UTEUZI WA WAGOMBEA URAIS -WANACHAMA 5 KUPELEKWA NEC YA 3.5.05

 

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi ilikutana tarehe

2 Mei, 2005,  Dodoma chini ya  Mwenyekiti wa Chama, Ndugu Benjamin William Mkapa.

 

Miongoni mwa mambo mengine, Kamati Kuu katika kikao hicho, ilifanya uchujaji wa majina ya wanachama wa CCM walioomba kuteuliwa kuwa wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.  Kwa mujibu wa vifungu vya 110(6)(b) na (d), Kamati Kuu ina jukumu la kupendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa majina yasiyozidi matano ya wanachama wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na majina yasiyozidi matatu kwa kiti cha Rais wa Zanzibar.

 

Katika kutekeleza jukumu lake hilo la Kikatiba, Kamati Kuu iliamua kupendekeza yafuatayo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa:-

 

1.                  Kuhusu Kiti cha Rais wa Zanzibar

         

Kamati Kuu iliafiki pendekezo la Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwamba lipelekwe jina moja tu la Ndugu Amani Abeid  KARUME kwa kupigiwa kura na Halmashauri Kuu ya Taifa.  Kwa hivyo, ilimuomba Dr. Mohammed Gharib Bilal, mwanachama mwingine aliyekuwa ameomba nafasi hiyo kuondoa jina lake.  Dr. Bilal alikubali na akaondoa jina lake.  Kamati Kuu ilimshukuru na kumpongeza Dr. Bilal kwa ujasiri huo wa kukiweka Chama mbele kuliko utashi wa binafsi.

 

2.                  Kuhusu Kiti cha Rais wa Jamhuri

 

Kamati Kuu iliamua kupitisha na kupendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa majina matano yafuatayo:-

 

(1)      Dk. Abdallah Omari KIGODA

(2)      Ndugu Jakaya Mrisho KIKWETE

(3)      Prof. Mark James MWANDOSYA

(4)      Dk. Salim Ahmed SALIM

(5)      Ndugu Frederick Tluway SUMAYE

 

Wanachama wote hao watapigiwa kura na Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha tarehe 03/05/2005 mjini Dodoma.  Ndugu Amani Abeid KARUME atapigiwa kura za Ndiyo/Hapana na waliobaki watapigiwa kura ili kupata watatu wa kupendekezwa kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa.

 

 

Omar Ramadhan Mapuri (Mb.),

KATIBU WA NEC

ITIKADI NA UENEZI