MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
Chama Cha Mapinduzi kimekwisha toa Toleo la 3 la
Jarida la Mkereketwa ambalo linafuatana na jarida dogo la Mafanikio
ya Sekta ya Elimu. Majarida hayo
hivi sasa yamo kusambazwa katika matawi na ofisi nyingine za CCM, taasisi mbali
mbali na kwa walengwa wengine.
Miongoni mwa mambo yaliyomo katika toleo hili la Mkereketwa
ni:-
Hata hivyo, mada kuu ya toleo hili ni Mapambano Dhidi ya
Rushwa. Mada hiyo imezungumziwa katika
Tahariri na makala nyingine mbili.
Katika makala hizo, miongoni mwa mengine tumejenga hoja na kuonyesha
yafuatayo miongoni mwa mengine.
(a)
Kuziba mianya ya rushwa
(yaani kutumia falsafa ya kinga ni bora kuliko tiba)
(b)
Kuwachukulia hatua
wanaothibitika kujihusisha na rushwa.
(a)
Kuundwa kwa TRA na
marekebisho ya sheria za kodi kumewezesha kuzibwa kwa mianya mingi ya ukwepaji
kodi inayoambatana na rushwa. Matokeo
yake ni kwamba makusanyo ya kodi na mapato mengine ya Serikali yameongezeka
zaidi ya mara nne.
(b)
Marekebisho ya Sheria
za Fedha na za Manunuzi Serikalini yamewezesha kuongezeka kwa udhibiti wa fedha
na mali za Serikali. Matokeo ni kwamba
upotevu wa fedha na mali za Serikali umepungua kwa kiasi kikubwa.
(c)
Kufutwa kwa kodi ya
maendeleo na kodi nyingine nyingi zilizokuwa kero na chanzo kikubwa cha rushwa,
kumeziba mianya ya rushwa iliyokuwa ikiwasumbua sana wananchi. Bila ya makelele na vishindo, rushwa zilizokuwa
zimeambatana na kodi hizo zimeyeyuka na hivi sasa hakuna Mtanzania anayedaiwa
rushwa za aina hiyo.
(d)
Kufutwa kwa ada ya
shule za msingi na kuanzishwa kwa mpango wa MMEM, kuliziba mwanya mwingine
mkubwa wa rushwa iliyokuwa ikiwasumbua wazazi.
Sasa hivi hakuna mzazi anayedaiwa rushwa kwa kumwandikisha mtoto
shule
Kwa bahati mbaya wakosoaji wengi wa
Serikali kuhusu suala la rushwa, hasa wapinzani, sura hii ya vita dhidi ya
rushwa hawaizungumzii; labda kwa sababu inaleta mafanikio makubwa. Wao wamekazania ile sura ya pili tu ya
kuwachukulia hatua wanaothibitika kujihusisha na rushwa. Lakini hata katika hili, hawazungumzii cho
chote kuhusu watu waliofungwa au watumishi waliofukuzwa kazi au kustaafishwa
kwa manufaa ya umma baada ya kubainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. Badala yake wakosoaji hao wamejikita katika
kuitaka Serikali iwahukumu watu kwa hisia tu, jambo ambalo ni kinyume kabisa na
kanuni za msingi za utawala bora na utawala wa sheria.
Katika makala za Mkereketwa kuhusu rushwa, tumetoa wito kwa wananchi
washiriki kikamilifu katika vita dhidi ya rushwa, kwani pamoja na mafanikio
yanayopatikana ambayo yanaashiria kupungua kwake, rushwa bado ipo nchini. Tumetoa wito maalum wakati huu tukielekea Uchaguzi
Mkuu wa 2005, kwamba wanachama wa vyama vya siasa wapambane na rushwa ndani
ya vyama vyao ili kuwazuwia wanasiasa
watoa rushwa wasije wakapata nafasi za kugombea. Aidha, tumewataka wapinzani wasidhani kwamba jukumu la kupambana
na rushwa ni la CCM peke yake na wao kazi yao ni kulaumu tu.
Vita hivi ni vya wote, lakini vipiganwe ndani ya
misingi ya Kanuni za utawala bora na utawlaa wa sheria. Vita hivi visitumike vibaya kupakana matope
na kuchafuliana majina kwa malengo ya kisiasa.
Tukifanya hivyo, rushwa hatutoiweza na badala yake tunaweza kujikuta
katika vurugu. Si sahihi kuishinikiza
Serikali kuhukumu watu kwa hisia tu, kwani kama itafanya hivyo hao
wanaoishinikiza watakuwa wa kwanza kuilaumu.
Ndiyo maana tunasisitiza umuhimu
wa kuwafichukua wala/watoa rushwa kwa ushahidi unaotosheleza.
Aidha, napenda kuongeza kwamba vita dhidi ya rushwa visitumike kudumaza ujasiriamali. Watanzania tusiendeleze makosa tuliyoyafanya mwanzoni katika safari yetu ndefu ya kujenga ujamaa. Itakumbukwa kwamba katika miaka ya sitini, sabini na themanini, chuki dhidi ya ubepari iliendelezwa hadi kuchukia utajiri ambapo wajamaa wakaanza kujinasibu kwa umaskini, na ujamaa ukapewa maana ya umaskini. Matokeo yake yakawa ni kudumaa kwa ujasiriamali.
Hivi sasa, katika mazingira mapya ya ujenzi wa
ujamaa, tumo katika jitihada za kufufua ujasiriamali. Na kwa lengo hilo, CCM kupitia Serikali yake imetunga Sera ya
Uwezeshaji wa Wananchi, na Sheria imo kutungwa, itayaowawezesha Watanzania
kujenga ujasiriamali ili waweze kuupiga vita umaskini kwa ufanisi.
Lakini ghafla umejitokeza mtindo wa kuwaandama
viongozi wanaojitokeza kuonyesha njia na mfano katika ujasiriamali. Kwa kutumia kisingizio cha vita dhidi ya
rushwa, wanapakwa matope na kuchafuliwa majina kwa kuhusishwa na rushwa bila ya
ushahidi wowote.
Halafu shutuma hizo zinaambatana na unafiki. Viongozi waliopata nafasi za uongozi wakiwa
matajiri wao hawaguswi. Lakini wale waliopata uongozi wakiwa maskini, wakianza
juhudi za kuondokana na umaskini kwa njia halali, wanaandamwa na kukatishwa
tamaa. Hivyo katika Tanzania wenye haki
ya utajiri ni matajiri tu? Maskini
akipata uongozi wajibu wake ni kuendeleza umaskini? Na ikiwa hivyo atatoa mfano gani kwa watu anaowahubiria sera za
kupiga vita umaskini? Jambo la kuchunga
wakati wote ni kuhakikisha kuwa viongozi hawajilimbikizii mali kwa kutumia
nyadhifa zao. Lakini wasikatishwe tamaa wanapotumia kipato chao
halali kujiendeleza kimaisha na kuhudumia familia zao.
Natoa wito kwa Watanzania waubaini na kupuuza unafiki
wa baadhi ya wanasiasa. Tusikubali
kuelekezwa kwenye kuamini kuwa ujasiriamali ni ula rushwa kama tulivyofikishwa
huko nyuma kuamini kuwa ujamaa ni umaskini.
Fikra kama hizo zitazidi tu kutuzamisha katika dimbwi la umaskini.
Namalizia kwa kutumia fursa hii kukanusha uzushi
uliochapishwa katika gazeti la Mtanzania la jana tarehe 9/8/2004
lililojaribu kutoa picha kana kwamba shamba la Kibaigwa la Mheshimiwa Waziri
Mkuu Frederick Sumaye lilikuwa la Magereza.
Shamba hilo liko umbali wa zaidi ya kilomita 6 toka eneo lililokuwa
likitumiwa na Magereza huko nyuma kama Kambi ya Kilimo ya Manyata chini ya
Gereza la Kongwa.
Magereza walilitumia eneo hilo la ekari 70 kwa
kuazimwa na kijiji cha Manyata toka 1980 hadi 2001 walipoifunga kambi
hiyo. Walipofunga kambi, Magereza
walilirejesha eneo hilo kwa uongozi wa kijiji cha Manyata ambao nao uliwagawia
wananchi ambao ndio wanaolitumia hivi sasa kujitafutia riziki zao. Magereza hawakuwahi kulimiliki eneo hilo.
Ni kitendo cha kuishiwa hoja kwa Mheshimiwa Slaa,
kupitia gazeti la Mtanzania, kujaribu kupotosha ukweli na kutaka Watanzania
waamini kwamba shamba la Mheshimiwa Waziri Mkuu linatokana na eneo lililokuwa
likitumiwa na Magereza. Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Mhe. Andrew Chenge alikwishaelezea kwa urefu Bungeni namna
Mheshimiwa Frederick Sumaye na familia yake walivyolipata eneo hilo
wanalolitumia kwa kukodishwa na kijiji kama inavyofanyika kwa wengi wengine
wanaolima maeneo hayo. Mwanasiasa
anapoishiwa hoja ni bora akanyamaza kuliko kujaribu kujenga chuki binafsi na
kupaka watu matope.
Omar R. Mapuri (Mb),
KATIBU WA NEC
ITIKADI NA UENEZI