TOLEO LA PILI LA JARIDA LA MKEREKETWA:

 

Napenda kuwaarifu wanachama wa CCM kwamba Toleo la Pili la Jarida la Mkereketwa tayari limekwishatoka na kusambazwa Matawini nchi nzima.  Miongoni mwa mambo yaliyomo katika toleo hilo ni Tamko la Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM wa tarehe 27-29 Januari, 2004.  Tamko hilo lina maazimio, maamuzi na maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu masuala yafuatayo:-

 

(a)    Ubinafsishaji

(b)    Mapendekezo ya Kamati ya Msekwa kuhusu Namna Bora ya Kuwapata Wagombea wa CCM katika Chaguzi za Dola.

(c)    Mapendekezo ya Kamati ya Kingunge Ngombale-Mwiru kuhusu Uhuishaji wa Muundo wa Chama.

(d)    Wagombea waliopitishwa kugombea nafasi mbali mbali katika chaguzi za Jumuiya za Vijana na Wazazi ngazi za Taifa na Mkoa.

(e)    Mengineyo mengi.

 

Toleo hilo la Mkereketwa pia lina makala mbali mbali za kusisimua kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, Taathira za siasa za Udini n.k.

 

Aidha, Toleo hilo limefuatana na jarida jingine liitwalo Mafanikio ya Ubinafsishaji ambalo limechapishwa mahsusi kwa lengo la kusahihisha upotoshaji ambao umekuwa ukifanywa dhidi ya zoezi la Ubinafishaji.

 

Majarida yote hayo yanaweza pia kusomwa katika Tovuti ya CCM: www.ccmtz.org.

 

Wanachama wanahimizwa kwenda katika Ofisi za Chama za Matawi, Kata, Majimbo, Wilaya na Mikoa zilizo karibu nao ili wasome na kujadili yaliyomo katika majarida hayo.

 

Kwa upande mwingine, nawaomba Makatibu wa CCM wa ngazi mbali mbali wakishirikiana na Makatibu wao wa Siasa na Uenezi kuandaa mikutano ya wanachama au Wajumbe wa Halmashauri Kuu au Kamati za Siasa wa ngazi husika ili kusoma kwa pamoja na kuyajadili yaliyomo kwenye majarida hayo.

 

PONGEZI KWA VIKUNDI VYA MUZIKI NA VITUO VYA UTANGAZAJI:

                       

Katika kipindi cha maadhimisho ya Miaka 40 ya Muungano, vikundi kadhaa vya muziki vilijitokeza kutunga nyimbo za maadhimisho hayo ambazo zilisikika katika vituo mbali mbali vya redio na televisheni na pia katika kumbi za muziki.

 

Napenda kuvipongeza vikundi vyote vya muziki vilivyotunga nyimbo hizo na vituo vya redio na televisheni vilivyozicheza.  Kitendo hicho ni cha kizalendo ambacho kinafaa kuendelezwa.

 

Pamoja na jamii ya Watanzania kupenda sana kusikiliza nyimbo za mapenzi na mipasho, ni vizuri tunapokuwa na jambo la kitaifa, la furaha au msiba, likatuunganisha wote angalau kwa kipindi hicho kifupi, kabla ya kuendelea na maisha yetu ya kawaida.

 

Naamini nyimbo zile zimewaelimisha watoto na vijana wengi kuhusu mambo ya msingi ya Muungano wetu, elimu ambayo bila ya hivyo pengine wasingeipata.

 

 

Omar R. Mapuri (Mb.),

KATIBU WA NEC.,

IDARA YA ITIKADI NA UENEZI

11/05/2004