TAMKO LA KAMATI KUU YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA KUHUSU VITISHO DHIDI YA WATANZANIA WENYE ASILI YA BARA HUKO ZANZIBAR

 

Katika kikao chake cha tarehe 19-20 Machi, 2004, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea kwa mshangao na masikitiko makubwa taarifa ya kujitokeza kwa vitisho vinavyotolewa dhidi ya wananchi wenye asili ya Tanzania Bara Visiwani Zanzibar.

 

Vitisho hivyo vya kibaguzi, chuki na uhasama havina mwelekeo mwema kwa hatima ya umoja na mshikamano wa Watanzania tulioachiwa na waasisi  wa Taifa letu la Tanzania, yaani Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.  Kwa maneno mengine ni vya kutaka kuvunja Muungano wa Tanzania.

 

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM inakemea vikali vitendo hivyo ambavyo inaviona ni vya kihuni na kihalifu.  Kama vitendo hivyo vina mkono wa kisiasa, vinadhihirisha pia jinsi wanasiasa wahusika walivyofilisika kisiasa kwa kukosa sera za kuwaelezea wananchi zenye kuleta matumaini kwa watu na Taifa.

 

Kamati Kuu inasisitiza kuhusu haki ya Kikatiba waliyonayo Watanzania ya kuishi katika sehemu yo yote ya Tanzania bila ya bughudha mradi hawavunji Sheria.  Ni kwa kutumia haki hiyo ndiyo maana maelfu  ya Watanzania wenye asili ya  Tanzania Bara wamefanya Zanzibar kuwa maskani ya kudumu kama vile maelfu ya Wazanzibari walivyofanya Tanzania Bara kuwa maskani yao ya kudumu.  Na kwa muda wote wa miaka 40 ya Muungano wetu wamefanya hivyo na kuendesha shughuli zao za kujitakfutia riziki bila ya bughudha, kila mmoja akijiona yuko huru na yuko nyumbani.

 

Kamati Kuu inatoa wito kwa Watanzania wote kuzikataa chokochoko hizi za kuwagawa zenuye mwelekeo wa kuitia nchi katika mtafaruku.  Watanzania wote tunao wajibu wa kudumisha urithi wa umoja na mshikamano wa Kitaifa tulioachiwa na waasisi wa Taifa letu.  Kila mmoja wetu na sote kwa pamoja tutekeleze wajibu huo na tusitoe nafasi kwa wachache wenye nia mbaya kutuondoa katika lengo hilo.

 

Mchanganyiko kati ya watu wa Bara na Visiwani ni mkubwa na historia yake ni ndefu kiasi kwamba leo siyo rahisi kuwatenganisha kwa vigezo vya asili ya mtu bila ya kusababisha mgogoro mkubwa wa kiusalama.

 

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

 

 

Omar R. Mapuri (Mb.),

KATIBU MWENEZI WA CCM TAIFA

20/03/2004