHAJI WA WANANCHI
Kupambana
na Umaskini
22. Katika
Mwelekeo wa Sera za CCM za Miaka ya Tisini Ibara ya 31 umefanyika uchambuzi wa
kina kuhusu Sekta ya Wananchi Wazalishaji Mali na Wafanyabiashara Wadogo. Uchambuzi huu ambao bado ni sahihi kwa Chama
Cha Mapinduzi, umebainisha hali halisi inayoikabili sekta hii, kwamba wananchi
wetu walio wengi wanaendelea kupata riziki zao wakiwa wazalishaji na
wafanyabiashara wadogo wadogo katika kilimo, uvuvi na ufugaji, viwanda
vidogo biashara na huduma mbali
mbali. Zaidi ya hayo, CCM
ilitambua kwamba sekta hii ilikuwa inakabiliwa na vikwazo vingi ikiwa ni
pamoja na urasimu wa kupata mikopo,
leseni, mahali pa kufanyia kazi, ukosefu wa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa
shughuli zao, na ukosefu wa masoko ya bidhaa zao.
23. Sera za Chama Cha
Mapinduzi za kupambana na umaskini zimeweka bayana mikakati inayoelekeza nini
kifanyike katika kufanikisha mapinduzi katika kilimo, ufugaji na uvuvi. Licha ya juhudi zilizofanyika hadi sasa,
kilimo, ufugaji na uvuvi wetu bado havijawa vya kisasa kwa sababu havitumii
sayansi na teknolojia. Hivyo mikakati ifuatayo itatekelezwa katika kuleta
mabadiliko hayo:-
24. Ili kuondokana na hali hiyo, msisitizo mkubwa utaendelea kuwa wa
kumwezesha mkulima kutoka katika
kilimo cha jadi na kuingia katika kilimo
cha kisasa kinachozingatia:-
(i)
Kanuni za kilimo bora.
(ii)
Matumizi ya samadi, mboji na mbolea ya viwandani.
(iii)
Kueneza matumizi ya majembe ya kukokotwa na ng’ombe
na punda nchini kote, pamoja na kutumia matrekta.
(iv)
Kueneza matumizi ya mikokoteni inayovutwa na
wanyamakazi badala ya mizigo kuendelea kubebwa na binadamu hususani wanawake.
(v)
Kuendelea kutumia mashine na teknolojia mbalimbali
za kilimo na kuhakikisha kuwa mashine
zinatumika zaidi katika kuchakata mazao
ili kuyaandaa kwa ajili ya soko la ndani na nje ikiwa ni mkakati wa kuyaongezea
thamani.