Tamko la
Chama Cha Mapinduzi kuhusu Kauli za Uchochezi za Mwenyekiti wa CUF
Katika gazeti la “Majira” la tarehe 27 Disemba, 2004, Chama Cha CUF kimeripotiwa kudai kupitia kwa Mwenyekiti wake, Ibrahim Lipumba, kwamba kikipokonywa ushindi katika Uchaguzi Mkuu ujao itamwagika damu.
Aidha,
gazeti hilo limemnukuu Lipumba kwamba amesema maneno yafuatayo:-
“Mwaka
1995 wananchi wa Zanzibar walichagua Serikali wanayoitaka wakanyang’anywa,
tukakaa katika muafaka, mwaka 2000 wakachagua tena Serikali yao wakapokonywa
tena, muafaka wa pili ukaja mwaka 2001, vipengele muhimu katika muafaka huo wa
pili havijatekelezwa hadi sasa licha ya makubaliano ya kutekeleza muafaka huo
hadi mwaka 2003.
Sasa iwapo hawatatekeleza na kuingia katika Uchaguzi Mkuu, na wananchi wakachagua tena Serikali yao wanayoitaka na kunyang’anywa, basi CCM ijue itaua watu wengi zaidi wasio na hatia kama ilivyotokea, kwani wananchi hawatakubali kupokonywa tena Serikali yao safari hii.”
·
Kwanza, kauli ya kumwaga damu
ambayo ni maarufu kwa viongozi wa CUF ni mwendelezo wa kudhihirisha kiu ya damu
ya Watanzania waliyo nayo viongozi hao.
La kusikitisha zaidi ni kwamba kauli hiyo inatoka mara tu baada ya
Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa kukemea kauli kama hizo na kuwaasa
wanasiasa kuachana nazo wakati akitoa salamu zake za Krismasi kwa
Watanzania. Aidha, kauli hiyo ya
Lipumba imetoka mara tu baada ya mahubiri yaliyotolewa makanisani nchi nzima
yaliyokemea kauli za shari za wanasiasa
zinazochochea vurugu na uvunjifu wa
amani na kuwataka wanasiasa waachane nazo. Mahubiri hayo yalitolewa karibu na Maaskofu, Makasisi na
Wachungaji wote wakati wa ibada za Krismasi ambao walikuwa wakiiombea amani
nchi yetu. Kauli hiyo ya kumwaga damu
kutoka mara tu baada ya mahubiri kama hayo ni kebehi na dharau kwa viongozi hao
wa kidini wenye heshima kubwa katika jamii yetu.
·
Pili, madai kwamba wananchi wa Zanzibar walipokonywa Serikali yao
waliyoichagua ni uongo wa mchana tena usio na haya. Serikali za Awamu ya 5 na 6 za CCM zilipata ridhaa ya wananchi wa
Zanzibar na ndio waliozichagua na kuziweka madarakani kihalali kwa mujibu wa
Sheria na Katiba. Serikali hizo
ziliingia madarakani baada ya kushinda uchaguzi na kuthibitishwa na Tume ya
Uchaguzi. Hapakuwa na Serikali nyingine yo yote waliyochagua wananchi wa Zanzibar
wakapokonywa. Ni chama cha CUF tu
ndicho kilichopingana na Katiba na Sheria kwa kukataa kushindwa. Lakini chama cha CUF na wananchi wa Zanzibar
ni vitu viwili tofauti.
·
Tatu, madai kwamba vipengele muhimu vya muafaka havijatekelezwa
ni upuuzi na upotoshaji mtupu.
Vipengele vyote muhimu vimetekelezwa.
Vipengele muhimu ni vile vilivyohitaji marekebisho ya Katiba na
Sheria. Hakuna asiyejua kwamba:-
(a) Marekebisho ya 8 na 9 ya Katiba ya Zanzibar yamefanywa kutokana na matakwa ya Muafaka.
(b)
Imetungwa Sheria ya Tume ya Muafaka.
(c)
Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar imefanyiwa
marekebisho katika kukidhi matakwa ya Muafaka.
(d)
Kutokana na marekebisho hayo ya Katiba na Sheria,
hatua kubwa kubwa zifuatazo miongoni mwa nyingi nyinginezo za utekelezaji wa
muafaka zimeweza kuchukuliwa:-
(i)
Kuundwa upya kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambapo
uteuzi wa wajumbe wake umeshirikisha wapinzani, hususan CUF;
(ii)
Kuundwa kwa Tume ya Muafaka yenye wajumbe kutoka CCM
na CUF;
(iii)
Ofisi ya Mwendesha Mashitaka imeanzishwa Zanzibar;
(iv)
Kufanyika kwa uchaguzi mdogo mwaka 2003;
(v)
Kuanzishwa kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Vipengele vichache vya muafaka vilivyobaki ni vya matokeo tu (consequential) na haviwezi kuwa na uzito wa umuhimu sawa na hivyo vya msingi vilivyogusiwa hapo juu. Vipengele kama vya ulipaji wa fidia vinahitaji fedha ambazo hazipo. Hata baadhi ya viongozi wenyewe wa CUF wamesaidia kuzifuatilia fedha hizo kwa wahisani waliokuwa wameahidi bila ya mafanikio.
·
Nne, madai ya Lipumba kwamba
CCM iliwahi kuua watu wasiokuwa na hatia na kwamba eti itaua wengine zaidi,
hizi ni tuhuma nzito ambazo lazima azithibitishe, vinginevyo CCM italazimika
kuchukua hatua za kisheria dhidi yake.
Kwanza tunazikanusha vikali tuhuma hizo. CCM ni chama ambacho hupitisha maamuzi yake kwenye vikao. Wakati tunakanusha vikali tuhuma hizo,
tunamtaka Lipumba ni lazima awaambie Watanzania ni vikao gani hivyo vya CCM
vilivyopitisha maamuzi ya kuua watu na vilikaa lini na wapi?
Kauli hiyo ya Lipumba ni ya kukichafulia jina na kukivunjia heshima Chama Cha Mapinduzi ambacho kinaheshimika ndani na nje ya nchi yetu kama chama pekee nchini kinachohubiri sera za amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kamwe hakiwezi kuachia heshima yake ivurugwe hivi hivi tu na wanasiasa muflis wa sera zenye matumaini kwa Watanzania kiasi cha kuishia kwenye sera za vitisho na kiu ya kumwaga damu.
Tunamtaka Lipumba aiombe radhi CCM kama kweli ametamka maneno aliyonukuliwa na Majira au akanushe kama hakuyatamka. Vinginevyo, CCM italazimika kwenda kutafuta haki yake ya kusafishwa jina lake na heshima yake kwenye vyombo husika vya sheria.
Omar R.
Mapuri (Mb.),
KATIBU WA
NEC
ITIKADI
NA UENEZI