Pongezi za Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwa Mheshimiwa Getrude Ibengwe Mongella kwa Kuchaguliwa kwa Kura nyingi kuwa Rais wa Kwanza wa Bunge la Afrika

 

 

Katika kikao chake kinachoendelea, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi leo imetoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Getrude Ibengwe Mongella kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Rais wa Kwanza wa Bunge la Afrika hapo tarehe 18 Machi, 2004.

 

Ushindi wake huo mkubwa na wa kishindo si wake peke yake bali pia ni wa Taifa zima na Watanzania wote.  Kuchaguliwa huko kwa Mheshimiwa Mongella ni kielelezo cha kutosha cha imani waliyonayo Wabunge wa Bunge la Afrika kwake.  Kwa vile Wabunge hao wanawakilisha Waafrika, basi imani hiyo ni ya Waafrika wote.

 

Aidha, ushindi huo mkubwa alioupata Mheshimiwa Mongella ni kielelezo kingine dhahiri cha heshima iliyonayo Tanzania katika Bara la Afrika na Jumuiya ya Kimataifa kwa jumla.

 

Chama Cha Mapinduzi kinafahari kubwa kwa imani hiyo iliyoonyeshwa na Bara la Afrika kwa mwanachama wake huyo mahiri na mzoefu wa kisiasa na shughuli za Kimataifa.

 

Huu ni ushahidi wa jinsi CCM ilivyo na hazina kubwa ya viongozi wenye busara na upeo unaoheshimika Kimataifa.

 

Kamati Kuu pia imewapongeza Ndugu Emmanuel Nchimbi na Abioud Mugini Maregesi kwa kuchaguliwa kuwa Wenyeviti wa Jumuiya za VIJANA na WAZAZI.

 


Ndugu Nchimbi alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa VIJANA uliofanyika Dodoma tarehe 28 Februari, 2004 na Ndugu Maregesi alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa WAZAZI uliofanyika pia Dodoma, tarehe 6 Machi, 2004.

 

Kamati Kuu imewapongeza pia waliochaguliwa kuwa Makamu Wenyeviti wa Jumuiya hizo, Ndugu Amina Iddi Mabrouk (VIJANA) na Ndugu Ramadhani Suleiman Nzori (WAZAZI).

 

Kamati Kuu imewatakia heri na fanaka viongozi hao na wenzao wote waliochaguliwa katika nafasi mbali mbali za Jumuiya hizo na kuwataka wote waelekeze nguvu zao katika kuhakikisha ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Dola mwaka 2005.       

 

 

 

 

Omar R. Mapuri (Mb.),

KATIBU MWENEZI WA CCM TAIFA

19/03/2004